Na Padri Privatus Karugendo

Mzee Ali Haji Pandu, mwanasiasa mkongwe wa Zanzibar

KATIKA uzinduzi wake wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2010 kule Zanzibar, Chama cha NCCR- Mageuzi kilijiandaa vizuri sana kufafanua sera zake ingawa hakikufanikiwa kuvutia wasikilizaji wengi ikilinganishwa na vyama vya CCM na CUF.

Pamoja na kuwa na wazungumzaji mahiri wenye uwezo wa kujieleza na kunadi sera za chama kwa Ufasaha, watu wachache sana walijitokeza kwenye uzinduzi wa NCCR-Mageuzi.

Ukilinganisha watu waliojitokeza kwenye uzinduzi wa CCM na CUF, unakuwa na mashaka kama kweli Zanzibar iko tayari kuingia kwenye muktadha mpya au bado inashikilia muktadha wa siasa wa zamani ambapo vyama viwili vya CUF na CCM, vinahodhi siasa za uchaguzi Zanzibar.

Baada ya uchaguzi imejionyesha wazi kwamba Serikali ya umoja wa kitaifa inaundwa na vyama viwili pamoja na ukweli kwamba Zanzibar ina vyama vingi vya sisasa. Kuna vyama kama SAU, Jahazi Asilia, UMD, CHADEMA, TLP na vingine.

Vyama vyote hivi vina wanachama na vingine vilijitahidi kufanya kampeni, lakini vilivyo vingi vilishindwa kufanya kampeni kwa kisingizio cha kutokuwa na fedha za kutosha kufanya kampeni.

Jambo la kushangaza na pengine ni la kufikirisha ni kwamba vyama hivi ambavyo si vikongwe wafuasi wake ni vijana wadogo.

Sababu wanazozitoa za kujiunga na vyama vipya huku wakisusia vyama vikubwa kama vile CCM na CUF ni kwamba vyama hivi vinameshindwa kabisa kuyashughulikia matatizo ya vijana; vyama hivi vimekuwa na upendeleo wa kuwapatia wazee nafasi za uongozi kwa kuzingatia kwamba woa ndo walishiriki mapambano ya kuikomboa Zanzibar.

Vijana wanabeza mfumo huo kwa kuelezea wazi kwamba mawazo hayo ya ukombozi yamepitwa na wakati. Leo hii nguvu ya pamoja inahitajika ili kuiendeleza Zanzibar.

Na kusema kweli swala lolote linalogusa masIlahi ya Zanzibar, watu hawa wanaungana bila kuangalia tofauti zao.

Mfano mzuri ni tetesi za Zanzibar kuwa na mafuta na gesi nyingi. Hili wamelifuatilia wote kwa makini; Muungano wa sasa wa serikali mbili unapingwa kwa nguvu zote na karibia Wazanzibari wote.

Uzinduzi wa kampeni za CCM, ulikuwa mkubwa na wa aina yake. Picha inayojitokeza ni kwamba uwanja wa kisiasa visiwani Zanzibar si sawa.

Rasilimali zilizotumika kuandaa mkutano wa uzinduzi wa kampeni za CCM, ni kubwa kupita kipimo ukilinganisha na rasilimali zilizotumika kuandaa mikutano ya uzinduzi ya NCCR na CUF.

CCM, waliweza kuwasafirisha wanachama wao kutoka kila sehemu ya Unguja na wengine walitoka Pemba.

Mwandishi wa habari hii alishuhudia magari ya abiria na yasiyokuwa ya abiria yakiwasomba watu na kuwamwaga kwenye uwanja wa Kibanda maiti, ambao siku hizi unajulikana kama Uwanja wa Demokrasia.

Wanachama wote waligawiwa T-shirt, kofia na kanga. Vipeperushi vyenye thamani kubwa viliupamba uwanja wa Kibanda maiti, picha za wagombea kuanzia Rais wa Zanzibar, Rais wa Muungano, wabunge, wawakilishi na madiwani zilijazana kila kona.

Ulinzi ulikuwa mkubwa kulinganisha na ulinzi wa NCCR na CUF, vipaza sauti vilikuwa vya kisasa, makundi ya ngoma na muziki yalikuwa pale, magari ya serikali yalitumika katika uwanja wa mkutano.

Ingawa viongozi wengi walikuja kwa magari ya binafsi, uchunguzi uliofanyika ulionyesha kwamba namba za magari zilibadilishwa, zilitolewa za serikali na kuweka za binafsi lakini waliobadilisha walisahau kwamba namba za magari ziko pia kwenye vioo vya gari.

Changamoto nyingine iliyojitokeza ni jinsi mikutano ilivyoendeshwa. Mikutano ya NCCR Mageuzi na CUF ilikuwa ni mikutano ya mjadala na hoja wakati CCM mkutano wao ulikuwa ni mbwembwe, majigambo na mipasho na kuonyesha kwamba wao ni chama tawala.

Mfano, Maalim Seif Sharif Hamad wa CUF, alitumia muda wa saa moja na dakika arobaini na tano, akielezea sera za chama chake wakati Dk. Shein wa CCM alitumia nusu saa tu kunadi sera za chama chake.

Ujumbe wa CUF, katika uzinduzi wa kampeni ulikuwa ni ujenzi wa Zanzibar mpya, uimarishaji wa malengo ya mapinduzi katika muktadha mpya wa kisiasa: Mishahara mizuri kwa wote, elimu kwa wote, afya bora kwa wote, huduma za kijamii, muungano wa serikali tatu ambao kila upande utaheshimiwa na kunufaika, katiba mpya ya Muungano na Zanzibar. Na walijitahidi kiasi cha kutosha kutotumia vijembe na mipasho ya kisiasa.

Ujumbe wa CCM ni tofauti na malengo ya muktadha wa Zanzibar mpya, maana viongozi wote hata na mgombea urais, waliendeleza ujumbe ule ule wa mapinduzi daima!

Bado wanaongelea mapinduzi kwa asili yake: Waliopindua ndio wataendelea kutawala. Pia wanaongelea muungano wa serikali mbili, hawakugusia katiba mpya.

Changamoto kubwa kwa muktadha mpya wa siasa Zanzibar ni kwamba CCM, bado wanaendeleza vijembe na mipasho. Mfano: “Wataweza? Hawawezi!” Huu ni mpasho uliotumiwa na kila kiongozi aliyekuwa akipanda jukwaani.

Hakuna msemaji wa CCM alisema lolote kuhusu serikali ya umoja wa kitaifa na majukumu yake.

Katika mikutano ya NCCR-Mageuzi na CUF, Suala la kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa lilijadiliwa.

Ingawa mikutano yote ya uzinduzi wa kampeni ilifanyika kwa amani na utulivu mkubwa na watu wengi kukiri kuwepo kwa mazingira ya kistaarabu katika maeneo ya kampeni, bado suala la kujadiliana baina ya wagombea na wapiga kura halikupewa nafasi.

Wapiga kura hawakupewa fursa ya kujadili namna serikali ya umoja wa kitaifa itakavyofanya kazi na wagombea.

Muktadha mpya wa kisiasa Zanzibar unatoa fursa nzuri ya watu kujadiliana katika mikutano ya hadhara na vilevile kupitia midahalo.

Chanzo: Tanzania Daima, Novemba 21, 2010

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.