Mpenzi Zanzibar

Mpendwa Zanzibar,

Natumai waendelea vyema na afya yako. Ni miaka mitatu karibu na nusu sasa tangu nimekuhajiri kuja Ughaibuni kufuta ujinga. Ingawa ndani ya kipindi hicho tumeshaonana mara mbili, mwisho juzi tu, lakini nahisi kama nimekukimbia kwa karne na karne. Natamani nikuone kila saa kila dakika. Mapenzi yangu kwako yanataka kila upumzi niupumuao basi niupumue nikiwa na wewe, lakini ndio bahati mbaya haiwezekani. Lazima niwepo hapa nikamlishe utumwa wako mpenzi! Ila jua kwamba nakupenda sana na nakutamani. Na ni nani asingaetamani kuwa na wewe?

Vipi ndugu yako Pemba hajambo? Bibi yule nae na visa vyake, mnh! Mashallah Mungu amuweke. Mara hii nilipomtembelea alinifanyia vituko vya wali wa maji, alinichekesha, nikacheka mpaka nikakatika mbavu… Na naona kabadilika kidogo, uso wake umekunjuka na umejaa bashasha kidogo, tofauti na miaka michache iliyopita. Ucheshi wake kwa watu si rahisi kutambua kuwa bibi yule yuna shida. Lakini mimi najua. Najua kuwa ana shida. Si ndio mpaka akatungiwa nyimbo mwanzoni mwa karne hii ni yule Muhiji Gora? Nampa heko kwa jinsi nyimbo ile ilivoendana na muimbwa!

Vipi naskia umepata walinzi wapya mpenzi, ni kweli? Vipi wanakusaidia vizuri au ni jora ileile ya zamani? Nilipata kuskia baadhi ya hadithi zao kuwa ati wajitahidi sana kusema na kugomba, lakini je wafuatilia matatizo yako, wakayapatia ufumbuzi na/au kuyachukulia hatua? Na naskia hao wawili wakubwa wote ni watoto wa ndugu yako, bi Pemba. Vipi angalau wamkumbuka mama yao. Najua huenda ikawa hawajafanya kazi kama ulivotarajia mpaka sasa, lakini wape mda kidogo. Kazi ulizowapa si ndogo hasa ukizingatia iliwabidi waanze alifu kwa ujiti. Ila watahadharishe, tena watahadharishe na maradhi ya kujisahau na umbilikivu. Si umeyaskia yaliyowatokea Abidina na Mbaraka? Nguvu za wanasesere!

Mpendwa Zanzibar,

Rafiki zangu nawasimulia sana kuhusu uzuri wako, wema wako, ukarimu wako kwa wageni na haiba yako kwa ujumla. Nyoyoni mwao wanatamani wangekuwa na uhusiano wa karibu nawe kama nilivo mimi kwako, lakini hawawezi. Na watawezaje? Mimi nimebahatika. Mimi ni mteule wa Mungu kuwa mpenzi wako. Pia nafarajika sana nikaapo na Waghaibu wakasimulia mazuri yako. Natamani ungeniona! Bichwa lazidi mwili, tabasamu likachana mdomo na jasho likageuka uturi. Utaniona nabadilisha mpaka mijendo, madaha kama ngamia. “Mimi ni wa Zanzibar… Mimi ni wa Zanzibar” utaniskia najilabu!

Lakini nikaapo na wengine wakujuao kwa undani, wakataja aibu zako, aahh! Wallahi najiskia vibaya kijuso kikawa kidogo kikaweza fumbatika kiganjani. Pamoja na hivo, siukani upendo wangu kwako. Nabaki kuwa ni wako na sijibadilishipo. Na kwa nini nijibadilishe? Niseme mie wa nani? Sisemipo mie ni wa mwengine! Sitavaapo guongwa hamba n’langu. Guo chafu min’gande, lanuka, launguza kwa joto… la hasha! Nitabaki mimi kuwa ni mimi na wewe ndiwe wangu. Nakupenda kama ulivo, uzuri wako ubaya wako. Kwani apendae jipu si hupenda na usahawe?

