UBAYA wa utumishi wa umma usiozingatia maslahi ya umma umejithibitisha. Nani waliomshauri Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein kufanya uteuzi wa majaji watano, akiwemo Haroub Shehe Pandu ambaye anakuwa Mwenyekiti wa Mahakama ya Ardhi?

Pamoja na Pandu ambaye anafahamika uwezo wake mkubwa kutokana na rekodi nzuri mahakamani, Rais amewateua Abdul-hakim Ameir Issa, Fatma Hamid Mahmoud, Mkusa Isaac Sepetu na Rabia Hussein Mohamed.

Wanasheria wa Zanzibar kupitia chama chao – Zanzibar Law Society (ZLS) – wamemwandikia Dk. Shein angalizo wakimjulisha wasivyoridhika na uteuzi wa baadhi ya majaji wakisema umekiuka utaratibu zikiwemo zile za kikatiba.

Kwanza, tufahamu kuwa majaji ni watendaji muhimu katika maendeleo ya nchi na ustawi wa jamii. Uteuzi wao unahitaji kutekelezwa kwa kuzingatia ukweli huo.

Majaji hutumikia Mahakama Kuu. Hii ndiyo mahakama yenye mamlaka makubwa zaidi ya kisheria nchini petu. Kinachoamuliwa na mahakama hii, kiameamuliwa.

Na kwa mabadiliko ya 10 yaliyofanywa katika Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kinachoamuliwa Mahakama Kuu hakipingwi popote kikiwa kinahusiana na masuala yaliyoanzia Mahakama ya Kadhi pamoja na masuala ya haki za binadamu.

Mahakama Kuu inaamua mtu kunyongwa. Na hii ndiyo adhabu kubwa kabisa katika adhabu zinazotolewa na mahakama. Kifo.

Unapoteua jaji inatakiwa mteuzi atambue umuhimu wa maamuzi yatakayofanywa na huyo anayekusudia kumteua.

Sasa Mshauri mkuu katika uteuzi wa majaji na watendaji wengine wa Mahakama, ni Jaji Mkuu. Jaji Mkuu wa Zanzibar ni Hamid Mahmoud Hamid.

Kulingana na kifungu cha 94(2) cha Katiba ya Zanzibar, rais huteua majaji kutokana na ushauri wa Tume ya Utumishi ya Mahakama iliyoanzishwa kwa Sheria Na. 13 ya mwaka 2003, tume ambayo mwenyekiti wake ni Jaji Mkuu wa Zanzibar.

Ndio kusema, Jaji Hamid ndiye kiongozi wa tume hiyo yenye wajibu wa kujadili wale wanaofikiriwa kuteuliwa ujaji, nafasi zinazofanana nazo kama vile mrajis wa mahakama, naibu wake pamoja na mahakimu wa mahakama za mkoa na wilaya.

Hatima yake, ni ushauri kwa rais anayeteua. Mmoja wa wajumbe katika tume hii kikatiba sharti atoke kwa miongoni mwa jumuiya ya wanasheria wa Zanzibar.

Jaji Hamid ana tatizo kubwa. Alipoipata nafasi ya kuongoza Mahakama, na kuzoea, aliamua kujiotesha uongozini. Alivyo sasa, asingependa aingie mtaalamu mwingine na akiingia, basi asiwe katika wale asiowapenda.

Ni kwa bahati mbaya, amesahau yeye ni mtaalamu wa kada muhimu na ambayo inaheshimika na kutegemewa sana katika jukumu la utoaji wa haki kwa watu na taasisi popote duniani.

Ni wasaa kumkumbusha kuwa madudu yote yanayofanywa na mihimili mingine ya dola – Serikali na Bunge – huishia mahakamani kwa ajili ya marekebisho.

Wanasheria wazoefu Zanzibar wanamtaja Jaji Hamid kama mtu aliyekomaa kitini lakini maendeleo ya idara ya mahakama yamedumaa kwa miaka.

Chini ya uongozi wake mahakimu na wanasheria wazuri waliacha kazi baada ya kuchoka mazingira magumu ya kazi. Wengi wao sasa ndio wanaoongoza katika kazi ya uwakili wa kujitegemea katika mahakama kuu na za chini ya hapo. Walikuja majaji kutoka Nigeria, wakafanya kazi nzuri, ikiwemo ya kupendekeza sheria za kurekebishwa, ili ziendane na wakati.

Aliyekuwa mkuu wa Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar, Ahmed Miskry alilazimika kuacha kazi kwa kupishana imani na Jaji Mkuu. Hakupatiwa vitendea kazi. Akahama nchi bila ya kupenda.

