Na Joseph Mihangwa

MAPEMA mwezi huu, Baraza la Wawakilishi limeifanyia marekebisho Katiba ya Zanzibar ya 1984, kuipa hadhi ya kuwa nchi (kamili) na kuondoa madaraka ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, ya kuteua Wakuu wa Mikoa kwa Zanzibar, hatua ambayo imetafsiriwa na wengi kuwa ni ukiukaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Ibara za Katiba ya Zanzibar zilizofanyiwa marekebisho kuingiza mabadiliko haya ni ya kwanza na ya pili, zinazotamka kuwa, Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania . Na kufuatia marekebisho hayo sasa inasomeka kama ifuatavyo:

“ Zanzibar ni nchi…..iliyofahamika zamani kama Jamhuri ya watu wa Zanzibar , ikiwa na mipaka yake ya Unguja, Pemba na Visiwa vidogo vinavyoizunguka, kama ilivyotambuliwa kabla ya kuungana na Tanganyika . Zanzibar ni moja kati ya nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ”.

Katiba ya Muungano wa Tanzania , kwa upande wake, inaiona Zanzibar kama sehemu tu ya eneo la Jamhuri ya Muungano, ambapo ibara ya 2 (1) inasomeka ifuatavyo:-

“Eneo la Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la Tanzania Bara na eneo lote la Tanzania Zanzibar, na ni pamoja na sehemu yake ya bahari ambayo Tanzania inapakana nayo”.

Katika mabadiliko hayo, Wazanzibari hawataki sasa Zanzibar itambuliwe kama “eneo lote la Tanzania Zanzibar”, bali ijulikane kama “nchi” yenye mipaka yake ndani ya Muungano.

Marekebisho hayo ya Katiba ya Zanzibar, yamegusa pia ibara ya 61 (1) ya Katiba hiyo, inayompa Rais wa Jamhuri ya Muungano uwezo wa kuigawa Zanzibar katika Mikoa, Wilaya au maeneo mengine baada ya kushauriana na Rais wa Zanzibar, kwa kumwondolea Rais wa Jamhuri ya Muungano uwezo huo, ambapo sasa mamlaka hayo yatakuwa ya Rais wa Zanzibar, kiwa ni pamoja na kuteua Wakuu wa Mikoa bila hata ya kumhusisha Rais wa Jamhuri ya Muungano kama ilivyokuwa hapo mwanzo.

Kama hivyo ndivyo itakavyokuwa, basi ibara (kuhusu eneo la Tanzania) ya 61 (3) (kuhusu uteuzi wa Wakuu wa Mikoa Zanzibar) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano lazima nayo irekebishwe.

Niharakishe kutamka mapema hapa kwamba, maneno “Tanzania Bara” na “Tanzania Zanzibar”, hayana msingi wowote, wala nguvu ya kikatiba tunapozungumzia suala la Muungano wa “Tanganyika na Zanzibar” kwa kuwa hayakutamkwa katika “Hati ya Muungango” (Articles of Union) ambayo ndiyo “Kanuni na msingi mkuu (grandnorm) wa Katiba sahihi ya Jamhuri ya Muungano.

Hii ina maana kwamba, bila Hati ya Muungano, ambao ni mkataba wa kimataifa wa Makubaliano ya nchi hizi mbili (Tanganyika na Zanzibar), hapawezi kuwapo Muungano wala Katiba ya Muungano. Kwa sababu hii, Katiba sahihi ya Muungano, lazima iheshimu na kutii matakwa ya Hati ya Muungano; na pia kwamba, Katiba inayokiuka Hati ya Muungano, inakiuka pia matakwa ya msingi mkuu wa Muungano, na hivyo ni batili kwa kiwango cha ukiukaji huo. Tutaona na kufafanua baadaye juu ya jambo hili.

Je, Zanzibar, kwa kujitangaza kuwa nchi, imekiuka Katiba ya Muungano na kuasi Muungano? Ndilo swali linaloulizwa sasa na Watanzania wengi.

