Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein (kulia) akimuapisha Makamo wake wa Pili, Balozi Seif

Na Janbir Idrissa, MwanaHALISI, 10 Novemba 2010

AMANI imeimarika Zanzibar kuliko ilivyokuwa kabla ya uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 31 Oktoba, 2010. Watu walikuwa na hofu kwamba utulivu uliokuwepo usingeendelea hasa baada ya dalili za awali kuoonyesha mgombea wa upinzani alikuwa anaelekea kunyakua ushindi mkubwa.

Maalim Seif Shariff Hamad aliyegombea kiti hicho kwa mara ya nne mfululizo na mara zote tatu akishindwa na kudai amedhulumiwa ushindi, alishangaza umma safari hii alipokubali matokeo ya mwisho yaliyompa ushindi mshindani wake, Dk. Mohamed Ali Shein, licha ya kwamba alikuwa na ushindi mkononi wa zaidi ya asilimia 60.

Ushindi wa Maalim Seif ulikuwa dhahiri mapema usiku wa manane wa siku ya uchaguzi pale kura za vituoni zilipokuwa zimetoka na ukabaki hivyo kwa saa kadhaa siku ya pili. Lakini matokeo ya kura ya urais yalikuwa yakibadilika kadiri yalivyokuwa yakitangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Khatib Mwinyichande.

Hapana shaka kimya kilichokuwepo hakikumfurahisha mtu yeyote aliyekuwa akitaraji uchaguzi huru, wa haki na ulioendeshwa katika misingi ya uwazi. Uthibitisho wa hilo ni ripoti za awali za waangalizi wa uchaguzi kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Kwa mfano, waangalizi waliotokana na kundi la TEMCO na lile la Umoja wa Ulaya walisema hakukuwa na uwazi kwenye hatua muhimu ya uchaguzi ya majumuisho ya kura.

Ulaya wamesema wameshangazwa kuzuiwa dakika za mwisho kushuhudia ujumuishaji matokeo, kinyume na makubaliano na Tume ya Uchaguzi kwamba wangeshiriki.

Baada ya Dk. Shein kutangazwa mshindi kwa kupata asilimia 50.1 ya kura halali, Maalim Seif ambaye alikwishatuliza wafuasi wake waliofika nje ya kituo cha kutangazia matokeo kushinikiza tume itangaze matokeo ya haki kwenye Hoteli ya Bwawani, alishika jukwaa na kumpongeza mshindi huku akiahidi kushirikiana naye kikamilifu.

Uamuzi wake huo ulibadilisha upepo. Ulichangamsha ukumbi. Uliamsha shangwe kubwa na vigelegele na kutia nuru matumaini kwamba maridhiano yataendelea kusimama kwa kuwa hakutakuwa na mgogoro wa kisiasa kama ilivyokuwa 1995, 2000 na 2005 baada ya uchaguzi pale yeye na chama chake walipoyakataa matokeo.

Sasa hatua za uundaji serikali mpya zimeanza. Tayari Dk. Shein ameteua mwanasheria mkuu wa serikali. Omar Othman Makungu ni mwanasheria wa siku nyingi aliyefikia kuwa jaji wa mahakama kuu.

Alikuwa makamu mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kabla ya hapo, alikuwa naibu mwanasheria mkuu wa Zanzibar kwa muda mrefu akiwa chini ya Idi Pandu Hassan ambaye anamaliza akiwa mgonjwa wa sukari.

Shauku kubwa waliyonayo wananchi ni kumtambua mtu atakayekuwa Makamu wa Pili wa Rais. Huyu kikatiba anatakiwa kutoka CCM na ni lazima awe mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa kuwa atakuwa kiongozi mkuu wa shughuli za serikali katika baraza hilo.

Uteuzi unatarajiwa kufanywa wakati wowote na Rais wa Zanzibar na juzi aliteua wajumbe wanane kuingia katika Baraza la Wawakilishi wakiwemo wawili kutoka CUF.

Wajumbe sita kutoka CCM ni Omar Yussuf Mzee, aliyekuwa mbunge wa Kiembesamaki na naibu waziri wa fedha na uchumi katika serikali ya Muungano; Mohamed Aboud Mohamed, aliyekuwa mbunge wa kuteuliwa na rais wa Tanzania na naibu waziri wa Afrika Mashariki; Balozi Seif Ali Idi, mbunge wa Kitope na aliyekuwa naibu waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa.

Wengine ni Zainab Omar Mohamed, aliyekuwa mwakilishi; Ramadhan Abdalla Shaaban, aliyekuwa mwakilishi wa kuteuliwa na waziri wa nchi, katiba na utawala bora, na Dk. H. Ubwa Mamboya, daktari wa binadamu katika hospitali kuu ya Mnazimmoja.

