Leo nimeamua kujitokeza kuitikia wito wa Zanzibar, apendae aje. Naamini wito huo hautoki kwa mtu binafsi au chama fulani cha kisiasa. Naamini huu ni wito ambao unaungwa na utaungwa mkono na Wazanzibari wote duniani na wenye kuongozwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar (SUK).

Mimi si mtaalamu wa mambo ya Sheria, Katiba au Mikataba, na naamini wengi wetu tutakuwa tunaona uzito kutoa maoni yetu juu ya suala la mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu tunajiona kuwa si wataalamu. Sifikirii kuwa tunatarajiwa tuwe magwiji wa Katiba ili tuweze kutoa maoni yetu juu ya mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tulichoombwa Wazanzibari ni kutoa maoni yetu juu ya misingi na mfumo wa hayo mabadiliko ambayo wataalamu wanaotusoma Zanzibar wataweza kugida na kuchuja yale ambayo watayaona yana faida na maslahi kwa Nchi ya Zanzibar, ya leo, kesho, na kesho kutwa.

Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, Rais Ali Mohamed Shein wa Zanzibar na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta, siku ya makabidhiano ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, Rais Ali Mohamed Shein wa Zanzibar na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta, siku ya makabidhiano ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.

Kuzaliwa tena Tanganyika na Mfumo Mpya

Jambo la kwanza ambalo kungwi la Katiba ya Zanzibar linatakiwa kulifanya ni kuisaidia Tanganyika IZALIWE tena Kikatiba na kila mtu, Zanzibar na Tanganyika, awe na chake au vyake kama walivyo wengi duniani. Oh! Wapenzi au wagonjwa wa mrengo wa aina fulani wa Pan-Africanism ndio watakaokuwa kwa kwanza kuruka na kujirusha. ”Si itakuwa mmeuvunja Muungano na Umoja wa Bara la Afrika – Pan-Africanism?” Kwani Pan-Africanism haiwezi ikafikiriwa kuwa na mfumo wa kama European Union (EU) au Gulf Cooperation Council (GCC)?

Na Harith Ghassany
Na Harith Ghassany

Kwa hiyo msingi wa kwanza wa Katiba mpya ni kuurejesha Muungano wa Jamhuri ya Tanzania kwenye nchi mbili zilizoungana tarehe 26 Aprili 1964, nazo ni nchi ya Zanzibar na nchi ya Tanganyika, na baada ya hapo ziingie katika mfumo wa cooperation wa aina ya EU au GCC. Tukumbuke pia kuwa chimbuko la kubadilishwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano lisingelitokea bila ya Zanzibar kuibadilisha Katiba yake mwaka 2010 na hiyo ndiyo maana halisi ya Maridhiyano na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ya Zanzibar. Katiba ya Muungano lazima IBADILIKE madam Katiba ya Zanzibar imefanyiwa mabadiliko iwe ya SUK. Inshaalla, hili ni lazima lifanyike na hakuna njia ya mkato! Sasa tunachoombwa kukifanya ni kuweka matakwa yetu ambayo yatakuwa ndio Msimamo wetu Wazanzibari popote pale tulipo na wa Mustaqbal wa Zanzibar!

Hili la safari hii ni ZITO, kubwa na la MWISHO na ni “mapinduzi” ya Zanzibar Daima. Nani alifikiria kuwa kutakuwa na Maridhiyano Zanzibar na Serikali ya Umoja wa Kitaifa? Lazima tuwe na matumaini na imani na tuisaidie Zanzibar ili Baraza la Wawakilishi liweze kufanya kazi yake kwa wepesi na wananchi wa Zanzibar waweze kuyapigia Kura ya Maoni mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ambayo ndio silaha ya kuiokoa Zanzibar na Tanganyika na isiyo na mlio hata ikiripuliwa!

Lakini Hawaaminiki Hawa!

“Hawaaminiki hawa, wakikwambia Mungu mmoja yuko juu tafuta ngazi ukachungulie kwanza!”

“Huwajui hawa? Ni ma Dracula ambao hata msalaba hawauogopi tena!”

Hawa nani? Kwani hili la kuibadilisha Katiba yenye kuitetea Zanzibar ni la Wazanzibari, la Zanzibar, au ni la chama fulani? Binafsi naamini kabisa kuwa suala kama hili lisingeletwa kwenye jukwaa la mtandao wa Kizanzibari, Zanzinet, bila ya kupata baraka za Zanzibar. Sasa tusimuamini nani? Rais wa Zanzibar Dkt Ali Mohammed Shein, au Makamo wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, au Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi,? Au potelea mbali, madam juzi CCM na CUF wamesheherekea miaka 47 ya Mapinduzi ya Zanzibar, basi Zanzibar yenyewe na ipotelee mbali!?

