Tanzanian President Julius Nyerere is pictured on January 16th when he addressed an open air rally where the detained former Tanzania Minister and Vice-President of Zanzibar was brought to face the people. Mr. Kassim Hanga (seated between two police officers) is under detention with a number of other top Tanzanians after allegedly boasting that he had been called from voluntary exile in Guinea to lead an army coup on Zanzibar. Image and caption by Bettmann/CORBISDATE, 1968

Na Ahmed Rajab

KUNA masuala kadhaa ambayo hayeshi kunihangaisha. Moja ni kwa nini na vipi utamaduni wa uvumilivu unavyoparaganyika hasa katika jamii zenye utulivu. Sishi kujiuliza kwa nini watu wenye utamaduni wa kustahmiliana ghafla hugeuka na kuwa kama wehu na kuanza kuparurana. Inakuakuaje kwamba watu wenye kuishi kwa amani kwa dahari mara hugeukiana wasiweze tena kuishi katika hali ya kuvumiliana? Tuseme wanachezewa na Ibilisi au hulka za wanadamu hubadilika katika mazingira fulani?

Au labda huo tunaoudhania kuwa ni uvumilivu ni povu tu, si madhubuti. Haushikiki, haukamatiki. Kwa ufupi, mara nyingi, kwa hakika, huo tunaoufikiria kuwa ni uvumilivu huwa ni chuki zinazofukuta, zinazosubiri tu wakati wake wa kuibuka na kupamba moto.

Tumeyashuhudia hayo nchini Rwanda pale Wahutu walipowachinja Watutsi katika mwaka 1994. Mara baada ya mara tunayasikia yakitokea ama Nigeria, Sudan au Kenya. Tuliyashuhudia hayo kwa kiwango fulani wakati wa, na baada ya, Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964, ambayo leo yanasherehekewa Tanzania nzima.

Aghalabu chanzo chayo huwa ni tofauti ama za kikabila au za kidini, tofauti ambazo katika mazingira fulani huwafanya watu waanze kuchukiana, kubaguana na hata kuchinjana.

Ni kweli kwamba visiwani Zanzibar watu wa makabila tofauti wamekuwa wakiishi pamoja kwa amani kwa karne chungu nzima. Lakini vile vile ni kweli kwamba ubaguzi wa kikabila ulikuwapo. Tukisema vingine tutakuwa wanafiki.

Lazima tuwe wajasiri kuikabili historia na tukubali kwamba ubaguzi ulikuwapo hapo zamani na ungalipo hadi leo miaka 47 baada ya Mapinduzi. Ubaguzi wa leo lakini haukushtadi kama ule wa kale.

Na ule wa kale hatuwezi kuulinganisha na jinsi Wazungu walivyokuwa wakiwabagua Waafrika huko Afrika ya Kusini au hata Kenya kabla ya Waafrika kuanza kujitawala katika nchi hizo mbili.

Visiwani Zanzibar ubaguzi wa kikabila ulijidhihirisha zaidi pale watu wa makabila tofauti walipotaka kuchanganya damu. Kwa mfano, pale Mzanzibari mwenye nasaba ya Kiafrika alipotaka kumuoa Mzanzibari mwenzake mwenye asili ya Kiarabu au ya Kihindi. Sisemi kuwa ndoa kama hizo zilikuwa hazifungwi, lakini zilikuwa za nadra.

Ubaguzi aina hiyo upo katika kila jamii. Makabila mbalimbali katika nchi mbalimbali za Kiafrika yanabaguana katika mambo ya ndoa. Katika nchi za Ulaya ubaguzi kama huo uko zaidi juu ya msingi wa kitabaka.

Wazee wa wenye kujiweza huko Ulaya kwa kawaida huwa hawapendelei mabinti zao waolewe na wafanyakazi. Na ikiwa hao wafanya kazi ni watu weusi, mama wee mambo ndo huzidi. Lakini kusema kuwa ubaguzi aina hiyo upo katika kila jamii si kuukubali au kuudekeza. Ukabila ni maradhi.

