Na Habel Chidawali, Dodoma

SERIKALI imesema mkutano ujao wa bunge itagawa kwa wabunge pamoja na kuweka katika maktaba mbalimbali pamoja na makumbusho Hati ya Muungano kwa kuwa ni haki ya kila mtu kuufahamu mkataba huo.

Aidha, pamoja na kuweka katika maeneo hayo, bado hati hiyo itawekwa katika mtandao maalumu kumuwezesha kila Mtanzania kuiona na kuisoma kwa urahisi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Mohamed Seif Khatibu aliwaambia wabunge jana kwamba hati ya Muungano ni nyaraka ya umma na kila raia ana uhuru na haki ya kuipata na kuitumia.

Khatibu alisema hati hiyo ni sehemu ya sheria za Muungano (The Act of Union) ya sheria nambari 22 ya mwaka 1964 na kwamba haki hiyo iliridhiwa na kupatikana na katika maktaba ya bunge pamoja na sheria namba 22 ya mwaka 1964.

Awali Mbunge wa Tumbe Salim Abdallah Khalfan (CUF) alitaka kujua hati ya mkataba wa Muungano “Article of Union” ni waraka muhimu wa historia ya nchi na akahoji ni kwa nini waraka huo hauonekani wazi. Mbunge huyo pia alitaka kujua ni ipi nafasi ya kawaida kuweza kuupata na kuutumia waraka huo na kama serikali itakuwa tayari kuusambaza waraka huo kwa Baraza la Wawakilishi, Wabunge pamoja na maeneo ya maktaba za vyuo na makumbusho ya Taifa.

Hata hivyo, Waziri aliwataka wabunge kutumia nafasi hiyo kusoma vitu mbalimbali katika maktaba ya bunge kwa kuwa waraka huo upo tangu Februari 11, 2002; hivyo aliwataka wabunge wanaohitaji kujua waende katika maktaba yao kwa ajili ya kuusoma.

Chanzo: Mwananchi la 29 Oktoba, 2009

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.