Niseme kwamba nimetiwa moyo sana na kufufuka upya kwa madai ya Katiba Mpya upande wa pili wa Muungano, Tanganyika. Miaka mitatu nyuma, nilikuwepo Tanganyika kwa ajili ya masomo na nikawa sehemu ya harakati zilizoanzishwa na ushirikiano usio rasmi wa vyama vya siasa kudai katiba mpya.

Yalifanyika mengi kwa kipindi kifupi, kwa maana ya hatua za awali. Kamati ziliundwa, makongamano yaliitishwa na dhamira iliwekwa wazi. Kwa hakika, hata rasimu ya Katiba Mpya iliandikwa.

Nilishiriki kama Mzanzibari, maslahi yangu yakiwa ni kuona namna ambavyo Katiba Mpya itabadilisha muundo wa Muungano na kuwa ule ambao Wazanzibari wengi tunautaka – wa Serikali Tatu.

Lakini, kisha mambo yakazongana: umoja dhaifu wa vyama vya upinzani, ambao ulikuwa injini nyuma ya harakati zile ukazidi kudhoofika, wengine wakauuita Loosers Alliance badala ya Loose Alliance. Vile vile suala la mazungumzo ya kutafuta Muafaka mwengine wa Zanzibar likawa limechukua nafasi kubwa zaidi kuliko madai ya Katiba Mpya. Almuradi mambo yakaenda mkorogovyogo. Mimi, kama walivyo wengine wengi kwenye harakati zile, tukajikuta hatuna tena dhima wala dhamana.

Lakini sasa inavyoonekana, kumbe ile hadithi haikuwa imeishia hapo. Ilipaswa kuendelea baada ya kusita kwa muda wa miaka mitatu mizima, ila safari hii inaendelea ikiwa imechochewa na hali tafauti. Hapa nitazitaja mbili: kushindwa kwa CHADEMA kwenye uchaguzi uliopita na Mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar. Je, yote mawili yatosha kuwa hoja za kudai Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? Je, mabadiliko hayo yangelitakiwa yakidhi vipengele gani na gani?

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.