Na Joseph Mihangwa
Septemba 1, 2010

KATIKA sehemu ya kwanza ya makala haya, tuliona kuwa msingi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni Hati ya (Mkataba wa Kimataifa wa) Muungano uliotiwa sahihi Aprili 22, 1965 na ambao juu yake Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inapashwa kusimama.

Nilisema, Katiba ya Muungano inayokiuka au kubeza misingi ya Mkataba huo wa Muungano ni batili kwa kiwango cha ukiukaji au ubezaji wa mkataba huo wa Kimataifa.

Nilijadili pia, kama Zanzibar ni nchi au la; na kubainisha kuwa licha ya kuwa nchi, Zanzibar ni taifa na pia ni dola ndani ya Jamhuri ya Muungano, jambo ambalo ni dhahiri kwa mujibu wa Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano (Acts of Union) ambayo Katiba ya Jamhuri ya Muungano inapashwa kuiheshimu na kuitii.

Nilihitimisha kwa maelezo kwamba kwa muundo wa Muungano wa Tanzania uliokusudiwa, inawezekana kabisa kwa dola zaidi ya moja kutawala ndani ya Muungano uliodhamiriwa kushughulikia mambo kadhaa tu ya Muungano, na yale yasiyo ya Muungano kuweza kushughulikiwa na dola za nchi husika.

Sasa tuendelee na sehemu hii ya pili kwa kuanza na swali: Je, ni aina gani ya Muungano uliokusudiwa? Tumejikwaa wapi kiasi cha kuzua mtafaruku uliopo?

Tunaweza kubaini mapema aina ya Muungano uliokusudiwa kwa kuongozwa na fikra na maneno ya mmoja wa waasisi wa Muungano, Mwalimu Julius K. Nyerere, katika kitabu chake “Uhuru na Umoja” (Freedom and Unity) uk. 300 – 304, anaposema:

“……Ni Serikali moja ya Muungano yenye madaraka kwa mambo kadhaa tu na kwa maeneo kadhaa ya Muungano. Zaidi ya hayo panaweza kuwa na Serikali (dola) nyingine zenye mamlaka yake na kwa mujibu wa Katiba zake, na si kutoka Serikali kuu hata kidogo…….”

Katika makala kwa gazeti la “The London Observer” la Aprili 20, 1968, Mwalimu alithibitisha mtizamo wa aina hiyo ya Muungano, na uwezekano wa nchi moja kujitoa, aliposema:

“Kama umma wa Watu wa Zanzibar, bila ya kurubuniwa kutoka nje, na kwa sababu zao wao wenyewe; wataona na kuamua kuwa Muungano una athari kwa uhai wao (kama Taifa), sitawalazimisha kuendelea kuwamo katika Muungano …….Na kwa sababu hiyo, Muungano utakufa punde wanachama (wa Muungano) watakapojitoa”.

Kwa maelezo haya, tunabaini bila ya shaka yoyote kwamba, Muungano uliokusidiwa ni wa aina ya Shirikisho lenye Serikali (dola) tatu. Katika Muungano uliokusudiwa ni mambo na maeneo kadhaa tu, yaliyoorodheshwa (ibara ya 4) ya Mkataba wa Muungano, na Serikali (dola) za nchi wanachama zilizoungana kuachwa kushughulikia mambo/maeneo mengine yasiyo ya Muungano.

Kwa uthibitisho, Mkataba wa Muungano (Articles of Union), ibara ya 5; na Sheria za Muungano (Acts of Union), ibara ya 8, zote zinatamka wazi kwa maneno yanayofanana kwamba:

“Kuanzia siku na baada ya Muungano, Sheria za Tanganyika na Sheria za Zanzibar kwa mambo yasiyo ya Muungano zitaendelea kuwa na nguvu na kutambuliwa kama Sheria za Tanganyika na Sheria za Zanzibar katika nchi hizo”.

Ndiyo kusema kwamba kufuatia Muungano, Tanganyika na Zanzibar ziliendelea kuwa nchi zenye dola kamili ndani ya Muungano.

