Kupitia mitandao, nimefuatilia hoja mbalimbali zitolewazo na Watanzania wa pande zote mbili za Muungano, baada ya jana Rais Jakaya Kikwete kutangaza baraza lake la mawaziri lenye wizara 26. Na huu hapa ndio mchango wangu.

Jambo moja napaswa kulitanguliza na mapema, kwamba ni nadra kukuta Wazanzibari na Watanganyika (natumia jina hili kwa kuwa naliamini) wanaegemea upande mmoja wa hoja, hata kwa jambo ambalo hawapishani imani. Na hili hapa ni mojawapo.

Hoja ya Watanganyika, kwa mfano Mchungaji Christopher Mtikila, ambaye anajinasibisha wazi na Utanganyika wake, ni kwamba Wazanzibari hawapaswi kuwamo kwenye serikali ya Muungano, ambayo yeye anaamini ni ya Tanganyika.

Hoja ya Wazanzibari, ambayo nimeisoma kwenye mitandao ya Mzalendo na Zanzinet ni kwamba, Wazanzibari waliongizwa kwenye serikali ya Muungano, wamepelekwa kwenda kuwa chambo cha kuimaliza Zanzibar.

Kwa hivyo, hata katika hili ambalo unaona wazi kwamba wanafanana kwa hoja ya kutokuwataka Wazanzibari kwenye Serikali ya Muungano, Watanganyika na Wazanzibari wanatafautiana juu ya sababu za kuwakataa huko. Tafauti ndani ya mapatano, labda ndivyo tunavyoweza kuyaita.

Tuliache hilo. Tuje kwenye hoja na upotoshaji wake, kwa kuangalia pande zote mbili. Ni muhimu kujua kinachozungumziwa hapa: Wazanzibari hawa wafuatao wameteuliwa na Rais Kikwete kuwa wajumbe wa baraza lake la mawaziri: Shamsi Nahodha, Hussein Mwinyi, Makame Mnyaa, Samia Suluhu, Umi Mwalimu, Abdallah Juma na Mahadhi Juma. Jumla yao ni saba. Nafasi walizopewa ni baina ya uwaziri na unaibu, wizara zao ni kati ya zile muhimu sana na zile zisizo muhimu sana. Kubwa kuliko yote, wizara hizo ni baina ya zile za Muungano na zisizo za Muungano.

Hoja inayotolewa na Wazanzibari ni kwamba wenzao waliongia kwenye Baraza hili, wana rikodi ya kuisaliti Zanzibar linapokuja suala la Muungano, na kwa hivyo watakachokifanya ni kuimaliza Zanzibar wakiwa ndani ya Serikali ya Muungano. Nini maana ya kuimaliza Zanzibar? Ni kuendelea kuchukua mamlaka na nguvu zake na kuzisalimisha kwenye Muungano, kwa mfano kukubali suala la mafuta liendelee kuwa la Muungano. Ushahidi uko wapi? Watakwambia ni Shamsi Nahodha, ambaye wanaona kuwa alipokuwa Waziri Kiongozi miaka kumi iliyopita, alijitahidi kuzima hoja za Wazanzibari waliokuwa wakitaka mafuta yatoke kwenye Muungano, kwa kukubali hoja ya kuwa lazima jambo hili likajadiliwe na liamuliwe kwenye Bunge na sio vikao tu vya Baraza la Wawakilishi. Ushahidi? Kimya!

Hapo ndipo ninapoona kuwa pana upotoshaji. Si kwamba namtetea Shamsi Nahodha, hapana. Nimeandika sana dhidi yake na hata leo na kesho nitafanya hivyo, nikishawishika kwamba nastahiki kuwa dhidi yake. Lakini si katika hili.

Inawezekana kuwa Nahodha alikuwa Waziri Kiongozi mwoga. Huwezi kuufananisha uwaziri kiongozi wake na ule wa Seif Sharif Hamad kwenye miaka ya ’80. Huyu hakuwa na haiba wala nguvu za Seif Sharif. Lakini huwezi kumtafautisha na Mohammed Bilal, ambaye sasa ni Makamo wa Rais. Wote wawili walikuwa na staili moja ya uongozi – kuzitenga shingo zao kando na panga la hasira za Dodoma.

