Na Salma Said, Zanzibar

SIRI zaidi za mkutano wa rais wa Zanzibar, Amani Abeid Amani Karume, na katibu mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad, zinazidi kuwekwa bayana baada ya Maalim Seif kusema lengo kubwa la faragha yao ilikuwa ni kuunganisha nguvu katika kutetea mambo yanayoihusu Zanzibar kwenye Muungano. Seif alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza na wananchi kwenye sherehe maalum za Baraza la Eid El-Hajj zilizoandaliwa na CUF kwenye ukumbi wa Jamat-khan ulio Mkunazini Mjini Unguja .

Seif, ambaye aliwahi kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi (SMZ), alisema kuwa Zanzibar iliyoungana itazaa Tanzania iliyoungana. Alisema kuungana kwa Wazanzibari kutasaidia kuimarisha Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar kuliko kugawanyika kwa Wanzibari kwa kuwa pande zote mbili zina malalamiko kuhusu suala hilo. “Wazanzibari wakiungana wataweza kudai haki zao na kuuimarisha Muungano kuliko wakigawanyika,” alisema.

Zanzibar imekuwa na madai kadhaa kwenye Muungano; ikidai kurejeshewa utaifa wao ili iweze kushiriki katika masuala ya kimataifa; inadai pia kuwa kuna baadhi ya mambo yameingizwa kinyemela katika mambo ya Muungano likiwemo suala la mafuta na baadhi wanataka rais wa Zanzibar arejeshewe hadhi yake ya kuwa makamu wa rais.

Seif na Karume walikutana Ikulu ya Zanzibar Novemba 5 mwaka huu; lakini hakuna taarifa rasmi iliyoeleza walichozungumza zaidi ya kila upande kueleza chake kwenye mikutano ya hadhara.

Hata hivyo, baada ya Maalim Seif kwenda Ikulu, aliitisha mkutano wa hadhara na kutangaza uamuzi wa CUF wa kumtambua Karume, tamko lililosababisha azomewe. Baadaye, jumuiya ya wanawake ya chama hicho ikawa ya kwanza kutamka kuwa imemuelewa na inamuunga mkono kwa uamuzi huo. “Pande zote mbili zina malalamiko juu ya Muungano; Wazanzibari wana malalalmiko yao na Wabara nao wana malalamiko yao. Wazanzibari tukikaa pamoja tutaweza kutetea malalamiko yetu kama wao watakavyoweza kutetea malalamiko yao katika muungano,” alisema Maalim Seif .

Alisema kuwa serikali ya Muungano ina matatizo yake na SMZ ina kilio kikubwa katika kudai haki zao za kisheria katika Muungano; hivyo, kuwepo kwa umoja na ushirikiano baina ya viongozi wa vyama viwili hivyo ni dhahiri kuwa kutasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuitetea Zanzibar na watu wake kwa kudai haki zao kisheria bila ya kuathiri Muungano. “Mazungumzo tuliyofanya kati yangu na Rais Amani ya kutaka kudumisha umoja na ushirikaino na kuzika chuki zetu yataweza kusaidia hata katika kuitetea nchi yetu katika masuala ya Muungano wa Tanzania ” alisema Maalim Seif .

Maalim Seif alitumia fursa hiyo kuwafahamisha wananchi kwamba mazungumzo yake na Karume hayana lengo la kuvunja Muungano ambao umedumu tangu mwaka 1964, na wala hayana ajenda ya siri kwa kuwa lengo kuu la mazungumzo hayo ni kuwaunganisha Wazanzibari ambao alisema wamegawanyika kwa miaka mingi. “Sisi ajenda yetu ni kuwaunganisha Wazanzibari wote; na hatuna ajenda nyingine kwa kuwa sote tunafahamu kwamba tumegawanyika kwa muda mrefu na hili tumeliona; sasa tunataka kuungana kwa pamoja ili kuleta maendeleo ya nchi yetu,”alisisitiza Katibu Mkuu huyo.

Alisema wapo baadhi ya wananchi wasioitakia mema Zanzibar wameanza kudai kuwa mazungumzo hayo hayataendelea kwa kuwa hayana lengo la kujenga umoja na maendeleo; lakini, akaongeza kuwa watu hao ni wachache na wanapaswa kuelimishwa au wapuuzwe iwapo wataendelea na msimamo huo.

Seif, ambaye alilazimika kuachia wadhifa wake SMZ kwa tuhuma za kuvujisha siri za vikao, alisema pande zote mbili zinafamu umuhimu wa Muungano na ndio maana wanaona ni lazima kwanza Wazanzibari waungane. “Kwa kuwa kuna mambo yanayolalamikiwa katika Muungano, ni lazima hayo malalamiko yapatiwe ufumbuzi na hilo ndilo tunalotaka lakini si kuvunja au kuukataa Muungano… hilo halipo kabisa,” alisema.

Aliwaeleza wananchi hao kwamba wameamua kwa hiari yao kufanya mazungumzo na Rais Karume kwa lengo la kuharakisha maendeleo na kuwaahidi kwamba yale yote ambayo wamekubaliana kwa upande wake atayasimamia kikamilifu na kuyatekeleza.

Hata hivyo, alisema ana imani kubwa kuwa Rais Karume pia atatekeleza yale waliyokubaliana ambayo yako chini yake kwa kuwa tangu walipofanya mazungumzo hayo hajaona ishara yoyote kutoka kwa rais huyo inayoonyesha kuwa hatatekeleza waliyokubaliana.

“Nathubutu kusema kuwa… hii inanipa moyo kwa kuona kuwa Rais Amani tayari ameshaanza kuchukua hatua za utekelezaji wa ahadi zake.” alisema Maalim Seif . ‘Imani yangu ni kuwa Mheshimiwa Karume atatekeleza makubaliano yetu kwa maslahi ya vizazi vyetu na naahidi kuyasimamia kuyatekeleza yale yaliyo kwangu. Inshallah, tutafanikiwa kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu.”

Seif pia aliongeza kusema: “Nakiri kusema kuwa ndani ya moyo wangu ni safi… safi… safi, hamna chuki hata kidogo kwa Rais Amani Karume na ninamuamini sana. Tokea siku ile alisema tuzike tofauti zetu na tuwe kitu kimoja na Inshallah iwe hivyo sasa na nyinyi mtuunge mkono viongozi wenu; sawa sawa?”

Aliwataka wananchi wote wakati huu mgumu kukaa pamoja na kujadiliana njia gani za kuweza kutatua matatizo na kujenga Zanzibar mpya yenye maendeleo na umoja, hasa katika kipindi hiki ambacho alisema kinatazamwa na maadui ili mazungumzo hayo yasizae matunda.

Awali akimkaribishwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, Makamu Mwenyekiti wa CUF, Machano Khamis Ali, alitoa wito kwa wananchi wote kuwavunja moyo watu wenye nia mbaya na mazungumzo hayo pamoja na kuwapuuza wenye chochochoko.

Chanzo: Mwananchi 30 Nov 2009

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.