Na hapa ndipo penye hoja za baadhi yetu wenye kutokuwa au kutokwa na hamu na huu wito wa kutoa maoni juu ya mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Ukizisoma kwa kituo hoja zao utaona kuwa ndugu zetu hawa wachache wana fikra yenye kusema hivi: tutayaunga mkono mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano itakayoirejeshea Zanzibar hadhi yake iwapo “mapinduzi” ambayo yameichafuwa na kuiangusha hadhi ya Zanzibar, litaondolewa. Hapana shaka hii hoja ina uhalali wake lakini wakati ndiwo? Si sawa kuadhini baa au kutamka kuwa huamini Mungu Vatican? Kuyaunganisha mawili, Mabadiliko ya Katiba na Mapinduzi kunatupa nguvu zaidi Wazanzibari au kunatudhoofisha mbele ya wajanja wasiotutakia kheri na wenye kupanga mchana na usiku kuuvunja umoja wetu.

Bila ya shaka yoyote ile kuna Wazanzibari wengi ambao hawafurahikiwa na kusheherekea siku ambayo maelfu ya Waislam na Wazanzibari wenzao wa kila kabila na asili na wasio na hatia waliouwawa kikatili na kuteswa. Si hoja ya Kiislam kuwa umewaokowa watu ambao labda wangeuliwa. Hoja (kuna aya maalumu ndani ya Quran tukufu) ya dini ya Kiislam, na hata ya Kikristo, ni ukimuuwa binaadamu mmoja bila ya haki ni sawa na kuuwa umati mzima. Na ukimuokoa binaadamu mmoja ni sawa na kuuokoa umati mzima.

Matamanio na matarajio yangu binafsi ni kuishuhudia siku moja ya tarehe 12 Januari na kumuona Rais wa Zanzibar akiitangaza siku hiyo kuwa ni siku ya kuwaomba Wazanzibari wote radhi na ya kurudi kwa Mwenye Enzi Mungu kwa yalioifika Zanzibar, na badala yake siku hiyo ikageuzwa na kuwa ni siku ya Zanzibar kusheherekea kuurejesha Utaifa na Uhuru wake Kikatiba kutoka Tanganyika! Na tarehe 10 Disemba ikaendelea kuwa ni siku ya kuusheherekea Uhuru wa Zanzibar kutoka Himaya ya Kiingereza. Ni muhimu mawili haya yakaingizwa ndani ya Katiba ya Zanzibar ili kuzituliza Zanzibar na Tanganyika moja kwa moja.

Kwanini yasifanyike hivi sasa?

Hili suala ni jepesi na zito na linahitajia hikma na busara kwa sababu kimsingi vyama vyote viwili, CCM na CUF, vinalazimika kuyakubali Mapinduzi na Muungano. Wakati huo huo, ukipeleleza utaona kuwa hotuba za Marais wa karibuni wa Zanzibar zimekuwa zikibadilika na hii ya juzi ya Mheshimiwa Rais Dkt Ali Mohammed Shein imepata sifa ya kuwa na mtizamo wa kihivi sasa wa mapinduzi ya maendeleo. Kwa Zanzibar hakuna wakati mzuri wa kulizika jinamizi la mapinduzi isipokuwa kwa kuwaletea wananchi maendeleo makubwa sana ya kiilimu na kiuchumi peke yake. Upotoshaji wa mapinduzi utakufa wenyewe pale ambapo yatakuja Zanzibar mapinduzi ya maendeleo ya kiilimu na kiuchumi ya kweli. Wananchi wakianza kuyaona hayo ndani ya maisha yao na bila ya kuambiwa, wenyewe watatafautisha baina ya pumba na ukweli wa historia ya mapinduzi ya Zanzibar.

Juu ya hivyo, na hakuna sababu ya kutafuna maneno, ni muhimu ikatafutwa njia ya Kikatiba itakayopiga marufuku tafsiri na taswira mbovu ya Mapinduzi ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari 1964 ili Wazanzibari wanaotiwa unyonge na sherehe za Mapinduzi zenye kuyatonesha majeraha yao, na wao wajisikie kuwa ni wananchi wenye kuipenda na kupendwa na nchi yao. Viongozi walioko leo madarakani Zanzibar hawana historia ya kumuuwa mtu kwa hiyo ni rahisi zaidi kwao kuleta mabadiliko ya tafsiri na maana ya tarehe 12 Januari yenye kukubalika na kukubaliwa na Wazanzibari wote popote pale walipo.

