Sisi ambao tuko hai tunapita katika kipindi cha kusisimua sana. Pepo burudani za matumaini zinavuma katika pembe zote za visiwa vyetu. Karibu katika kila sehemu ya Zanzibar mijadala ya kuvutia inaendeshwa kuhusu hatima za kisiasa za baadae. Ni siri iliyowazi kuwa wananchi bila ya kuogopa au kujificha wanajadili hatima ya nchi juu ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kila mtu tayari ameshatoa uamuzi wake juu muungano huo ambao sasa umeshatimiza miaka 46 tokea kuundwa. Matokeo ama mambo mbali mbali yaliyojitokeza au kufanyika huko Zanzibar katika siku za hivi karibuni yamezidi kuchangia mijadala na maamuzi yanayotolewa kutoka katika sehemu mbili za Muungano.

Hapa itafaa tujiulize na tuwe waadilifu kuwa jee tatizo ni nini?

Kuna dhana mbili ambazo zinazungumzwa, moja ni ile isemayo kuwa tatizo ni muundo wa muungano na nyingine ni ile inayodhaniwa kuwa hayo matokeo yaliyotokea Zanzibar ndiyo yamezidi kuchangia kuleta mashaka ya Muungano.

Ni lazima tukubali kuwa tangu kuasisiwa kwa Muungano mwaka 1964 matatizo kadhaa yamejitokeza. Juhudi zimekuwa zikichukuliwa kutatua matatizo hayo, lakini kilichojitokeza ni kuwa baadhi ya hatua hizo zimeongeza zaidi matatizo baada ya kuyatatua.

Tume na Kamati nyingi zimeundwa ili kuainisha matatizo ya muungano na kupendekeza njia za kuyatatua. Mikutano ya ushirikiano nayo imefanyika katika nyakati tofauti, lakini yote hayo yameshindwa kutoa ufumbuzi wa kudumu.

Kwa hali hiyo, inaonyesha kuwa kiini cha matatizo ya Muungano ni kuwepo kwa mfumo wa sasa wa serikali mbili ambao haukuweka bayana mipaka, haki na majukumu ya pande zote mbili za Muungano. Mfumo uliopo hauna uwazi hata kidogo kwani haufafanui uendeshaji wa Muungano kisiasa, kisera, kisheria na kibajeti.

Kwa upande mwingine, mwelekeo wa Muungano haufahamiki.Mpaka sasa haieleweki kama washirika wakuu wa Muungano (Zanzibar na Tanganyika) wapo au hawapo, na kama wapo uwezo wao na mchango wao ndani ya muungano haujabainishwa mahala po pote. Kama hawapo nani ana uwezo wa kuamua lipi la muungano?

Tatizo kubwa liliopo hapa ni kuwa hakuna chombo cha kuratibu na kujadili kwa uwazi juu ya masuala ya muungano.

Kutokana na mfumo wa serikali mbili ambao hauna ufafanuzi wala uwazi, matatizo kadhaa ya kikatiba na kisheria yamekuwa yakijitokeza;miongoni mwa matatizo hayo ni kuwepo kwa masuala mengi juu Muungano kama vile:

a. Je, nani washirika wa muungano wapo au hawapo na wanawakilisha mawazo ya pande hizo mbili katika kikao gani? Je, wanatoa maamuzi katika kikao gani?

b. Baada ya Rais wa Zanzibar kutolewa katika wadhifa wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, sasa ana hadhi gani katika Muungano? Na Zanzibar, kama mshiriki katika Muungano, inawakilishwa namna gani katika Muungano huo?

c. Kutokana na kuwepo kwa mambo ya Zanzibar ambayo si ya Muungano na ambayo hata Bunge halina uwezo wa kuyatungia sheria, ni vipi Serikali ya Muungano inapata uwezo wa kuyashughulikia mambo hayo katika ngazi zote za kimataifa?

d. Je, baina ya katiba mbili, yaani ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar, ni ipi iliyo juu na katika mambo yapi, eneo lipi na mipaka ipi?

e. Je, kwa namna gani uchaguzi wa Rais wa Muungano unazingatia muelekeo wa kimuungano, ikiwa wananchi wa Zanzibar, kutokana idadi yao hata wakimkataa mgombea fulani wa nafasi ya uraisi huo, mgombea huyo bado anaweza kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano kwa kura za Watanganyika tu?

f. Kwa nini hakuna utaratibu wa kudumu wa kupokezana nafasi ya Urais kutoka pande hizi mbili za Muungano?

