Weblog hii imeanzishwa kwa lengo la kujenga jukwaa la mawasiliano kati ya Zanzibar na ulimwengu kupitia mtazamo wa Kizanzibari. Dhamira ni kuiwasilisha na kuiwakilisha Zanzibar. Imani kuu ya weblog hii ni Uzanzibari, ambalo ni jambo la fakhari kwa kila Mzanzibari awe anaishi ndani ya mipaka ya Zanzibar au nje yake. Hii ndiyo sababu ya weblog hii kuitwa Zanzibar Daima, kwa maana ya kwamba nchi hii ya Zanzibar ilikuwepo jana, ipo leo na itakuwepo kesho. Imani hii inaelezeka kwa maelezo haya yafuatayo:

Kwanza, wakati ni sawa kwamba Zanzibar ni visiwa vinavyopatikana kwenye bara la Afrika, si sawa kuutafsiri Uafrika wa Zanzibar kwa kutumia rangi za watu, kwamba wenye miliki ya Zanzibar ni Waafrika Weusi tu na wengine wote wasiokuwa na rangi nyeusi na au wasiotokea ndani ya Bara la Afrika ni “wakuja” tu na hivyo hawana haki walizonazo “wenyeji”. Mwanzilishi na mwendeshaji wa Zanzibar Daima anasimamia imani kwamba Uzanzibari ni zaidi ya rangi, asili, au itikadi ya mtu kisiasa. Uzanzibari ni uzalendo wa Zanzibar. Kwa hivyo, vyovyote awavyo, Mzanzibari ni Mzanzibari kwa uzawa na uzalendo wake na wala si kwa rangi ya ngozi yake au asili ya wazee wake. Zanzibar ni nchi ya watu mchanganyiko – mchanganyiko wa rangi, wa asili, wa dini, na wa itikadi. Zanzibar ni nyumbani pa wote ambao mapenzi na imani yao ni Uzanzibari na hao wote wana haki sawa.

Pili, wakati pia ni sawa kwamba Zanzibar imekuwa katika Muungano na Tanganyika kwa zaidi ya miaka 40 sasa, si sawa kwamba kwa kuingia kwake kwenye Muungano huu, Zanzibar imepoteza au ilitakiwa ipoteze kila kile kinachoifanya kuwa Zanzibar – unchi, udola, utaifa na uhuru wake. Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 – ambayo ndiyo muhimili mkuu wa uhusiano wa nchi mbili hizi – hayakuifuta Zanzibar wala Tanganyika kama nchi, madola na mataifa huru.

Badala yake Makubaliano haya yaliunda – na au yalitakiwa yaunde – Jamhuri moja na kuendelea kuzitambua nchi waasisi kama nchi. Kwa hivyo, Zanzibar ilikuwa nchi kabla ya Muungano, imekuwa nchi wakati wa Muungano, na itaendelea kubakia kuwa nchi hata baada ya Muungano huu.

Tatu ni imani juu ya utamaduni wa Zanzibar, ambao kama ulivyo mjengeko wa kijamii, ndivyo ulivyo pia utamaduni wa jamii yenyewe, yaani mchanganyiko. Ni katika ardhi ya nchi ya Zanzibar ambapo kwa karne na karne zimekuwa zikichanganyika tamaduni, asili, dini, na jamii tafauti na kuzaa huu leo tunaojifakharishia nao kama utambulisho wetu – Uzanzibari!

Kuanzia lugha, mavazi, na mapishi hadi fasihi na mahusiano ya kila siku, kinachoshuhudiwa Zanzibar ni ladha ya mchanganyiko na mchangiano na raha ya kuchanganya na kuchangiana huko. Hiyo ndiyo Zanzibar na huo ndio Uzanzibari – mithali ya ndege tausi, ambaye kama angelikuwa mweupe tu asingekuwa tafauti na njiwa manga na kama angelikuwa mweusi tu asingekuwa tafauti na kunguru. Utausi wa tausi ni mchanganyiko wake wa rangi na maumbile yake; na basi Uzanzibari wa Zanzibar ni vivyo hivyo.