Kufikia hapo, msomaji anaweza kujiuliza: je, dola hizo zilijiendeshaje ndani ya Muungano; na ipi na vipi ilikuwa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano?

Ibara ya 3 (b) ya Mkataba wa Muungano inazungumzia uteuzi wa Makamu wawili wa Rais kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano (kwa mambo ya Muungano tu), ambapo Makamu wa Kwanza atatoka Zanzibar na ambaye pia atajulikana kama Rais na Mkuu wa Serikali ya Zanzibar (Angalia Mkataba, ibara 3 (b) na 6 (b)).

Makamu wa Pili atatoka Tanganyika na ambaye pia ndiye atakuwa Msaidizi Mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa mambo ya Muungano nchini Tanganyika, na ndiye pia atakuwa Kiongozi wa shughuli za Serikali katika Bunge la Jamhuri ya Muungano (Angalia Mkataba wa Muungano ibara 3 (b) na Amri ya Rais (Decree), G/N 246 ya 1/5/1964).

Niharakishe kutamka hapa kwamba, baada ya Muungano, Makamu wa Rais wa Tanganyika, aliendelea kuwa Makamu wa Rais wa nchi hiyo, na Amri ya Rais ya 1/5/1964, ibara ya 4 inatamka: “Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Tanganyika, kuanzia siku ya Muungano, atahesabiwa ameteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, na kuteuliwa pia kuwa Msaidizi Mkuu wa Rais katika kutekeleza kazi (za Rais) kuhusiana na Tanganyika na Kiongozi wa Shughuli za Serikali katika Bunge”.

Nini tafsiri ya mpangilio/mfumo huo wa madaraka ndani na kwa ajili ya Muungano?.

Kwanza ni kwamba, hata baada ya Muungano, Jamhuri ya Tanganyika iliendelea kuwapo, kama ambavyo Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ilivyoendelea kuwapo.

Pili, kulikuwapo Serikali ya Muungano chini ya Rais, akisaidiwa na Makamu wa Rais wawili ambao walikuwa na mamlaka ya kiutawala kwa Tanganyika na Zanzibar kwa mambo yasiyo ya Muungano, na ambao ni wasaidizi wakuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano katika nchi zao kwa mambo ya Muungano pekee.

Kwa mantiki hii, Rais wa Jamhuri ya Muungano hakupaswa kuwa pia Rais au Kiongozi wa Serikali ya Tanganyika, kama ambavyo hakupashwa kuwa pia Rais au kiongozi wa Serikali ya Zanzibar.
Kama ambavyo Rais wa awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi alivyolazimika kuacha Urais wa Zanzibar alipoteuliwa kuwa Rais wa Tanzania mwaka 1985, ndivyo Rais wa Jamhuri ya Tanganyika, Mwalimu Nyerere, alivyopaswa kuacha Urais wa Tanganyika alipoteuliwa kuwa Rais wa kwanza wa Serikali ya Muungano mwaka 1964, lakini kinyume chake haikuwa hivyo; na hapo ndipo ukawa mwanzo wa tufani ya uparanganyaji wa mamlaka ndani ya Muungano ambao haukukusudiwa na Mkataba wa Muungano, na huo ukachochewa zaidi na Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano ambayo haikuzingatia mgawano sahihi wa madaraka ndani ya Muungano.

Ni kwamba, kwa jinsi Muungano huo ulivyobuniwa na kutekelezwa kwa njia ya dharura (ulibuniwa 18/4/1964; ukatiwa sahihi 22/4/1964 na kutangazwa 26/4/1964) hapakuwa na muda kwa Serikali mbili hizi kuandaa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, wakati huo Tanganyika na Zanzibar, ziliendelea kuwa na Katiba zake.

Ili kuokoa hali ya Serikali mpya ya Muungano kutokuwa na Katiba, ilielekezwa chini ya ibara za 2, 3 na 7 (b) za Mkataba wa Muungano kwamba, hadi hapo Jamhuri ya Muungano itakapotunga na kupitisha Katiba yake ndani ya mwaka mmoja tangu siku ya Muungano,

“Katiba ya Jamhuri ya Tanganyika itatumika vile vile kama Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano ya 1965 (Sheria Namba 43 ya 1965) kwa kuifanyia marekebisho ili kuingiza mambo yote ya Muungano”.

