Hii ni taarifa ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar juu ya mapendekezo ya uendeshaji wa kazi za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia nchini Zanzibar kama ilivyowasilishwa na wizara ya Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi ya Zanzibar katika Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, tarehe 2 Aprili 2009

Mhe Spika,
Waheshimiwa wajumbe,
Naanza kwa kumshukuru mwenyezi Mungu kwa kutukutanisha tena leo ni kwa kujadili kwa mara nyengine suala la utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na gesi asilia. Kikao cha awali kilikuwa tarehe 18 Septemba, 2008 kikiwa ni Semina ya Mshauri mwelekezi kuhusiana na utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia.

Mhe Spika,
Tumuombe Mwenyezi Mungu atupe busara na hekima ya kujadili hoja hii mbele yetu kwa uadilifu, ili hatma yake iwe ni manufaa na maslahi kwa Wazanzibari wote. Ni hoja ambayo inahitaji tuwe katika kiwango cha juu cha mizani kwa vile hoja yenyewe kimsingi linahusu suala linaloigusa moja kwa moja Zanzibar na wananchi wake na hatima yake.

Bado nitaomba michango ya kila Mjumbe wa Baraza hili tukufu kwa vile tunawapa heshima wananchi tunaowawakilisha hapa. Katika hotuba yangu ya mwisho katika kufungwa kwa semina ya tarehe 18 Septemba 2008 nilisema yafuatayo.

“Waheshimiwa wajumbe wa Baraza hili nianze kuwashukuru sana kwa michango yenu. Itatusaidia sana na itaturahisishia sana kazi kwa huko twendako.”

Basi ninarejea na kauli hio hiyo leo hii, ili kazi ya mbeleni iwe rahisi zaidi.

Mhe Spika,
Leo hii napenda kutekeleza ahadi niliyoitoa siku ile ya kujadili ripoti hiyo tangulizi ya kuwasilisha rasimu ya mwisho ya Ripoti hiyo hapa Barazani na kwamba maamuzi ya Baraza hili la wananchi wa Zanzibar ndio yatakuwa maamuzi ya nchi yetu juu ya utaratibu wa uendeshaji wa mambo yote yanayohusiana na utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia.

Imefikia katika hatua muhimu hatua ambayo inahitaji,kujadiliwa kwa kina na kupata ushiriki wa kila mjumbe katika kutoa maoni ya Wazanzibar wa Jimbo lake na ushauri wake, maoni na ushauri ambao utakuwa ni kutoka kwa jumla ya Wazanzibari wote bila ya kujali itikadi za kisiasa (Bi-paratisan).

Hatua hii ni imani yangu kuwa itazisaidia serikali zetu mbili, ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufikia katika uamuzi endelevu katika suala hili la utafutaji na uchimbaji wa Mafuta na Gesi asilia.

Ni budi kwanza kutanabahisha matatizo ambayo yanaendelea katika nchi mbali mbali kusini ya jangwa la Sahara kwa zile nchi ambazo zimebahatika kuwa na rasilimali ya mafuta na gesi asilia kama Algeria, Libya, Nigeria, Sudan, Chad, Gabon, Equatorial Guinea, Angola, Congo-Brazzaville, Democratic Republic of Congo (DRC), Uganda, Ghana, Sao Tome & Principe, Mauritania, Western Sahara, Gambia, Madagascar na Afrika Kusini.

Nchi nyingi kati ya hizi zimegubikwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababishwa na kutokuitenda haki katika mgao wa faida zinazotokana na rasilimali za mafuta na gesi asilia na mikataba aidha inayokandamiza sehemu fulanio au mibovu inayolinda maslahi ya wachache dhidi ya matakwa ya wengi.

Ni dhahiri sasa tuwe tunasoma kutoka nchi hizo kwa kutandika mikataba ya uwazi na madhubuti yenye msingi ya kukubalika kisiasa na kiuchumi. Ni dhahir kuwa hatua hii ya leo ni mwanzo muhimu wa kufikia hayo.

Mhe Spika,
Ninawashukuru wajumbe wa Baraza kukubali kuliona suala hili kwa upeo wa umoja wetu na kwamba suala hili halihusiani na khatma ya baadhi yetu,bali ni suala la hatma yetu sote na vizazi vyetu, njia pekee ya kulisimamia hili ni kwa umoja wetu.

Nimshukuru Mhe Rais wa Zanzibar na Mwenuyekiti wa baraza la Mapinduzi,Dk.Amani Abeid Karume kwa hekma kubwa na busara alioitumia na anayooendelea kuitumia katika kuliongoza suala hili la utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia kwa maslahi ya nchi yetu Zanzibar na watu wake.

Sote tukiwa wanasiasa ndani ya Baraza hili tunaelewa kwamba bila ya ujasiri wake akiwa Rais wetu na upeo wake tusingeshuhudia siku hii.

Aidha niwashukuru pia wajumbe wa Baraza la Mapinduzi kwa maamuzi yao thabit, Mwenyezi Mungu awajaalie wao na familia zao afya, kheri na Salama.

Mhe Spika,
Tangu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuzuiya kazi ya Utafutaji Mafuta na Gesi Asilia kwa Kampuni ya Antrim ya Canada mwaka 1997 licha ya kuitolewa leseni na TPDC kwa kazi hio katika eneo la Zanizbar, eneo la utafiti ambao linahusisha maeneo ya Zanizbr kama yalivyoelezewa katika katiba ya Zanziabr 1984,Sura ya kwanza Kifungu 2.(1), kumekuwa juhudi kadhaa za kidiplomasia na kisiasa katika kulipatia ufumbuzi suala hilo.

