HATA kama hupendi kusoma vitabu; hiki si cha kukosa. Kwanza kimeandikwa kwa Kiswahili fasaha; lugha yetu mama inayoanza kufifishwa na kuchujwa na kizazi kisichosoma vitabu siku hizi. Pili, kimepikwa na mtaalamu halisi. Dk Harith Ghassany alizaliwa Zanzibar akapata shahada ya udaktari wa Falsafa Chuo Kikuu cha Harvard, Massachussets, Marekani. Harvard ni chuo cha kale sana; kilianzishwa mwaka 1636 na kwa muda mrefu kimeorodheshwa na magazeti, watalaamu na chama cha vyuo vikuu duniani kuwa cha kwanza duniani.

Fani yake kuu ni utafiti. Dk Ghassany ambaye anasema alitafiti kitabu hiki muhimu kuanzia 2004 hadi 2009 alikuwa awali Profesa Msaidizi Chuo cha Udaktari na Sayansi za Afya , Chuo Kikuu cha Sultani Qaboos, kilichoko Muscat, Oman, Uarabuni. Nilipomhoji kutokea Marekani anakoishi, Dk Ghassany alifafanua lengo la kuandika kigongo hiki chenye kurasa 500: “Nia yangu ni kuziondoa fitina za upotoshaji wa historia ili uhusiano mkongwe baina ya Wazanzibari, baina ya Wazanzibari na Watanganyika (Watanzania) na baina ya Waafrika na Waarabu, upate kuendelea kutiririka na kuimarika kwa maslahi ya kujenga amani na neema kwa faida ya walio wengi na vizazi vya baadaye vya pande zote.” Sijawahi kusoma kitabu kinachomhusu kila Mtanzania kama hiki.

Licha ya kuhadithia, kinatafakari maswali mengi. Je, neno Afrika asilia yake nini? Vipi tukaitwa Tanzania? Vipi Wazanzibari wengine hawautaki Muungano? Mapinduzi ya Unguja yalianzia wapi? Nani hasa alihusika? Je, viongozi waliopindua ndiyo waliotawala? Ndani ya sura ya pili, inayohusu Mirengo ya Kizalendo na Mapinduzi, ukurasa 23, mwandishi anatueleza bila kupepesa macho: “Msomaji anatakiwa awe makini kabisa na hata kabla hajaendelea kusoma inampasa afahamu kuwa viongozi wakubwa wa Chama cha Afro Shirazi kama marehemu, Mzee Abeid Amani Karume, marehemu Mzee Thabiti Kombo Jecha au Sheikh Aboud Jumbe hawakushiriki katika mipango halisi ya mapinduzi ya Zanzibar.” Si kitabu cha kisasi chenye azma ya kusakama wakuu wa nchi na mashujaa wetu wa zamani kibwege; au kuwachafua. Dk Ghassany anakiri hana kabisa mshawasha wa kutaka kuja kuwa mwanasiasa au mgombea kiti cha urais. Zamani Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipenda kutuambia wasomi tusisahau tulikotoka. Kambarage alimlinganisha msomi na kijana aliyetumwa na kijiji chenye njaa kukitafutia ahueni kisha arudi kuwasaidia wanavijiji wenzake.

Dk Ghassany ni msomi wa kabila hilo. Katimiza wajibu wake. Anasema kitabu kilikuwa kigumu kukiandika na pia kigumu kukisoma. Moja ya msingi mahsusi wa kazi za historia ni kutukumbusha watu tuliowasahau na mafunzo yake.

Tunamkumbuka John Okello? Je, Oscar Kambona, mpinzani mkuu wa hayati Nyerere na ujamaa aliyeishia uhamishoni hapa London, alihusikaje katika mapinduzi ya visiwani? Je, nini kilitokea wakati wa maasi ya wanajeshi wa Tanganyika mwaka huo huo wa 1964? Je, silaha za mapinduzi ya Zanzibar zilitoka wapi? Je, vyama vingine kama Umma Party cha hayati Abdulrahaman Babu vilifanya nini? Kassim Hanga ni nani? Je, kwanini Kassim Hanga akanyongwa miaka michache baada ya mapinduzi ya Unguja, 1964? Je, aliyekuwa zamani kiongozi wa Algeria, Ahmed Ben Bella (ambaye yu hai) alihusikaje? Je, wanamapinduzi maarufu wa Cuba Fidel Castro na Che Guevara walihusika? Kwanini shirika la Upelelezi la Marekani, CIA lilikuwa likiogopa sana Unguja? Je, vipi maelfu ya Wazanzibari wamezagaa ulimwenguni wakiishi Ulaya, Marekani na Uarabuni, baada ya kuikimbia nchi yao? Je, mwanajeshi maarufu Kanali Ali Mahfoudh alifanya nini? Maswali mengi yamejibiwa si tu kwa utafiti maridadi alioufanya mtaalamu huyu bali pia kupitia midomo ya waliohusika.

Kitabu kimejazana hati za siri, za kiserikali na pia mahojiano na wazee hai walioshika mapanga enzi hizo. Wengine wao kama Victor Mkello (aliyekuwa zamani mmoja wa viongozi wakubwa wa Chama cha Wafanyakazi na TANU wanahadithia kinauga ubaga ama walivyotiwa ndani, walivyosakamwa na nani alifanya nini katika ngazi za juu. Hiki si kitabu cha mchezo. Kuna pia mchango wa mzalendo na mwanahistoria mwingine Mohamed Said (aliyeandika vitabu viwili vinavyohusika na historia ya TANU, kimojawapo Uchaguzi wa mwaka 1958 katika kutafiti habari kibao.

Alivyokuwa mkweli, mbali ya utafiti na picha lukuki; Dk Ghassany aliwaonyesha viongozi wa sasa Unguja na bara muswaada wa kitabu kabla ya kuutoa. Anasema : “Mustakbali utakuwa mzuri iwapo utajiri wake mkubwa wa kihistoria wa kijiografia wa Zanzibar na Tanzania utatumika kuuimarisha Muungano wake na Tanganyika baada ya Baraza adhimu la wawakilishi kuipitia na kuifanyia marekebisho katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuyalinda maslahi ya Zanzibar na kuonyesha njia mpya ya Muungano wa Jamhuri ya Tanzania.” Unguja na Pwani kijumla ndiko lilipo chimbuko la lugha ya Kiswahili. Kama kazi ya fasihi ya lugha hii tukufu, kitabu kitakusaidia msomaji (hata uwe si mpenzi wa mambo mazito ya kihistoria na kisiasa) kuboresha ujuzi wako wa Kiswahili fasaha, hasa vijana. Kwa watu wa makamo na wazee, wataalamu na wapenda nchi yetu watapata changamoto na jopo la kufanya majadiliano, kupitia mambo ambayo tuliyasikia tu mitaani miaka 40 iliyopita.

“Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru- Mapinduzi ya Afrabia” rahisi kupatikana. Kipo maduka ya vitabu mbalimbali Dar es Salaam (TPH, Manyema Mosque, Ibn Hazim) Dodoma (Chuo Kikuu ) Arusha (Kase ), Tanga (Mohamed Said, 0787-265766) na Unguja (Masomo Bookshop). Kwa wanaotumia mtandao pitia tovuti mahsusi ya kitabu : http://www.kwaherikwaheri.com au nenda maduka maalum ya Lulu.com na Amazon.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.