Lakini kwa nini tuamini kwamba Zanzibar imeasi Muungano? Je, haikuandikwa ndani ya Hati ya Muungano kwamba Zanzibar ni nchi, kama ilivyo Tanganyika? Je, si kweli kwamba, Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano, ndiyo iliyokiuka Mkataba huo wa Kimataifa, kati ya Tanganyika na Zanzibar?

Kwa Zanzibar kujitangaza kuwa nchi, Muungano utadumu? Ni aina gani ya Muungano uliokusudiwa chini ya Mkataba wa Muungano kutufanya tuamini kwamba Muungano wa sasa utavunjika?

Awali ya yote, naomba kuwasilisha kwamba muundo wa Muungano haueleweki; na vivyo hivyo mgawanyo wa madaraka ndani ya Muungano, jambo ambalo limechochea kero za Muungano tangu kuundwa kwake. Ni tatizo pia linalosababisha viongozi na Serikali kuchanganya mambo kuhusu Zanzibar.

Katikati ya tufani hii, kuna maneno manne tofauti ambayo ni muhimu kuyaelewa, na ambayo ndiyo yanayozua mkanganyiko. Maneno hayo ni; nchi, Taifa, dola na Serikali.

Nchi, maana yake ni eneo la ardhi yenye mipaka ambayo inatambulika, na eneo hilo lina utambulisho wake. Je, kwa tafsiri hiyo, Zanzibar ni nchi?

Katiba ya Jamhuri ya Muungano inaposema (ibara ya 2) kwamba, “Eneo la Jamhuri ya Muungano ni eleo lote la Tanzania Bara (sema Tanganyika, kwa sababu nilizozielezea hapo juu) na eneo lote la Tanzania Zanzibar (sema Zanzibar), ni maana ile ile kwamba Zanzibar na Tanganyika ni nchi (au maeneo) kwa kuzingatia mipaka yake ndani ya Muungano.

Taifa, maana yake ni jumuiya ya watu wenye historia, utamaduni, lugha na mahusiano ya kijamii ambayo wao wenyewe wanayatambua na ndivyo wanavyotambuliwa na watu wengine.

Mara nyingi, Taifa [race] au mataifa [races] yanaweza yakaishi katika eneo moja la kijiografia linaloitwa “nchi”. Kwa mfano, India ina watu wa mataifa mbali mbali ndani ya nchi moja. Lakini, Wapalestina ni Taifa, lakini hawana nchi (eneo) kwa sababu walifukuzwa na Waisraeli katika nchi ya mababu zao. Je, Zanzibar ni Taifa?

Sehemu ya Utangulizi ya Hati ya Muungano, iliyotiwa sahihi Aprili 22, 1964 na waasisi wa Muungano, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na hayati Abeid Amani Karume, inatamka kuwa:

“WHEREAS the Governments of the Republic of Tanganyika and the Peoples’ Republic of Zanzibar, being mindful of the long association of the peoples of these lands… have met and considered the Union of the Republic of Tanganyika with the Peoples Republic of Zanzibar.

Tafsiri isiyo rasmi ya maneno haya ni kama ifuatavyo: “Kwa kuwa Serikali za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, kwa kuzingatia uhusiano wa muda mrefu wa mataifa ya nchi hizi…..; zimekutana na kudhukuru Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar”.

Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiingereza – Kiswahili, iliyotolewa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam (toleo la 3), neno “Peoples”, lina maana pia ya “watu wa eneo (nchi)/jamii fulani, Taifa. Kwa hiyo Zanzibar ni Taifa ndani ya Muungano.

Dola ni chombo au mamlaka yenye uwezo wa kutawala eneo (nchi) maalumu la kijiografia. Kwa hiyo, inawezekana kuwa na Taifa lenye dola yake ambayo inatawala eneo [nchi] maalumu. Lakini unaweza pia ukawa na dola moja ikatawala mataifa zaidi ya moja katika nchi moja.

Vivyo hivyo, unaweza ukawa na dola zaidi ya moja, zikitawala katika nchi moja, hasa kwa nchi zenye Muundo wa Muungano wa Shirikisho, na hivyo kuna mgawanyo wa madaraka katika mamlaka ya utawala. Ni sifa zipi zinazofanya dola?

