Saa 1:45 usiku. Kituo kikuu cha treni Hamburg. Treni ya kwenda Bonn inafika. Ilikuwa ifike saa 1:46; lakini imewahi kwa dakika moja. Hifadhi hiyo: imewahi, haikuchelewa. Wajerumani wenyewe wanajisifu kwamba ni pünktlich – wanaofuata wakati. Dakika moja ni nyingi na dakika tano hazivumilikii. Sharti moja la kuishi hapa ni kupoteza uhuru wako wa kuutumia wakati na kujikubalisha uwe mtumwa na wakati. Saa yako anakuwa ndiye bwana wako. Akuamshe, akuhimize, akuongoze, akukimbize. Huo ndio uhuru wa Ulaya.

Baina ya Hamburg na Bonn ni kilomita zikaribiazo 600, lakini treni itachukuwa masaa 4 na dakika 20. Ndani ya treni, nitakaa kiti chochote chenye alama iliyoandikwa bahn.comfort. Viti hivi ndivyo vya akina miye, pata-sote, lakini wala usivifananishe na viti vya mabasi yetu yatokayo Darajani kwenda Michamvi au vya daladala za Bububu ziendazo kwangu Mwanyanya. Hii ni alama nyengine ya uhuru wa Ulaya.

Ndani ya usafiri wa umma, Ulaya

Lakini kuna alama nyengine ya uhuru huu: Wenyeji wangu walinikatia tiketi ya usafiri huu kwa Euro 152, ni takriban shilingi 300,000 za Tanzania (hili la kulinganisha thamani ya fedha ni ugonjwa wa kwanza tunaougua wageni hapa; nami nimeshaambukizwa). Kazi ya kutafsiri kurasa 12 za Kijerumani kwa Kiswahili imenichukua masaa 12 kwa malipo ya Euro 300. Fedha hizi silipwi taslim wala sipewi mkononi. Zinaingizwa kwenye akaunti yangu kupitia mtandao wa kompyuta na mtumaji anapaswa kueleza sababu ya kunitumia pesa. Si kwa kuwa ni nyingi, ila ndivyo utaratibu ulivyo. Kwa kuwa haya ni malipo ya kazi nami naishi hapa kwa kibali, basi ninakatwa kodi kwa chochote nizalishacho. Asilimia 19 kwa serikali, 5 kwa benki. Jumla wanachukuwa Euro 72, yaani shilingi 144,000. Akaunti yangu itapokea kilichobakia, ambacho nacho kila nitakapochomoa kumi, moja itakwenda kwenye kasha la benki.

Ninachokwambia ni kwamba, uhuru huu wa kukaa kwenye bahn.comfort una gharama zake. Zigo la kodi linalovunja mgongo. Wiki niliyofika hapa, nikapewa hiyo hesabu ya makato nitayokatwa, basi hapo hapo niliwapigia simu jamaa zangu wa nyumbani waje wanipokee uwanja wa ndege wiki inayofuata! Kodi ya mshahara, mfuko wa huduma za jamii, pensheni, kodi ya kupoteza ajira, bima ya afya, kodi ya nyumba, tiketi ya basi. Mwisho kinachobakia ni robo, ambacho ndio cha kula, cha kunywa, cha kuosha nguo, cha kuwasiliana, na cha mengineyo. Huzimii?

Sura ya makato ya kodi nchini Ujerumani

Ndio maana ninapokaa hapa kwenye comfort.bahn na kutoa kompyuta yangu kuandika kumbukumbu hizi, sijioni mgeni wala mkando. Sijioni Mjerumani, lakini pia sijisikii kuwa nimetendewa fadhila kuwepo hapa. Kila kilichopo hapa nimekilipia kwa jasho, nguvu na pumzi yangu. Kwa gharama ya kuwaacha mama zangu wawili watu wazima na nchi yangu tukufu ya Zanzibar, kuja huku kuutafuta uhuru wa Ulaya.

Nitakwambia uhuru mwengine. Mwanzo nilikuwa nimepanda treni nyengine ya kunifikisha hapa stendi kuu. Kama ulivyo usafiri mwengine wa umma, treni hii nayo ilikuwa safi kwa kila maana ya neno. Mwalimu wangu, Kijackson, pale sekondari ya Utaani kisiwani Pemba, alinifundisha kwamba usafi ni kitu kukaa mahala pake. Mwalimu Hamad Bakari Mshindo pale Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni akaja akaniongeza fasili nyengine ya usafi: akanambia usafi ni nidhamu. Humu kwenye treni, muna maana zote hizo mbili. Allah awazidishie baraka walimu wangu hawa.