Mhe Spika,

CHIMBUKO LA TATIZO

Kibali cha utafiti kwa eneo la Visiwa vya Zanzibar na bahari iliyozunguka visiwa hivyo kilitolewa kwa TPDC katika mwaka 1997 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, TPDC na Kampuni ya Antrim ziliingia katika mkataba wa uchimbaji (Production Sharing Agreement) tarehe 29 Januari 1997 kwa mkataba ambao ulitengenezwa na Wizara ya Nishati na madini (SMT).

Antrim kwa mujibu wa mkataba huo walitakiwa kuanza kazi za kukusanya taarifa za kitaalam za mtetemo (SEIMIC data ) kwa kuhusisha eneo la kilometa 100 kisiwa ni Pemba, kilometa 100 kisiwani unguja na kilometa 200 kwa eneo la bahari kwa gharama ya Dola za kimarekani Millioni 3.5 kwa mika miwili ya mwanzo kuanzia April 2002 mpaka April 2004.

Kwa kipindi cha miaka miwili mnyengine inayofuata kuanzia April 2004 mpaka April 2006 walitakiwa wachimbe kisima cha utafiti wa mafuta kwa maeneo ya kaskazini Pemba kwa gharama ya Dola za Kimarekani Millioni 4.

Kwa Mujibu wa ramani ya eneo la utafiti huo (Antrim Block) vilihusisha visiwa vyote vya Zanzibar na bahari yake bila ridhaa na ushauri wa serikali ya Mapinduzi ya Zanizbar.

Mhe Spika,
Baada ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanziabr kuanzia Kampuni hiyo kuanzia utafiti huo kwa maeneo hayo, hatimayae suala hili likawa ajenda moja wapo ya kikao cha kwanza cha kujadili kero za Muungano baina ya Waziri mkuu na Waziri kiongozi.

Ndani ya Kikao hicho, Msimamo wa Serikali ya Mapinduzi ukawa ni kuliondoa suala mafuta na gesi kuliondoa kutoka katika orodha ya mambo ya Muungano au kuyafanya madini yote kwa jumla kuwa ni ya Muungano.

Hata hivyo, katika vikao vilivyofuata pande mbili hizi zikakubaliana kutafuta mshauri Mwelekezi atakaezishauri serikali zote mbili juu ya namna bora ya kugawana rasilimali hiyo.

Mshauri huyo alipewa hadidu rejwea zilizoridhiwa na pande zote mbili kama muongozo wa kukamilisha kazi hiyo na Kampuni hiyo ilianza kazi tarehe 20 Jun 2007.

Mhe Spika
M aelezo yangu haya yanalenga kufafanua mapendekezo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kupata mwongozo makini wa baraza hili utakao tuongoza katika muelekeo wa Zanzibar.

Baada ya kukutana na washiriki kadhaa wa suala hili kwa kila upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mshauri Mwelekezi aliwasilisha kwa serikali zote mbili ripoti tangulizi (Inception Report) ilioainisha namna alivyoliona sula lenyewe, namna ya kulishughulikia na mwelekeo wa ujumla wa kazi yenyewe.

Lengo la ripoti hii ilikuwa ni kwa kila upande kuijadili na kuitolea maoni yatakayomweesha mshauri kuandaa rasimu ya ripoti yake ya kwanza (Draft Report) ambayo itapitiwa na pande zote mbili kabla ya kufikia ripoti kamili. Kwa upande wa Zanzibar upitiaji wa ripoti hiyo haukuishia kwa watendaji na washiriki mahsusi wa suala hili tu bali pia baraza zima hili la Wawakilihsi ambalo liliandaa semina maalum iliyompa fursa Mshauri Mwelekezi kuwasilisha ripoti hiyo tarehe 18 Septemba 2008.

Mhr Spika,
Mshauri Mwelekezi huyo alitakiwa kutekeleza yafuatayokatika hadidu za rejea (Term of Reference):

 1. Kukusanya na kuzipitia nyaraka zote zinazohusiana na muundo wa Tanganyika na Zanzibar ikiwa ni pamoja na katiba ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutoa maoni kuhusiana na suala la mafuta na gesi asilia.
 2. Kuzielewa sheria zilizohusiana na Muungano kwenye sekta zote zitakazo husiana na utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia.
 3. Kuielewa sheria ya mafuta ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1980 (Exploration and Production Act 1980) na kutoa maoni ya jinsi gani sheria hiyo itakithi haja ya utekelezaji mzuri kwa serikali zote mbili.
 4. Kuelewa na kutafiti muundo wa sheria ya shirika la mafuta la Tanzania (Tanzania Pertroleum Development Coorporation – TPDC) kama chombo cha muungano na kutoa maoni ya uendeshaji wa shirika hilo.
 5. Kuielewa na kutoa maoni kuhusu mikataba ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia katika Tanzania (Production Sharing Agreements PS”A 2004) na kutoa maoni.
 6. Kuelewa na kutoa maoni kuhusu mkataba wa utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi asilia (Production Sharing Agreement) baina ya serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania na kampuni ya Antrim Resoures wa 1997.
 7. Kuielewa na kutoa maoni kuhusu mkataba wa utafutaji na uchimbaji mafuta nagesi asilia (Production Sharing Agreement) baina ya kampuni ya Sheli International petroleum Company na Serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania.
 8. Kutoa maoni kuhusu mgawanyo (fiscal terms) wa gharama na mapato mrahaba (Royalties) zinazohusiana na mikataba ya utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi asilia katika jamhuri ya Muungano wa tamnzania.
 9. Kutoa maoni ya kuhusu mgawanyo wa gharama na mapato kwa kulinganisha nchi nyingine zenye Muungano na zenye rasilimali kama hii, kama Uingereza, India, Brazil, Canada, Nigeria na Australia na kutoa maoni ni jinsi gani Tanzania inaweza kutumia utaratibu kama huo wa mgao.
 10. Kutoa maoni na mapendekezo ya fidia katika sehemu zitakazo athirika kimazingira na kijamii kutokana na utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia.
 11. Kutoa maoni ya jumla kwa tanzania Bara na Zanzibar ni utaratibu gani utumike katika kutafuta suluhu katka suala la mgawanyo wa gharama na mapato kwenye utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia.

