NI Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyetuonya: “Afichaye maradhi, kilio kitamuumbua”.
Usemi huu una uhusiano muhimu leo na hali ya sasa ya Muungano wetu ulioasisiwa Aprili 26, 1964, kuunda nchi inayoitwa sasa Tan–zan-ia.
Muungano wa Tanzania unaumwa; umekuwa hivyo tangu 1964. Maradhi yanayousibu tunayajua, lakini hatuyasemi ili kuyapatia tiba stahili. Kwa hiyo, wiki hii tunasherehekea miaka 45 ya Muungano unaoumwa, unaogwaya kwa maumivu makali katika chumba cha wagonjwa wasio na matumaini; maarufu kama “Intensive Care Unit” (ICU).
Magonjwa ni mengi mno; lakini baadhi tu ya yale yaliyojionyesha na yanayojionesha kwa njia ya dalili za ugonjwa, ni pamoja na Zanzibar kudai na kupata bendera yake, wimbo wa Taifa na majeshi yake ya usalama.
Mengine ni pamoja na Zanzibar kutaka kujiunga na Jumuiya ya Kimataifa ya Nchi za Kiislamu (OIC), na sasa ni mwanachama wa Shirikisho la Mpira la nchi huru barani Afrika (CAF), kama nchi.
Dalili mbaya zaidi ni hizi kwa Zanzibar sasa kudai jambo la “Mafuta, pamoja na mafuta yasiyochujwa ya motokaa na mafuta ya aina ya petroli na aina nyinginezo za mafuta au bidhaa, na gesi asilia”, liondolewe katika orodha ya mambo ya Muungano; ili Zamnzibar iweze kumiliki maliasili zake bila kuingiliwa na Serikali ya Muungano.
Dalili nyingine za ugonjwa tunazoziona zikianza kujitokeza ni pamoja na mambo mengine ya Muungano kuhusu mikopo na Biashara ya Nchi za Nje; Elimu ya Juu, mambo ya Nchi za Nje, na Utafiti.
Kwa muda wote huo, na kwa sababu ya tabia yetu ya kuficha maradhi eti kwamba ni dhambi kuhoji mambo ya Muungano, tumekuwa tukijaribu kutibu tu dalili za ugonjwa badala ya ugonjwa wenyewe hadi Muungano huu umefikia hali ya umahututi.
Zaidi ya mara moja, mitafaruku kati ya sehemu hizi mbili za Muungano imeutikisa nusura ya kuufikisha Muungano kikomo. Moja ya sababu za mitafaruku hiyo ni utata katika tafsiri juu ya aina na muundo wa Muungano uliokusudiwa, utata ambao licha ya kupigiwa kelele na wengi, kama tutakavyoeleza baadaye, tumeamua kuiga tabia ya “ujanja” wa mbuni wa kuzika kichwa mchangani, eti kukwepa janga. Labda tujikumbushe kidogo kwa hili.
Mdahalo wa kwanza juu ya mfumo na muundo wa Muungano ulianza kwa njia ya maoni juu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano mwaka 1983/84. Hapo, kwa mara ya kwanza ilibainika kuwa viongozi wa juu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, wakiongozwa na Rais Aboud Jumbe, na wale wa Serikali ya Tanzania, wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mwalimu Julius Nyerere, walikuwa na mitazamo tofauti inayokinzana juu ya Muungano.
Jumbe na timu yake walitaka Muungano uwe na Serikali tatu kwa maana ya Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar (iliyopo sasa) na Serikali ya Muungano yenye kushughulikia mambo ya Muungano tu, ambayo yameainishwa katika Ibara ya 6(a) ya Katiba ya Muungano (Articles of Union) na kifungu cha 8 cha Sheria ya Muungano (Acts of Union) Namba 22 ya 1964, na hatimaye ibara ya 4 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977.
Jumbe alikwenda mbali zaidi kwa kuandaa Hati ya Maombi ya kuhoji na kutaka ufafanuzi kwenye Mahakama Maalum ya Kikatiba juu ya muundo sahihi wa Muungano kwa kutumia ibara ya 125 ya Katiba.
Tofauti hizi kati yake na Mwalimu hazikwisha salama kwa Jumbe kuthubutu kukanyaga mahali “patakatifu” bila kuvua viatu. Jumbe alilazimishwa kuachia ngazi zote za uongozi wa nchi kuanzia Urais wa Zanzibar, Umakamu wa Rais wa Muungano, na nafasi zote za kichama Januari, 1984.
