Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein

“Mhe. Rais, sisi mawakili ambao tumetia saini barua hii tukiwa ni wadau wakubwa katika sekta hii, tuna imani kubwa nawe Mheshimiwa Rais, lakini tunaamini washauri wako hawakukutendea haki walipokushauri uwateue Mhe. Fatma, Mhe. Mkusa na Mhe. Rabia kuwa ni Majaji wa Mahkama Kuu. Mhe. Rais, haitoshi tu kusema kwamba Jaji Mteule ametimiza masharti ya Katiba na hivyo anafaa kuwa Jaji wa Mahkama Kuu. Mhe. vipo vigezo vyengine ambavyo ni lazima viangaliwe kabla ya uteuzi wa Jaji wa Mahkama Kuu kufanyika. Nafasi ya Ujaji ni nafasi ya juu kabisa katika ngazi ya Mahkama zetu na pia ni nyeti. Utaalam uliobobea, rekodi iliyothibitika, umakini wa hali ya juu, kujiamini, uadilifu na umahiri wa hali ya juu – vyote kwa pamoja vinahitajika.”

Barua iliyoandikwa na Chama cha Mawakili wa Zanzibar kwa Rais Ali Mohammed Shein dhidi ya uteuzi wake wa majaji wa Mahkama Kuu. Je, hili ni kosa la kwanza la rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa au ni kimbelembele cha wanasheria wetu? Tuisome kwa makini, halafu tuchangiane mawazo tukizingatia dhamira ya kuisaidia Zanzibar kusonga mbele.


Our Ref:ZLS/IKULU/001

Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi
Ikulu, Zanzibar

Mheshimiwa Rais,

KUH: “PETITION” YA CHAMA CHA MAWAKILI WA ZANZIBAR JUU YA KUTORIDHIKA KWAO NA UTEUZI WA MAJAJI WA MAHKAMA KUU ULIOTANGAZWA TAREHE 29 NOVEMBA 2010

Kwanza kabisa sisi Chama cha Mawakili wa Zanzibar tunapenda kukupa pongezi zetu za dhati kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika utaratibu mpya wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Tunakuombea kheri na mafanikio katika kuwatumikia Wazanzibari ambao wamekupa ridhaa zao na kuonesha imani kubwa juu yako

Chama cha Mawakili wa Zanzibar (ZLS) ni Chama kinachowaunganisha Mawakili wote wa Zanzibar ambao wanafanya kazi ya uwakili katika Mahkama Kuu ya Zanzibar pamoja na mahkama zinazofanya kazi chini ya Mahkama Kuu isipokuwa Mahkama za Mwanzo na Mahkama za Makadhi. Mawakili hawa pia huendesha kesi katika Mahkama ya Rufaa ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Katika nafasi yao hiyo, Mawakili wanakuwa ni maofisa wa mahkama. Chama hiki kimeanzishwa mwaka 1998 chini ya Sheria ya Jumuiya ya mwaka 1995. Chama kinaongozwa na Baraza lake lenye Rais, Katibu Mkuu, Mshika Fedha na wajumbe wengine wawili.

Mhe Rais, tarehe 29 Novemba 2010 ulitangaza uteuzi wa majaji wanne wa Mahkama Kuu pamoja na Mwenyekiti wa Mahkama ya Ardhi. Uliowateua kuwa Majaji ni:

 1. Mhe: Abdul-hakim Ameir Issa
 2. Mhe. Fatma Hamid Mahmoud
 3. Mhe. Mkusa Isaac Sepetu, na
 4. Mhe. Rabia Hussein Mohamed

Mhe. Rais, katika uteuzi wako huo, ulikuwa unatumia mamlaka uliyopewa na Katiba ya Zanzibar, 1984 kifungu cha 94(2) na (3). Aidha Chama cha Mawakili hakina mashaka na uteuzi wa Mhe. Abdul-hakim Ameir Issa, wala uteuzi wa Mwenyekiti wa Mahkama ya Ardhi, Mhe. Haroub Shehe Pandu. Mashaka yetu yapo katika uteuzi wa waheshimiwa kuanzia nambari 2 mpaka 4 hapo juu.

Mhe. Rais, sisi tunaelewa kwa dhati kabisa kwamba wewe binafsi humjuwi wala huna sababu ya kumjuwa yeyote katika Majaji wanne uliowateua. Uteuzi wako, tunaamini kabisa, unatokana na ushauri uliopewa na Tume ya Utumishi ya Mahkama iliyoanzishwa chini ya Sheria Namba 13 ya mwaka 2003 ambayo Mwenyekiti wake ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Hamid Mahmoud Hamid pamoja na wasaidizi wako wengine katika sekta ya sheria.

