Wakati leo Watanzania wanaadhimisha miaka 45 ya Muungano, Kiongozi Mwandamizi katika Ofisi ya Waziri Kiongozi, Enzi Talib Aboud ameshauri serikali ya Tanganyika irudishwe ili iweze kusimamia mambo yasiyokuwemo katika orodha ya mambo ya Muungano kwa upande wa Tanzania Bara.

Alitoa tamko hilo alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu Zanzibar katika Muungano kwenye kongamano la kitaifa lililofanyika jana mjini hapa.

Akiwasilisha mada hiyo kwa Niaba ya Enzi, mwanasheria maarufu Zanzibar, Ali Omar, alisema Serikali ya Tanganyika ina umuhimu wa kurudishwa kwa vile itapata nafasi ya kusimamia mambo yasiyokuwa ya muungano kwa upande wa Tanzania Bara kama ilivyo hivi sasa kwa upande wa Zanzibar.

Aidha alisema wakati umefika Baraza la Wawakilishi Zanzibar lipewe nafasi ya kuridhia mkataba wa Muungano uliofikiwa 26 Aprili 1964 baina ya hayati Baba wa Ttaifa Mwalimu Nyerere na hayati Sheikh Abeid Amani Karume.

Alisema baada ya kufikiwa kwa Muungano mwaka 1964, Baraza la Kutunga Sheria la Zanzibar ambalo lilikuwa ni Baraza la Mapinduzi halikupewa nafasi ya kuridhia Muungano huo.

“Lazima Baraza la kutunga sheria la Zanzibar kwa sasa ambalo ni Baraza la Wawakilishi lipewe nafasi ya kuridhia mkataba huo ili kuupa uhalali wa kisheria kwa upande wa Zanzibar,” alisema Enzi katika mada yake iliyowasilishwa na mwanasheria Ali Omar.

Alisema katika kutatua kero za Muungano mkataba wa Muungano upitiwe upya na kurekebishwa maeneo ambayo yalikuwa na utatanishi baina ya pande mbili za Muungano.

Enzi ambaye ni mwandishi wa habari mkongwe nchini alisema, ili kuondosha mivutano ndani ya Muungano, Zanzibar inapaswa kuruhusiwa kunufaika na misaada ya kibajeti ya moja kwa moja na iwe na utambulisho wake wa kidola na utambulisho wake katika duru za kimataifa ili iweze kujimudu kiuchumi na kufanikisha mpango wa kuondoa umasikini kwa wananchi wake.

“Zanzibar ipate haki zake zote za misaada, utambulisho wake wa kidola na uwakilishi wake katika duru za kimataifa,” alisema.

Alisema orodha ya mambo ya Muungano hivi sasa inaongezeka kutoka mambo 11 yaliyomo katika orodha ya awali ya Muungano hadi 38 na kusababisha kutoka pande mbili za Muungano kwa vile baadhi ya maeneo yaliyoongezeka yamekuwa kikwazo katika nyanja za kiuchumi.

“Muundo wa serikali mbili umepelekea wengi kuamini kwamba kilichofanyika ni kiini macho tu kwani ni Zanzibar iliyokabidhi sehemu muhimu ya mamlaka yake mahusiano ya nchi za nje, ulinzi na usalama, uraia, kodi na sarafu kwa Tanganyika na kisha Tanganyika ikajigeuza jina na kujiita Jamhuri ya Muungano,” alihoji Enzi katika mada yake.

Hata hivyo, alisema hakuna awezae kubisha kuwa Muungano tangu kuasisiwa kwake umejengeka kutokana na misingi ya hofu, kutiliana shaka na kutoaminiana baina ya pande mbili za Muungano huo.

Wakichangia mada hiyo wanafunzi kutoka vyuo vikuu mbali mbali vya Zanzibar na viongozi kutoka vyama vya CUF, CCM, NCCR-Mageuzi, UPDP pamoja na watafiti akiwemo Profesa Abdul Sharrif ambao walishauri kero za Muungano zitafutiwe ufumbuzi kwa muda muafaka.

Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini UPDP, Haji Othman Haji alisema kasoro kubwa iliyofanyika katika muungano ni kufikiwa kwa Muungano wenyewe kabla ya kushirikishwa wananchi wa pande mbili za Muungano.

Hata hivyo alisema matatizo ya muungano yataondoka kwa kujadiliwa kwa uwazi na kuwepo kwa nia njema ili kuhakikisha umoja wa kitaifa kuendelea kudumishwa chini ya mfumo wa muungano.

Hata hivyo Ali Mohammed Said alisema wakati umefika kuungalia muungano wenyewe kabla ya kuangalia kero za muungano kwa kile alichodai kuwa Muungnao umechangi kwa kiwango kikubwa kuathiri sekta ya uchumi visiwani.

Naye Profesa Abdul Sharrif ambaye ni mtaalamu wa mambo ya historia alisema hivi sasa wananchi wamegawanyika makundi mawili wapo wanaosema Muungano uvunjwe na uundwe upya na wengine wakiamini ipo nafasi ya kutatua kasoro za Muungano kwa lengo la kuimarisha umoja wa kitaifa.

SOURCE: Nipashe

One thought on ““Serikali ya Tanganyika irudishwe””

  1. aa,sasa kidogo paka anatolewa kwenye gunia/kiloba,huu muungano wa kwetu ni wa mashaka kwani kama zanzibar haujaridhiwa tangu 1964 mpaka leo,hii ina maana kuwa muungano ni batili.jambo la 2 ni kuwa hii aina ya muungano tushaona kuwa haufai na kuwa suluhisho ni serikali 3,kila 1 ikiwa na mamlaka yake yanayojulikana ili kuepusha mgongano.jambo la 3 ni kuwa sasa SMZ imekubali kuachia kwa kiasi fulani huu mjadala kwani ingekuwa zamani,hmawa wanaojadili na kutoa maöni wangekiona cha mtema kuni! suala hili linahitaji kujadiliwa na watu wote wa tanzania,kwani CCM sio muungano wao bali ni wa wananchi.wakati umefika kwa mjadala wa kitaifa kuhusu muungano,kama raia wanautaka au uvunjwe! kama wanautaka uwe wa serikali ngapi? 1,2 au 3 ? na maoni ya raia ndo yafuatwe sio ya wanasiasa wachache!

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.