Dola yoyote, lazima iwe na mihimili au vyombo vitatu vifuatavyo: Kwanza , lazima kuwe na chombo cha kutunga Sheria, kwa maana ya Bunge, au kwa jina lingine lolote kuwakilisha shughuli hiyo.

Pili, kuwe na chombo cha kutoa haki, kwa maana ya Mahakama. Tatu, kuwe na chombo cha utendaji, kwa maana ya Serikali au utawala unaowekwa madarakani na watu wa nchi hiyo.

Hapa nifafanue kidogo. Chama cha Mapinduzi (CCM) Visiwani, au Chama cha Wananchi (CUF), kinaweza kushinda uchaguzi na kuunda Serikali, iwe ya CCM pekee au ya Umoja wa Kitaifa; lakini hakiwezi kuwa ndiyo dola, kwani dola, kwa maana ya Baraza la Wawakilishi, Serikali ya Zanzibar katika ujumla wake, si ya CCM wala CUF, bali ni ya Wazanzibari wote.

Kufikia hapo, sasa tunaweza kutamka, kwanza kwamba, Zanzibar ni nchi kwa sababu ina eneo lenye mipaka inayotambulika na lenye utambulisho. Marekebisho ya ibara ya 1 na 2 ya Katiba kutamka kwamba Zanzibar ni nchi, yanafafanua tu kile kilichopo na kinachotakiwa, au kilichopashwa kuwapo.

Kabla ya Rekebisho hilo la kumi la Katiba ya Zanzibar , ni ibara ya 9 (1) pekee ya Katiba hiyo, iliyotamka “ Zanzibar is a democratic State based on Social justice”, kwa maana ya, “ Zanzibar ni nchi ya kidemokrasia inayozingatia haki za kijamii”.

Pili, Zanzibar ni Taifa, kwa sababu ni jumuiya ya watu wanaoitwa Wazanzibari, wenye historia, utamaduni, lugha na mahusiano ya kijamii yanayotambuliwa na watu wengine.

Tatu, Zanzibar ni dola (ndani ya Muungano), kwa maana ina eneo (nchi) la kijiografia lijulikanalo kama “ Zanzibar ” kwa mambo yasiyo ya Muungano. Ili kuweza kutawala, ina Bunge lake (la kutunga Sheria) liitwalo Baraza la Wawakilishi; ina Mahakama na ina Serikali, vitu ambavyo katika ujumla wake vinaitwa dola, ambayo haiwezi kuingiliwa na Serikali ya Muungano.

Aidha, Rais wa Zanzibar anayesimamia dola hiyo, hachaguliwi na Watanzania, bali anachaguliwa na Wazanzibari (kama Taifa) na hawajibiki kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano katika kutekeleza shughuli za nchi ya Zanzibar .

Kuhusu kelele za sasa, juu ya Zanzibar kuvunja Katiba na kuasi Muungano, tatizo liko wapi?,

Kama nilivyoeleza mwanzo, tatizo ni kutoeleweka vizuri (na pengine kwa makusudi) kwa Muundo wa Muungano uliokusudiwa. Nimesema, inawezekana kabisa kwa dola zaidi ya moja kutawala katika nchi moja kwa Muungano aina ya Shirikisho.

Na ndivyo ilivyo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa dola mbili kutawala, dola ya Zanzibar kama nchi, na dola ya Jamhuri ya Muungano, kwa mambo ya Tanganyika na ya Muungano.

Je, Mkataba wa Muungano (Hati ya Muungano) inataka muundo gani wa Muungano? Je, Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya 1977, imejikwaa wapi kiasi cha kupotosha Watanzania waamini kwamba Marekebisho ya sasa ya Katiba ya Zanzibar ni uasi dhidi ya Muungano? Je, Muungano wa Tanzania na Zanzibar ulifuta nchi na dola ya Tanganyika?

Chanzo: Raia Mwema

Kusoma mwendelezo wa makala hii, bonyeza hapa

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.