Ile treni haikuwa na abiria wengi. Viti vingi vilikuwa na mtu mmoja mmoja tu, ilhali vimetengenezwa kwa watu wawili. Kutoka kituo hicho mpaka kwenye kituo kikuu cha treni ni vituo vinane, na kila kituo treni ilichukuwa watu, lakini kila aliyeingia alisimama na sio kukaa kwenye vile viti vitupu vyenye mtu mmoja mmoja. Tafsiri hapa ni mbili: moja, hakuna anayetaka kuubughudhi uhuru wa mwenzake wa kufaidi kitu kikubwa na chote peke yake na, mbili, hakuna aliye tayari kuugawa uhuru huu na mwenziwe. Wengi wa waliotangulia wamekaa viti vya mwanzo na sio vya dirishani, kama wanamwambia anayeingia kwamba: “Hapa pote pangu peke yangu”.

Ndani ya usafiri wa umma nyumbani. Tunaiita daladala

Jengine, kwenye usafiri wa umma hapa, uhuru unamaanisha pia ukimya wa kutisha. Kama mtu hasomi gazeti au kitabu, basi anabonyeza simu yake anachati na au kajinyamazia tu, anazungumza na uliwemwengu wake kimoyomoyo. Huo ndio uhuru wa Ulaya.

Nikipanda humu, siachi kuukumbuka usafiri kama huu huko kwetu namna ulivyo hai na halisi. Rusha roho kutoka DJ Dereva. Makelele kutoka kwa MC Konda. Hadithi za kuchekesha au kuliza kutoka kwa abiria. Kila safari moja kwenye usafiri kama huu huko nyumbani, ni mithali ya filamu nzima ya sinema. Kwetu, usafiri wa umma sio tu kwamba ni chombo cha kukufikisha uendako, bali pia ni chombo cha mawasiliano: ni kitu hai chenye sauti, pumzi na nishati. Na huu kwetu ndio uhuru.

Lakini kwenye usafiri wa umma hapa Ulaya, muna kila alama ya mauti. Muna kukatika kwa mkufu wa kawaida wa mawasiliano ya kibinaadamu. Ni kama vile umepanda jeneza lenye maiti wengi. Ukimya ndio unaotawala. Alama ya watu wasiopenda kujihusisha wala kuhusiana na wengine. Ni kama kila mtu anakwambia: “Tafadhali tusiulizane. Hunijuwi, sikujuwi!”

Basi nitajizuiaje kuikumbuka daladala ya Fuoni, nyimbo ya Bi Kidude “Muhogo wa Jang’ombe”, special dedication kutoka kwa DJ Dereva, kelele za MC konda ambaye kila kituo atasimama kutafuta na kusubiri abiria bila ya kujali kama waliomo ndani wanachelewa huko waendako, miguno ya kugugumia machungu ya kukanyagana na vicheko vya hadithi usizozijua zilipoanzia wala zitakapoishia? Nina moyo gani wa kuyazuia machozi yasiroweshe mashavu yangu?

Guido Westerwelle (kulia) na Michael Mrotz. Wanandoa wapya wakielekea kwenye fungate yao

Nitakupa uhuru mwengine wa Ulaya. Wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa hapa Ujerumani, Guido Westerwelle, alifunga ndoa na mpenzi wake wa zamani, Michael Mrotz. Linalouelezea uhuru wa huku hapa si la kufunga ndoa, bali ukweli kwamba hawa wote ni wanaume. Kabla hujamaliza kushangaa, nitakwambia na la meya wa zamani wa Hamburg, mzee wa kiume wa zaidi ya 50 mwenye mchumba wa kiume wa miaka 19. Huo ndio uhuru wa Ulaya. Wa kuamua, kufanya na kujitangaza na kisha ukalindwa na sheria. Haidhuru kama jambo hilo ni kinyume na imani, maumbile au ubinaadamu. Mahala hasa pa ule msemo wa bezo kule kwetu: “hunilishi hunivishi, wanitakiani” ni huku. Maana huko kwetu, kusema hivi ni alama ya uasi kwa mfumo wa kitamaduni na kijamii, huku ni alama ya uhuru na ustaarabu. Uhuru wa Ulaya!

Lakini uhuru huu hauishii hapa. Unakwenda mbele zaidi. Wenyeji wangu niliowaendea Hamburg, hawakuweza kuja kunipokea, maana nao pia walikuwa wako njiani kutoka Berlin kulikokuwa na maandamano ya kitafa dhidi ya mpango wa Ujerumani kurefusha muda wa kuendelea kutumia vinu vyake vya nyuklia kuzalisha nishati. Ujerumani, kama zilivyo nchi nyengine za viwanda, ina mahitaji makubwa ya nishati, lakini waandamanaji wanaitaka serikali yao kutumia vyanzo vyengine vya nishati na sio nyuklia.

