Na Mwinyi Sadallah
3 Septemba 2010

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Haroun Ali Suleiman

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imezuia hati idhini (charter) za vyuo vikuu vya Zanzibar kusainiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete, kutokana na mgongano wa kisheria.

Uamuzi huo umesababisha Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza) kutopatiwa hati idhini na Kamisheni ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kama ilivyofanyika kwa baadhi ya vyuo vilivyopo Tanzania Bara.

Sherehe ya kukabidhiwa hati hizo zilifanyika Agosti 18, mwaka huu, Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Haroun Ali Suleiman, alithibitisha kutokea kwa mgongano huo wa kisheria, lakini alisema suala hilo tayari limeanza kutafutiwa ufumbuzi wake.

Waziri Haroun alisema ni kweli Rais Kikwete ametoa hati hizo kwa vyuo vikuu tisa, lakini vyuo vikuu vya Zanzibar havikukabidhiwa hati hizo kwa kuwa Rais wa Zanzibar ndiye anayetakiwa kuzikabidhi kwa vyuo vikuu vya Zanzibar.

Alisema Zanzibar inataka hati hizo zikabidhiwe Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na baadaye kutayarishwe sherehe ya kuzikabidhi kwa vyuo vikuu husika.

Alisema Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar kimeanzishwa kwa sheria namba 8, ya mwaka 1999 na Baraza la Wawakilishi Zanzibar na mkuu wa chuo hicho ni Rais wa Zanzibar.

Waziri Haroun alisema Elimu ya Juu ni suala la Muungano, lakini alisema hati idhini ya vyuo vikuu vya Zanzibar zinatakiwa zitolewe na kukabidhiwa na Rais wa Zanzibar.

“Elimu ya juu ni ya Muungano, lakini sheria haituzuii kuanzisha vyuo vyetu na ndio sababu Zanzibar ikaanzisha Suza,’’ alisema.

Inafahamika kwamba Vyuo vikuu Zanzibar ambavyo vinatambuliwa na TCU ni Chuo Kikuu Tunguu na Chuo Kikuu cha Elimu Chukwani.

Hata hivyo, Waziri Haroun alivizuia vyuo vikuu hivyo kupokea hati idhini jambo ambalo inaripotiwa kuwasononesha TCU.

Lakini habari kutoka ndani zimesema kumekuwa na mvutano kati ya Wizara ya Elimu Zanzibar na ile ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ya Muungano kuhusu sheria namba 5 ya vyuo vikuu nchini.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar, Profesa Ali Seif Mshimba, alisema hana uwezo wa kuzungumzia mvutano uliojitokeza kuhusiana na sheria hiyo. “Nasikitika sana mie siwezi kuzungumzia chochote kuhusiana na suala hilo, mimi siyo mwenye chuo waulize wenye chuo, hasa Waziri husika, ” alisema.

Uchunguzi zaidi ya NIPASHE umegundua Chuo Kikuu cha Tunguu ambacho tayari kinatambuliwa kilikuwa kipokee hati idhini yake, lakini ghafla wahusika walitakiwa waondolewe katika orodha ya vyuo vikuu ambavyo vilitakiwa vikabidhiwe hati hizo kutokana na mvutano uliojitokeza.

Vyuo tisa vilivyokabidhiwa hati idhini hizo na Rais Kikwete ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (Duce) na Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa (Muse).

Vingine ni Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hebert Kairuki (HKMU), Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU), Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro (MUM), Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (Teku), Chuo Kikuu cha Tumaini na Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Stefano Moshi.

Vingine ni Chuo Kikuu cha Sebastian Kolowa (Sekuco), Chuo Kikuu Kishiriki cha Tiba Kilimanjaro (KCMC), Chuo Kikuu cha Matakatifu Augustine Tanzania na vyuo vyake vishiriki, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohana kilichopo Dodoma, Chuo Kikuu cha Sokoine pamoja na Chuo Kikuu cha Ushirika na Stadi za Biashara mjini Moshi.

Mgogoro huo ni mpya katika masuala ya elimu ya juu na hadi sasa haijafahamika ni lini vyuo vikuu vya Zanzibar hati idhini zake zitasainiwa na kukabidhiwa wahusika. Vyuo vikuu vya Zanzibar ni Suza, Tunguu na Chukwani ambavyo vimekuwa vikipokea wanafunzi kutoka nchi za kigeni tangu kuanzishwa kwake.

Hivi karibuni Baraza la Wawakilishi Zanzibar lilipitisha mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar pamoja na mambo mengine yakiitambua Zanzibar kuwa nchi, kumuongezea Rais wa Zanzibar madaraka ya kugawa mikoa na wilaya ambayo kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania ni madaraka ya Rais wa Muungano.

Kumekuwa na mjadala mkubwa juu ya mabadiliko hayo, lakini hivi katibuni Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe, alisema kuwa haoni mgongano wowote kwenye mabadiliko hayo kisheria.

ChanzoÖ Nipashe

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.