Wajumbe wawili kutoka CUF ni Juma Duni, naibu katibu mkuu wa chama na aliyekuwa mgombea mwenza wa Profesa Ibrahim Lipumba katika uchaguzi wa urais wa Jamhuri ya Muungano. Mwingine ni Fatma Ferej, aliyekuwa mwakilishi wa Mji Mkongwe na mbunge kupitia Baraza la Wawakilishi.

Haieleweki iwapo Dk. Shein atateua makamu wa pili kutoka wajumbe hao sita wa CCM au atachota kutoka wajumbe waliochaguliwa majimboni. Majina makubwa yamekuwa yakitajwa yakiwemo yaliyomo kwa aliowateua wajumbe tayari. Mzee, Balozi Seif na Abdalla ni miongoni mwao.

Bali uteuzi wake utakuwa kipimo kizuri cha wananchi kujua hatima ya maridhiano kwa kuwa ndani ya CCM wapo wanasiasa wanaopinga waziwazi maridhiano.

Ingawa yaliidhinishwa na wananchi kwa asilimia 66.4 kupitia kura ya maoni iliyopigwa 31 Julai, mwaka huu, maridhiano hayo yamekuwa asali chungu kwa makada wengi ndani ya CCM. Baadhi yao walihamasisha kwa siri kura ya HAPANA.

Kampeni yao ilileta majibu kwenye majimbo yao kwani maridhiano yalikataliwa kwa zaidi ya asilimia 70. Majimbo haya ni Makunduchi atokako Shamsi Vuai Nahodha aliyekuwa waziri kiongozi, Pandu Ameir Kificho, aliyekuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi, Haroun Ali Suleiman, aliyekuwa waziri wa elimu na mafunzo ya amali na Samia Suluhu Hassan aliyekuwa waziri wa biashara, uwekezaji na utalii.

Majimbo mengine ni Kitope atokako Balozi Seif, Uzini atokako Muhammed Seif Khatib, mbunge na aliyekuwa waziri wa nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais wa Tanzania
(Muungano), na jimbo la Donge atokako Ali Juma Shamhuna, aliyekuwa mwakilishi, waziri wa habari na naibu waziri kiongozi wa Zanzibar.

Maridhiano yaliasisiwa na rais aliyeondoka madarakani baada ya kumaliza muda wake wa kikatiba wiki iliyopita, Amani Abeid Karume, na Katibu Mkuu wa Chama cha
Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad.

Ili maridhiano haya yaendelezwe na kuletea wananchi wa Unguja na Pemba matumaini ya ujenzi wa Zanzibar mpya, lazima kiongozi mkuu wa serikali katika Baraza la
Wawakilishi awe mtu ambaye ndani ya moyo wake anayaamini hasa maridhiano na kwamba hiyo ndiyo njia mwafaka ya kuihakikishia nchi mustakbali mwema.

Dk. Shein anatakiwa kuteua mtu anayeamini kuwa maridhiano yameleta uimara katika amani, utulivu na umoja wa kitaifa na kwamba yanapaswa kulindwa kwa nguvu zote.

Kwamba ni maridhiano hayo yaliyomsukuma Maalim Seif na CUF kukubali matokeo yaliyotangazwa na Tume na kutoa hotuba iliyovutia wengi ikiwa na malalamiko ya uvurugaji uchaguzi.

Haitarajiwi hata kidogo Dk. Shein aje na jina la mhafidhina wakiwemo wale wenye rekodi ya kufanya uhuni katika siasa pale kulipokuwa na mwafaka kati ya CCM na CUF. Watu bado wanakumbuka namna Shamhuna alivyopindua bango la muafaka wa mwaka 2001 na wanajua Nahodha alivyoshindwa kumsaidia Rais Karume kupitisha kura ya NDIYO.

Zanzibar inahitaji kiongozi anayejali umoja wa kitaifa na yule atakayetambua wajibu wake wa kumshauri vizuri Dk. Shein katika mwelekeo huohuo wa kujenga umoja na mshikamano kwa wananchi huku akishajiisha maendeleo ya jamii na uchumi.

Anahitajika makamu wa pili atakayekuwa anathamini haki na wajibu wa CUF katika serikali ya umoja wa kitaifa itakayoundwa. Kwamba anajua ushirikiano kamili wa viongozi wa vyama hivi ni matakwa ya Waanzibari na siyo ya kibinafsi.

Anatakiwa kiongozi aliye tayari kuonyesha ukomavu wa kisiasa na kusimama madhubuti kuongoza chini ya misingi ya ukweli, uwazi, uadilifu, utawala bora na utawala wa sheria. Atambue kwamba huu sasa si wakati wa siasa za chuki na ubinafsi bali siasa njema za kusaidia ujenzi wa Zanzibar mpya.

Anahitajika kiongozi ambaye ataunganisha wawakilishi wa wananchi kwenye baraza la wawakilishi kwa kusimamia haki na sheria wakati wa mijadala. Na hakika anatakiwa kuwa kiongozi mvumilivu na mwenye busara na hekima kwa viongozi wenzake, walio chini yake na wananchi.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.