Mkasa wa waandamanaji waliopo hivi sasa kwenye viwanja vya Tahrir, mjini Cairo, Misri, umesadifiana na mambo mawili, kwa kiwango ambacho mimi binafsi ninahusika.

Sadfa ya kwanza ni kwamba, mwaka 2001, kwetu Zanzibar tulifanya maandamano ya kulalamikia uchaguzi wa 2000, ambao kwa mtazamo wa sisi tulioandamana, haukuwa uchaguzi hasa, bali fujo ambayo ilipelekea mgombea wa chama tawala kutangazwa mshindi.

Bila ya shaka, tulikuwa na madai mengine, likiwemo la mabadiliko ya Katiba, uundwaji mpya wa Tume ya Uchaguzi na kurudiwa kwa uchaguzi huo. Maandamano haya yaliungwa mkono na wenzetu walioko Tanganyika.

Serikali ilijibu kwa mauaji, ubakaji, uharibifu wa mali na ukandamizaji wa haki za binaadamu. Ripoti ya shirika la kutetetea haki za binaadamu duniani, Human Rights Watch, iliyoitwa: “Risasi zilimiminika kama mvua!” inaeleza undani wa mkasa wenyewe.

Wakati huo nilikuwa na miaka 23 na mwanafunzi katika Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni, nikichukua Diploma ya Lugha, Kijerumani likiwa somo langu kuu.

Leo hii nikiwa na miaka 33 na nikiwa ndani ya Ujerumani, waandamanaji wako kwenye uwanja wa Tahrir wakidai kitu kisichopishana sana na tulichodai sisi miaka kumi iliyopita. Haki. Usawa. Kusikilizwa!

Maandamano haya ya Tahrir yalianza karibuni na siku ile ile ambayo ya Zanzibar yalianza. Ijumaa ya tarehe 26 Januari 2001, vikosi vya serikali vilimpiga risasi Imamu wa Msikiti wa Mwembetanga, Unguja, na tangu hapo hasira zikaanza kutupanda, na siku ya pili tukamiminika barabarani bila kujali vitisho na risasi za vyombo vya dola. Ya Tahrir yalianza Ijumaa ya tarehe 25 Januari 2011 na tangu hapo hayajanyamaza tena, licha ya mauaji, vipigo na mateso mengine.

Lakini pana sadfa nyengine. Katika kipindi hicho cha giza, Zanzibar tulitegemea zaidi Idhaa za Kiswahili ya BBC, Uingereza na Deutsche Welle Ujerumani. Siku ya nne ya maandamano kuanza, yaani tarehe 30 Januari 2001, Deutsche Welle ilitangaza kupokea taarifa zinazosema kuwa, helikopta za jeshi zilikuwa zikiwafuata watu ambao walikuwa wanakimbia kwenye majahazi kuelekea ukimbizini Kenya na kuwamiminia risasi.

Mimi na mwenzangu, Khamis Makame, tulikuwa tunatoka kuswali swala ya Adhuhuri pale Msikiti wa Sharifu, mtaa wa Mkunazini, karibu na kwa Battashi. Ninakumbuka kuwa aliyekuwa akitangaza taarifa hii, alikuwa ni Othman Miraji, ambaye alimfanyia mahojiano mtu mmoja, lakini sikumbuki ni muda gani nilipokaa kitako kwenye kibaraza cha ambalo sasa ni duka la vifaa vya magari la Buda, nikaanza kulia.

Mwenzangu, Khamis, akanishika bega: “Usilie Mohammed, utakusanya watu bure!” Ndivyo alivyonambia.
“Waache wakusanyike!” Ndivyo nilivyomjibu!

Leo hii, ni mimi ndiye niliyepo kwenye studio za Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle, hapa Ujerumani, nakitangazia yale yanayotokea kwenye uwanja wa Tahrir. Milio ya risasi. Mabomu. Machozi. Vilio. Maiti. Damu. Kwa uzito na uchungu ule ule aliokuwa nao Othman Miraji wakati wa ripoti ile miaka kumi iliyopita. Ila sina hakika, ikiwa huko Misri kuna ambaye anafahamu lugha ninayotangazia, japokuwa nina hakika wenzetu wa Idhaa ya Kiarabu, wanasikikana na wanasafirisha hisia zile zile kwa hadhira yao.

Nilipotoka hapo, nikaenda kuandika shairi lifuatalo, ambalo nililibandika kwenye ubao wa matangazo ya Taasisi, bila ya hata kupata saini ya Waziri wa Habari wa Serikali ya Wanafunzi, ambaye wakati huo alikuwa ni Ali Saleh Careca:

Kuna yapi ya uchungu, kama kumwagiwa damu?
Ya watoto damu changa, ‘liyotarajiwa
Ya vijana damu mbichi, ‘liyotegemewa
Ya wazazi damu pevu, ‘liyohishimiwa
Tukufu damu kumwagwa, pasipo ubinadamu
Ya mabavu serikali, watawala madhalimu
Kudhulumu watu wangu
Lakini, kesho, kwa jina Mungu
Tutainuka, tupambane hadi ushindi!