Mpenzi,

Nakumbuka kwa ulimi wako mtamu ulinifundisha kuwa “akwambiae ndie akupendae.” Nlitaka kukwambia zamani dukuduku langu, tangu enzi zileee ulipokuwa ukilindwa na makomando lakini nikaogopa. Nisiogope? Naam niliogopa. Ningekwambia siku zile ungenikosa. Ungenitafuta usinijue nilipo. Hata ungeniona aahh wapi! Sifai. Ninyan’ganyan’ga. Hawakiambilika wale. Ila sasa nahisi ndio wakati muwafaka wa kukwambia. Na nakwambia ili ujirekebishe. Na nakwambia kwa kuwa nakupenda, wewe ni wangu wa milele. Nakwambia kwa kuwa naamini walinzi wako wapya waweza niruhusu nikwambie bila ya kunidhuru. Wao pia naamini wanaamini nnayokwambia ni muhimi kwako na kwa maslahi yao wao, watumishi wako.

Mpendwa Zanzibar,

Siku moja kwenye mizunguko yangu huku Ughaibuni nilipita kigahawani kustaftahi. Wakati nikinywa chai yangu ya kutengeneza, si ya kupika kama ile yako ya tangawizi na midalasini na michaichai na karafuu, macho yangu yakagongana na maandishi yaliyorembwa kwa nakshi pale kaunta yakisomeka “If you are happy with our services tell others, if not please tell us!” Kwa ulimi wako ungesema “Ukifurahia huduma zetu wambie wengine, usipofurahia tafadhali twambie sisi” Ujumbe huu uliganda mawazoni mwangu na nikasema nitautumia katika kuimarisha mapenzi yetu mimi na wewe. Sifa zako nzuri ntawaambia watu wengine, na aibu zako ntakwambia mwenyewe tu ili ujirekebishe.

Mpendwa,

Pamoja na kubadilisha walinzi na mfumo mzima wa maisha yako bado unahitajika kujiboresha. Ujiboreshe kimiundombinu na kimawazo. Zamani ulijibweteka sana ukawa hujiwezi kwa lolote. Ukawa hata mavi ya kuku huwezi yaondowa mlangoni kwako kama hujapata msaada kutoka nje. Hii haikuwa, na si tabia nzuri kwa mrembo kama wewe. Uyawezayo yafanye mwenyewe mpenzi. Yatakayokushinda nambie mie, nami yakinishinda ntakutafutia viumbe vyenzio, vyenye nia njema vikusaidie. Hivi mpenzi nikuulize, kweli wewe unashindwa kudhibiti uchafu wa mazingira yako?

Najua vyanasesere vyako vishajijengea tabia ya kutupa uchafu ovyo popote pale. Hata vile ulivoviweka kwenye yale makasri ya Michungwani, yale marefu kwa urefu na marefu kwa upana, vyovyo pia hutupa takataka zao kwa madirishani, zikapeperuka na hatimae kutua musimohusika. Hivi nikuulize tena, kama ungeliweka madoo speshel ya kutupia taka kila mita hamsini mitaani, kisha ukavijengea uelewa vyanasesere vyako juu ya umuhimu wa kuhifadhi taka humo isingewezekana? Hilo lingekupa wewe haiba njema ya umaridadi, na lingekupunguzia gharama za kuwalipa wale wasafishaji wako ambao hawana wasafishapo. Unalionaje wazo hilo?

Najua utatoa hoja kuwa vyanasesere vyako havielewi, lakini sikubaliani na wewe. Vyaelewa. Mbona mwaka jana ulipo vijengea uelewa ukaviradulisha mseto na wali mweupe mbona vilielewa? Vikaradua mseto? Mi binafsi naamini vyaelewa kama wewe mwenyewe utaonesha umuhimu na kukerwa na uchafu wa mazingira yako. Ni juu yako tu kufanya jitihada kama ile uliyoifanya wakati wa uradulishaji.