Sasa ikiwa hoja ni kwamba, Mzanzibari huyu ni muoga, hilo haliwezi kumfanya asistahiki kuwa Waziri wa Muungano, hasa kwa kuzingatia nafasi aliyopewa ya uwaziri wa Mambo ya Ndani. Lakini na hilo la woga nalo, tunapaswa kuliangalia kwa macho mapana. Kwani si wakati huo yeye akiwa Waziri Kiongozi, ndipo Katiba ya Zanzibar imebadilishwa na kupeleka madaraka zaidi kwa serikali ya Zanzibar? Kwani si hata haya Maridhiano yamepitishwa wakati akiwa Waziri Kiongozi? Kwani hii serikali ya Umoja wa Kitaifa si imepata upumzi wake kutoka utawala ambao yeye alikuwa mtu muhimu? Kauli zitakuja kwamba, kama si Rais Mstaafu Amani Karume kusimama kiume, basi Nahodha angelikwisha kuyaua Maridhiano kitambo. Nayo ni dhana. Kilichoko mezani hakisemi hivyo. Kinasema kwamba alishiriki hatua kwa hatua, kwa kiwango chake, kufanikisha alichotumwa na bosi wake, hata kama ingeliwezekana kwamba mwenyewe hakukipenda!

Upande wa Tanganyika, upotofu wa hoja ya kuwakana Wazanzibari ina upotoshaji wa pande mbili. Kwanza, kinara wa hoja hii (ingawa naamini hayuko peke yake) ameathiriwa na msimamo wake mkali wa kidini. Tangu mwanzo walipoteuliwa Shamsi, Mnyaa na Zakia Meghji kuwa wabunge, alishasema kwamba Kikwete muislamu kawateua Waislam wenzake kuwa wabunge. Jambo hili lilizungumzwa sana kwenye mitandao ya Jamii Forums na Facebook. Kwa hivyo, udini, kama kawaida yake, ukaipotosha makini ya hoja.

Lakin upotofu mkubwa upo kwenye ukweli wenyewe. Na ukweli wenyewe ni kwamba hii ni Jamhuri ya Muungano yenye pande mbili. Upande mmoja, Tanganyika, umenyimwa serikali na utambulisho wa wazi (nasema ya wazi, maana ya kificho ipo) kwa muda mrefu. Upande mwengine, Zanzibar, umeachiwa kuwa na serikali na utambulisho wake. Hisabu yake ni kuwa kila Mzanzibari ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwa hivyo ana haki za uraia sawa na Mtanzania ambaye si Mzanzibari. Kwa hivyo, kwa akina Mtikila hapa panatumika tu upotoshaji wa mambo, lakini sio uhalisia.

Lakini je, kipo ambacho kinaweza kuitwa hoja kwa pande zote mbili?  Kwa mtazamo wangu, kipo. Nacho ni hiki kinachopingana na wazo la hapo juu: Mzanzibari kuwa waziri katika wizara isiyokuwa ya muungano kwenye Serikali ya Muungano. Ni kizungumkuti, lakini kinafahamishika.

One thought on “Madai dhidi ya Wazanzibari kwenye Serikali ya Muungano: Hoja na Upotofu”

  1. Asalaam alaikum
    Nimesoma nakala yako, kwa muona wangu kuchaguliwa viongozi kutoka zanzibar kuingia katika serikali ya muungano kwa kweli Nahoza hastahiki kuingia kwa sababu kwanaza ni muoga kama unavyosema,pili yahupo tayari kuiteteza zanzibar kwa maslahi ya wazanzibari.

    Kuchukuliwa na serikali ya muungano inampa fursa kubwa na nguvu zaidi ili aweze kuimaliza zanzibar kwani Nahoza hakusoma,pili ni muogoa,tatu ni mbinafsi,huyu jamaa wanaweza kumtumikia kama chambo kwa wazanzibari, ulieka nakala hii unafahamu fika ila umejaribu kutumia elimu yako ya uwandishi ili kuleta hoja.
    Sisi wazanzibar tunataka watu imara ambao wenye misimamo na wasio na woga katika kuitetea nchi yetu sio kama Nahoza,Viongozi kama hawa ni hatari sana katika nchi,wanaweza kuchafua hali za hewa.
    Nawakilisha.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.