Libya twende!

Ni bahati mbaya sana kwamba kiongozi ambaye alikuwa amejijenga kama mgumu, asiyegusika, asiyetukusika, asiyeanguka, Muammar Gaddafi wa Libya, sasa ameamua kuonesha sura yake halisi linapokuja suala la upinzani dhidi yake.

Taarifa za tangu jana zinaonesha kuwa anatumia vikosi vyake vya jeshi na wanamgambo kuuwa raia wake wanaoandamana kwenye miji ya Benghazi na Tripoli dhidi yake. Hesabu ya Shirika la Haki ya Binaadamu la Human Rights Watch zinaonesha kwamba kwa siku nne tu, tayari Gaddafi ‘ameshakunywa damu’ za Walibya 300!

Ufalme wa Al-Khalifa wa Bahrain ulijaribu kufanya hivyo siku nne zilizopita, lakini baada ya siku moja ukatambua kwamba hiyo si dawa. Utawala wa Ali Abdullah wa Yemen nao ulidhani kwamba ungeweza kukabiliana na waandamaji kwa staili ya risasi na mabomu. Sasa nao unasema unataka kuzungumza na wapinzani.

Lakini, tawala zote mbili, za Bahrain na Yemen, zinatumia staili ile ile ya, kwanza, Zine el-Abidine Ben Ali wa Tunisia, na kisha Hosni Mubarak wa Misri, mbele ya madai ya waandamanaji. Kwanza walitoa kidole, kisha wakatoa kiganja, kisha mkono. Lakini kwa kuwa waandamanaji walikuwa wanataka kichwa, hawakuwa radhi mpaka walipopewa shingo wakaikata. Ka! Na huo ukawa mwisho wa watawala hao.

Bila ya shaka mwisho wa Saleh na Al-Khalifa nao unakuja. Lini? Siku si mbali, lakini kunaweza kukawa na staili tafauti kidogo, kutokana tu na namna waandamanaji watakavyojiunga na kujipanga.

Lakini mwisho wa Gaddafi utakuwa mbaya zaidi. Zaidi kuliko wa Saddam Hussein, ambaye alikuja kuondoshwa madarakani na majeshi ya kigeni na kunyongwa na mahakama yenye ushawishi wa mataifa ya kigeni. Gaddafi atamalizwa na raia wake mwenyewe. Naogopa sana, tena sana, kuja kuiona maiti ya Gaddafi ikiburuzwa mitaani kama ile ya Samuel Doo wa Liberia. Lakini nachelea kwamba huko ndiko tunakoelekea.

Kwa nini? Kwa sababu, yeye amezidi mno katika hatua zake za kuwadhibiti waandamanaji. Usiku huu tumepokea taarifa kwamba ameanza hata kutumia ndege za kijeshi kuwapiga mabomu raia wake mwenyewe. Natokea nchi ambayo kuna wakati ilifanya maandamano mfano wa haya, na yakakabiliwa kwa nguvu za kupindukia mpaka zinazokaribiana na hizi. Najua makovu yake yanavyokuwa vigumu kupona, hata baada ya jitihada kubwa za kuyaponesha zinapofanywa.

Kwa sasa, naungana na ndugu zangu wote katika ardhi za Libya, Bahrain, Yemen, Algeria na kwengineko. Nawaambia wanachokipigania ni cha haki. Machungu makubwa yatawakabili. Makubwa sana. Lakini hizo ndizo gharama zinazolipwa kwa mabadiliko ya kweli. Tusonge mbele. Tufafika tu!

Na mwanzo wa kufika umeanza kuonekana. Kijeshi, tunasema vita vinaanza kukugeuka unapoona ama majemedari wako wanakukimbia au wanaungana na adui yako. Yote mawili yameanza kumtokezea Gaddafi. Mabalozi wake katika nchi mbalimbali duniani usiku huu wamejiuzulu nafasi zao kupinga ukandamizaji wake. Makamanda wa kijeshi wanaungana na waandamanaji. Wengine wanakaidi amri ya kufyatua risasi kwa raia na wanaamua kukimbilia nje ya nchi. Hata mawaziri wanaanza kumuacha mkono.

Mwisho u karibu! Lakini kwetu husema pia kuwa “jiti kubwa likigwa, hugwa na n’shindowe.”. Kwa maana ya kuwa mti mkubwa unapoanguka, huanguka na vishindo vyake. Kwa mfano, huacha shimo kubwa pale ulipong’oka, na hicho utakachokiangukia huko mbele, hukihasiri: nyumba huvunjwa, barabara huzibwa, na kama kiumbe pia hukiua, ikiwemo miti midogo iliyo jirani yake.

Ndivyo Gaddafi anavyong’oka. Maana hapana shaka kuwa yeye ni mti mkubwa, kwa namna yoyote utakayomueleza. Lakini si mkubwa kuliko Libya na Walibya. Libya twende!

5 thoughts on “Libya twende!”

  1. Alhabib,

    Unahasira gani na Viongozi wetu na Kiarabu? mbona umekuwa na hamasa za kuona wanaondoka madarakani kupindukia?

    1. @Issa. Wallahi sina hasira za binafsi na kiongozi yeyote yule wa Kiarabu, Ila nina hasira na dikteta yeyote yule, ambaye anawakandamiza watu wake, awe Mwarabu, Muafrika au Mzungu. Kwangu sauti ya haki haina mipaka ya kijiografia, kiwakati wala kirangi. Kila dhalimu mwisho wake huwa ni hasara, na hivi ndivyo inavyoonekana kwa hawa watawala wanaopinduliwa sasa, ambao bahati imetokea kuwa ni Waarabu. Lakini si kwamba nawachukia wao kama wao, nachukia mifumo ya utawala wao, kama vile ninavzowachukia watawala wa Kiafrika kwa ufisadi na ukandamizaji wao na wa Kizungu kwa unafiki wao.

    1. @Stumai. Usahihi na ukosefu wa usahihi, si mimi na wewe wa kuamua. Unapofika wakati watu wamekandamizwa kwa siku nyingi, wanabadilika kutoka kuwa viumbe wa khofu na kuwa vumbe wa ujasiri. Akina Gaddafi na wenzake, wametumia muda miwngi kuwakandamiza watu wao kwa kuonesha ulimwengu kwamba wao ni majabari. Sasa umma umetoka khofu na unachukua hatua mikononi mwao

  2. @Issa. Wallahi sina hasira za binafsi na kiongozi yeyote yule wa Kiarabu, Ila nina hasira na dikteta yeyote yule, ambaye anawakandamiza watu wake, awe Mwarabu, Muafrika au Mzungu. Kwangu sauti ya haki haina mipaka ya kijiografia, kiwakati wala kirangi. Kila dhalimu mwisho wake huwa ni hasara, na hivi ndivyo inavyoonekana kwa hawa watawala wanaopinduliwa sasa, ambao bahati imetokea kuwa ni Waarabu. Lakini si kwamba nawachukia wao kama wao, nachukia mifumo ya utawala wao, kama vile ninavzowachukia watawala wa Kiafrika kwa ufisadi na ukandamizaji wao na wa Kizungu kwa unafiki wao.

    @Stumai. Usahihi na ukosefu wa usahihi, si mimi na wewe wa kuamua. Unapofika wakati watu wamekandamizwa kwa siku nyingi, wanabadilika kutoka kuwa viumbe wa khofu na kuwa vumbe wa ujasiri. Akina Gaddafi na wenzake, wametumia muda miwngi kuwakandamiza watu wao kwa kuonesha ulimwengu kwamba wao ni majabari. Sasa umma umetoka khofu na unachukua hatua mikononi mwao

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.