Mwenyekiti wa MUWAZA, Dk. Yussuf Salim

MUWAZA inawapongeza kwa dhati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dk. Mohammed Ali Shein, Makamo wa Rais wa Kwanza Mheshimiwa. Maalim Seif Shariff Hamad na Makamo wa Rais wa Pili na Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi kwa kuweka mbele maslahi ya Zanzibar na kusahau siasa za chuki na uhasama baina ya vyama vyao viwili, kuleta maridhiano na kuteua Baraza la Uwiano la Mawazi la Serikali ya Umoja wa Kitaifa Serikali ambayo itafungua milango ya kheri kwa Zanzibar YA LEO NA YA KESHO

MUWAZA inaamini kwamba Serikali ya Umoja wa Kitaifa na Baraza lake la Mawaziri zitaingia katika vitabu vya historia na kukumbukwa milele na vizazi vya NCHI ya ZANZIBAR, kwamba ni kutokana na ujasiri wao ndipo Zanzibar kwa mara ya kwanza ikaacha kuwa mtumwa wa historia yake ya vurugu za kisiasa na uhasama usiokwisha.

MUWAZA inawapa pongezi wale Wazanzibari waliounga mkono Maridhiano na kuihakikishia Zanzibar na watu wake wanaweka mfano wa kihistoria wa kukubali kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Zanzibar leo baada ya maridhiano umeunda Baraza la Mawaziri ambalo litajenga imani na kuanza kuona mwanga wa matumaini wa Zanzibar ya kesho yenye ustawi, mapenzi na mshikamano,

MUWAZA inatoa HEKO kwa uundaji wa Baraza la Mawaziri ambalo litawaletea Wazanzibari wote nuru na haiba na kuifanya Zanzibar iwe kama kivutio kwa Wana wa Zanzibar walio ndani na nje ya visiwa hivi vyenye rutba na zawadi kemkem kwetu kutoka kwa Muumba.

MUWAZA inampongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dr. Mohammed Ali Shein kwa hotuba yake ya ufunguaji wa Baraza la Wawakilishi.

MUWAZA inampongeza Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Maalim Seif Shariff Hamad kwa matamshi yake ya kijananchi ya hivi majuzi ya kusisitiza kwamba Wazanzibari tusirudi tunakotoka.

MUWAZA inampongeza Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi kwa hotuba yake ya kutetea Mustakbal wa Zanzibar wakati wa kulifunga Baraza la Wawakilishi

MUWAZA inawapa hongera waheshimiwa Wawakilishi wote, wakiongozwa na Spika, Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho kwa kuchaguliwa kutetea maslah ya Zanzibar na kusahau tofauti zao za kisiasa katika kusimamia na kuelekeza Maridhiano ya kisiasa kwa mustakbal wa Zanzibar kwa jumla.

MUWAZA inawasisitiza Wabunge wa Zazibar walinde umoja wao bila ya kujali siasa za kichama na kuhakikisha wanasimama pamoja kulinda maslahi ya Zanzibar Bungeni.

MUWAZA inawapongeza vile vile Wazanzibari wote waliopiga kura ya kuichagua Serikali hii ya Umoja wa Kitaifa kwa madhumuni ya kuiendeleza Zanzibar na watu wake.

MUWAZA inasisitiza kutoka sasa kwamba kila Mzanzibari katika nafasi yoyote aliyonayo atumie Uzalendo wake kuwaunganisha Wazanzibari wote wachaguwe amani na mshikamano na kujitayarisha kuitumikia kwa dhati Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Asasi za kiraia pamoja na jumuiya za kidini ziwe mstari wa mbele katika kuendelea kuelimisha wananchi wenzao kwenda mbele bega kwa bega katika kuiimarisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa..

.MUWAZA inawashauri tena na tena viongozi wote wa kisiasa kuacha ushabiki na utashi wa kisiasa wa kibinafsi na kivyama na kuangalia mustakbal mwema wa Zanzibar.

.MUWAZA inapendekeza kwamba Baraza la Wawakilishi waisuke Katiba kwa maslahi ya kila Mzanzibari na mustakbal wa Zanzibar kwa jumla.

MUWAZA inatarajia kwamba Baraza la Mawaziri na Baraza la Wawakilishi yatahakikisha katika uendeshaji wa Serikali na utungaji wa Katiba kwamba siku za usoni Upigaji Kura utatumika kuchagua wajumbe na Serikali ya kiadilifu yenye kulinda na kutetea mustakbal wa nchi ya Zanzibar

MUWAZA inanasihi Baraza la Mawaziri na Baraza la Wawakilishi yaendelee na mtindo wa nia ya hivi sasa wa kulinda haki za kila Mzanzibari bila ya kujali itikadi ya aina yoyote

MUWAZA inawashauri Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Mheshimiwa Dr. Mohammed Ali Shein pamoja na Ma-Makamo wake wote wawili, Mheshimiwa Maalim Seif Shariff Hamad na Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi wazihakikishie Wizara kupata Watendaji wakuu kama Makatibu Wakuu, Wakurugenzi, Maafisa Wadhamini wanye sifa za kitaalamu za hali ya juu na wenye uzoefu uliobobeya ili kuleta maendeleo ya sifa bora na ya haraka kwa Zanzibar.

Vile vile MUWAZA inaiomba Serikali itumiwe vilivyo hazina kubwa ya wataalam Wakizanzibari walio nje ya nchi katika kuijenga nchi yao.

Ni matarajio ya MUWAZA kwamba vyama vyote vya siasa vitawashajiisha Wataalamu wa Kizanzibari wajiunge katika harakati za kisiasa ili Zanzibar ipate Wawakilishi wa Kitaalam katika jukumu la kuijenga Zanzibari siku za mbele..

MUWAZA INATOA HONGERA TENA KWA WAZANZIBARI WOTE KWA KUICHAGUA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA MUWAZA INAWANASIHI WAZANZIBARI WOTE WALIO NJE YA ZANZIBAR WAWE TAYARI KUITUMIKIA ZANZIBAR KWA NJIA YEYOTE NA KUJITAYARISHA KURUDI ZANZIBAR KUTUMIKIA NCHI

MUNGU IBARIKI ZANZIBAR NA WATU WAKE
AMIIN
EID MUBARAK
DR. YUSSUF S. SALIM
MWENYEKITI WA MUWAZA
15.11.20

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.