Balozi Seif Idd

Na Jabir Idrissa

BALOZI Seif Ali Idi umejenga msingi imara. Unaonyesha na kuthibitisha kwamba uongozi ni kuonyesha njia. Haitoshi, ni kuonyesha njia sahihi.

Hata vitabu vya dini vinamtambua kiongozi kama mtu maalum. Mwenye upeo na weledi wa mambo; hekima na busara. Kiongozi anatakiwa kujali watu anaowaongoza. Kuwajali unaowaongoza ni kujali shida zao, matumaini yao, fikra zao. Kujali kila wakionacho ni bora kwa ustawi na maslahi yao. Wasikilizwe. Alhamdulillah! Balozi unajali ardhi. Unaijali kwa sababu unaamini ni raslimali muhimu kwa ustawi wa watu. Unaamini ardhi kutumika vizuri kwa maslahi ya kila mtu nchini.

Balozi hakika unajipambanua vizuri na viongozi wengi waliopita na hata waliopo katika baraza la mawaziri la Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Mhhh, inashangaza lakini kwa kweli unatia matumaini tunaposikia unakemea matumizi mabaya ya ardhi. Unapokemea ufisadi juu ardhi unafurahisha umma.

Kwa nafasi yako ya Makamu wa Pili wa Rais, Balozi unatumainisha wananchi wanyonge wa Unguja na Pemba ambao wanatamani kupata hatimiliki ya kipande kidogo cha ardhi walichowahi kugaiwa na serikali.

Unaposema wanyonge nao wana haki ya ardhi ujuwe unashtua na kusuuza nafsi zao. Wanajua hilo, lakini hawajapata kulisikia kwa viongozi waliopita. Kama lilitajwa, ni kwa maneno matupu.

Ni matamshi yaliyojaa hekima na busara. Ni matamshi yaliyohitajika zamani Zanzibar si zama hizi pekee. Watu wanajua umuhimu wa ardhi, ila kwa bahati mbaya, viongozi wengi wakiamini wana haki zaidi ya wengine.

Walijimilikisha mapande kwa mapande ya ardhi kwa kutumia nguvu ya madaraka na fedha. Pita kwenye miji, vitongojini na vijijini utajionea. Mpaka maeneo ya makaburi yanahodhiwa kibiashara.

Kote Unguja na Pemba utakuta mapande ya ardhi yamehodhiwa na wakubwa. Wenyewe wameyazungushia makuta ambayo thamani yake inapita thamani ya nyumba ya kuishi familia.

Pita kwenye maeneo mazuri kibiashara. Utakuta viwanja vimehifadhiwa vikisubiri kujengwa mahekalu.

Sasa unajua Mombasa Kwa Mchina wakubwa walivyokatiana viwanja mbele ya nyumba zilizojengwa kwa hisani.

Kwa wakubwa, watu wakubwa ni wao lakini hata watu wa chini ni wao. Ni wao maana walipobaki kuishi wao, waliwapa ndugu na jamaa zao. Nyingine walitunuku hawara zao.

Tazama wakubwa walivyo khiyana. Mara tu utawala wa Dk. Salmin Amour Juma – kwa umahiri wa kutawala kwa mabavu akaitwa Komandoo – akapata pigo.

Aliowahifadhi wakadhalilishwa. Wakatolewa mkuku ili kupisha wa SAS – Serikali ya Awamu ya Sita. Wakaingia huku televisheni ya serikali ikitumika kudhalilisha watokao. Ukubwa bwana, kama mzaha vile!

Yaliyotendeka kipindi kile yalikuwa kama sinema. Hakuna aliyeamini kwamba ndiyo ilikuwa moja ya dhamira za wanasiasa waliotafuta uongozi.

Hivi kweli, inaingia akilini mtu anatafuta urais au ujumbe wa baraza la wawakilishi ili akipata uwaziri ashiriki kutoa watu kwenye nyumba ili aingize ndugu zake? Na huko si kufisidi juu ya ardhi? Mzaha kweli.

Waziri mmoja aliyekuwa na Dk. Salmin na akaja kuingizwa Baraza la Mapinduzi (BLM) kwa mkakati alipata kusema, “Kutesa kwa zamu.”

Wakati huo alijua akiwaambia wawakilishi wa Chama cha Wananchi (CUF), waliokuwa wakipiga kelele kukemea maovu na maonevu dhidi ya raia masikini wasio hili wala lile.

Sijui alikusudia mateso gani na dhidi ya nani. Kwa jumla, ilionyesha naye alitaka au labda alishaanza kutesa. Sijui kama anajua ubaya wake kutesa.

Chukua njia ya Amani kwenda Mwanakwerekwe na ukipita tu mduara, nyoosha kama unaenda Kwa Mchina angalia kushoto. Kuna eneo limezungushiwa ukuta. Nimechoka kuuliza wahusika nani amehodhi hawajibu.