Ni upi kwani msiba, kama kupoteza watu?
Wako watu wa nyumbani: watoto, wazazi
Wako watu wa biladi: rafiki, wapenzi
Wako watu wa karibu: jamaa na wenzi
Watu walio dhalili, na woga wenye nidhamu
Yawajia serikali, kwa mitutu na mabomu
Kuwauwa watu wangu
Lakini kesho, naapa kwa Mungu
Tutainuka tupambane hadi ushindi!

Ni upi hasa unyama, kama kuvunjwa hishima?
Hishima ya wenye dini, wastaarabu
Hishima wenye imani, wanao adabu
Hishima ‘nojithamini, ‘nojuwa aibu
Kwao wao watu wangu, huu mkubwa unyama
Serikali is’o haki, nguruwe wake kutuma
Idhilali watu wangu
Lakini kesho, shahidi ni Mungu
Tutainuka tupambane hadi ushindi!

Ni yupi mwema mpenzi, kama mtu nchi yake?
Jamaa zangu watenzwa, waikimbie
Ndugu zangu wafukuzwa, watokomee
Aila inatatizwa, iselemee
Hata mbiyo wakitoka, kwa khofu na vilio
Yawendea serikali, na risasi juu yao
Tu! Tu! Tu! Watu wangu
Lakini kesho, kwa nguvu za Mungu
Tutainuka tupambane hadi ushindi!

Upi utungo nitunge, kukifu hii huzuni?
Ewe Damu ulomwagwa, hujakauka
Ewe Roho ulotwawa, hujaondoka
Ewe Ndugu ulopigwa, hujasahaulika
Vyovyote ewe muhanga, i hai yako dhamira
Mumepasi mtihani wa subira
Kwa kujitolea watu wangu
Nasi kesho, kwa msaada wa Mungu
Tutainuka tupambane hadi ushindi!

Kuanzia siku hiyo niliyolia na kuandika shairi hili, niliapa kwamba sikuwa na tena la kulipoteza kwenye mapambano, maana tayari nilishapoteza yote. Nikajiapia kwamba, mbele ya yeyote na wakati wowote, nitapigania kitu ninachokiamini. Wanaonijua wanaweza kunihukumu, ikiwa kiapo hiki nimekuwa nikikitimiza au la, lakini mwenyewe nataka kukiishi hadi mwisho wa uhai wangu!

Leo hii, mashirika mbalimbali ya habari ulimwenguni yameripoti kuwa, usiku wa jana ulishuhudia risasi zikimiminwa kwa waandamanaji kutokea juu ya nyumba zinazozunguka uwanja wa Tahrir na watu wanaofikiriwa kuwa ni wafuasi wa Rais Mubarak na polisi waliovalia kiraia. Hadi sasa watu 12, kwa uchache wameshauliwa uwanjani hapo na wengine zaidi ya 1,000 wameshajeruhiwa. Hapa hatuzungumzii wengine 200, ambao wameuawa kwa kipindi cha siku 10 hizi tu.

Leo hii, kijana mmoja aitwaye Abdullah Ghozli, ambaye kaka yake ni miongoni wa waliouawa usiku wa jana, amejitokeza tena uwanjani hapo na kuhutubia waandamanaji. Akawaambia: “Kaka yangu jana aliuawa hapa. Leo tumeshamzika. Baada ya maziko, mama yangu amenijia na kuniambia: ‘Abdullah toka nenda zako Tahrir alipokufa ndugu yako. Nenda kakipiganie alichokifia mwenzako!’” Nimelia tena kama siku ile pale Kwa Buda, Mkunazini, Unguja.

Nimelia nikiamini kuwa Abdullah na mama yake sasa wana nishati ile ile niliyokuwa nayo mimi kuanzia siku ile ya tarehe 30 Januari 2001. Nimelia niiwaombea kuwa, nishati hiyo itaendelea kuwaka ndani yao hadi angalau miaka kumi ijayo, kama si zaidi ya hapo. Nimelia nikijua kuwa ushindi mwishowe huwa kwa wale wenye haki.

Na hilo sina wasiwasi nalo, maana mimi mwenyewe ni ushuhuda wa hayo. Na Allah ni mbora wa mashahidi!

One thought on “Tahrir 2011 Vs Zanzibar 2001 kwa jicho la Mzanzibari”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.