Na Joseph Mihangwa

KATIKA sehemu ya pili ya makala haya, tuliona jinsi wazo la awali la kuunda Shirikisho la Tanganyika na Zanzibar, lenye Serikali tatu, lilivyopotoshwa baadaye, licha ya Muundo huo wa Muungano kufafanuliwa vyema katika Mkataba [Hati] wa Muungano [Articles of Union] na Sheria za Muungano [Acts of Union] za mwaka 1964 zilizosimika Muungano huo.

Tuliona jinsi Rais wa Jamhuri ya Muungano alivyojivika taji la kuwa pia Rais wa Jamhuri ya Tanganyika, na hatimaye Tanganyika kuwa ndiyo Tanzania, wakati Zanzibar iliendelea kubakia kama Zanzibar [kama nchi] yenye mipaka na dola inayojulikana na kutambuliwa.

Nini kilichosababisha upotoshaji huo wa muundo na ukiukaji wa Mkataba wa Muungano? Kwa nini hali hiyo imeachwa kuendelea hadi leo? Je, kwa Zanzibar kujitangaza kuwa nchi, imekiuka Katiba au kuasi Muungano? Kupata majibu, tuendelee na sehemu hii ya tatu na ya mwisho.

Muungano wa Tanzania ulibuniwa na kutekelezwa kwa njia ya dharura kiasi kwamba hapakuwa na muda wa kutosha kuweza kuandaa Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Kwa sababu hiyo, Katiba ya Jamhuri ya Tanganyika ndiyo iliyotumika pia kama Katiba ya Muungano kwa makubaliano, lakini kwa kufanyiwa marekebisho kwa njia ya Amri [Decree] ya Rais.

Amri hiyo ya kuifanyia marekebisho Katiba ya Jamhuri ya Tanganyika kuwa pia Katiba ya Jamhuri ya Muungano ilitolewa kama Tangazo la Serikali [G/N] Namba 245 la 1/5/1964, kwa kuingiza mambo yote kumi na moja yaliyokubaliwa chini ya Mkataba wa Muungano na mgawo wa madaraka ndani ya Muungano, kwa mujibu wa makubaliano hayo, kama yalivyoridhiwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi Zanzibari, na kujulikana kama Sheria za Muungano [Acts of Union] kwa utekelezaji.

Ni sharti Kuu la Sheria za Kimataifa kwamba, ili Mkataba wowote kati ya nchi na nchi uweze kupata nguvu ya Kisheria na kuheshimiwa kwa utekelezaji, lazima kwanza uridhiwe [to ratify] na vyombo vya kutunga Sheria vya nchi husika kwa njia ya Sheria [Acts] za nchi hizo.

Amri hii ilibadili jina la Katiba ya Jamhuri ya Tanganyika na kujulikana kama “Katiba ya Muda ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 1969; kwa matarajio kwamba Jamhuri ya Muungano nayo ingepata katiba yake ndani ya mwaka mmoja, kama ilivyoelekezwa katika Mkataba wa Muungano, ibara ya 8 (a) na (b), na kifungu cha 9 (1) na (2) cha Sheria za Muungano.

Ibara ya 2 ya AMRI hiyo ilisomeka hivi:
“Subject to the provisions of this Decree, the Constitution of Tanganyika shall have effect from the Commencement of the Interim Constitution as if (a) the references ……were references to the United Republic of Tanganyika and Zanzibar; ………….
Maudhui ya ibara hii yalikuwa kwamba, Katiba ya Tanganyika ilikuwa pia Katiba ya Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Zanzibar, tangu kuanza kutumika kwa Katiba ya Muda ya Muungano.