Na vipi kuhusu ujinga?

Nakumbuka ulipobiruana arba’a w’ sitina ulitangaza nia thabiti ya kutaka kuondoa ujinga, mbona siuoni kuondoka –au, mbona nauona hauondoki? Nahisi afadhali ile miaka ya mwanzo kuliko sasa. Nilipokuuliza mara moja kuhusu maendeleo ya kuondoa ujinga ulinijibu “nshapiga hatua kubwa sana mpenzi, nshajenga mabanda telee kuvitia vyana vya vyanaserere visome.” Wako waliokupinga kwa kukuhoji “kwani kuwa na mabanda tele ndio kuwa na ilmu bora?” Sikumbuki uliwajibu nini. Lakini hoja yao ilikuwa na mashiko maana nilipokuja kukuona juzijuzi nikatembelea huko mabandani, imani iliniingia. Vyereje chumba kimoja ukafyekenyeza vyanasesere zaidi ya sabini? Wavisomeshaje? Vyafahamuje? Vyazingatiaje? Na vyapasije? –kama huko kupasi kuko.

Imani yangu hiyo ndio iliyoniamsha usiku huu, ikanambia “haya, kopoka… ruka ukitoja, uzinge njia ya kumsaidia mpenzio vile vyanaseserevye…” ndipo hapa nipo. Kitu cha kwanza nikasema nifanyie utafiti hili jambo la kufuta ujinga. Nijue kuna mabanda mangapi kwako na kwa nduguyo, bi Pemba. Nijue mna kiwango gani cha ujinga (sikusudii kukudharau wala kukutukana mpenzi, usinielewe vibaya),na taarifa nyingine za kunisaidia mimi kukusaidia wewe kuvisaidia vyanasesere vyako kujisaidia. Kwani nlipata taarifa? Sina nlichokipata.

Kwa nini? Kwa kuwa huku ughaibuni tuna mazowea mabaya. Kuna hili dude laitwa kompyuta, ambalo ndani yake mna mashine ya kutafutia mambo popote yalipo duniani, laitwa Gugul, kama sikosei. Hili lishatuathiri kiasi ya kwamba wakati mwingine mwanasesere akipoteza kitu ukumbini basi hutamani akitafute kwa humo kwenye Gugul. Basi humo ndimo nami nlimokimbilia kutafuta hizo taarifa za ujinga, zako na za nduguyo. Nilifurahi nilipoona utando wako wa dablyudablyudablyu, ambamo ndani yake muna vitando vidogovidogo vya viungo vyako. Cha ajabu, na pia cha aibu ni kuwa vitando vya viungo vyako hakuna hata kimoja chenye taarifa yoyote, si za ujinga tu. Hivi mpenzi nikuulize tena, ‘ivi ni kweli washindwa hata kuuhuisha huo utando, ukaulisha taarifa na habari zako ili wasio kujua wakujue, na watakao habari zako wazipate? Washindwa? Washindwa?

Mpenzi Zanzibar,

Tambua kwamba wakati unabadilika, na katika wakati huu tulionao viumbe kama wewe mnaolingana kwa umbo, umri na kipato wameshakuacha nyuma kwa miongo kadhaa… Dunia ya sasa mpenzi kiumbe kama wewe lazima uende na wakati hasa katika mambo kama haya ya tekinolojia. Na hili mpenzi waweza lifanya mwenyewe, bila kutegemea msaada wa waghaibu. Mpenzi, unajua kama saivi hata vyanasesere kimojakimoja vina mitando yao wenyewe, na huilisha habari kila siku, kama si kila saa?. Si unawakumbuka akina Yatmia, Akhash, na wenziwao? Wao pia wameanzisha utando wao, waitwa MPENDAKWAO, ambao sehemu kubwa ya kazi yao ni jitihada ya kutaka kukusaidia wewe na pia kukutangaza.