Mhe Spika,
Mshauri ameonesha mapungufu kadhaa ambayo yamejitokeza katika utekelezaji wa kazi hii ya utafutaji wa uchimbaji wa mafuta na gesi ndani ya Jamhuri ya Muungano Tanzania, mambo ambayo zaidi yanaiathiri Zanzibar kimapato.
Mhe Spika,

Shirika la kuendeleza shughuli za mafuta Tanzania (TPDC) Shirika la mafuta la Tanzania (Tanzania Pertroleum development Corporation) lilianzishwa kwa tamko la rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 26 Mei 1969 (Presidential Decree 1969) na Sheria ya Makampuni ya Umma ya 1969 (Public Corporation Act 1969) ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kurekebishwa na Sheria mpya ya mwaka 1992 inayotumika hivi sasa huko Tanzania Bara.
Japo kuwa TPDC ina sura na tafsiri yachombo cha Muungano kinachosimamia utoaji wa leseni za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia katika jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,ushirikishwaji wa serikali ya Mapinduzi hususan kwa masuala yanayohusiana na mafuta na gesi asilia haupo.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inawakilishwa na mjumbe mmoja tu kutoka Wizara ya maji, Ujenzi Nishati na Ardhi ndani ya bodi ya TPDC.

Mhe Spika,
Katiba ya Zanzibar katika sura ya 13 kifungu namba 132 (1) kinaeleza kuwa hakuna sheria yeyote itakayopitishwa na Bunge la muungano ambayo itatumika Zanzibar mpaka sheria hiyo iwe kwa mambo ya Muungano tu na ipitishwe kulingana na maelekezo yaliyo chini ya vifungu vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Kifungu 132 (92) kinaeleza kuwa Sheria kama hiyo lazima ipelekwe baraza la Wawakilishi na Wiziri anayehusika na kifungu 132 (3) kinaendelea kueleza “pale sheria ndogo inapoundwa kwa mujibu wa uwezo uliowekwa chini ya kifungu cha (1) na (2) cha sheria hii, itatumika tu pale itakapotimiza shuruti zote zilizowekwa kwa matumizi ya sheria mama kama ilivyoainishwa katika kifungu hiki.”

Kutokana na kifungu hicho cha katiba ya Zanziabr (katiba yetu yenye uawezo wa mwisho (supremet) kwa Zanzibar , ni dhahir kuwa ,sheria ya kuundwa kwa TPDC 1969 na ile sheria ya Mafuta 1980 hazikukidhi haja na zimekiuka katiba ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mhe Spika
Majadweli yafuatayo yanaonyesha makampuni yote yaliyopewa mikataba na TPDC maeneo husika (blocks) na mauzo ya gesi asilia kutoka Songosongo kuanzia 2004 – 2007 bila ya kuhusisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar

Jadweli 1.0
COMPANY NAME COUNTRY OF ORIGIN AREA/BLOCK
Antrim Resources Canada Zanzibar/Pemba
Artumas group Canada Mnazi Bay
Dominion oil & gas UK Mandawa Kisangire Selous & Deep Sea Block#7
Dodsal Resources UAE Ruvu
KEY PETROLEUM Australia
West Songosongo
Mauriel et prom France Bingwa & Mafia Channel
Ndovu Resources Australia Nyuni Ruvuma
Ophir energy Australia Deep Sea block #1,3,&4
Pan African Energy UK Songo songo
Petrobras Brazil Deep sea Blocks # 5,6,8
Pertrodel Resoures UK Tanga Kimbiji Latham
Statoilhydro asa Norway Deep Sea Block #2
Rak – gas Company UAE East Pande
Shell international Holland Deep Sea Blocks # 9,10,11,&12
Statoilhydro asa Norway Deep sea Block #2

Mhe Spika,
Katika ripoti hii mshauri mwelekezi anapendekeza kuundwa kwa Wizara itakayoshughulikia Mafuta chini ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hii maana yake ni kwamba Wiza za Muungano.

Mshauri Elekezi pia anashauri kuundwa upya kwa TPDC ili chombo hiki kiwe na sura ya Muungano, kwani hivi sasa hakina sura hiyo ya kimuungano.Vyombo hivi viwili, yaani Wizara ya Mafuta na TPDC, ndiyo vitakavyokuwa na mamlaka ya kuyasajili makampuni yote yatakayokuja kufanya shughuli za uchimbaji wa mafuta na gesi asilia hata kwa upande wa Zanzibar.

Vyombo hivyo viwili pia ndivyo vitakavyokuwa na mamlaka ya kutoa leseni kwa makampuni mbali mbali yatakayojihusisha na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia.

Endapo suala hili la uundwaji wa Taasisi hizi mbili latika sura ya Muungano litakubalika, Zanzibar itakosa mapato yote yatakayotokana na usajili wa makampuni hayo ya uchimbaji wa mafuta.