Tofauti na ilivyotokea baadaye, Katiba ya Muda ya 1965, iliyotanguliwa na AMRI YA KATIBA ya Muda [The Interim Constitution Decree] ya 1964 [GN 246 ya 1/5/1964], ilitambua kuwapo kwa nchi za Tanganyika na Zanzibar na Serikali zake ndani ya Muungano. Kwa mfano, ibara ya 2 (1) ya Katiba hiyo ilisomeka hivi:

“The territories of Tanzania consist of Tanganyika and Zanzibar, and include territorial waters”.
Tafsiri yake ni kuwa, maeneo [nchi] yanayounda Tanzania ni [nchi za] Tanganyika na Zanzibar, na yanajumuisha maeneo [yake] ya bahari”

Nayo Ibara ya 13 ya Katiba hiyo ya Muda, ilitambua uteuzi wa Makamu wawili wa Rais – Makamu wa Kwanza wa Rais ambaye alikuwa pia ndiye Rais wa Zanzibar, kumsaidia Rais wa Muungano kwa mambo ya Muungano nchini Zanzibar; na Makamu wa Pili wa Rais kama Msaidizi Mkuu wa Rais huyo kwa mambo ya Muungano nchini Tanganyika, na kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni. Kusema kweli, jukumu hili la mwisho lilikuwa ni sawa na nafasi ya Waziri Mkuu kama Kiongozi wa Serikali ya Tanganyika.

Ibara ya 20 ilimpa Rais wa Tanganyika [na hivyo Rais wa Muungano] mamlaka ya kuteua Wakuu wa Mikoa kwa kila mkoa ndani ya Tanganyika, ambapo ibara ya 55 ilimpa Rais wa Zanzibar mamlaka ya kuteua Wakuu wa Mikoa nchini Zanzibar, mamlaka aliyonyang’anywa baadaye na Rais wa Jamhuri ya Muungano, na ambayo ni moja ya marekebisho ya sasa ya Katiba ya Zanzibar kwa kumrejeshea mamlaka hayo.

Ibara ya 25 (1) ilitamka wazi kuwa, “Tanganyika itagawanywa katika majimbo mengi ambapo kila jimbo litapaleka mjumbe mmoja mwakilishi Bungeni”.

Lakini, Katiba hiyo ilikuwa makini kutaja neno “Tanzania” kwa mambo yale ya Muungano pekee, kadri yalivyoonekana katika Katiba hiyo kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano, Sheria za Muungano na Amri ya Rais ya Marekebisho ya Katiba ya Tanganyika kwa Tangazo la Serikali Na. 246 la Mei 1, 1964.

Kwa mfano, Katiba ilitaja “Tanzania” kwa mambo ya Muungano yanayohusu mambo kama Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Mambo ya Nje, Ulinzi, Polisi, Mambo kuhusu hali ya hatari kwa nchi, Uraia na Uhamiaji.
Mengine ni biashara ya nje na mikopo, utumishi katika Jamhuri ya Muungano, kodi za mapato na forodha, bandari,mambo ya anga na simu.

Suala la sarafu halikuwa la Muungano, lakini liliongezwa baadaye mwaka 1965. Vivyo hivyo, mambo ya Usalama wa Taifa hayakuwa ya Muungano, yaliongezwa tu kufuatia kuchafuka kwa hali ya hewa ya Kisiasa Visiwani”, baada ya Rais wa nchi hiyo, Aboud Jumbe Mwinyi, kuondolewa madarakani na NEC ya CCM, mwaka 1984 kwa “kosa” la kuhoji muundo wa Muungano.

Ninachosema hapa ni kwamba, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar haukuuwa Serikali ya Tanganyika wala ya Zanzibar; kwani kwa mujibu wa ibara ya 5 ya Mkataba wa Muungano, na kifungu cha 8 (1) cha Sheria ya Muungano, nchi hizo zilibakia na mamlaka yake kwa mambo yasiyo ya Muungano na kutumia Sheria zake ambazo ziliendelea kuwa na nguvu.

Kufafanua zaidi jambo hili, sehemu za Hati hizo zinasomeka ifuatavyo: Kwanza, Mkataba wa Muungano, ibara ya 5: “The existing laws of Tanganyika, and Zanzibar shall remain in force in their respective territories….”