Juu ya yote hayo, hata hivyo, kuna ukweli kwamba kutokana na athari zake, basi dini ya Kiislam ndiyo inayoutawala na kuutafsiri utamaduni wa Zanzibar, ambapo zaidi ya asilimia 98 ya Wazanzibari ni Waislam. Lakini linalosisitizwa hapa tena na tena, ni kwamba, kwanza, Uislam wa Wazanzibari hauonekani kwenye rangi za ngozi zao wala asili ya wazee wao na, pili, kuna ukweli mwengine wa kihistoria kwamba Zanzibar pia ni nyumbani pa waumini wa imani nyengine kama vile Ukristo, Uhindu na Ubuddha. Wote hao wanachangiana utamaduni mpana na mchanganyiko wa Zanzibar.

Nne, kwenye uchumi, Zanzibar ni nchi zaidi ya kibiashara kuliko ilivyo nchi ya kilimo, viwanda na mifugo. Biashara, hasa za mpito, ndizo zimekuwa chachu ya mabadiliko ya kiuchumi, kiutamaduni na kijamii kwa nchi hii kwa karne na karne sasa. Pale biashara inapoanguka au kuangushwa Zanzibar, sura nzima ya uchumi, jamii na utamaduni hubadilika – kama ilivyo hivi sasa.

Kwa nafasi yake ya kijiografia na kihistoria, Zanzibar ina fursa ya kuwa kama Hong Kong, Dubai ama Singapore, nchi za Asia ambazo sasa zinakaribia kuingia katika dunia ya kwanza kwenye uchumi wa dunia. Kwa hali hiyo, udhibiti wa kiuchumi unaowekwa na Serikali ya Muungano kwa Zanzibar kupitia mifumo ya kodi, ushuru na ukusanyaji mapato ni adui namba moja kwa maendeleo ya kiuchumi ya nchi ya Zanzibar. Weblog hii inasimamia katika mtazamo wa Zanzibar iliyo huru zaidi kiuchumi na kijamii.

Tano, kuhusiana na siasa, Zanzibar ina historia ya kisiasa iliyotukuka kwa upande mmoja na iliyochafuliwa kwa upande mwengine. Ni historia iliyotukuka, kwa kuwa hii ni nchi iliyotangulia sana kwenye ustaarabu wa siasa za kilimwengu kuliko nchi nyengine yoyote ile katika eneo hili la Afrika. Kwa mfano, Zanzibar ilikuwa dola, taifa na nchi huru zaidi ya karne moja kabla ya Tanganyika hata kujuilikana kuwa itakuwa Tanganyika. Hii ni tareikh ya kisiasa ya kujivunia na ya kujifakharishia.

Lakini pia ni historia iliyochafuliwa kutokana na siasa za kikoloni za “wagawe uwatawale” zilizoanzishwa miaka ya 1800 na wakoloni wa Kiingereza na kuendelezwa hadi hivi sasa na aina nyengine ya ukoloni wa Dodoma kwa Visiwa hivi. Kwa hili hakuna la kujivunia wala kujifakharishia, zaidi ya kujutia kila hatua iliyopigwa kuelekea idhilali na mateso haya ya nchi yetu ya uzawa. Kwa hili, kwa hivyo, weblog hii inasimamia kwenye imani kwamba Umoja wa Wazanzibari ndilo jukumu kubwa la harakati zozote zile ziwazo na kwamba rafiki wa Wazanzibari ni yule anayewaunganisha. Vivyo hivyo, adui wa Wazanzibari ni yule anayewagawa kwa namna yoyote ile.

Katikati na juu ya mtazamo huo, ndipo weblog hii ilipoanzishwa kwa lengo la kusimamia na kuiendeleza imani ya Uzanzibari. Hii ni imani ya Wazanzibari na ndiyo matakwa yetu. Kwa hivyo, basi weblog hii ni jukwaa la mawasiliano baina ya Wazanzibari na Wazanzibari, Wazanzibari na Watanzania wengine na baina ya Wazanzibari na walimwengu wote.