Hoja zote hizo za kikatiba na kisheria ni miongoni mwa matatizo ya msingi ya muungano. Kwa sasa hayazungumzwi ama yanazungumzwa na kuamuliwa kisiasa tu badala ya kuandaliwa utaratibu mzuri wa kisheria.

Kwa maana hiyo, ipo haja kubwa ya kuyaandalia utaratibu mwafaka ili yasimamiwe vyema. Ni dhahiri kuwa matokeo yaliyotokea au kufanyika Zanzibar hayana uhusiano na hali waliyonayo wananchi kuhusu Muungano.

Vipi Tutoke Hapa Tulipo?

Sasa ni miaka 46 tangu uundwe Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kulikuwa na wakati wa kutosha kurekebisha kasoro zilizopo. Hilo halikuwezekana kutokana na ubabe wa Mwalimu Nyerere ambaye aliamua kuwafunga shemere Wazanzibari na kuhakikisha Muungano unakwenda kama alivyotaka yeye hata baada ya ‘kuondoka madarakani’.

Si jambo la kuficha kwamba wananchi wa pande zote mbili za Muungano wamechoshwa na unafiki uliopo na wanadai Katiba ya kweli kweli itakayoweka misingi mipya ya ushirikiano.

Kama inavyoelezwa kuwa, kiini cha matatizo ya Muungano ni kutokuheshimiwa kwa Mkataba wa Muungano (Articles of Union) ambao kisheria ni Mkataba wa Kimataifa unaopaswa kuheshimiwa kwa kuzingatia masharti yote yanayohusu mikataba ya kimataifa.

Haidhuru sasa ni miaka 46 tokea kuanza kwa hatua za kuukanyaga kanyaga Mkataba wa Muungano mara tu baada ya kutiwa saini na Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, na Rais wa Jamhuri ya Tanganyika, Marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, lakini ukweli utabaki kuwa huo ulikuwa ndiyo msingi pekee, nasisitiza tena, pekee, uliokubaliwa na viongozi hao wawili kuongoza mahusiano ya nchi zetu mbili kupitia Muungano.

Wakati sasa umefika tukubali kwamba suluhisho la matatizo haya siyo kuendelea kuunda Tume au Kamati au kuandaa warsha, semina, makongamano na mikutano. Suluhisho ni kutekeleza kwa dhati Mkataba wa Muungano (Articles of Union) ambao ni mkataba wa kimataifa wa nchi mbili huru.

Kujaribu kulazimisha kutumia Katiba inayoitwa ya Jamhuri ya Muungano kama ilivyo sasa ambayo inakosa uhalali wa kisheria kuzima madai ya wananchi wa Zanzibar hakuwezi kukubalika tena katika zama za sasa.

Kwa msingi huo, hakuna njia ya mkato ya kuyashughulikia matatizo ya Muungano bila ya kwenda kwenye kiini cha matatizo hayo ambacho ni kutokuheshimiwa kwa Mkataba wa Muungano. Wahenga wamesema, “Mwiba uchomeapo ndipo utokeapo”. Ili kuyaheshimu Makubaliano ya Muungano, yafuatayo ni lazima yafanyike:

Kwa kuwa Baraza la Kutunga Sheria la Zanzibar la mwaka 1964 ambalo lilikuwa ni Baraza la Mapinduzi halikupewa nafasi ya kuuridhia (ratify) Mkataba wa Muungano, hivyo basi kwanza kabisa, na kabla ya kuchukua hatua nyengine yoyote, ni lazima Baraza la Kutunga Sheria la Zanzibar kwa sasa ambalo ni Baraza la Wawakilishi lipewe nafasi ya kuuridhia Mkataba huo ili kuupa uhalali wa kisheria kwa upande wa Zanzibar na hivyo kuupa uhalali wa kisheria Muungano wenyewe kama yalivyo masharti ya kifungu cha (viii) cha Mkataba huo wa Muungano.