Mpenzi,

Najua ungependa kujua vipi naendelea na maisha yangu huku niliko. Alhamdulillah, maisha yangu ni mazuri. Na ni mazuri kwa kuwa tu nimemkabidhi Mungu kuyaongoza. Hivo hakuna liharibikalo. Kwa maswala ya kujikimu usiwe na wasiwasi. Kama walivowanasheria kutegemea migogoro ya watu kuwa ndio riziki yao, au wachimba makaburi kutegemea vifo vya watu kuwa ndio pato lao, ndivo mimi ninavotegemea manyaji ya watu kuwa vuno langu. Siku watu wajapoamua kugoma kufanya shughuli hii basi na mimi nitakuwa tabuni. Siombi kuwa waongeze kasi kwani huo utakuwa ni ugonjwa, lakini naomba waendeleze japo kwa kasi hiihii ya sasa ili nami nipate mradi wangu.

Ni hayo tu kwa leo mpenzi. Natumai niliyokwambia utayafanyia kazi. Jihadhari na mashoga wanaojifanya kukupenda ati muunge urafiki sijui ndio udugu. Hao hawana nia njema na wewe. Wataka wakulie vyako tu, wao wanenepe wewe uangamie. Si unakumbuka siku zile wakakunyanganya mpaka kibatari ati kwa kuwa hujawalipa pesa za mafuta? Dumisha usafi wa mazingira yako, fanya kila unaloweza kwa mikono yako bila ya kutarajia msaada wa yoyote, kwani hakuna msaada usio na lengo. Kuwa mbunifu wa njia za kutatua matatizo. Hakikisha walinzi wako hawakorogwi au kukorogana akili wakawa kama wale waliotangulia. Wasimulie mara kwa mara hekaya za Abidina na Mbaraka ili yasije yakawapata na wao yaliyowapata wao.

Hadi mara nyingine mpenzi, nakutakia kila la kheri. Kumbuka nakupenda na nakutamani sana!

Nimi wako wa daima,

Hamad²

2 thoughts on “Barua kwa Mpenzi Zanzibar kutoka kwa Hamadi wa Hamadi!”

  1. Asalam Alaykum
    Napenda nichukue fursa hii kukushukuru ww mwandishi wa baruahii adhimu na adimu kwa mpenzi wako Zanzibar , lakini hata na sisi wanasesere imetuelimisha na imetufunza sana. Hofu yangu ni kwa walizi wa Mpenzi wako na hasa pale wanapoendelea kuteuwa wasaidizi wao katika ngazi za chini inasikitisha na inatia huzuni kuona baadhi ya walinzi walikuwepo vipindi vingi vilivyopita na kazi zao sisemi hazikuwa nzuri ila pia hazikuwa bora. pia umri pia unawatupa mkono katika karne hii na mrembo wako kupangiwa walinzi waliochoka hapo awali na kustaafu leo hii wanarejeshwa tena? ah! nasikitika kuona kimwana kitarudi tena nyuma kutoka pale kilipofika.

    Ahsante kwa kuzingatia maoni yangu
    Sesere aliepo kwa shoga mkuu kumalizia masomo yangu.

  2. Nikweli ya hamadi na si Hamadi pekee akupendae ila hamadi yahitaji uchukue hatua za makusudi kuvielimisha hivi vijana kele vya mpenzio kuhusu matumizi ya miytandao kuleta mabadiliko ya mamengwa.
    Maana nawaona wamejikita zaidi katika mapenzi na udaku , nawaona kwenye FACEBOOK hawanajambo zidi ya upuuzi wakumbushe kua mapinduzi ya kiuchumi, siasa,ata yaliowazunguka ni ustaarabu wa mtandao ktk dunia ya leo, au ndio ujinga anaoendelea kutupa huyu mpenzio ZANZIBAR?

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.