Naielewa vizuri hali ya mtafaruku iliyofuatia hatua hii na kule kutangazwa “kuchafuka” kwa hali ya kisiasa Visiwani, kwani nilikuwa mmoja wa Watanzania kutoka Bara walioshiriki kwa njia moja au nyingine kupatanisha / kutuliza (harmonise) hali hiyo. Lakini pamoja na kurejea kwa hali ya kawaida, bado matatizo ya Muungano yaliendelea kutawala agenda za vikao vingi vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.
Utata huu uliibuka tena kwa nguvu mpya zaidi wakati Wabunge 55 (maarufu kama G55) wa Bunge la Muungano, walipowasilisha bungeni mwaka 1993, hoja ya kutaka kuundwa/kurejeshwa kwa Serikali ya Tanganyika kwa kukasirishwa na hatua ya Zanzibar kujiunga na OIC kama nchi huru nje ya Muungano, Desemba 1, 1992.
Ukweli, Bunge lilikuwa limekwisha kupitisha kwa kauli moja, Azimio la kuanzishwa kwa Serikali ya Tanganyika Agosti 24, 1993 kwa maana ya kuwa na Serikali ya Muungano inayoundwa na Serikali hai zenye Mamlaka huru, za Tanganyika na Zanzibar, kama vile tu alivyotaka Rais Jumbe mwaka 1983.
Hata hivyo, Azimio hilo lilipigwa rungu zito na Mwalimu Nyerere na likavunjika.. Na kama ilivyokuwa kwa Jumbe, hapa napo mambo hayakuisha salama; safari hii Waziri Mkuu wa wakati ule, John Malecela (hongera kwa kutimiza miaka 75) na Katibu Mkuu wa CCM, Horace Kolimba, walipoteza nyadhifa zao kwa sababu ya ama kunyamazia au kuunga mkono hoja / Azimio la G 55.
Utata uko wapi juu ya Muundo wa Muungano wetu, utata unaozua ugonjwa?
Muungano wa Tanzania ulifikiwa mwaka mmoja tu baada ya kuundwa kwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (O.A.U), Mei, 1963 kwa kukubalika kwa hoja ya Nyerere juu ya kuundwa kwa Serikali moja ya Shirikisho la Afrika, kwa kuanza na mashirikisho ya kikanda, dhidi ya hoja ya Kwame Nkrumah, aliyetaka Afrika iungane mara moja.
Tukiacha migogoro ya ndani ya Zanzibar ya enzi hizo, ambayo inahesabiwa ni moja ya mambo yaliyomsukuma Rais Abeid Amani Karume kuingia katika Muungano, sababu kubwa kwa Nyerere na Karume kufikia Muungano zilikuwa ni pamoja na azma yao ya kuanzisha Muungano / Shirikisho la Afrika; na pili, msukumo wa vita baridi kati ya nchi za Magharibi za kibepari na za Mashariki (Ukomunisti) zilizokuwa zikigombea kupandikiza ushawishi na uhusiano na nchi za Afrika Mashariki.
Kwa jinsi nchi hizi mbili zilivyoweza kuungana kwa dharura katika mazingira ya “kuokoa hali”, hapakuwa na muda wa kuweka sawa mambo mengi muhimu ya kisheria na kiutendaji ndani ya Katiba.
Kilichofanyika ni kwa Nyerere na Karume tu kufikia makubaliano ya msingi (kwa hati ya dharura) na mambo mengine yakaburuzwa. Aidha, Mkataba huo wa Muungano ulitoa mwelekeo tu na kuacha mambo mengine muhimu kushughulikiwa baadaye na Tume ya Katiba ambayo chini ya Mkataba huo, ingeundwa katika muda usiozidi miezi 12 kuandaa Katiba ya Muungano. Katika kipindi hiki, Muungano uliendelea kutumia Katiba ya Tanganyika (kama ilivyorekebishwa) hadi hapo Muungano utakapopata Katiba yake.
Tunachofahamu ni kwamba, si Tume ya kupendekeza Katiba wala Bunge la Katiba (Constituent Assembly) lililoundwa au kuitishwa katika muda wa makubaliano hadi miaka 13 baadaye ilipotungwa Katiba ya kudumu ya 1977, kinyume na utaratibu unaotajwa kwenye Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano.
Madhumuni ya kuunda Tume ya Katiba na Bunge la Katiba kipindi kile, yalikuwa ni kutoa nafasi kwa raia wa nchi hizi mbili kushiriki, kutoa maoni yao kuhusu aina ya Katiba ya Muungano wanayotaka, Muundo wa Muungano na mgawanyo wa madaraka ya kiutendaji ndani ya Muungano.