Maandamano ya kupinga nyuklia jijini Berlin, Ujerumani

Zaidi ya wiki moja nyuma, mabango yaliwekwa kila kona kuyatangaza maandamano haya. Hatimaye, umma ukakusanyika katika mji mkuu wa Berlin kuiambia serikali kwamba: “Sisi hatutaki nyuklia”. Maandamano yakamalizika bila ya mtu kupigwa risasi wala kigongo na polisi. Huo ndio uhuru wa Ulaya.

Hili likanikumbusha maandamano ya Januari 2001, ambayo yalimalizika kwa vifo, mateso na chuki ambazo kama si Maridhiano ya karibuni kati ya vyama viwili vya siasa huko kwetu, basi katika nyakati kama hizi za harakati za uchaguzi tungekuwa tunazungumzia adhara nyengine kwa heshima ya nchi yetu.

Basi, uhuru huu wa Ulaya – wa kuihoji na kuikosoa serikali – natamani nami niwe nao. Siku nikiondoka hapa, iwe zawadi ya kuifunga na kuiweka begini na nikishuka uwanja wa ndege niigawe kwa kila nimkutaye. Lakini uhuru huu tu!

Polisi wa kwetu wakiyashughulikia maandamano ya Januari 2001

Sio ule uhuru unaonila machango kila nikianda mafunzoni na kurudi mule kwenye jumba la wanafunzi ninalokaa. Humu tunaishi umayamaya wa watu, wengi wa aina yangu – wageni na wanafunzi. Lakini huu ni mwezi unakatika, siwajui majirani zangu wala wao hawanijui. Hata tunapokutana kwenye lifti, huwa hapana salamu baina yetu. Ninapojaribu kujichekesha na kutikisa kichwa kwa ishara ya kuwasalimia, huwakuta wanashangaa mshangao usiokuwa na mwisho kama masanamu. Huu nauita uhuru wa kununa. Ila hawa si Wajerumani, ni Waafrika, Waarabu na wageni wengine, lakini wamekuwa Wajerumani kuliko Wajerumani wenyewe!

Ama uhuru huu mimi siuwezi. Kwetu nitokako kucheka ni sehemu ya uhai. Nitaishi vipi bila kucheka mja miye? Lakini ili nicheke, lazima sio tu niwe na la kunichekesha, bali pia niwe na wa kucheka naye. Nikijichekesha peke yangu, ili nijipe raha nizikosazo hapa, naogopa kuonekana chizi, ingawa uhuru wa kuwa chizi hapa pia upo.

Ngoma ya asili kutoka Kaskazini Pemba, Msewe

Nakumbuka kisa cha kaka yangu, Seif Hamad wa Shengejuu. Katika miaka ya 1970 alikuwa anauza duka jijini Dar es Salaam. Kuna siku Radio Tanzania Dar es Salaam, katika kipindi chake cha Ngoma Zetu, ikapiga msewe. Akiwa amekaa siku nyingi hajapata kuusikia wala kuucheza msewe, Seif hakuweza kujizuia. Akawaacha wateja dukani, akashuka uwanjani, akaanza kuusakata. Kidogo bosi wake akatokezea. Anaona dukani pamejaa wateja lakini badala ya kununua bidhaa wanafaidi sinema ya bure. Muuza duka yupo uwanjani anadimka. Akamuuliza kwa hasira: “Seif, hivi ndio unafanya nini?“ Naye akamjibu kwa kumuuliza: “Aka, kake, wataka n’fuge ugonjwa na dawa ipo?“ Basi kwa nini nisimwage machozi nikikumbuka kwakwakwa za nyumbani?

7 thoughts on “Uhuru wa Ulaya: Kwa nini nisiliye?”

 1. huo ni ustarabu wa kwao ni sisi lazima tuwe na utaratibu wa kwetu. usilinganishe ustarabu wa kagera na chokocho au sumbawanga. kijana tahadhari, lakini Allah atakulipa kwa ulilokusudia. unababaika na vitu vidogooooooooooo vya uhaibuni, fanya kazi ulioendea broooooo. kama maridhiano hatukusimamiwa na hao na wala wao hawajafika hatua hii, ujue kila watu wana utamaduni wao.

 2. Umesahau mambo mengine mawili kwenye uhuru wa Ulaya, Khelef. Moja ni uhuru wa kuwa mnafiki. Na huu ni uhuru walionao ndugu zetu wa kike na kiume wanaotoka nyumbani Zanzibar kuja hapa Ulaya. Kwa mfano, wakati wanawake wakiwa huko nyumbani wanajitanda hijabu au shungi zao vizuri, wakifika hapa Ulaya huzivua airport na hawazivai tena mpaka waende kwao. Huo ni unafiki. Wanaume ambao huko hawanywi ulevi wala hawakosi kipindi cha sala, hapa wanafanya yote. Wanakunywa ulevi na hawasali kabisa. Waulize kuchukuliana wake zao. La pili, huku Ulaya pia kuna uhuru wa kuiona kodi unayolipia ikifanyiwa kazi na serikali. Wanajenga miundombinu na huduma nzuri. Sio kama kwetu ambako serikali zinakusanya kodi kubwa lakini zinaishia matumboni mwa viongozi na familia zao.

