Na Salim Said Salim

PEMBA kunafuka moshi, muda si mrefu moto utawaka. Mengi yasiyokuwa na sura nzuri tunayasikia kila kukicha…Leo yameokotwa mabomu (yametoka wapi ni kitendawili), siku ya pili matawi ya CUF na CCM yamechomwa moto na wakati huo huo wananchi wenye hasira wamelizuia zoezi la uandikishaji wapiga kura.

Mwenye kuvitakia mema visiwa vya Unguja na Pemba na Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kwa jumla hujiuliza tunaelekea wapi? Jawabu si rahisi kupatikana, lakini ni wazi balaa tuliokuwa tunataka kuiepuka sasa ipo pembezoni.

Moto unawaka Pemba na hatujui mzimaji nani, lakini moto huu ukiendelea kuwaka ni wazi wengi tutaungua na kuteketea, kama hatupo tayari kujifunza kutokana na balaa zilizoanza kama tunavyoshuhudia Pemba katika nchi nyingi za Afrika.

Rais Amani Abeid Karume ameiona hatari iliyopo mbele na mara mbili katika kipindi cha wiki tatu, ametaka kila mwenye haki ya kupata kitambulisho apatiwe na kila mwenye haki ya kupiga kura aandikishwe.

Mara ya mwisho kusema hayo ni wiki hii alipokutana Ikulu na wakuu wa mikoa na wilaya. Kwa hili anafaa kupongezwa kwa sababu ameonyesha njia sahihi ya kufuatwa na si kukaa kimya na kucheka cheka au kufanya dhihaka wakati nchi inaelekea pabaya.

Lakini nilisema katika waraka wangu mwezi uliopita kwamba kauli ya Rais itakuwa na maana tu kama maagizo yake yatafuatwa na kuheshimiwa. Kwa bahati mbaya wahusika wanaonekana hawataki kuheshimu maelekezo ya Rais Karume. Hili lipo wazi na kwa maana nyingine wahusika wamejifanya kama vile hawawajibiki kwa Rais.

Mkurugenzi wa Vitambulisho, Mohammed Juma Ame, ametoa taarifa ya kuwalaumu masheha kwa kutowapa fomu wananchi ili wapatiwe vitambulisho na baadaye kuandikishwa kuwa wapiga kura. Mkurugenzi amesema vitendo hivi vya masheha ni uvunjaji wa sheria.

Hapa unajiuliza hawa masheha wanapata wapi ujabari wa kufanya mambo kinyume na kwa nini wasichukuliwe hatua za kisheria kwa kufanya vitendo vya uhalifu!

Kama masheha hawataki kutoa fomu kwa nini Idara ya Vitambulisho kama kweli haitaki kuwawekea watu vikwazo kupata vitambulisho, isibebe jukumu hili na kuzigawa badala ya kuwapa masheha ambao wanaonekana kuwa kwenda tofauti na hawajali sheria?

Kuwaachia masheha kufanya wanavyotaka hakutoi tafsiri yoyote ile isipokuwa wanafanya hivyo kwa kufuata amri za wakubwa na wana uhakika wa kulindwa na sheria za nchi kufumbiwa macho.

Hii ni hatari kubwa. Hakuna ubishi kuwa masheha – wengi wao wakiwa wastaafu wa jeshi, polisi, Usalama wa Taifa, magereza na KMKM – ndio waliokuwa chanzo cha balaa katika chaguzi zote zilizopita za mfumo wa vyama vingi. Sasa wanazusha balaa jipya, tunajua tupo wapi, lakini hatujui masheha wanatupeleka wapi.

Njia pekee ya kutuepusha na balaa ni kwa kila mwenye haki ya kujiandikisha kupiga kura anapewa haki hiyo kama sheria ilivyo na kama alivyoagiza Rais Karume. Vinginevyo ni kuchochea balaa ambayo tunaiona Pemba hivi sasa.

Kama Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ambayo inayoyasema si inayoyatenda na Idara ya Vitambulisho haitaki Wapemba wajiandikishe kupiga kura, basi ielezwe wazi na si kudai kila mwananchi anayo haki ya kupiga kura ilihali na haki hiyo haitolewi.

Niliwahi kusema vipo vielelezo vingi vinavyowapa nguvu Wapemba kudai wanaonewa na kubaguliwa na SMZ na Serikali ya Muungano. Kuwanyima haki ya kupiga kura huku wakibaguliwa katika ajira na watoto wao kukosa nafasi za elimu ya juu kama alivyofanya aliyekuwa Waziri wa Elimu wa Zanzibar, Omar Ramadhani Mapuri, aliyewafukuza wanafunzi 200, kwa vile kutaka kujiandikisha kupiga kura, hakutapewa tafsiri nyengine isipokuwa ni kuendeleza ubaguzi.

Nilisema na ninarudia kuwa Wapemba ni watu kama walivyo Watumbatu, Wamakunduchi, Wachagga, Wasukuma, Wahaya, Wafipa, Washihiri, Wamanga, Maithnaasheri, Wadigo, Wazanaki, Wamaasai na wengine hapa nchini.

Kama ni kuendeleza mbinu ya CCM ya kutesa kwa zamu, basi sasa iwe zamu ya kuwatesa wengine. Wapemba wameteswa vya kutosha katika medani ya siasa za Zanzibar. Kama kunyimwa haki ya kupiga kura wamenyimwa, kama kutandikwa mijeledi naamini migongo yao inabeba ushahidi wa kutosha na kama kufukuzwa kazi na nyumba zao kubomolewa kwa sababu za kisiasa hayo yameshawakuta.

Kwa vyovyote vile, inaonekana ni kuchoshwa na huo wanaouita uonevu na ubaguzi ndio uliosababisha huu moto kuwashwa Pemba. Sasa moto upo paani, sijui mzimaji nani.

Njia pekee ya salama, amani na utulivu ya kuuzima ni kuhakikisha kila mwananchi, Wapemba wakiwamo, anapata kitambulisho kama anastahiki na anapewa haki ya kupiga kura. Wale ambao hawapo tayari, kama walivyoonyesha jeuri masheha, kuona haki hii inatolewa wawajibishwe kisheria.

Masheha kama wawakilishi wa serikali mitaani na vijijini, wanapaswa kuwa mfano mzuri kwa jamii katika kuheshimu sheria na sio kuwa mstari wa mbele kufanya uhuni unaoweza kusababaisha balaa.

Kuwajibishana na kuachana na kauli za kejeli na jeuri zinazotolewa na viongozi wa CCM Zanzibar, ndiyo suluhisho pekee la kurejesha hali ya amani katika visiwa hivyo ambavyo sasa vinaonekana si shwari tena

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.