Pili, Sheria ya Muungano, kifungu cha 8, kinasema: “….. on and after Union day, the existing law (s) of Tanganyika and Zanzibar shall continue to be law (s) in the territories of Tanganyika and Zanzibar respectively…… and the operation of the existing law (s) shall not be affected by the cessation of the Constitution of Tanganyika for the government of Tanganyika as a separate part of the United Republic”.

Tafsiri ya ujumla ya Hati zote mbili nilizozitaja ni kuwa, “Kuanzia siku ya Muungano na baada ya hapo, Sheria za Tanganyika na Zanzibar zilizopo, zitabakia kuwa na nguvu na kutumika katika nchi hizo; na kwamba, kuendelea kutumika kwa Sheria hizo hakutaathiriwa na kukoma kwa Katiba ya Jamhuri ya Tanganyika [kwa kubadili jina na kujulikana kama Katiba ya Muda] kwa ajili ya Serikali ya Tanganyika [pekee] kama sehemu tofauti [kwa mambo yasiyo ya Muungano] ya Jamhuri ya Muungano”.

Hapa hakuna ubishi kwamba Tanganyika na Zanzibar ni nchi ndani ya Muungano. Swali linalozuka ni Je, Tanganyika ilifia wapi na Zanzibar ikabakia kama nchi?

Kifo cha Tanganyika kilitokana na matumizi mabaya ya Rais wa Kwanza wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, ambaye pia ndiye alikuwa Rais wa Tanganyika, ya mamlaka aliyopewa ya kurekebisha Katiba ya Tanganyika ili kuingiza mambo ya Muungano kwa mujibu wa ibara ya 2 na 3 ya Mkataba wa Muungano, na Kifungu cha 5 (1) © na 5 (2) cha Sheria ya Muungano, kwa njia ya AMRI [Decrees].

Hapa ni kwamba, badala ya Rais kushughulikia mambo ya Muungano pekee katika kuyaingiza ndani ya Katiba mpya, yeye alivuka mipaka hadi kugusa mambo yasiyo ya Muungano yaliyokuwa yanashughulikiwa kihalali na Serikali ya Tanganyika; lakini hakuthubutu kugusa mambo ya Zanzibar kwa sababu Karume alikuwa macho na makini mno na jambo hilo.

Kwa mfano, AMRI ya Rais [Transitional Provision Decree, 1964] iliyochapishwa kwenye gazeti kama Taarifa ya Serikali [G/N] Namba 245 ya 1/5/1964, iliwahamishia watumishi wote wa Jamhuri ya Tanganyika kwenye utumishi wa Jamhuri ya Muungano, na kwamba, Sheria za ajira za Tanganyika zitatumika pia katika Utumishi wa Jamhuri ya Muungano; na zaidi kwamba, Mahakama Kuu ya Tanganyika ikawa ndiyo Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano, wakati Mahakama hiyo haikuwa moja ya mambo 11 ya Muungano, kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano.

Amri hiyo, licha ya kuagiza kuwa Mhuri [seal] wa Tanganyika utumike pia kama mhuri wa Jamhuri ya Muungano hadi itakapopata mhuri wake, iliagiza pia kuwa “mali zote na haki kwa mali za Jamhuri ya Tanganyika za aina yoyote; na mali zote na haki kwa mali za Jamhuri ya Watu wa Zanzibar [lakini] zinazomilikiwa au kutumika kuhusiana na mambo ya Muungano [pekee], zitamilikiwa na Jamhuri ya Muungano”.

Amri ya Pili, iliyochapishwa kama Taarifa Namba 246 tarehe 1/5/1964, ambayo, kusema kweli ndiyo iliyozaa mgogoro wa sasa juu ya hadhi ya Tanganyika na Zanzibar ndani ya Muungano, ibara yake ya 4 (2), ilisomeka hivi:
“Executive power(s) with respect to all Union matters in and for the United Republic and with respect to all other matters in and for Tanganyika is vested in the President”.

Maana yake ni kuwa, “Mamlaka ya utendaji kuhusiana na mambo yote [11] ya Muungano ndani na kwa ajili ya Jamhuri ya Muungano na kuhusiana na mambo yote [ya Muungano na yasiyo ya Muungano] ndani na kwa ajili ya Tanganyika ni ya Rais [wa Jamhuri ya Muungano]”.