Mhe. Rais, sisi mawakili ambao tumetia saini barua hii tukiwa ni wadau wakubwa katika sekta hii, tuna imani kubwa nawe Mheshimiwa Rais, lakini tunaamini washauri wako hawakukutendea haki walipokushauri uwateue Mhe. Fatma, Mhe. Mkusa na Mhe. Rabia kuwa ni Majaji wa Mahkama Kuu. Mhe. Rais, haitoshi tu kusema kwamba Jaji Mteule ametimiza masharti ya Katiba na hivyo anafaa kuwa Jaji wa Mahkama Kuu. Mhe. vipo vigezo vyengine ambavyo ni lazima viangaliwe kabla ya uteuzi wa Jaji wa Mahkama Kuu kufanyika. Nafasi ya Ujaji ni nafasi ya juu kabisa katika ngazi ya Mahkama zetu na pia ni nyeti. Utaalam uliobobea, rekodi iliyothibitika, umakini wa hali ya juu, kujiamini, uadilifu na umahiri wa hali ya juu – vyote kwa pamoja vinahitajika.

Mhe. Rais, kifungu cha 94(2) cha Katiba kinasomeka ifuatavyo:

Majaji wa Mahkama Kuu watateuliwa na Rais kutokana na mapendekezo ya Tume ya Utumishi ya Mahkama.

Mhe. Rais, Chama cha Mawakili kina mjumbe katika Tume ya Utumishi ya Mahkama. Pia wajumbe wengine wa Tume ni watu walio karibu na Chama cha Mawakili. Tunapenda kukuthibitishia kwamba hakuna kikao chochote cha Tume hiyo ambacho kimejadili jina la Mhe. Rabia Hussein. Hivyo uteuzi wa Mhe. Rabia umefanywa kinyume kabisa na Katiba ya Zanzibar na hauwezi kusimama katika macho ya sheria.

Mhe. Rais, sisi kama Chama cha Mawakili, tunaamini hata uwepo wa Mhe. Hamid Mahmoud kama Jaji Mkuu wa Zanzibar una mashaka tele ya kikatiba. Inaeleweka kwamba Mhe. Hamid Mahmoud alistaafu kwa hiari alipotimiza miaka 60. Baada ya hapo, Kikatiba, alisita kuwa Jaji Mkuu na Jaji wa Mahkama Kuu. Iwapo alitakiwa kuendelea kushika wadhifa, alipaswa kwanza kupewa mkataba wa kuwa Jaji wa Mahkama Kuu. Mkataba wa aina hiyo ulilazimu kujadiliwa na Tume ya Utumishi ya Mahkama kwa mujibu wa kifungu cha 95 cha Katiba ambacho tunaomba kukinukuu:

95(1) Bila ya kuathiri masharti ya kifungu hiki, Jaji wa Mahkama Kuu ataendelea kushika wadhifa wake hadi kufikia umri wa miaka sitini ambapo anaweza kustaafu kwa hiari ama kuendelea hadi kufikia umri wa miaka sitini na tano ambapo atastaafu kwa lazima.

(2) Bila ya kuathiri masharti ya kijifungu cha (1) cha kifungu hiki, Rais kwa kushauriana na Tume ya Utumishi ya Mahkama anaweza kumteua tena Jaji aliekwisha staafu kushika madaraka ya Jaji wa Mahkama Kuu kwa muda au kwa ajili ya kesi maalum. (Msisitizo ni wetu).

Mhe. Rais, ni wazi kwamba pale Mhe. Jaji Mkuu alipoamua kustaafu kwa hiari alipotimiza umri wa miaka 60, hakukuwa na sababu yoyote kuendelea kufanya kazi katika mkataba kwa kuwa Katiba ilikuwa inamruhusu kuendelea na ajira hadi kufikia miaka 65. Vyovyote iwavyo, endapo Mhe. Jaji Mkuu alitakiwa aendelee na nafasi yake baada ya kumaliza utumishi wake, ililazimu mambo yafuatayo yafuatwe kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar (kifungu cha 94(1), 94(2), 94(6)(a) na (b). Mambo yenyewe ni:

a) Ateuliwe kuwa Jaji wa Mahkama Kuu;

b) Mapendekezo ya (a) yatokane na Tume ya Utumishi ya Mahkama;

c) Endapo ni Jaji wa Mkataba, “masharti ya kazi, marupurupu na kiinua mgongo cha Jaji wa mkataba wa kipindi maalum yataamuliwa na Tume ya Utumishi ya Mahkama.” (Kif.94(6)(b).

d) Iwapo atateuliwa kuwa Jaji basi atakula kiapo cha Jaji wa Mahkama Kuu.