Kuna utata namna Katiba ya 1977 ilivyotungwa. Utaratibu unaotajwa katika Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano unaelekea ulivunjwa kidogo, kwamba badala ya kuundwa Tume huru mahsusi kwa ajili ya kupendekeza Katiba, Tume ya vyama vya TANU na ASP ya watu 20 (ambayo haikuwa na Mwanasheria hata mmoja, bali wakereketwa wa siasa watupu), iliyoundwa mahsusi kuunganisha vyama hivyo viwili, iligeuzwa kuwa ndiyo Tume ya Katiba ya Chama na kupendekeza Katiba.
Mapendekezo ya Tume hiyo na ya Bunge la Katiba kama ilivyotakiwa, badala yake yaliwasilishwa na kujadiliwa kwenye Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama na baadaye kwenye Bunge la kawaida. Pamoja na hayo, Bunge hilo halikuyajadili mapendekezo ya “Tume” kwa sababu alizozitaja Waziri Mkuu wa wakati huo, Rashidi Kawawa, kwamba “Kwa kuwa NEC ilikuwa imeijadili, Bunge halikuwa na mamlaka ya kujadili wala kubadili kitu”.
Utata wa Muundo wa Muungano ulijitokeza tena kama hoja wakati wa Tume ya Jaji Nyalali na kupatiwa suluhisho kwa njia ya mapendekezo ya kurekebisha Katiba. Lakini badala ya mapendekezo ya Tume hii makini kufanyiwa kazi, yalitiwa kapuni na hivyo kupoteza nafasi nyingine nzuri ya kutibu ugonjwa unaousumbua Muungano wetu.
Lakini, kwa nini Tume ya Katiba haikuundwa kwa mujibu wa Mkataba na Sheria ya Muungano? Moja ya sababu ni kwamba waasisi wa Muungano huo, Nyerere na Karume, walianza kugundua kwamba walikuwa tofauti mno kwa kila hali; kuanzia maumbile, kitabia na kifikra, elimu na mtazamo juu ya Muungano waliotia sahihi.
Hapa, kulikuwa na Nyerere msomi, mwenye haiba ya mvuto (charismatic); na kulikuwa na Karume, asiye na elimu ya shule, mwenye kutumia hoja ya nguvu badala ya nguvu ya hoja na mwenye msimamo usiobadilika.
Baya zaidi, inasemekana (taarifa za CIA) kwamba Karume alitia sahihi Hati/Mkataba wa Muungano akiamini kwamba ilikuwa ni kuunda Serikali tatu; lakini jinsi Muungano ulivyoanza kuburuzwa akabadilika kabisa na kutishia zaidi ya mara moja akisema “kama ni hivyo, basi tuvunje Muungano”. Kuanzia hapo Muungano ukaanza kwenda mrama.
Ni kwa sababu ya tofauti za mitizamo za watu hawa wawili kwamba Tume ya Katiba na Bunge la Katiba halikuweza kuitishwa kwa mujibu wa mapatano ya Muungano. Matokeo yake ni kwamba mipango ya mpito iliyowekwa kidharura mwanzoni ikaachwa kwa muda mrefu na kuzidisha madhara kwa Muungano.
Vivyo hivyo, viraka tunavyopachika kwenye Katiba ya sasa haviwezi kuondoa kero za Muungano kwa sababu vingi havishabihiani na ama Mkataba na Sheria ya Muungano, au na Muundo wa Muungano uliokusudiwa. Matokeo ya yote haya ni kwamba tunajaribu kutibu dalili za ugonjwa badala ya ugonjwa wenyewe.
Kwa mapungufu haya, yanayozua kila mara kuyumbisha Muungano wetu, tunatakiwa kuziba ufa ili kuepuka kujenga ukuta kwa gharama zinazoepukika. Wakati ni huu, vinginevyo historia itakuja kutuhukumu.

One thought on “Muungano unaumwa, lakini tunatibu dalili”

  1. mambo yamekuwa mengi kuhusu muungano lakini kiukweli sisi wazanzibar tumechoshwa na huu, maoni ni mengi sisi kama watoto wa hao walounganisha huo muungano sasa tunahaki ya kusema kwamba babazetu walifanya lakikini sisi watoto hatuutaki. tupewwe nchi yetu. kaka wanataka muungano basi tuungane na kenya, uganda, malawi kisha rais atoke kenya. bank kuu ikaye huko. kama muungano ni mzuri

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.