Kwa amri hii, mambo yote [11] ya Muungano na mengine yote [hata yasiyo ya Muungano] kwa ajili ya Serikali ya Tanganyika yaliunganishwa kuwa kitu kimoja chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano [ambaye pia alikuwa Rais wa Tanganyika], na hivyo kufanya kila kitu kilichokuwa cha Tanganyika kuwa cha Muungano kuweza kutumiwa na Watanganyika na Wazanzibari bila ubaguzi ndani ya Muungano.

Haikuishia hapo; Rais, kupitia amri nyingine [Provisional Decree No. 2, 1964] ya 1/5/1964, aliagiza kufutwa kwa jina “Tanganyika” popote linaposomeka hivyo [katika Katiba na Sheria zote], na badala yake liwekwe na kujulikana kwa jina la “Jamhuri ya Muungano”.

Hapo ndipo jina la “Tanganyika” na Serikali ya Tanganyika inayotambuliwa na Mkataba wa Muungano na Sheria za Muungano, ikafutika; na kuanzia hapo, Tanganyika ikawa ndiyo Tanzania; Rais wa Tanganyika akawa Rais wa “Tanzania”; tofauti na mwanzo alipokuwa Rais wa Serikali mbili – Serikali ya Muungano na Serikali ya Tanganyika.
Lakini wakati huo, na wakati wowote mwingine kabla na kufuatia mtafaruku huu, Zanzibar imebakia kama nchi yenye mamlaka na madaraka kamili ya ndani kwa mambo yote yasiyo ya Muungano, wakati mshiriki wa pili katika Muungano, yaani Tanganyika, alikwishafutika.

Hapa ndipo dhana ya Serikali mbili ndani ya Muungano ilipoanza kupigiwa debe kwa sababu hapakuwa na mshiriki tena wa tatu – Tanganyika; badala yake, kulikuwa na Tanzania [ambayo haitambuliwi hivyo kwenye Mkataba na Sheria za Muungano] na Zanzibar pekee, lakini yote hayo na kwa kwenda kinyume cha Mkataba wa Muungano ambao ndio mama wa Katiba sahihi ya Jamhuri ya Muungano.

Kwa hiyo, Zanzibar na Wazanzibari hawajakosea wala kuvunja Katiba, wanapodai kuwa Zanzibar ni “nchi”; kama tu ambavyo “Watanzania Bara” wasingekosea wala kuasi Muungano, kwa kuiita Tanganyika “nchi”, kama isingeuawa kwa amri ya Rais wa Jamhuri ya Muungano.

4 thoughts on “Zanzibar kujitangaza nchi imekiuka katiba? 3”

  1. Zanzibar imekiuka sheria haswa, haikupaswa kufanya hivyo, kabla ya kujadiliwa kwanza na wenzao, kwani kuungana kwao kulijumuisha pia wenzao.

  2. Dear Mwanakwetu, kwa mujibu wa Joseph Mihangwa, hakukuwa na suala la kushauriwa mtu wakati Muungano ulipoundwa, si Wazanzibari wala Watanganyika. Na juu ya yote, suala walilolifanya Wazanzibari kupitia Baraza lao la Wawakilishi ni kama lile linalokuwa kila mara linafanywa na Watanganyika kupitia wingi wao Bungeni, pale walipokuwa wakiyachukua mambo ya Zanzibar na kuyafanya ya Muungano kwa kisingizio cha kuimarisha Muungano.

  3. Wahenga wanasema, samaki mmoja akioza, wote wataoza!!!!, Si fikra za Watanganyika wote, hivyo si vizuri kuwalaumu wote, hayo yalikuwa maamuzi ya watu wachache, hivyo lawama msiwabebeshe Watanganyika wote. Na si vizuri lawama kutupa bara, kasoro muanze kuichunguza kwanza hukohuko visiwani.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.