Halikadhalika, Zanzibar itakosa mapato yote yatakayotokana na utoaji wa leseni pamoja na Renewal ya leseni hizo kila mwaka kama ambavyo inavyojitokeza hivi sasa, ambapo Kampuni ya Zantel imekuwa ikilipa jumla ya dola za Kimarekani 3,000,000 sawa na shilingi za Kitanzania 3,900,000,000 kila mwaka kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ambayo ndiyo inayotoa leseni yake kila mwaka huku Zanzibar ikiwa haipati hata shilingi.

Zaidi ya hayo, suala hili la kuundwa kwa Taasisi mbili hizi na kuwa na sura ya Kimuungano, zitainyima Zanzibar Mapato ya Mrahaba “Royalties” ambayo kwa mujibu wa taratibu yatatakiwa kulipiwa katika taasisi inayosimamia usajili na utoaji wa leseni ambayo itakuwa ni wizara ya Mafuta na TPDC.

Hivi sasa kampuni ya Zanztel inalipa jumla ya dola za kimarekani $200,000 sawa na TZ shs 260,000,000 Ikiwa ni malipo ya mrahaba Royalties, ambayo yanakwenda Tanzania Bara.

Mhe Spika,

ATHARI KWA KODI YA MAPATO

KODI YA MAPATO INCOME TAX

Kodi ya Mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika ni suala la Muunagno na linasimamiwa na sheria ya kodi ya Mapato ya mwaka 2004. Kwa hali ya sasa hivi kwa mujibu wa sheria hii mapato yanayotokana na kodi ya mapato kwa upande mmoja wa Muungano yanapokusanywa kuwa yanabakia katika sehemu ile ya Muungano.

Hivi sasa, kwa upande wa Mashirika kodi ya mapato kwa kampuni husika huwa inalipwa pale kampuni iliposajiliwa na yalipo Makao makuu yake. Kutokana na mapendekezo ya mshauri mwelekezi ya kuundwa kwa Wizara ya mafuta na TPDC kupewa mamlaka ya kusajili, kutoka leseni na usimamizi wa utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia kampuni zote za uchimbaji wa mafuta zitasajiliwa na vyombo hivyo viwili na mapato yote ya kodi ya mapato kwa makampuni italipwa Tanzania Bara na hivyokutokuchangia chochote katika mfuko wa serikali ya Mapinduzi Zanziabr.

Mhe Spika,
Zaidi ya hayo kwa kuwa mishahara ya wafanyakazi wa makampuni hayo itakuwa inatayarishwa Makao makuu ya Kampuni, ambayo yatakuwa Tanzania Bara ,malipo ya kodi ya mapato kw wafanya kazi hao(PAYE) nayo yatakuwa yanalipwa Tanzania Bara kila Mwezi .Mfano wa taasisi hizo ni BOT,JWTZ Jeshi lapolisi Usalama wa Taifa.

Mhe Spika,
Kodi nyengine ya mapato ambayo itakosekana kwa upande wa Zanziabr ikiwa Makampuni yatakuwa yanapewa leseni na kusajiliwa Tanzania Bara ni kodi ya ufundi stadi (SDL) ambayo huwa inalipwa kila mwezi kwa mujibu wa asilimia ya mishahara ya wafanyakazi. Mfano wa taasisi hizo ni BOT, JWTZ, Jeshi la Polisi Usalama wa Taifa.

Kodi za mapato ndizo ambazo zina uhakika kupatikana kwa asilimia kubwa katika nchi yeyote ile duniani. Hivyo kodi hizi kutokusanyawa hapa Zanzibar, itakuwa ni kasoro kubwa katika ukusanyaji wa mapato yatokanayo na uchimbaji mafuta hapa Zanzibar.

Hali hii ya ukosekanaji wa mapato yanayotokana na kodi ya mapato ndiyo inayojitokeza hivi sasa kwa wafanyakazi wote wa serikali ya Jamhuri ya Muungano ambapo kodi yote inalipwa Tanzania Bara ingawa wafanyakazi hao wanatumia huduma zote za Zanzibar ikiwemo matibabu, elimu, maji na barabara.

Katiba ya Zanzibar katika kifungu 133 (1) kinaeleza kuwa hakuna kodi ya aina yoyote itayotozwa isipokuwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi au kwa utaratibu uliowekwa kisheria na uliotiliwa nguvu ya kisheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.

Kifungu cha 133 (2) kinaendelea kueleza kuwa masharti yaliyomo katika kijifungu (1) cha kifungu hichi hayatalizuiya Bunge kutumia mamlaka yake ya kutoza kodi ya aina yoyote inayohusiana na mambo ya Muungano kwa mijbu wa madaraka ya bunge hilo kwa kujuwa kwamba mashauriano baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano yamefanywa na kukubalika sehemu zote mbili kabla ya kupitishwa sheria.

Kwa mujibu wa nyongeza ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania mapato yaliyoainishwa kuwa ni mapato ya Muungano ni:

 1. Kodi ya mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika
 2. Ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazotengenezwa Tanzania

Hapo ni dhahiri kwamba kodi zinazotozwa kwenye sekta ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta si za Muungano na Bunge limekiuka mamlaka yake kwa kupitisha sheria na kutoza kodi hizo bila ya kuwepo mashauriano kama vifungu hivi vya katiba vinavyoelekeza.

Mhe. Spika,

SHERIA NA KATIBA

Suala ya mafuta liliingizwa katika Katiba mwaka 1984 baada ya Bunge la Jamuhuri ya Muungano kupitisha sheria ya mwaka 1980 inayosimamia utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia.

