Na Francis Godwin, Iringa

SIKU moja baada ya kujiuzulu kwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Hamad Yusuph Masauni na Naibu Katibu Mkuu, Mohamed Moyo, kutokana na kuibuka kwa tuhuma mbalimbali na makundi ndani ya umoja huo, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, amewataka viongozi na vijana wanaoendekeza makundi kuondoka ndani ya umoja huo wenyewe.

Amesema hafurahishwi na njama chafu zinazofanywa na baadhi ya vijana ndani ya CCM kwa kuendesha makundi ya kuwachafua wenzao na kuchochea fujo ndani ya umoja huo, na kuwa kamwe wenye tabia kama hiyo hawatavumiliwa na wasitegemee kupata nafasi za uongozi daima hata kama watagombea.

“Nasema Umoja wa Vijana ni tegemeo kubwa kwa CCM, hivyo vijana wagomvi tokeni wenyewe…nasema acheni kabisa vijana kuishi maisha ya kujengeana chuki na kuendesha makundi ya kuwang’oa wenzenu kupitia vyombo vya habari.

“Ni vizuri penye tatizo kutumia vikao, kulumbana na kumalizana ndani ya vikao badala ya kuita waandishi na kueneza chuki,” alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana katika Chuo cha Vijana Ihemi, Wilaya ya Iringa Vijijini wakati akifungua kambi ya mafunzo ya uongozi kwa wenyeviti na makatibu wa wilaya zote za Tanzania Bara na Visiwani pamoja na wajumbe wawili kutoka kila wilaya.

Alisema kamwe hatamvumilia mtu yeyote anayechochea vurugu ndani ya UVCCM na CCM na kuwa anayeshindwa kutumia vikao kufikisha malalamiko yake ni vema ajiondoe mwenyewe katika nafasi ama umoja huo.

Aidha, Rais Kikwete alisema akiwa mwenyekiti wa chama taifa anapenda kuwahakikishia vijana kuwa hakuna kijana ambaye atagombea nafasi yoyote ya uongozi katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu na kuenguliwa jina lake kwa zengwe.

Alisema vijana wote wenye sifa za kuongoza wajitokeze kugombea nafasi mbalimbali ndani ya chama bila kuwaogopa waliopo katika nafasi hizo na wala kuhofu majina yao kufyekwa katika vikao vya juu.

Pia alisema hatakubaliana na sababu ambazo zimekuwa zikitolewa kwa vijana kuwa bado hawajakomaa kisiasa ama waongezeke kidogo na kuwa vijana wenye sifa, na kama uzoefu wataupata wakiwa katika nafasi za uongozi.

“Mimi hapa mwaka 1995 nilipogombea urais kwa mara ya kwanza niliambiwa na Baba wa Taifa kuwa bado umri na kunitaka nikue kidogo na baada ya hapo nilivuta subira, ila sikufanya vurugu zozote, hivyo nawaomba vijana kama mtashindwa kuchaguliwa endeleeni kuwa wavumilivu na kuepuka kuwa chanzo cha fujo kama kina Fulani, sipendi kuwataja hapa …ila nasema hakuna atakayeenguliwa safari hii kama amefuata kanuni na taratibu zote za kugombea,” alisema.

Katika hatua nyingine, Rais Kikwete alisema CCM imejiandaa vya kutosha kuingia katika Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu na kuwaonya wale wote wenye kawaida ya kufanya fujo katika mikutano ya kampeni za CCM kuanza kuepuka kufanya hivyo, kwani vijana wamejipanga kuhakikisha vurugu hazitokei.

“Nasema hakuna mtu ambaye anapenda kuonewa, hivyo kwa kuwa tumefanya maandalizi yetu, ni vizuri vijana kujiandaa kwa lolote, ili mtu atakayefanya fujo katika mikutano ya CCM kuwajibishwa na kukoma kurudia tena kufanya fujo kama zile za Jimbo la Busanda na majimbo mengine ambayo uchaguzi ulirudiwa,” alisema.

Alisema chama kimeanza kuziwezesha jumuiya zake kwa kutoa magari pamoja na kuanzisha utaratibu wa watu kuchangia chama kwa sms na kuwa hata wagombea wanapaswa kutafuta fedha za kampeni kihalali bila kutoa nafasi kwa wapinzani kuhoji utaratibu huo.

Awali, Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigella, akimkaribisha Rais Kikwete kufungua mafunzo hayo, alisema hali kwa sasa ndani ya umoja huo ni shwari, pamoja na siku za nyuma kabla ya kikao cha baraza kuu la UVCCM kuwapo makundi mbalimbali.

Chanzo: Tanzania Daima, 20 Mei 2010

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.