Kwa ujumla tuupitie tena Mkataba wa Muungano na kurekebisha vifungu vyenye utatanishi. Kama Muungano huu haukuwa na mtego, ulikuja kwa ridhaa za Serikali zetu mbili, vipi tunashindwa kukaa tena tukaupitia baada ya miaka 46 na kuuweka kwenye hali ya kuvutia hata majirani zetu wakajiunga?

Katiba ya Zanzibar itumike Zanzibar kwa mambo yote yasiyo mambo ya Muungano kama yalivyo masharti ya kifungu cha (v) cha Mkataba wa Muungano.

Katiba ya Tanganyika (ile iliyokuwepo kabla ya kurekebishwa kuingiza mambo ya Muungano) nayo irejee kutumika Tanganyika kwa mambo yote yasiyo mambo ya Muungano kama yalivyo masharti ya kifungu cha (v) cha Mkataba wa Muungano.

Kwa kutumia Katiba ya Tanganyika, iundwe Serikali ya Tanganyika inayoshughulika na mambo yasiyo ya Muungano, kama Serikali ya Zanzibar inavyoshughulika na mambo yake ambayo si ya Muungano.

Serikali ya Muungano ishughulike na yale mambo 11 tu ya asili yaliyokubaliwa kuwa ndiyo mambo ya Muungano kwa mujibu wa kifungu cha (iv) cha Mkataba wa Muungano.

Mambo mengine yote 12 yaliyoongezwa katika orodha ya mambo ya Muungano kinyume na Mkataba wa Muungano yaondolewe katika orodha hiyo na yarudi katika mamlaka za Zanzibar na Tanganyika.

Wafanyakazi wa Tanganyika wasihusike na mambo ya Muungano, wawe katika “civil service” (mfumo wa wafanyakazi Serikalini) wa Tanganyika, kama walivyo wa Zanzibar kwa Zanzibar (wasio wa taasisi za Muungano).

Urejee utaratibu wa kuwepo kwa Makamu wawili wa Rais wa Muungano kama yalivyo masharti ya kifungu cha (iii) (b) cha Mkataba wa Muungano ambapo Rais wa Zanzibar na Rais wa Tanganyika wawe Makamu wa Rais wa Muungano kwa mujibu wa nyadhifa zao.

Iundwe Tume ya kutayarisha rasimu ya Katiba ya Kudumu ya Muungano ambayo itakuwa na idadi sawa ya wajumbe kutoka Zanzibar na Tanganyika kama yalivyo matakwa ya kifungu cha (vii) (a) cha Mkataba wa Muungano.

Liundwe Bunge la Katiba (Constituent Assembly) litakalokuwa na idadi sawa ya wajumbe kutoka Zanzibar na Tanganyika ambalo litakuwa na majukumu ya kupokea rasimu iliyotayarishwa na Tume ya Katiba na baada ya hapo kupitisha rasmi Katiba ya Kudumu ya Muungano kama yalivyo matakwa ya kifungu cha (vii) (b) cha Mkataba wa Muungano.

Itaonekana kwamba msingi wa hatua zote zilizoorodheshwa hapa ni kuheshimu mapatano ya nchi zetu mbili yaliyomo katika Mkataba wa Muungano. Haya yalibidi yafanyike ndani ya mwaka mmoja tokea kusainiwa kwa Makubaliano ya Muungano. Hata hivyo, Waingereza wanasema, “Better late than never” (Bora kuchelewa kuliko kutofanya kabisa). Wakati ndio huu ikiwa tunataka Muungano wa kweli, Muungano wa haki kwa pande zote mbili.

Makala ya Rashid Ali Saleh

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.