 3. Asante kwa khabari yako nzuri ambayo kwa jinsi ulivyo ipangilia imenipa picha ya misha ya maisha ya ulaya na uhuru wao, isjuwi uhuru huo wanaufurahia kweli au ndio wamerithi nao wanaendeleza tu1.

 4. Nimefuatilia vizuri makala yako na nimevutiwa na namna unavyojaribu kutuonyesha jinsi tunavyotofautiana miongoni mwa jamii za ulaya na zile za Africa na hata za Africa zenyewe binafsi, yote hayo ni sehemu tu ya mafunzo na kukuza uzoefu katika kuuelewa utamaduni na silka za walimwengu.
  Wakati mwengine ni vigumu kupambana ila ujasiri ni lazima, na hapa tunajifunza kua kumbe hata ulaya kuna mengi si mazuri kama yalivyo huku kwetu mbali na muamala wa kiuchumi bali nasi kumbe tuna cha kujivunia ingawaje wapo wataohoji kipi kama uchumi wetu ndio hivyo.
  Yote kwa yote kaza moyo ndio mtirirko wa maisha ya kila siku, hongera na endelea kutufahamisha yajirio kihalisia huko ..

 5. Assalaamu Alaykum Al-Habiib !
  Wengine watashangaa ila siwezi kuuficha ukaribu wetu kaka yangu popote niwapo au niwapo… na huu ni utamaduni wetu mzuri.

  Binafsi yangu niliulizwa suali na wenyeji wangu nilipo tembelea Hispania mnamo mwaka 2008, wakati wakinikaguza majengo marefu, na viunga vya jiji la Barcelona.
  SUALI LILIKUWA:
  JE VIPI KAMA IKITOKEA WANIOMBE NIBAKIE PALE KWA MAISHA YANGU YOTE NA NIHAME AFRIKA NIKO TAYARI?

  JAWABU langu halikugegesa, ila nilisema “hapana” na kuweka bayana kwamba siku zilizobaki zinahisabika ila kiu yangu ya Afrika haikufichika.

  Sababu ni nyingi ila la msingi sikuona misingi ya furaha ile iliyojengeka huku kwetu. Wao wanamaendeleo, miundo mbinu sanifu, burudani nyingi, uhuru wa kupita mipaka na mengi kama ulivyo ieleza. Ila kamwe hawana Upendo, huruma wala furaha za Kweli. Maana kila kitu ni gharama. Shabuka zote za mawasiliano ila hawana tuka za moyo…nafsi zaenda mbio na wasiwasi. hakuna Tabasam na Kuridhika kamwe… kila mtu analalamikia kodi, hasra, gharama. Huo ndio utamaduni wao si mgeni wala mwenyeji.. na hii kaka ndiyo lugha yako(na wewe kwa sasa). kinyume na kwetu FURAHA waweza pata buree… kwerekwe hata barabarani watu watipuka kwenye magari, tukishiba mihogo kazi kuyataja Masharubu na Madevu tukiyananga tukichekaa mpaka tukome…! Furaha tunajipa wenyewe tusipopewa. Haya husahaulisha maumivu na kusema InshaaAllahu tungojee kesho na matumaini mema.

  Kaka cha msingi Unalijua ulilolieendea, pole sana stahmili na muda utafika utarudi nyumbani.. Huku maisha ni ya kawaida sana na InshaAllah utayakuta. Ila NAAMII UHURU MWINGINE AAH… UTAKUWA UMEKUKUNA… TAFADHALI TWAMBIE USICHOKE KUTUKHABARISHA WALA USIVUNJIKE MOYO… NAJUA MENGINE MENGI YANABAKI MAZURI….

 6. @Khatib. Ahsante mpenzi wangu kwa mchango wako ninaouthamini sana. Wasioutujuwa mimi nawe tulivyo, watashangaa wakisikia nakwambia NAKUPENDA. Watajiuliza, aka vipi, haya si ndiyo hayo ya uhuru wa Ulaya? Lakini kama ulivyo uhuru, mapenzi nayo yana mbeya nyingi. Yetu miye nawe ni mbeya moja kati ya hizo, wala si ya Westerwelle na mume-mke wake, Mrotz. Najitahidi kujikubalisha kuukubali ukweli kwamba haya ndiyo maisha ya hapa na kwamba nami nimekuja kujifunza kheri inayopatikana kwa maisha haya.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.