Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad

Mapema jana, Maalim Seif alijitokeza kupiga kura katika kituo cha Mtoni Mtopepo na kusema hakutegemea vitendo vya uvunjaji sheria za uchaguzi kujitokeza katika uchaguzi huo wa marudio.

Alieleza kwamba tayari amesikia kuna watu wanajaribu kuvuruga sheria za uchaguzi, vitendo ambavyo alisema havikupaswa kufumbiwa macho kwa sababu vinaweza kurudisha nyuma hali ya amani na utulivu iliyopo
Zanzibar.

“Sikutegemea wakati kama huu turudi nyuma, watu waachane na vitendo hivyo,” alisema Maalim Seif wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupiga kura.

Mgombea ubunge wa CUF katika jimbo la Mtoni, Faki Haji Makame, alisema lilijitokeza tatizo kubwa la kupandikizwa wapiga kura hasa katika kituo cha Mtoni Kigomani, kitendo ambacho alisema ni kinyume cha sheria.

Alisema majira ya saa 7:00 usiku wa kuamkia jana, yalionekana magari yakipeleka watu katika kituo hicho wakisindikizwa na askari wa Kikosi cha Valantia.

Alieleza kwamba yeye mwenyewe akiwa pamoja na Mwakilishi wa jimbo hilo, Nassor Mazrui, alishuhudia wapiga kura hao hewa wakiingizwa kituoni hapo na ndio waliokuwa wa kwanza kupiga kura.

“Uchaguzi huu una tofauti kubwa na uliopita, watu wasiokuwa na sifa wanaletwa katika vituo na wanasindikizwa na askari,” alisema mgombea huyo.

Mgombea ubunge kupitia CCM katika jimbo hilo, Ussi Ame, alisema uchaguzi katika jimbo hilo umekwenda vizuri isipokuwa kuna tatizo kwa baadhi ya wanachama wa CUF kuwazuia watu kwenda kupiga kura katika vituo.

Alisema kwa mujibu wa sheria, wananchi baada ya kupiga kura wanatakiwa kukaa umbali wa mita 200 kutoka kwenye kituo, lakini kwa bahati mbaya walikuwa wakipiga kura na baadaye kuzunguka katika vituo kuwahoji vitambulisho vya kupigia kura watu waliokuwa wakielekea katika vituo.

“Wananchi wengi wanashindwa kufika katika vituo kwa vile kuna watu wamekuwa wakiwataka waonyeshe shahada za wapiga kura wakati wao si tume wala wakala wa vyama vya siasa,” alisema mgombea huyo.

Alisema yeye aliamua kuripoti tatizo hilo Polisi, lakini alijibiwa
kuwa jukumu la askari ni kuhakikisha usalama katika maeneo ya vituo na sio maeneo ya nje ya vituo vya kura.

Katika hatua nyingine, mtu mmoja, Faki Ali Bakar (42), mkazi wa Magogoni amejeruhiwa kwa kupigwa mapanga na watu watatu wanashikiliwa na Polisi katika kituo cha Mwanakwerekwe kwa tuhuma za kutaka kupiga kura wakiwa na shahada zisizokuwa zao.

Faki amelazwa katika Hospitali ya Al-Rahama akiwa na majeraha ya kichwani na shingoni huko katika eneo la Mtoni baada ya kuvamiwa na watu waliokuwa katika magari yasiyopungua manne yaliyokuwa yameegeshwa.

Alisema watu hao wasiopungua 50 walimvamia alipokuwa na wenzake majira ya usiku akiwa katika ulinzi wa Polisi jamii.

Alieleza kwamba ana wasiwasi watu waliomvamia ni vijana wapiga kura wasiokuwa na sifa waliokuwa wakielekea katika vituo vya kura katika jimbo la Mtoni.

Watu watatu waliokamatwa na Polisi walikamatwa katika kituo cha kupigia kura Mwana kwerekwe B na baadaye walichukuliwa na Polisi hadi kituo cha Mwanakwerekwe ambapo hadi mchana walikuwa wakishikiliwa na kituoni hapo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Aziz Juma, alisema Polisi wamelazimika kuimarisha ulinzi katika vituo vya upigaji kura, ikiwemo askari wa FFU kuhakikisha usalama wa raia unakuwepo katika maeneo hayo.

Alieleza kwamba wamepokea taarifa za mtu mmoja kupigwa mapanga na Polisi inafuatilia tukio hilo, lakini alisema hadi jana mchana shughuli ya upigaji kura vituoni ilikuwa ikiendelea vizuri huku ulinzi ukiwa umeimarishwa.

NIPASHE ilishuhudia askari wa FFU katika kituo cha Shule ya Mtopepo wakiwataka wananchi waondoe mikusanyiko karibu na vituo vya kupigia kura.

Watu 9,671 wameandikishwa kuwa wapiga kura katika Jimbo la Mtoni wakati katika Jimbo la Mwanakwerekwe walioandikishwa ni 8,061. Katika Jimbo la Magogoni wapiga kura walioandikishwa ni 10,155 na Jimbo la Wete Pemba walioandikishwa ni 8,421.

Na Mwinyi Sadallah, Nipashe, 14 Novemba 2010

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.