• Ataka wananchi wajifunze kilichotokea Uingereza

na Mauwa Mohammed, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Amani Abeid Karume, amesema Wazanzibari wanapaswa kuamka na kujifunza kutoka nje kuhusu mabadiliko ya kisiasa yanayotokea na kuhimiza umoja na mshikamano.

Alisema hakuna hata mtu mmoja aliyetarajia kwamba nchi kama Uingereza ingekubali mabadiliko ya kisiasa kama yanayotokea katika nchi za Bara la Afrika kwa kuunda serikali za umoja.

Rais Karume alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na waalikwa katika hafla ya makabidhiano ya Uwanja wa mpira wa Amani uliokuwa ukifanyiwa matengenezo na Serikali ya Watu wa China mjini Unguja.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na ujumbe wa Chama cha Wananchi (CUF) ulioongozwa na Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad, msaidizi wake, Ismail Jussa, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Umma, Salum Bimani, wabunge na wawakilishi wa chama hicho.

“Amkeni ndugu zangu na nyinyi mambo yanabadilika siku hizi mnaona huko Uingereza mambo yamekuwa vingine, kwa hivyo hili si huko tu, kila pahala katika nchi zetu hizi sasa wale wenye ndoto ya kuwa huku hayafiki shauri zao,” aliwaambia waalikwa hao.

Akikumbushia Zanzibar ilipotoka, alisema ilikuwa haina utulivu kama ilivyo sasa, na kwamba hali ya sasa imetokana na maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa kati yake na Maalim Seif Sharif Hamad.

“Mambo mnayaona wenyewe sasa, hali imetulia, hekima na busara zimetawala jazba na ndiyo ukaona maendeleo hivi sasa yanaonekana vizuri na haya yote yamepatikana kwa sababu ya maelewano. Hakuna sababu ya kuendelea kulumbana, hili nalisema wazi kabisa na kwa nia safi, kwa sababu tunataka maendeleo na maendeleo hayaji kama hakuna umoja na mshikamano,” alisisitiza Rais Karume.

Wakati huohuo alirudia msimamo wake wa kuwataka wananchi kupiga kura ya ‘ndiyo’ ifikapo Julai 31, mwaka huu kwa ajili ya kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa baada ya Uchaguzi Mkuu, ili Zanzibar izidi kuendelea kuwa katika utulivu na amani na kuondokana na migogoro ya kisiasa isiyoisha.

“Siku zile nilizungumza na vijana wengine wakasema, ‘ahhh si alizungumza na vijana wake tu?’ Sasa leo nazungumza na wananchi wote, maana najua wananchi wengi sasa wananisikia, televisheni ipo wazi …ipo laivu, kwa hivyo wananchi wananitizama sasa watasikia ninachosema … sasa nasema mtie kura ya ndiyo ili tuunde serikali ya umoja wa kitaifa,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, wakati Rais Karume akiwasisitiza wananchi kutia kura ya ndiyo, baadhi ya wana CCM wamekuwa wakipita mitaani na kuwataka wananchi wasikubali kura ya maoni, kwa kuwa serikali ya umoja wa kitaifa haina faida na chama chao.

Viongozi hao hao wenye kupita katika matawi ya CCM mjini na mashambani wana mtandao mkubwa, na baadhi yao wanadaiwa kuchochewa na viongozi wenye kutaka kuwania urais. Wamesema watahakikisha suala la kura ya maoni halifanikiwi Zanzibar.

Mbinu wanazotumia ni kupita kwa wananchi na kuandika ujumbe katika sehemu za maskani za CCM, ikiwamo maskani mama ya Kisonge iliyoanzishwa na Dk. Salmin Amour Juma, ambayo ujumbe huo huandikwa na kukaa wiki moja na baadaye kuandikwa ujumbe mwingine ambao unasema mseto kwa Zanzibar ni ndoto.

Ujumbe mwingine umesomeka kuwa ‘hatudanganyiki, mseto umeoza, hauliki na tutadumisha mapinduzi daima, ASP ndiyo mkombozi wetu, mseto hautowezekana hata siku moja.’ Ni mengi ambayo huonyesha kutokuunga mkono serikali ya umoja wa kitaifa.

Mbali ya viongozi hao wa CCM kupita matawini na kuwapotosha wananchi ambapo wameshawahi kuonywa juu ya tabia hiyo, lakini sasa wamevumbua mbinu mpya ya kutumiana ujumbe wa sms katika simu za kiganjani wakiwataka watu wasipige kura ya ndiyo.

“Ewe mwana CCM usidanganyike siku ya tarehe 31. 7. 2010, ukipiga kura ya maoni kataa mseto, kwani hautoiva, ni serikali ya vurugu ambayo hata ilani haitatekelezeka. Hakuna ushirika na CUF, usidanganyike. Ujumbe huu utume kwa wana CCM 15.” Unasomeka ujumbe huo ambao wananachi wengi yatari wamesharushiwa.

Ujumbe huo ambao unasambazwa na kuwafikia watu mbalimbali umemtaka kila anayeupata kuutuma kwa mwana CCM mwenzake kwa ajili ya kufikisha ujumbe na taarifa hiyo muhimu.

Tayari Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Khatib Mwinyichande, ametangaza Julai 31 kuwa ni siku ya kupiga kura ya maoni kuhusu hatima ya muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na iwapo wananchi wataridhia kutaundwa serikali ya umoja wa kitaifa baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka huu.

Mwenyekiti huyo alisema ZEC haijawahi kumtuma ofisa wake kupita kutoa elimu ya kuwataka watu wapige kura ya ndiyo au hapana, kama inavyodaiwa na baadhi ya watu wenye kutumia nafasi hiyo ya kupotosha umma juu ya kuwataka wananchi waikatae kura ya maoni.

Rais Karume na Rais Kikwete mara kadhaa wamekuwa wakitamka hadharani kuwa serikali ya umoja wa kitaifa ndiyo pekee itakayoweza kuistawisha Zanzibar na kuiondoshea matatizo na migogoro inayoendana na chuki na uhasama katika visiwa vya Unguja na Pemba na kuwataka wananchi kutokubali kurejeshwa nyuma na watu ambao wamekuwa wakipotosha dhana nzima ya umoja na mshikamano.

Chanzo: Tanzania Daima, 20 Mei 2010

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.