Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein (katikati), Makamo wake wa Kwanza, Maalim Seif Sharif (kushoto) na mtangulizi wake Amani Karume

Na Jabir Idrissa

HAPA Zanzibar wapo watu wanachekesha sana . Wanaishi katika ndoto za alinacha. Bado wanaamini hadithi za Alfu lela u lela. Zile za miaka ya ujima. Hawataki kuamini hali ya mambo imebadilika. Wapo nyuma mno kiwakati.

Walipomsikia Dk. Ali Mohamed Shein – sasa Rais wa Zanzibar ya maridhiano – akiahidi kuwa hatoshirikiana na mtu asiyependa na kuamini katika zama mpya ya siasa za maridhiano Zanzibar, walimbeza. Walimguna.

Wakati ule Dk. Shein alikuwa anatafuta mamlaka ya chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kubeba bendera na kukiwakilisha katika mbio za kugombea kiti cha urais wa Zanzibar. Waliona hakuwa kiongozi wa maana.

Walimchukulia kama kiongozi asiye mamlaka yenye nguvu yoyote katika chama na ndani ya serikali. Walimuona yu makamu wa rais tu wa Jakaya Mrisho Kikwete, akijitahidi kupalilia kula yake. Kama wasemavyo wengine, walimuona si mali kitu.

Kinachowasumbua ni wehu tu katika kufikiri na kuchukulia hali halisi ya mambo. Bado ni wehu huohuo unawasakama. Hawajijui wala kujitambua. Wamelala usingizi wa pono; lakini ajabu ni kuona hawajazinduka kamwe wakati ishara zote za mabadiliko zimetimia.

Hali tulivu inayoonekana tangu Dk. Shein atangazwe rais wa kwanza wa Zanzibar yenye maridhiano kisiasa; amani na utulivu wa kweli; na inayoshuhudia watu wake wakicheka na kujadiliana bukheri wa afya bila ya kujali tofauti zao za itikadi ya kisiasa, wala haijawashitua.

Bado hawajatafakari vizuri kusudi wajitambue na kuzinduka. Wangali wameshikilia mjiti wa saa unaoendelea mbele bila ya wasi na wanahangaika kuuzuia usipige kasi yake. Wanataka kuusimamisha ili wakati nao usimame. Wallahi watu hawa wamelala fofofo.

Bora waingie darasani. Nawapa somo japo la sekunde tatu. Mjiti wa saa haujapata kusimama. Ukifanya hivyo dunia nayo inasimama. Dunia ikisimama na viumbe vitasita kuchechegua.

Huo utakuwa wakati wa muumba wa viumbe vyote. Si wakati wetu huo. Hautakuwa tena wakati wa kiumbe kujitambua. Huo ni wakati wa kila kimoja kupimwa kwa kilichoyafanya uhaini kwake. Tunaita “amali.”

Ni amali tu ya mja ndiyo itamtambulisha. Aliishi duniani kwa kuweka akiba au alijikalia tu akijinasibu yu karibu na manani kumbe afanya kufuru na ufisadi katika ardhi yake manani? Je, alifikiria itakavyokuwa kesho? Ni mtihani mkubwa kwetu viumbe.

Na ewe Mwenyeezi Mungu, tujaalie salama katika siku hiyo. Tuondolee mashakil yote na utusadikishe kupata pepo yako kwa wakati muafaka. Amin. Amin. Amin.

Kuna watu, viongozi watendaji katika serikali ya mapinduzi Zanzibar – wanagoma kubadilika. Wanataka kupigana na ukuta. Wanataka kufilisi wakati na kudhihaki wananchi na matumaini yao. Lakini wanachokifanya si kuuona mjiti wa saa unabadilika. Laa hasha. Wanataka mjiti ugande pale. Radhi yao watu wote wasiowapenda wafe baki peke yao. Eti ndipo watafaidi dunia!

Hakika, madhali siku hazigandi, kilicho dhahiri hapa ni kwamba wao – hawa watendaji serikalini – wasipobadilika na kwenda na wakati kwa kukubali yanayopita na kutendeka sasa, wataanguka kwa lazima.

Mtendaji mmoja katika taasisi mojawapo ya habari katika zile za serikali, alisikika akisema “Unamuona yule; ameiuza nchi yule. Ameiuza nchi yeye na Sefu.

Alimlenga Amani Abeid Karume ambaye alikuwa anampisha Dk. Shein kuchukua kijiti cha kuiongoza Zanzibar. Asemapo Sefu alimaanisha Maalim Seif Shariff Hamad, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) ambaye sasa ni Makamu wa Kwanza wa Rais.

