SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imeionya Jumuiya ya Nchi za Ulaya (EU) na mabalozi kutoingilia kabisa mambo ya ndani ya visiwa hivyo na kuponda matokeo ya utafiti kuhusu mbio za urais wa Zanzibar mwaka 2010.
EU pamoja na nchi 10 za barani Ulaya na Amerika Kaskazini, zilionya dhidi ya kasoro zilizojitokeza kwenye zoezi la uboreshaji Daftari la Kudumu la Wapiga kura na kuitaka SMZ kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuondoa kasoro hizo kwa kuwa zinasababisha kukiukwa kwa demokrasia.
“SMZ haiongozwi kwa kumwogopa mtu au kwa shinikizo lolote, ina katiba yake na sheria zinazosimamia masuala mbalimbali na upana mkubwa wa maendeleo ya demokrasia,” alisema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma, alipoongea na waandishi wa habari ofisini kwake jana.
Waziri huyo alisisitiza kuwa, SMZ ina utawala wake kamili, ikiwa ni pamoja na sheria inayosimamia uchaguzi iliyopitishwa na Baraza la Wawakilishi kama chombo cha kutunga sheria.

“Hatuongozwi na EU wala AU (Umoja wa Afrika). Sisi ni nchi yenye kuheshimu sheria zake na kufuata utawala bora, demokrasia na kuheshimu haki za binadamu. EU wanatakiwa wafanye utafiti wa kutosha huko Pemba kabla ya kutoa shutuma,” alionya.

Alieleza kuwa, mazingira ya zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura kisiwani Pemba, yanakwamishwa na wanasiasa wa vyama vya upinzani wanaowachochea wafuasi wao wavunje na kukiuka sheria, jambo ambalo alidai kamwe halitavumiliwa na vyombo vya serikali.
Zoezi hilo lilisitishwa kutokana na wananchi kulipinga wakidai kuondolewa kwa kigezo cha kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi kuwa ndio sifa kuu ya kuandikishwa kupiga kura. Wananchi wanadai kigezo hicho kinapingana na katiba ya Zanzibar ambayo inamtambua mtu yeyote mwenye nyaraka nyingine zinazomtambulisha kuwa ni Mzanzibari.

Hata hivyo, Waziri Juma alimtupia lawama nyingi katibu mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad na kumtaja kuwa mmoja wa watu waliofanya mikutano ya hadhara ya uchochezi ili kuhatarisha amani katika kisiwa cha Pemba.
“Serikali haitamtazama na kumvumilia mtu yeyote ambaye ataamua kuvunja na kukiuka sheria. Vitambulisho vya ukaazi vinatajwa katika sheria ya uchaguzi, hivyo kila anayetaka kuandikishwa ni lazima awe na sifa ya ukaazi wa miaka mitatu mfululizo,” alisema.
Kuhusu matokeo ya utafiti wa kampuni ya Synovate ambayo yalionyesha kuwa Maalim Seif ndiye anayeweza kumrithi rais wa sasa, Amani Abeid Karume atakapostaafu mwakani na kufuatiwa kwa karibu na Mohamed Gharib Bilal, waziri huyo alipingana na ripoti hiyo.
Alisema Synovate iliwasilisha maombi Ofisi ya Waziri Kiongozi ili ifanye utafiti juu ya masuala ya kiutamaduni na kiuchumi, lakini kwa makusudi imekiuka taratibu na kufanya utafiti wa kisiasa kinyume na ombi lao la msingi.

Waziri Juma alisema, Juni 18 mwaka huu kampuni hiyo iliwasilisha barua ikiomba kufanya utafiti juu ya masuala ya hali ya kiuchumi na kiutamaduni na siyo kutafuta kura ya maoni kuhusu mbio za urais mwaka 2010 na kuupotosha umma.
“SMZ inaitaka kampuni hiyo kuomba radhi kupitia vyombo vya habari kuhusu upotoshaji wa habari uliofanyika kwamba, Seif Sharif Hamad ndiye anayekubalika kwa nafasi ya urais wa Zanzibar,” alisema.

Alisema kwa kukiuka mantiki ya ombi lao la awali katika kuendesha kwao utafiti walioukusudia, ni wazi kampuni hiyo itakuwa imeidanganya serikali, Ofisi ya Waziri Kiongozi na kuupotosha umma.
Alipotakiwa ataje athari zinazoweza kusababishwa na matokeo ya utafiti huo, alisema zimeutikisa mfumo wa siasa za Zanzibar na pia kuwapotezea mwelekeo na matarajio watu wenye kiu ya kuwania urais.

“Hata naibu katibu mkuu wa CUF, Juma Duni Haji, pengine alikuwa na nia ya kuwania urais ili ashindane na Seif, inawezekana amekatishwa tamaa, lakini pia si msingi wa ombi la kampuni husika, bali kilichofanyika ni hadaa,” aliongeza.

Katika hatua nyingine, Juma alibainisha kuwa, SMZ kamwe haitamkamata Maalim Seif Sharif Hamad na kumweka korokoroni licha ya madai ya kufanya uchochezi wa makusudi, ambao alisema ni kosa la jinai.

Alisema Maalim Seif anachochea wafuasi wake ili wavunje sheria na kusema atazidi kufanya hivyo bila kuchoka kwa kutegemea akamatwe ili apate umaarufu wa kisiasa.

“Hatuna mpango wa kumkamata Maalim Seif na kumfikisha kortini. Yule atamalizika kidogo kidogo mpaka wananchi watampuuza. Ni jamaa yetu; mwenzetu; analipwa masilahi yake na SMZ, hakuna wa kumkamata na kufanya hivyo ni kumjenga,” alisisitiza.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.