Hata hivyo mukumbuke kwamba katika mkataba wa muda wa muungano wa Jamuhuri ya Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964 (Interim Constitution of the United Republic) haikuhusisha kabisa suala la mafuta katika vipengele kumi na moja vya kushirikiana vya makubaliano hayo kama ifuatayo:

 1. Katiba na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Bunge na Serikali na vilivyotajwa kuwa na mamlaka ya mwisho juu ya mambo yote yahusuyo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 2. Mambo ya Nchi za Nje
 3. Ulinzi
 4. Polisi
 5. Mamlaka juu ya mambo yanayohusika na hali ya hatari
 6. Uraia
 7. Uhamiaji
 8. Mikopo na biashara ya nje
 9. Utumishi katika Jamhuri ya Muunagno awa Tanzania
 10. Kodi ya mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika ,ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazotendenezwa nchini na kusimamiwa na Idara ya Forodha
 11. Bandari, mambo yanayohusu usafiri wa Anga, Posta na simu

Ni dhahir kuwa suala la Mafuta na gesi halikuwemo katika makubaliano ya Muunagno ya mwanzo (matters within the firt schedule to the Uniited Constitution).

Mhe. Spika
Ni wazi kwamba Zanzibar na Tanganyika zimeanzisha Muungano wa kisiasa na kila nchi kubaki na utawala wake isipokuwa mambo maalum yaliyoainishwa katika Makubaliano ya Mwanzo ya Muungano (Articles of the Union) na ndio maana katika sura ya pili ya katiba ya Zanzibar, kuna sura inayoeleza malengo na maaamuzi muhimu ya sera ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Katika kifungu cha 10(3), Katiba ya Zanziabr inaeleza bayana kwamba serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itadhibiti uchumi wa nchi kufuatana na misingi ya madhumuni yaliyoelezwa na katiba hii. Pia katika utaratibu utakaohakikisha huduma bora kabisa na itathibiti na kuendesha sekta muhimu za uchumi.

Mhe Spika,
Ushauri uliotolewa na Mshauri Mwelekezi kimsingi una mapungufu kadhaa kama yalivyoainishwa katika uchambuzi wa hadidu rejea. Kwa mfano, kutokuzingatia sheria za ndani za Zanzibar katika sekta nyingi ambazo zitahusika katika shughuli za utafutaji na uchimbaji wa mafuta hapa Zanzibar. Sheria za sekta ambazo si za Muunagno ambazo zitahusika moja kwa moja masuala ya utafiti na uchimbaji wa mafuta nagesi asilia ni kama zifuatazo:

 1. Sheria za Ardhi
 2. Sheria ya mazingira
 3. Sheria zinazotumika na mrajis wa makampuni
 4. Sheria zinazotumika na bodi ya Mapato ya Zanzibar
 5. Sheria ya misitu
 6. Sheria za Ajira
 7. Sheria ya Bima
 8. Sheria ya Uvuvi na bahari
 9. Sheria ya nishati (ambayo itakuwa tayari baada ya kukamilika matayarisho ya sera ya nishati hivi karibuni)

Mhe Spika,
Kabla hata suala hili la utafutaji na uchimbaji wa mafuta halijaanza katika sura ya sasa, ni vyema ikumbukwe kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikipoteza mapato mengi yanayotokana na utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi imekuwa ikichimbwa na kuuzwa, lakini Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haijapata mapato ya aina yeyote na kwa ngazi ya Wizara hii, hakujawahi kufanyika mawasiliano ya kushauriana kuhusiana na hilo, haidhuru kuwa ni rasilimali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa katiba.

Rasilimali ya mafuta na gesi asilia inatokana na ardhi. Kinachoshangaza hapa ni kuona kwamba Tanzania Bara ina maliasili nyingi zinazotokana za ardhi ambazo hazikuingizwa katika orodha ya Mambo ya Muungano.

Suala hili lina mantiki ya kufaidika kwa vilivyomo ardhini kwa Watanzania isilengwe kwa mafuta tu, ambayo tokea mwanzo ilionekana wazi kuwa ni rasilimali ambayo itafanyiwa kazi miaka ya mbeleni kabisa kufuatana na matokeo ya utafiti na teknolojia wakati dhahabu, almasi, makaa ya mawe na kadhalika yanaendelea kunufaisha upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mhe. Spika,
Kutokana na ukweli huo, kuna wasiwasi wenye ushahidi kwamba endapo mafuta yatachimbwa katika sura ya Muungano, yale yanayotokezea katika uchimbaji wa gesi asilia yatajirudi kwenye uchimbaji wa mafuta kwa sababu tayari hilo lipo.

Hakuna taarifa yoyote kwa Wizara yangu hata kuhusiana na yale mapato ambayo kwa sasa yanapatikana kwa vibali na kodi nyengine zinazohusiana na shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi wakati shughuli hizo zimekuwa zikiendelea kwa muda mrefu sasa.

Bila kuangalia uhalisi wa mapendekezo yake, maoni ya Mshauri Mwelekezi huyo yanaungana kwa kiasi kikubwa na madai ya Zanzibar juu ya masuala kadhaa yanayohusiana na suala la utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia nchini.