Suala si kama tafsiri ya Mapinduzi ya Zanzibar ibadilike au isibadilike. Suala ni lini na vipi kujenga mazingira mapya yatakayowageuza wananchi wawe na muelekeo tafauti na ule ambao wameshauzowea kwa takriban nusu karne. Mbali ya faida na maafa yake, kama kuna kitu kizuri ndani ya neno ”mapinduzi” basi ni ile itikadi ambayo bado haijamalizika Zanzibar, ya kuleta mageuzi na katika wakati huu tulionao, bila ya ncha ya upanga au sururu. Na ndio maana Zanzibar bado ina uwezo na ina nafasi kubwa ya kihistoria kuleta mageuzi ya Kikatiba ambayo yatakuwa ni Mapinduzi ya Kikatiba yatakayoirejeshea Zanzibar hadhi yake na kuipa nguvu Tanganyika kuidai nchi yao; kutafuta njia ya kushirikiana baina nchi mbili zilizo SAWA badala ya Katiba ya Muungano wa nchi, moja ipo nayo ni Zanzibar, na ya pili (Tanganyika) haipo! Wakati huo huo nchi ambayo haipo (Tanganyika) inasheherekea Uhuru wake kwa jina la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, na nchi ambayo ipo (Zanzibar) haisheherekei Uhuru wake wa tarehe 10 Disemba 1963. Haya pia ni misingi ya kuzingantiwa katika mabadiliko ya Katiba ya Muungano.

Matakwa yetu na mabadiliko ya katiba

Hapana shaka yoyote wenye ati ati na wito huu wana uhalali wa kujadili chochote kile kwa uwazi kabisa na hakuna ambaye ana uwezo wa kumzuia mwenzake asiuseme ukweli au asiipiganie haki ya nchi ya Zanzibar. Almuradi wasiutumie uhuru wao kusambaza fikra potofu yenye kuinyima Zanzibar nafasi ya kihistoria ya kuutambua na kuurejesha Utaifa wake na wa Tanganyika. Kwa hivi sasa yenye faida kubwa zaidi kwa mustakbal wa Nchi ya Zanzibar ni haya yafuatayo:

a. Kulinda na kuhami mustaqbal wa Nchi yetu ya Zanzibar Kikatiba.
b. Kusaidia kuirudisha/kuzaliwa tena Tanganyika ndani ya Katiba ya Zanzibar na kuifufua G55 (ya aliyekuwa Mbunge wa Chunya, Njelu Kasaka, na akina Phillip Marmo na Paschal Degera) iliokuwa ikiidai Serikali ya Tanganyika na kuzimwa na Mwalimu Nyerere.
c. Zanzibar na Tanganyika kuwa na viti vyao Umoja wa Mataifa na kuwa na uwakilishi wao katika Bunge la Afrika Mashariki, Kikatiba.

Baraza la Wawakilishi na Kura ya Maoni

Inafaa pia ikumbukwe kuwa maoni tunayoombwa kuyatoa juu ya misingi ya mabadiliko ya Katiba yatapokelewa na kufanyiwa kazi Zanzibar. Ule mchezo wa sijui kuunda ”Tume ya Kero za Muungano” na kukaa na wenzetu kutoka ”Danganyika” hauko tena. Tukikaa nao watatuzidi maarifa tu. “Ah! Ngojeni tupige kura kwanza baina ya Wabunge wenu na wetu! Nyie lakini mko kidogo sisi wengi! ”

Halafu tusisahu kuna ujanja wa makusudi ambao sitaki kuufafanua kwa hivi sasa. Upi? Ni ule mpishano wa kiuchaguzi wa miaka kumi kumi 10/10, baina ya Zanzibar na Tanzania Bara. Mtakumbuka wakati wa chama kimoja, marehemu Mzee Idrisa Abdul Wakil alikaa kwenye utawala miaka mitano (1985-1990). Akaja Dokta Salmin Amour (1990-2000) akakaa miaka mitano ya mwanzo katika mfumo wa chama kimoja. Ulipoanzishwa mfumo wa vyama vingi hakuanza ZERO na kukaa kwenye utawala miaka 10. Alikaa miaka mitano tu.

