Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Jakaya Kikwete

“Sura ya pili ya umoja wa nchi yetu ni Muungano wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika uliozaa nchi moja mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 26 Aprili, 1964. Tunalo jukumu la kihistoria la kuhakikisha kuwa Muungano wetu unadumu na unazidi kuimarika. Nafurahi kusema kuwa Muungano wetu ni imara licha ya changamoto za hapa na pale. Na, kinachonipa faraja zaidi ni ule ukweli kwamba pande zetu zote mbili za Muungano zinayo dhamira ya dhati ya kutatua kero zilizopo kwa lengo la kuuimarisha.”

Dondoo za hotuba ya Rais Jakaya Kikwete katika uzinduzi wa Bunge la 10, Dodoma, hapo Novemba 18, 2010.

Muungano

Mheshimiwa Spika;

Sura ya pili ya umoja wa nchi yetu ni Muungano wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika uliozaa nchi moja mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 26 Aprili, 1964. Tunalo jukumu la kihistoria la kuhakikisha kuwa Muungano wetu unadumu na unazidi kuimarika. Nafurahi kusema kuwa Muungano wetu ni imara licha ya changamoto za hapa na pale. Na, kinachonipa faraja zaidi ni ule ukweli kwamba pande zetu zote mbili za Muungano zinayo dhamira ya dhati ya kutatua kero zilizopo kwa lengo la kuuimarisha.

Mheshimiwa Spika;

Nafurahi kwamba dhamira yangu ya kuimarisha kamati ya pamoja ya Serikali zetu mbili kuhusu masuala ya Muungano imefanikiwa. Kamati hiyo imefanya kazi nzuri sana na mambo mengi yaliyokuwa yanaleta usumbufu na misuguano yamezungumzwa kwa uwazi na kupatiwa majawabu. Yale machache yaliyosalia tutaendelea kuyapatia ufumbuzi ulio muafaka kwetu sote.

Mheshimiwa Spika;

Niruhusu nimshukuru na kumpongeza kwa dhati aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, wakati akiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake mzuri. Aidha, nawapongeza kwa namna ya kipekee Wajumbe wa Kamati hiyo wakiongozwa na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda na Mheshimiwa Edward Lowassa kabla yake, kwa upande wa Serikali ya Muungano na aliyekuwa Waziri Kiongozi, Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Nawapongeza kwa umakini wao, moyo wao wa uzalendo na kwa juhudi zao zilizozaa matunda mema.

Umoja wa Watu

Mheshimiwa Spika;

Sura ya tatu ya umoja wa nchi yetu ni ile ya wananchi wetu kuwa wamoja, wanaopendana, kushirikiana na kushikamana. Pamoja na changamoto za hapa na pale, Watanzania wameendelea kuwa watu wamoja, wanaopendana na kushirikiana licha ya tofauti zao za rangi, makabila, dini, maeneo wanayotoka na ufuasi wa vyama vya siasa. Kubaguana na kuchukiana kwa sababu za tofauti zao hizo ni mambo mageni kabisa kwao. Nafurahi kwamba hata pale waliposhawishiwa wengi wao walikataa na waliunga mkono kwa wingi sana juhudi za kutafuta suluhu.

Mheshimiwa Spika;

Bila ya shaka sote tunaikumbuka hali tete ya kisiasa na kiusalama iliyokuwepo Zanzibar katika miaka ya hivi karibuni. Katika hotuba yangu ya Desemba 30, 2005, nilielezea kusononeshwa na hali hiyo na kuahidi kushirikiana na viongozi wa kisiasa wa pande zote kulitafutia ufumbuzi. Nafurahi kwamba ahadi hiyo imetimia. Zanzibar sasa ni shwari na watu wanaishi kindugu. Serikali ya umoja wa kitaifa imeundwa na hasama zimeisha.

Napenda kutumia nafasi hii kuwapongeza kwa dhati kabisa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Mheshimiwa Seif Shariff Hamad ambaye sasa ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kwa uongozi wao thabiti uliowezesha kupatikana maridhiano ya kisiasa yaliyomaliza mzozo Visiwani humo. Nawapongeza wananchi wa Unguja na Pemba kwa kuwaunga mkono viongozi wao. Zanzibar sasa ni nzuri kwa kila mtu kuishi.

Mheshimiwa Spika;

Kwa mara nyingine nampongeza Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Nampongeza Mheshimiwa Maalim Seif Shariff Hamad kwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi kwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais. Tunawatakia heri katika kazi yao ya kujenga Zanzibar mpya. Nawahakikishia utayari wangu wa kushirikiana nao kwa lolote watakaloona naweza kuwa wa manufaa. Ahadi yangu hiyo ni ahadi ya Serikali ya Muungano pia.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.