Kwenye kitabu chake kiitwacho Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru Dk. Harith Ghassany ameeleza aliyotwambia Abdallah Kassim Hanga, aliyekuwa makamu wa rais wa Zanzibar na baadaye waziri katika serikali ya Tanzania aliponiita mimi na mwenzangu Salim Hamdan kwenda kuonana naye. Hayo yalitokea Hanga alipokuwa London baada ya kutolewa kwenye Baraza la Mawaziri na Mwalimu Julius Nyerere.

Hanga aliwahi kunisomesha Kiingereza katika shule ya msingi ya Darajani, Unguja. Hiyo ilikuwa ni safari yake ya mwisho kuja London. Baada ya kukutana naye alirudi Tanzania akipitia Guinea na Misri. Alipowasili Dar es Salaam alikamatwa kwa amri ya Nyerere, akapelekwa Zanzibar alikokuwa akitakiwa na Sheikh Abeid Amani Karume. Huko aliuawa kikatili.

Tulikutana na Hanga nyumbani kwa Oscar Kambona, aliyekuwa waziri wa mwanzo wa mambo ya nje wa Tanganyika na baadaye waziri wa ulinzi wa Tanzania. Ninayabania mengi kuhusu Hanga na mazungumzo yetu ya siku hiyo kwa vile ninayaandika kwenye kitabu. Kwa sasa nitadokeza tu kwamba Hanga alitupa wasia adhimu, nao ni kuupinga ukabila.

Hanga alitueleza kwamba yeye aliwahi kuwa na chuki za kikabila lakini baadaye aliuona ubaya wake. Alipopelekwa Bara kuwa waziri, alifanya mpango wa kuwapatia ajira Dar es Salaam waalimu waliokuwa wamefukuzwa kazi Zanzibar wakibaki wakizurura.

Wote walikuwa na asili ya Kiarabu. Miongoni mwa aliowataja walikuwa Maalim Shaaban Saleh Farsy, Maalim Salim Sanura na Maalim Amour Ali Ameir —mabingwa katika taaluma ya elimu.

Hanga akatueleza kwa masikitiko kwamba wapinduzi wenzake wa Afro-Shirazi Party (ASP) huko Zanzibar wakaanza kumsema kwamba akipendelea Waarabu. ‘Lakini mimi nilipowaleta Dar sikuwaona kama ni Waarabu, niliwaona kama Wazanzibari,’ Hanga alitueleza.

Msimamo kama huo wa Hanga uliafikiana sana na itikadi zangu. Sababu moja kubwa iliyonivutia mimi binafsi na vijana wenzangu wengine Zanzibar tukiunge mkono chama cha Umma Party ni msimamo wake dhidi ya ukabila. Chama hicho kiliundwa kwa msingi huo.
Ingawa chama hicho hakikuwa na umri mrefu kiliweza, hata hivyo, kuwapika wafuasi wake na kuwafanya wawe na sifa ya kutokuwa na woga hasa katika itikadi ya kuwatetea watu wa matabaka ya chini katika jamii.

Baadhi yetu tulitoka katika koo zilizojiweza, wenzetu wengine walikuwa wa hali duni. Muhimu ni kwamba tulizizika tofauti zetu za kitabaka na za kikabila na badala yake tukawa na utambulisho wa Kizanzibari.

Ni mwiko kumuona mfuasi wa Umma Party akiuweka mbele ukabila au hata kujadili mambo kwa mtizamo wa kikabila. Sote twajinata kuwa na kabila moja, la Uzanzibari. Ni taabu kuuelezea udugu wetu japokuwa tumetokana na matumbo tofauti.

Chama cha Umma Party kilinuia pia kuziondosha tofauti za kitabaka ambazo zilichangia kuupalilia ukabila.