Leo, Miskry, amekuwa na maisha ya furaha nchini Oman kiasi cha yale maumivu ya kichwa yaliyokuwa yakimsumbua alipokuwa kwao, labda kwa mawazo mabaya ya kazini, kutoweka.

Kwa muda mrefu, mahakama imekuwa ikilalamikiwa kwa utendaji mbovu lakini hakujaonekana mabadiliko. Ni tofauti kabisa na maendeleo yanayoonekana katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka wa Zanzibar inayoongozwa na Othman Masoud Othman, mwanasheria aliyemkuta Hamid kazini.

Ofisi ya DPP ilianza mwaka 2002 baada ya muafaka wa pili. Sasa inatajika kila mahali ikiwemo kwa wafadhili.

Moja ya mafanikio yake makubwa, ni kule kujenga wanasheria vijana wanaosifika katika kushughulikia kesi za jinai kwa ustadi, baada ya kazi hiyo kufanywa kimazoea na Jeshi la Polisi.

Wanatimiza wajibu lakini imekuwa ni kilio chao kikubwa kutaka maendeleo yaonekane pia katika ofisi muhimu wanazoshirikiana nazo kikazi. Moja ya ofisi wanazomaanisha, ni Idara ya Mahakama.

Laiti kama Mahakama iliwezeshwa ikiwemo majengo yake kutengenezwa ikianzia na makao makuu Vuga, na watendaji wake kusaidiwa, nisingelazimika kueleza haya leo.

Kwanza mahakama ingekuwa na majaji wengi na ambao si tu wana sifa, bali pia wana uwezo wa kiutendaji unaozingatia vigezo muhimu.

Unakuta ofisi ya kiongozi inavuja, utashangaa nini? Wenyewe wanasema mazingira ya kazi hayavutii. Lilivyo jengo la Vuga leo, ndivyo lilivyokuwa miaka 20 iliyopita.

Utawala bora ni moja ya nyenzo muhimu. Unaposimamia kikao kinachojadili mwanao, unahalifu utawala bora. Washiriki wengine watajisikiaje huru? Na uhuru ni jambo muhimu, na pia, uungwana ni vitendo.

Mawakili kupitia chama chao wanapolalamika kuhusu uteuzi wa majaji watatu akiwemo Fatma Hamid Mahmoud Hamid, wamekosea wapi?

Wanamwambia rais, “…lakini tunaamini washauri wako hawakukutendea haki walipokushauri uwateue Mhe. Fatma, Mhe. Mkusa na Mhe. Rabia kuwa ni Majaji wa Mahkama Kuu.

Uchungu walionao si kwa sababu yumo Fatma. Siamini kama mawakili wanamchukia Fatma, kama ambavyo siamini wanawachukia Sepetu na Rabia.

Wanasema hivi: Haitoshi tu kusema jaji mteule ametimiza masharti ya Katiba na hivyo kufaa kuwa jaji wa mahakama kuu. Vipo vigezo vingine vinavyopaswa kuangaliwa kabla ya uteuzi wa jaji kufanywa.

“Nafasi ya ujaji ni nafasi ya juu kabisa katika ngazi ya mahakama zetu na pia nia nyeti. Utaalamu uliobobea, rekodi iliyothibitika, umakini wa hali ya juu, kujiamini, uadilifu na umahiri wa hali ya juu – vyote kwa pamoja vinahitajika.”

Uzuri ni kwamba wateule wanaohojiwa na chama cha wanasheria, wanajulikana kwani wanafanya kazi nao.

Wanasheria wanamwambia rais, “Siri ya maiti aijuwae muosha; na sisi mawakili ndio waosha wa waheshimiwa majaji na mahakimu wetu. Mhe. Rais, bila ya kuzunguka, tunataka tukuthibitishie kwamba (hao watatu) hawana sifa kiutendaji na kiuwezo za kuwa majaji wa Mahkama Kuu ya Zanzibar.”

Sitaki kuamini rais wetu anataka migogoro mapema hivi tangu akae Ikulu. Nimjuavyo Dk. Shein ni mtatuzi na muelekezaji. Bali haki ni yake. Anaweza kusikiliza ushauri wa wanasheria akachukua hatua au kupuuza na kuendelea kuwaapisha wakaanza kazi.

Kinachosemwa na wanasheria ni utaratibu. Rais hatakuwa na haki ya kutafuta mchawi maana kwa maoni yao, alikubali mwenyewe kulikoroga.

Ngoma inabaki: utumishi uliotukuka ndio unaosaidia uchumi kukua na ustawi wa jamii kuimarika. Yaliyobaki ni matatizo tu.

Chanzo: Makala ya Jabir Idrissa katika MwanaHalisi la 08 Disemba 2010

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.