Na kwa sababu Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika (chini ya Rais Nyerere) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano (hapa tena, chini ya Rais Nyerere) zilitumia Katiba moja, kipenyo hasidi kilitengenezwa chini ya Katiba hiyo ya muda na kusomeka ifuatavyo:-

Ibara 12 (1) “Executive power with respect to all Union matters in and for the United Republic and with respect to all other matters in and for Tanganyika is vested in the President”.

Kwa tafsiri isiyo rasmi ni kwamba, “Mamlaka ya utawala kwa mambo yote ya Muungano ndani na kwa ajili ya Jamhuri ya Muungano na kwa mambo mengine yote ndani na kwa ajili ya Tanganyika yatakuwa kwa Rais”.

Na kuhusu mamlaka ya Bunge, ibara ya 49 ya Katiba hiyo ya muda ilitamka ifuatavyo:
“Legislative power with respect to all Union matters in and for the United Republic and with respect to all other matters in and for Tanganyika is vested in Parliament”.
Tafsiri yake ni kuwa,

“Mamlaka ya kutunga Sheria kwa mambo yote ya Muungano ndani na kwa ajili ya Jamhuri ya Muungano na kwa mambo mengine yote ndani na kwa ajili ya Tanganyika yatakuwa kwa Bunge” [la Muungano].

Kupitishwa kwa Katiba hiyo ya Muda kulifungua mlango kwa vurugu za Muungano; hapo,

Serikali ya Muungano ikambadili na kumfanya Rais wa Tanganyika kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Tanganyika kuwa Serikali ya Muungano; na mwisho wa yote, mambo yasiyo ya Muungano ndani na kwa ajili ya Tanganyika yakafanywa kuwa mambo ya Muungano,

wakati Zanzibar (kwa mujibu wa ibara ya 53 na 54) iliendelea kusimamia Serikali yake na mambo yote yasiyo ya Muungano.

Ni vyema hata hivyo, niweke wazi hapa kuwa mamlaka aliyopewa Rais wa Jamhuri ya Muungano, ya kuitawala Tanganyika, ni kwa sababu ya kutambua kuwapo kwa nchi inayoitwa Tanganyika na mamlaka ya Muungano wenyewe.

Kwa sababu hiyo, ni makosa kuchukulia hivi hivi kwamba, kwa sababu Muungano ulivishwa mamlaka ya muda juu ya Tanganyika (kwa sababu ya kutumia Katiba moja), uhuru na Sheria za Tanganyika zilikoma, la hasha!

Ingelikuwa hivyo, ingekuwa kwenda kinyume cha ibara ya tano ya Mkataba wa Muungano na ibara ya 8 (1) ya Sheria ya Muungano Na. 22 ya 1964, zinazotambua kuendelea kuwapo kwa Sheria za Tanganyika na Zanzibar katika nchi hizo tangu siku ya na baada ya Muungano.

Kwa kuzingatia kwamba Tanganyika na Zanzibar ni nchi zinazojitegemea kwa mambo yasiyo ya Muungano, Katiba ya Muda ya 1965 hata hivyo iliipa manufaa makubwa kadhaa Zanzibar ambayo haikustahili hadi sasa.

Kwa mfano, wakati Tanganyika haina mamlaka ya kutunga Sheria juu ya mambo ya Zanzibar yasiyo ya Muungano, Zanzibar, kinyume chake, inashiriki kutunga Sheria juu ya mambo ya Tanganyika yasiyo ya Muungano kupitia wawakilishi kutoka Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Hali hii si tu kwamba inafifisha muundo sahihi wa Muungano uliokusudiwa chini ya Mkataba wa Muungano, bali pia inafanya Tanganyika ijione kuwa ndiyo Tanzania au kaka mkubwa ndani ya Muungano. Je, Katiba ya 1977 nayo imejikwaa wapi?

Chanzo: Raia Mwema

Kusoma sehemu ya tatu ya makala hii, tafadhali bonyeza hapa

One thought on “Zanzibar kujitangaza nchi imevunja Katiba? – 2”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.