Mafuta na gesi asilia kuwa chini ya Wizara isiyo ya Muungano muundo wa TPDC kutokana na sura ya Muungano na kwa hivyo uhalali wake kuwa mashakani, utaratibu wa kupata mikataba ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia na kadhalika ni masuala yalioelezwa wazi wazi na Mshauri huyo kuwa na walakini mkubwa. Kwa namna nyingine mshauri mwelekezi huyo anathibitisha kwamba Zanzibar ilikuwa sahihi katika kuizuiya Kampuni ya Antrim kufanya shughuli zake Zanzibar kwa leseni ya TPDC.

Jambo hili lilikuwa gumu zaidi kwa mshauri mwelekezi kuelezea bayana ni juu ya lini mgawano unaopendekeza uanze, hali inayoweza kuonekana kama ni kutozingatia hisia za Wazanzibari za kutokunufaika na mgao wa gesi inayoendelea kuzalishwa sehemu kadhaa Tanzania Bara.

Vyenginevyo ni rahisi mtu kukaa na kufikiria kuwa upande wa pili wa Muungano tayari wameanza kutekeleza sehemu ya ushauri ulotolewa na Mshauri mwelekezi wa kutumia rasilimali kwa eneo iliopo (derivative principle) lakini wameshindwa kujua upeo wao kwa mujibu wa “principle” hio.

Mhe. Spika,
Kuridhia majadiliano kwa misingi ya ripoti ya Mshauri Mwelekezi huyo, ingawa kunaendana na makubaliano ya vikao vya kujadili kero za Muungano, huenda hatimaye kukaonekana kuwa ni ukiukwaji wa matakwa ya Wazanzibari walio wengi.

Ndani na nje ya vikao mbali mbali vya washiriki waliojadili suala hili wametaka kwamba masuali ya uchimbaji mafuta na gesi upande wa Zanzibar ushughulikiwe na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa vile taasisi zinazoshughulikia suala hilo kwa sasa haziwakilishi maslahi ya Zanzibar kwa ukamilifu na ipasavyo.pande zote mbili za Muungano zifanye maridhiano ya haraka kuandaa taratibu za kufikia hilo.

Ikumbukwe kuwa kila suala linapochukuliwa muda mrefu ndio Zanzibar inapokosa mapato yake kwa wakati na hilo ni kosa kubwa kiuchumi kuendesha kuwanyima wananchi maendeleo kwa wakati kwa visingizio vya kukosa mapato na kuendelea kuchukua mikopo ya nje kwa kutokuzitumia fursa za kiuchumi ziliopo ni kosa kubwa zaidi.

Kudhibiti uchumi wanchi kumesisitizwa katika katiba ya Zanzibar kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Hili limesisitizwa na sura ya pili kifungu cha 10 (3) cha katiba ya Zanizbar ya mwaka 1984 katika malengo ya kisiasa na Uchumi na sekta ya mafuta na gesi ni sekta nyeti na muhimu.

Mhe. Spika,

YA KUZINGATIA KWENDA MBELE (THE WAY FORWARD)

Katika ufafanuzi wa mshauri mwelekezi wa kampuni ya AUPEC juu ya suala la utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi, ripoti ya mshauri huyo ilielezea mifano na vigezo kutoka nchi mbali mbali za dunia (angalia uk.32-39) juu ya mfumo wa mgao wa gharama na mapato zikiwemo nchi za Canada, USA, UK, Nigeria, Australia na kadhalika. Mifano yote hiyo inaonyesha jinsi ya makubaliano yanavyopewa nguvu katika mgawanyo huo.

Hata kwa Serikali za Majimbo, seuze muungano wa nchi mbili kamili (two sovereign republics), Australia ikiwa ni shirikisho, serikali za shirikisho (State Governments) zimepewa mamlaka ya kutoa leseni na udhibiti na mrahaba kwa shughuli za utafutaji na uchimbaji wa mafuta katika nchi kavu na bahari za mamlaka zao (territorial water).

Serikali kuu nayo imekabidhiwa kazi ya kutoa leseni kwa bahari kuu (offshore), hata hivyo mapato ya kodi nyengine na mirahaba bado inakuwa inagawiwa kwa viwango vya makubaliano kati ya Serikali kuu na zile za shirikisho. India nayo inatoa leseni kwa mali asili kwa serikali kuu kwa maeneo ya bahari zote (off-shore) na Serikali za majimbo kutoa leseni kwa maeneo ya nchi kavu (on-Shore).

Serikali ya Muungano ya Falme za Kiarabu (U.AE) ni mfano mwengine ambao unaweza kutoa muongozo thabit. Muungano huu ulifanywa na nchi huru ambazo ni Abudhabi, Dubai, Sharjah, Ajman, Umm Al Quwain, Fujairah na Ras Al Khaimah. Kwa mujibu wa katiba yao, kila nchi (Imarati), ndani ya Muungano huo wa Falme za Kiarabu inasimamamia pekee masuala yote yanayohusiana na utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia na sekta nyingine nyeti za kiuchumi kama vile kodi zinazotokana na shughuli hizo.

Kifungu vya 22 na 23 vya katiba ya Muungano huo vinaweka wazi umuhimu wa mali ya umma na kuwa mali asilia za kila Imarat ni mali ya umma na zitasimamiwa na Imarat yenyewe na kuwa jamii itahifadhi na kutumia rasilimali hizo kwa maslahi ya uchumi wa nchi hiyo pekee.

Mhe Spika,
Mafuta na gesi asilia sio rasilimali endelevu. Uvunaji wake hupelekea kumalizika rasilimali hizo. Vile vile, tayari gesi imeendelea kuchimbwa na kuvunwa kila siku huko Tanzania Bara na Zanzibar ikiwa haijafaidika nayo ingawa ni rasilimali ya Muungano.

