Na Salma Said, Zanzibar

RAIS Wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Amani Abeid Karume amesema yeye na Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad wamesafisha nyoyo na kusameheana kwa dhati kama maadili yao yanavyowaelekeza.

Akihutubia katika hafla ya baraza la Eid El-Hajj lilifanyika katika ukumbi wa Jumba la Wananchi Forodhani Mjini hapa, Rais Karume amesema walikutana na Maalim Seif kwa kuelezana ulazima wa kuleta amani na utulivu kwa nia ya kujenga misingi ya kuleta maendeleo makubwa zaidi ya wananchi na nchi yao.

“Tumesafisha nyoyo na kusameheana kwa dhati kama itikadi na maadili yetu yanavyotufundisha. Zaidi ni kuwa tumejenga msingi wa kuaminiana.” amesema Rais Karume na kupigiwa makofi mengi na hadhara iliyokuwa ikimsikiliza.

Alisema msimamo huo ni kwa niaba ya wananchi wote ambao wanaamini kuwa umoja, masikilizano, mshikamano,amani na utilivu ni mambo muhimu zaidi kuliko kuzingatia mengine kwa ajili ya mustakabali wa Zanzibar na watu wake.

Katika hutuba yake hiyo alisema lengo ni kuishi aktika umoja daima ili kupatikane mafanikio ya kila jambo hivyo kila siku zinavyokwenda hali izidi kuimarika zaidi kuliko ilipotoka “Namuomba Mwenyeenzi Mungu ajaalie siku zetu zote za umri wetu ziwe ni furaha ili tuishi katika umoja, upendo na tupate mafanikio ya kila jambo. Lengo letu liwe, leo iwe bora kupita jana na kesho kuliko leo. Hakika Mwenyeenzi mUngu yeye ni Msikivu, Yu karibu na wenye kukubali dua za waja wake” alisema Rais huyo.

Rais Karume alisema ni vyema wananchi wakafahamu kwamba maslahi ya nchi yanakuwa mbele kuliko nafasi za watu hivyo aliwataka wananchi wote kuunga mkono juhudi hizo zilizooneshwa na viongozi wawili kwa lengo la kuendeleza mazungumzo hayo ambayo yana faraja kubwa kwa taifa.

Amesema utamaduni wa kufahamiana na kuacha tofauti utaeleweka kwa wale wenye kutaka kuelewa huku akisisitiza furaha yake kutokana na mazungumzo hayo ambayo amesema wananchi wote watakuwa wenye furaha.

“Ni jambo la kufurahisha kwamba wananchi kwa wingi wao wameridhia na kufurahia misimamo huo. Hii ni sababu moja kwa upande wa kidunia kusherehekea Eid kwa mtizamo mwengine ulio mzuri. Napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza na kuwashukuru wananchi wote, viongozi wote wa kisiasa na marafiki zetu wa ndani na nje ya nchi kwa kutuunga mkono kwa dhati katika mafanikio haya” alisisitiza Rais Karume ambaye mara kwa mara hutuba yake ilikatizwa na makofi.

Aliwakumbusha wananchi kwamba dunia yote imo katika misukosuko mbali mbali, ikiwemo ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na mabadiliko ya hali ya hewa na maumbile ambapo alisema Zanzibar ni miongoni mwa nchi zenye matatizo hayo lakini hakuna atakayeweza kuyaondosha matatizo ya Zanzibar kama sio wenyewe.

“Wananchi wa Zanzibar hatuna budi kutafakari hali hiyo ya kidunia na kujiuliza tutafanya nini kuchangia kupata suluhisho. Zanzibar haipo pweke katika dunia na ina matatizo yake kutokana na hali hiyo ambayo ni sisi wenyewe ndio tunaweza kuyapatia ufumbuzi” alisema huku akiungwa mkono na watu waliohudhuria ambao walikuwa wakitikisha vichwa kuonesha kuunga mkono.

Rais Karume alitumia muda mwingi kuelezea masuala ya amani na kusisitiza kwamba Zanzibar inapaswa kuanza kuyafanya wenyewe kabla ya kuja kufanyiwa ili wengine wenye nia ya kutaka kusaidia waweze kuja baadae kusaidia maendeleo hayo.

“Wajenga nchi ni sisi wenyewe wananchi na nguvu zinazidi tunapokuwa na umoja na mshikamano.Wahenga wanasema umoja ni nguvu basi na tuitumie nguvu hiyo ya umoja kujiridhisha wenyewe kwa maendeleo yetu ya nchi yetu na mustakabali wetu.” Alisisitiza.

Kitabu cha tutuba ya Rais Karume chenye kurasa 12 kimelezea kwa kina umuhimu wa umoja na mshikamano hukua kisisitiza utamaduni wa kupanda miti na kwuahimiza wananchi kuwa wamoja ili kuendeleza mazuri yanayofanywa na serikali yao kwani bila ya umoja na kuunga mkono mazuri nchi haiwezi kufanikiwa.

Viongozi mbali mbali walishikiri katika sikukuu ya Eid El- Hajj ikiwa pamoja na wanasiasa, mawaziri, manaibu mawaziri na wawakilishi wa upinzani ambao ni mara yao ya kwanza kuhudhuria katika hafla hiyo tokea kuingia madarakani kwa Rais Karume katika wamu yake ya uongozi 2000.

Chanzo: Mwananchi

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.