Mtendaji huyu alikuwa kwenye jukwaa akishuhudia wageni wanawasili uwanja wa Amaan kwa ajili ya sherehe ya kumwapisha Dk. Shein, siku ya tatu ya Novemba.

Mtendaji kama huyu hayupo peke yake. Ana wenzake. wahafidhina maarufu ndani ya serikali. Kiilivyo watendaji kama yeye wanabanwa na sheria ya utumishi kutoshabikia siasa, lakini wanatamba hakuna wa kuwagusa maana wao ni CCM damdam.

Tatizo kubwa kwao ni kuamini bado wangali katika wakati uleule wa siasa za chuki, fitina na ubinafsi. Siasa za huyu katoka Unguja ni mwenzetu na yule Mpemba hana haki.

Wanaamini nafasi ya Mzanzibari kupambanuliwa kwa asili ya kule atokako haijafutika. Kwamba lipo kundi la wenye haki zaidi na Zanzibar bali kundi jingine ni la watu baki; watu wa kudharauliwa na kubezwa. Watu wa kunyimwa haki zao, hata zile za msingi zisizopaswa mtu kunyimwa.

Hawa ningefurahi wakaachwa nje ya wigo. Si vizuri kuwathibitisha kwenye nafasi walipo kiutendaji. Wasubiri muda wastaafu maana hawabadiliki. Mtumishi wa serikali, awe wa juu au katikati, asiyetaka kubadilika, asipewe nafasi ya kudanganya wengine. Asilani abadan. Aonyeshwe mlango wa kutokea.

Dk. Shein anapounda serikali, ni vema atambue kwamba wahafidhina hawafai kuwemo. Na akiwaweka kando atakuwa ametembea kwenye maneno yake. Ahadi ya kutoshirikiana na wapinga maridhiano. Mia fil mia.

Watu hawa wanaendelea kuzuga watu. Wanatumia udhaifu wa unyonge walionao watu wengi wa vijijini na kuwajenga chuki. Kuhamasisha wasijenge imani kwa serikali mpya ya umoja wa kitaifa. Waichukie. Eti ni serikali ya waarabu. Leo Dk. Shein naye mwarabu.

Walishasema Maalim Seif ni mwarabu. Wanajua huyu kwao ni Mtambwe, Kaskazini Pemba; basi tu kuzuga watu. Kijana mmoja wa Makunduchi alipofunga safari kwenda mjini siku ya uchaguzi, 31 Oktoba, alilazimishwa kubeba mwanawe anayelelewa na bibi yake. Kisa? Ati wahafidhina wamepakaza kule kwamba serikali ya umoja ikiwa chini ya Maalim Seif itaongozwa na Waarabu ambao meli zao mbili na vitu vyao zilishatia nanga bandari ya Malindi.

Haya, Maalim Seif si rais. Lakini hata sasa akiwa ni makamo wa kwanza wa rais, anaambiwa hana kazi ya kufanya pale Ikulu. Wanasema yupoyupo tu anasubiri kugawiwa kazi za kufanya na Dk. Shein.

Maalim Seif yupo Ikulu tena chini ya mabega ya Rais Dk. Shein. Ni msaidizi wake kwelikweli. Yupo tayari kumsaidia kazi ya kujenga Zanzibar mpya; Zanzibar ya maridhiano; Zanzibar inayotaka maendeleo na siyo hadithi mbovu, uzandiki na mawazo mgando kama wanayoyawaza wao.

Wakati nampa heko Dk. Shein kwa kutoka na jina la Balozi Seif Ali Idi kama makamo wake wa pili, akiaminika si mtu wa anasa na makundi, bali mtulivu, muadilifu na mchapa kazi, wananchi hawajali atachukua muda mrefu vipi kutaja baraza la mawaziri. Watu wanataka kimya kiwe na mshindo mkubwa utakaoadhirisha wanaopita na kujitia wameshapewa uwaziri.

Kwa kuwa Dk. Shein amechukua ahadi ya kutoshirikiana na asiyependa maridhiano yaliyojenga mwelekeo mpya wa Zanzibar, namsihi asitizame nyuma wala pembeni kumhofia yeyote. Ni jambo zuri kuthamini mchango wa mtu aliyetumika kabla, lakini lazima mtu mwenyewe awe msafi na anayeheshimika kwa watu anaowatumikia.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa haimfai mtu anayejinasibu kwa nchi wakati ana kashfa chungu nzima za ufisadi kwa yale aliyoyatenda chini ya mgongo wa serikali iliyompa madaraka kutumikia wananchi na washirika wao katika maendeleo.

Chanzo: MwanaHALISI, 17 Novemba 2010

One thought on “Rais Shein, usiwasikilize hawa”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.