Bila ya kuzama sana kwenye matini ya Ripoti Tangulizi yenyewe, wajumbe wako wa jinsia zote, wa itikadi zote, wa dini zote, wa rika zote, wa safu zote, walikuwa na sauti moja ambayo mwangwi wake unaendelea kurindima. Nao ni kwamba kila upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ushughulikie kivyake rasilimali ya mafuta na gesi asilia.

Kwa bahati mbaya, kila mwangwi huu unaporindima kwa nia thabiti ya kuondoa manung’uniko na kutoaminiana ndani ya Muungano wetu, wasiwasi wa kuwa hii ni suala la kikatiba hudumaza dhamira za utatuzi wa tambo hii ambayo kwa Wazanzibari wengi inaonekana kuwa ndio kero mama miongoni mwa kero za Muungano.

Labda wenye wasiwasi wa aina hii, unatokana na tahadhari yao dhidi ya kuhalifu katiba ya Jamhuri ya Muungano wetu, wangejiuliza maswali matatu ya msingi ambayo naomba baadaye niruhusiwe kuyajibu:

 1. Bila ya kujali usahihi wa kifungu fulani cha katiba ya Muungano wa pande mbili, ni hekima kung’ang’ania kuwepo kwake ikiwa upande mmojawapo wa Muungano huo hatimaye unatokea kutoridhishwa nacho?
 2. Ni kipi bora: kubaki na kifungu cha katiba kinachotishia hatma ya Muungano au kukirekebisha, hata kama kwa kukiondoa, ili kuondoa tatizo hili?
 3. Je, hakuna njia ya kila upande wa Muungano kushughulikia rasilimali ya mafuta na gesi asilia kivyake bila ya kuvunja katiba ya Jamhuri ya Muungano?

Mhe. Spika,
Jawabu ya maswali matatu hayo, kwa maoni yangu, ndio dira ya kutupeleka kwenye bandari iliyo salama ya kulifumbua tatizo hilo. Maana wengi wetu hatuonekani kutafakari kwa kina zaidi dhana ya mafuta na gesi asilia kuwa ni suala la Muungano.

Suala la Elimu ya juu limeorodheshwa pia kuwa ni la Muungano, lakini bado elimu ya juu kwa Zanzibar inasimamiwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, wala wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ya SMT si ya Muungano, bila ya shaka kuna namna ya Wizara mbili hizi kushirikiana na kushauriana linapokuja suala mahsusi linalolazimu mtizamo wa pamoja kama swala la Muungano. Tume ya kuratibu vyuo vikuu ni mfano mmoja wapo.

Hali kama hii iko kwenye masuala ya takwimu, bandari, Usafiri wa Anga, n.k, ambapo kila upande wa Muungano unayaendesha kivyake kupitia Wizara zisizo za Muungano huku kukiwa na mashauriano na mashirikiano ya pamoja pale unapohitajika msimamo wa pamoja kimuungano.

Kama kwa masuali hayo imewezekana, bila ya kusemekana kuvunja Katiba, kwa nini isiwezekane kwa suala la mafuta na gesi asilia?

Inawezekana taratibu za kuyashughulikia maswali haya na mengineyo kwa namna hii zikawa zinakinzana na katiba ya Jamhuri ya Muungano.lakini kuendeshwa kwake kwa namna hii ni fundisho kwamba katiba ipo kutumikia watu sio watu kuitumikia katiba. Inapofikia wananchi kujiona wanaitumikia katiba kama wanavyoona Wazanzibari kwa swala hili, badala ya katiba kuwatumikia wao, marekebisho ni jambo la lazima. La sivyo vyote viwili, katiba na watu, vitaishia kwenye mtafaruku.

Hatma ya mtafaruku huu ni kubaki na ama Muungano bila ya katiba ambalo si jambo jema sana, au katiba bila ya Muungano ambalo maana na athari yake havihitaji kufafanuluwa zaidi.

Mhe Spika,
Kwa maana hiyo, maswali matatu niliyowahoji wale wanaoweka tahadhari ya kuvunja katiba kwa kuipitia badala ya kuizamia katiba yenyewe, yanapata jawabu tatu sahihi na rahisi:

 1. Si busara kubaki na kifungu cha katiba ya Muungano wa pande mbili iwapo upande mmoja utakuwa na sababu za msingi za kutoridhishwa na kifungu hicho
 2. Ni bora kurekebisha kasoro iliopo kwa kurekebisha, ikibidi hata kuondosha, kifungu kisichoridhisha upande mmojawapo kuliko kuhatarisha Muungano wenyewe
 3. Inawezekana kila upande wa Jamhuri ya Muungano kushughulikia suala la mafuta na gesi asilia kivyake bila ya kuvunja katiba ya jamhuri ya Muungano

Mhe Spika,
Ningeweza kuishia hapo na kusema kwamba hoja yangu imefikia tamati, lakini sitakuwa nimeutendea haki mchakato wa kutafakari ripoti ya Mshauri mwelekezi kwa mujibu wa makubaliano ya pande mbili za Muungano. Kadhalika nitakuwa nimeteka nyara dhamira halisi ya hoja yangu, ambayo ni kutafakari ripoti hiyo na hatimaye kuitolea mapendekezo.

Lakini nisingekuwa nimeitendea haki hoja yenyewe, iwapo nisingesema nilivyotangulia kuyasema, maana ushauri wa ripoti hii umeegemea kwenye nguzo ya kuwa mafuta ni swali la Muungano, na haukuangalia jinsi ya kuliingia swali hilo kwa mujibu wa maoni yetu wakati wa kujadili ripoti tangulizi, bila ya kuvunja katiba yenyewe.