Tizama upande wa bara sasa namna miaka 10 ya utawala unavyopishana na Zanzibar! Rais Mstaafu Benjamin Mkapa ametawala kuanzia 1995-2005, wakati Dokta Salmin aliwekewa amalize mwaka 2000. Imepishana miaka mitano na bara wakawa wana miaka mitano mbele ya Zanzibar. Rais Mstaafu Dokta Amani Karume alitawala kuanzia mwaka 2000 mpaka mwaka 2010. Ameondoka madarakani wakati Rais Dokta Jakaya Mrisho Kikwete ataendelea mpaka mwaka 2015. Sasa atakapoondoka madarakani Rais Kikwete hatujui atakuja kukaa nani na kwa hiyo inahitajika busara tena kubwa sana tusije tukafanya ujinga wa kuipoteza fursa ya kuiokoa Zanzibar kwa ajili tunataka kwanza tuvimalize vita vya jana na vya juzi! Hawa hawa viongozi waliomo kwenye Maridhiyano na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ili waweze kufaulu itabidi waendelee na kazi ya Nchi ya Zanzibar kujitambua na kutambulika kitaifa. Kwa hiyo hii kazi ya kuleta Mabadiliko ya Katiba lazima tuifanye kwa HARAKA tena SANA. Tukipoteza wakati kujadiliana mambo yasioyokuwa ya msingi basi itakuwa tumeisaliti Zanzibar kwa kujuwa au kwa kutokujuwa! Mungu atatuhukumu na historia itatulaumu vibaya vibaya.

Kwa mukhtasar, Zanzibar imetoka mbali na imefika mbali. Leo hii Zanzibar (na Tanzania kwa jumla) ina uhuru mkubwa na wa kistaarabu wa kufikiri ambao haupatikani bila ya uhuru wa kujieleza. Uhalali mpya wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar utazidi kukuwa kwa kuyajadili yote kwa uwazi kabisa kabisa ili wananchi popote walipo wajionee uhalali wa kulinda na kuhami mustaqbal wa Nchi Yetu! Lakini kamwe hatutoweza kuujenga uhalali huo iwapo tutaiwachia fursa ya kuiokoa Nchi KIKATIBA ambayo imeshaanza kupata miguu kwa kutaka kujenga hoja ya kuwa miaka 47 iliopita uongozi fulani ambao leo haupo tena ulitukata mikono au hata kututoa roho.

Tukiikosa fursa hii kwa sababu labda tunaona tutapata faida zaidi Wazanzibari tukiendelea kupigishana makelele na kukichakura kisima kikavu chenye kulirusha vumbi la jana na la juzi basi, itatubidi tusubiri watoto watakaozaliwa na watoto wetu miaka mia (100) ijayo!

Tumuombe Mwenye Enzi Mungu atupe akili zenye kutulia tusije tukakosea njia.

Naomba kuwakilisha hoja.

2 thoughts on “Wito wa Kungwi la Zanzibar na Kuzaliwa kwa Tanganyika”

  1. Kwanza ongeroni Waanzanzibari kwa kusherekea mapinduzi matukufu ya januari 12-1964.Cha kutambua hapa ni nmna gani tulinde muungano wetu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania sie sote ni wamoja hilo lajulikana saku zote japokuwaserikali imekuwa na kiburi sana,kwa sababu miafaka mingi mpaka damu za watu zimwagike ndipo ichukue hatua za makusudi,Tumashaidi juu yaliyotokea Arusha januari5-2011,PEMBA na UNGUJA mwaka 2001 mpka tulipata wakimbizi waliojificha shimoni nchini Kenya,kumbe tatizo la msingi ni katiba mbovu ya kizamani pia watu wachache.Inshalaaaaaaaaa tuombe MUNGU TUFIKE

  2. Ninakuunga mkono dr, Harith kwa mtizamo wako huu, assaa ukatuletea mafanikio makubwa huko tuelekeyapo, lakini cha kutiawasi wasi ni kule kuitikiwa na jamii hii ya leo !! wengi wetu tumechoshwa na hali hii ya kuburuzwa na neno mapinduzi juu yakuwa nchi imeingia katika vinyaganyiro vya uchaguzi bandia !! nafikiri iko haja ya kuwacha tabia hii mapema kabla hatukuanza safari yetu hii ya kushirikiana kwa kuijenga Zanzibar mpya!!

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.