Ni misimamo hiyo iliyowafanya wafuasi wa chama hicho wenye asili ya makabila yote yaliopo Visiwani humo wayaunge mkono Mapinduzi ya mwaka 1964, mapinduzi ambayo yaliasisiwa na wafuasi wa ASP.

Si dhamiri yangu hapa kuzungumzia jinsi ma-Comrade, kama waitwavyo wafuasi wa Umma, walivyoshiriki katika mapinduzi na mchango wao, hasa katika miezi minne ya mwanzo ya Mapinduzi.

Labda niutaje ukweli mmoja tu: kwamba kama si wao basi idadi ya watu waliouawa kwa chuki za kikabila kwenye mapinduzi hayo ingekuwa kubwa sana.

Sina pia dhamiri ya kujadili iwapo hayo yaliyojiri Zanzibar Januari 12, 1964 yalikuwa ‘mapinduzi’ au ‘machafuzi’ kama wanavyodai baadhi ya wenye kuyapinga mapinduzi hayo. Tukumbuke tu kwamba njia ya mapinduzi imetumiwa na wengi katika historia kuleta mabadiliko katika jamii. Kuna yaliyoleta kheri, na kuna yaliyozusha shari.

Mmoja wa hao waliofanya mapinduzi ni Sultan Qaboos bin Said wa Oman ambaye Julai 1970, kwa msaada wa Waingereza, alimpindua baba yake Sultan Said bin Taimour.

Tofauti ya mapinduzi hayo mawili ni kwamba kwa jumla kinyume na ya Zanzibar, yale ya Oman yamewapatia neema wananchi wa huko, licha ya kuwa tawala hiyo ya kifalme haiendeshwi kidemokrasia. Na wala mapinduzi ya Oman hayakusababisha kuuawa watu kama walivyouawa Zanzibar.

Bila ya shaka, kuna madhambi mengi, yakiwa pamoja na ya jinai, yaliyofanywa Zanzibar wakati wa Mapinduzi. Matokeo yake ni kuzorota kwa maendeleo ya visiwa hivyo na kuoza kwa mengi katika kipindi kinachokaribia nusu karne.

Hivyo, serikali ya Umoja wa Kitaifa chini ya Rais, Dk. Ali Mohammed Shein inakabiliwa na changamoto kubwa. Kwanza, ya kusaidia kuziondosha hizi chuki zisizokwisha. Pili, ya kuzifufua na kuzinyoosha sekta nyingi za Zanzibar.
Sina budi ila nikiri kwamba ma-Comrade si malaika na kwamba kuna wenzetu wachache (wanahesabika kwa vidole vya mkono mmoja tu) ambao pia walifanya madhambi wakati wa hekaheka za Mapinduzi. Sitokuwa mkweli nikiyakana hayo.

Aidha, hamna shaka kwamba makosa yao yamewapaka matope wafuasi wote wa chama hicho na kutuharibia jina letu. Kati ya madhambi hayo ni kusaidia kuwakamata na kuwaweka watu kizuizini.

Kuna waliokuwa wakifanya ujeuri, kinyume kabisa na mafundisho ya Umma Party kuhusu namna ya kuingiliana na watu. Kuna mmoja aliyewapiga watu bakora hadharani huko Pemba. Wawili wanashtumiwa kuua. Vitendo vyao havikuwa sera ya Umma Party, wala hawakuvitenda kwa kuagizwa na viongozi wa chama chao.

Kulingana na sifa yao hao ma-Comrade waliokosa wamejuta na walikuwa na ujasiri wa kutaka radhi.

La kusikitisha ni kuwa kuna miongoni mwa waliokoswa, waliokuwa wafuasi wa chama cha Zanzibar Nationalist Party (Hizbu) na chama cha Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP), wanaoendeleza chuki wakikataa kusamehe.

Chanzo: RAIA MWEMA. 12 Januari 2011

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.