Pita Maruhubi, upande kilipo kilichokuwa kiwanda adhimu cha maziwa, siagi na samli. Unakaribishwa na ukuta wa gharama. Uliza mwenyewe. Wewe watakwambia.

Badala ya kujengea mabanda ya biashara ya wananchi wanaotaradadi barabarani, amehodhi mheshimiwa gani sijui kwa ajili ya biashara zake. Lakini huu ni ufisadi. Ukomeshe.

Msomaji mmoja amelia nisaidie kukwambia Mwanakwerekwe hakuna tena nafasi ya kuzika wafu. Makaburi ya miaka ya juzi tu yanafukuliwa ili wazikwe wa leo. Elekeza makaburi mapya Selem, futa ufisadi kule.

Wakubwa wakatwaa majengo ya umma yakiwemo ya kihistoria na kitamaduni. Hakuna aibu, wamechukua, wakaweka waa. Kila mtu wao kapata. Lahaula.

Sheria za ujenzi zinalazimisha panapoendelea ujenzi pawekwe tangazo linaloonyesha nini kinajengwa; nani anagharamia; kwa kibali gani; nani fundi wake. Haya muhimu sana.

Nilishangaa hata jengo wanalotumia Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) mkabala na Soko la Mwanakwerekwe mpaka limemalizika kujengwa hakukuwekwa tangazo lolote kuonyesha hayo. Kuvunja sheria.

Jengo lililokuwa la Shirika la Zanzibar Wharfage, baadaye Shirika la Taifa la Biashara (ZSTC) Forodhamchanga mpaka limemalizika matengenezo makubwa hakukuwa na tangazo la aina hiyo. Kuvunja sheria.

Sasa kuna uzio wa mabati pembeni mwa Hoteli ya Tembo, Forodhani. Umekwenda mpaka jengo la kihistoria na kiutamaduni la Mambo Msiige. Bado hakuna tangazo la kueleza umma nini kinajengwa. Ufisadi na uvunjaji sheria.

Wakati mwingine inawezekana hakuna uchafu. Uzuri wananchi waelezwe mapema. Watajuaje wakati hakuna uwazi wala ukweli haujawekwa hadharani? Ni kinyume na utawala bora.

Hivi kweli inaingia akilini serikali kuruhusu uzio eneo lile bila ya kuwepo tangazo la kuonyesha kinachojengwa? Sijui kama viongozi wanajua adha wanayoipata watu wanaoishi jirani?

Wamenituma niulize kwani panajengwa nini Mambo Msiige hadi Tembo Hotel? Una nafasi ya kuwajibu maana u mkubwa.

Utawala bora unahimiza uwazi na utolewaji wa taarifa kwa wakati. Nahofia siku zikizidi wananchi wanaokosa pa kupumzisha watoto wao, watakasirika. Kitakachofuata? Sikijui.

Balozi Idi haya ni maeneo yanayohitaji macho makali. Muhali haufai, umeumiza sana jamii. Kila hatua yapasa iendane na utaratibu wa sheria na utengamano.

Jamii ya wanadamu hwenda kimpangilio, tofauti na ya wanyama. Wao, hawana sheria porini isipokuwa “mwenye nguvu mpishe.” Kule mkubwa humla mdogo, basi!

Binadamu tumehulukiwa taratibu na tuna stara. Tujitofautishe basi nao. Tuheshimu na kufuata sheria. Tuheshimu watu hata wale dhalili. Na tuheshimu serikali. Bali nanyi viongozi heshimuni watu, mtaheshimiwa.

jitambueni. Wala msidhani kwa madaraka labda na fedha, ndio mmemaliza kila kitu. Hapana. Nyote, kama siye, udongo mtupu.

Balozi Idi najua unania. Waziri anohusika na ardhi, Ali Juma Shamhuna, naye labda anayo. Huyu ni mzoefu, anajua kilichoharibu ardhi alipokuwa waziri tangu awamu ya tano. Mtumie.

Mfalme wa Donge’ anajua ardhi ya Fumba imekaaje. Nani anahodhi palipotengwa kwa Mji wa Kisasa wa Uwekezaji – Star City. Alishiriki kupanga. Anajua kilichokwamisha.

Nina hakika moto ulioanzisha Balozi hauzimiki. Wananchi wanakutegemea sana na wapo tayari kukusaidia. Wanayajua. Wengine waliporwa ardhi na nyumba kifisadi. Wengine zao zilivunjwa kishenzi.

Ongeza mwendo. Ufisadi huo ulishaipeleka Zanzibar kuzimu. Itoe irudi mstarini. Hakuna aliyejali. Mipango inataka kiongozi. Thibitisha unaweza.

Chanzo: MwanaHALISI la 12 Januari 2011

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.