Mhe Rais, Jaji Mkuu wa sasa ambae ndio Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi ya Mahkama, alipostaafu kwa hiari, utaratibu ulioainishwa hapo juu haukufuatwa na magazeti yaliripoti na jamii ya wanasheria pia ilifadhaishwa mno. Aidha, iwapo Mhe. Hamid Mahmoud alitakiwa awe Jaji Mkuu, pia ilipaswa masharti ya Katiba yafuatwe. Vyenginevyo kuendelea kwake kuwa Jaji Mkuu kunakuwa na mashaka ya Kikatiba na sisi tusingependa nchi yetu iwe na Jaji Mkuu ambae uteuzi wake umegubikwa na kasoro kadhaa za Kikatiba.

Hata suala la kuwa Jaji au Jaji Mkuu wa Mkataba ni suala linalopigwa vita sana katika Mahkama za Jumuiya ya Madola kwa sababu mikataba inaondowa kinga ya Kikatiba aliyonayo Jaji wa Mahkama Kuu na hivyo kudumaza uhuru wa Mahkama (independence of the Judiciary). Aidha Jaji wa Mkataba hawezi kufanya kazi yake bila ya hofu wala woga kwa mamlaka ya uteuzi.

Mhe. Rais, siri ya maiti aijuwae muosha; na sisi mawakili ndio waosha wa waheshimiwa majaji na mahakimu wetu. Mhe. Rais, bila ya kuzunguka, sisi tunataka tukuthibitishie kwamba Mhe. Fatma na Mhe. Mkusa hawana sifa kiutendaji na kiuwezo za kuwa majaji wa Mahkama Kuu ya Zanzibar. Mhe Rais, uwezo wa Jaji unapimwa kwa namna anavyoendesha kesi na kuandika hukumu zake. Chombo cha Mahkama ni chombo cha kutoa haki. Na haki inatakiwa isifanywe tu lakini ionekane waziwazi kuwa inafanywa. Mhe Rais, haki haiwezi kupatikana ikiwa wanaosimamia haki hiyo ni watu wasiokuwa na sifa zinazotakiwa.

Mhe. Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, tunakuhakikishia kwamba sisi Mawakili wa Zanzibar ambao saini zetu zimetiwa hapa chini tuna imani kabisa na wewe binafsi na wala hatuandiki barua hii kuhoji mamlaka yako ya Kikatiba ila tunatoa tahadhari hii kama mchango wetu katika kujenga mahkama iliyotukuka, hasa kwa vile wananchi wamepoteza imani kwa mahkama zetu ziliopo sasa. Ni vyema kuepuka mambo yanayoonekana dhahiri kulenga katika kudumaza zaidi ufanisi wa mahkama katika suala zima la utoaji haki. Tujinasuwe sasa kuliko kuendelea kujizamisha kwa kuweka watendaji wasiofaa.

Sisi, kama wadau wa jamii, tunahisi tuna wajibu wa kukutanabahisha kuhusu uteuzi huu. Aidha tusingependa Mahkama Kuu ambayo tayari kuna malalamiko mengi ya utendaji usiokidhi haja iendelee kuchukuwa Majaji bila ya ushauri wa Tume ya Utumishi ya Mahkama na bila ya umakini katika tathmini ya wateule hao.

Mhe. Rais, wateule wa Ujaji tuliowataja hapo juu, hawatokuwa Majaji rasmi Kikatiba na kuanza kazi ya Ujaji wa Mahkama Kuu mpaka baada ya kula kiapo. Hilo likishafanyika, itakuwa dhiki sana kuondosha uteuzi huo. Hivyo, tunakuomba Mhe. Rais, utafakari upya juu ya uteuzi huo na uridhike kuusitisha. Tunaamini wanasheria wenye sifa na maadili yanayotakikana wapo na wanaweza kufanya kazi ya ujaji, Zanzibar.

Wako katika kusimamia haki,

Yahya Khamis Hamad Salim Rais
H. B. Mnkonje Katibu Mkuu
Abdulla Juma Mohammed Mshika Fedha
Salma Ali Hassan Mjumbe, ZLS
Mussa Kombo Mjumbe, ZLS

 1. Ajar Amar Patel …………………………..

 2. Ussi Khamis Haji …………………………….

 3. Hamid A. S. Mbwezeleni …………………………….

 4. Salum Toufiq Ali ………………………………

 5. Awadh A. Said ……………………………….

 6. Nassor Khamis Mohammed ……………………………….

 7. Adam S. Abdulla ………………………………

 8. Is-Haq Ismail Shariff ………………………………..

 9. Uhuru Hemed Khalfan ………………………………..

 10. Mahadhi J. Maalim (ameridhia)

 11. Masoud H. Rukazibwa ………………………………..

 12. Ramadhan Makame ……………………………….

 13. Mbwana J. Mbwana ………………………………

 14. Fatma A. Karume …………………………….

 15. Rajab Abdalla Rajab ……………………………….

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.