Kwa maana hiyo ushauri wake umejenga kwenye dhana dhaifu – kama sio potofu kabisa. Umelenga sio kwenye kugawana gharama na faida za rasilimali hiyo kwa kadri inavyowezekana, bali kwa kadri inavyoonekana! Si kwa namna endelevu ya kulihitimisha tatizo hili lisilo la lazima, bali kulirutubisha kwa lishe ya woga na hadhari isiyo ya lazima, hali ambayo inalifanya kuwa sugu zaidi kutatuka kadri siku zinavyosonga.

Mhe. Spika,
Sisemi haya kwa kubeza kazi ngumu na nzito aliyofanya mshauri mwelekezi. Kila aliyeipitia ripoti hatakosa kupata elimu zaidi katika fani ya ugawanaji wa rasilimali ya mafuta na gesi asilia ulimwenguni. Ripoti imesheheni vigezo halisi vya jinsi nchi mbali mbali zinavyotegua mtego huu thakili unaotukabili, kwa namna ambayo uasilia na uhalisia wa tatizo hili kwao unabaki kuwa ni historia. Ripoti kwa namna yake, imetoa mapendekezo yanayozungumziwa na pande zote mbili zinazoshauriwa hivyo kupunguza ukubwa wa meza ya majadiliano na wingi wa muda unaohitajika.

Lakini kwa kuangalia zaidi Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuliko ile ya Zanzibar, naishia kuifananisha Ripoti hii na mapendekezo yake kuwa kama jahazi iliyochongwa ikachongeka, lakini ikachelezwa kwenye kina kifupi cha maji kuliko uzito wake. Itabaki kuwa ni mfano wa jahazi, lakini haitamvusha yeyote kuelekea hatma ya safari yake.

Mhe Spika
Ripoti ya Mshauri imelenga zaidi kwenye kulibakisha swala la mafuta kuwa ni la Muungano, ndio maana ikashauri mabadiliko kadhaa ya msingi ndani ya taasisi za Muungano na za Zanzibar, lakini imeshindwa kubaini kwamba Tanzania ina katiba mbili ambazo zinatakiwa kuoana, sio kukinzana.

Ushauri wa ripoti hii ukitekelezwa utaishia kwenye mgongano mkubwa wa kikatiba, kisheria, kiuchumi na kijamii. Tutajikuta tunarejea tena kwenye mtihani wa kutaka kulifumbia tatizo hili kwa maridhiano ya dharura badala ya makubaliano ya kudumu. Nitatoa mifano michache muhimu.
Kifungu cha 10(3) cha Katiba ya Zanzibar kinaekeza bayana kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itadhibiti uchumi wa nchi kufuatana na misingi iliyoelezwa na katiba yenyewe, pia katika utaratibu utakaohakikisha huduma bora kabisa.

Na itathibiti kuendesha sekta muhimu za Uchumi ili matakwa haya ya katiba yatekelezeke, maana yake ni kwamba usimamizi wa rasilimali ya Zanzibar unapaswa moja kwa moja kuwa mikononi mwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Katika utaratibu unaopendekezwa na ripoti hii, matakwa haya ya katiba ya Zanzibar hayatatekelezeka abadan. Kutazuka mgongano wa wazi baina ya katiba mbili zinazoongoza nchi yetu na pande mbili za Muungano.

Ardhi si mipngoni mwa mambo ya Muungano, na kwa hivyo kila upande wa Jamhuri ya Muungano una sheria zake za ardhi. Mafuta na gesi asilia ni rasilimali zinazopatikana chini ya ardhi pekee, iwe ardhi iliyofunikwa na maji au nchi kavu kabisa. Hakuna jinsi ya kuifikia rasilimali bila ya kugusa ardhi ya eneo husika ambayo, kama nilivyosema awali, si suala la Muungano.

Ni dhahir basi kwamba, bila ya kusawazisha sheria za ardhi zikalenga kwa makusudi kuyafanya mafuta na gesi asilia kuwa masuala ya Muungano, dhana ya mafuta na gesi kuwa ni ya Muungano ni ya nadharia tu. Kwa maana hiyo, ni rahisi zaidi kushughulikia swala la mafuta kama yanavyoshughulikiwa maswala ya Elimu ya Juu na mengineyo niliyoyaeleza awali, kuliko kurekebisha katiba yenyewe ili utata wa swala la mafuta kuwa ni la Muungano ukaondoka.

Maana sheria zinazopaswa kurekebisha ili swali hili lisiendelee kuwa ni la nadharia ni nyingi kwa pande zote: Mazingira, Usajili wa makampuni, misitu, bodi za mapato, Ajira, Bima, Uvuvi na Bahari, Nisahati na kadhalika.

Kifungu cha 4 cha Sura ya Kwanza ya Katiba ya Zanzibar kinaipa nguvu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutawala mambo ya ndani ya Zanzibar. Hii haitekelezeki na haitatekelezeka iwapo swala la utafutaji, uchimbaji na uuzaji mafuta kwa maeneo yaliyotambuliwa kuwa ya Zanzibar na Kifungu 2 (1) Sura ya Kwanza cha Katiba ya Zanzibar yatakuwa moja kwa moja chini ya usimamizi wa taasisi isiyo ya Zanzibar.

Mhe. Spika,
Mifano hii, kwa niaba ya mengine ndani ya ripoti hiyo, inapunguza kazi ya kuendelea kuichambua zaidi ripoti hii ya Mshauri Mwelekezi. Itasaidia zaidi kazi yake iwapo mawazo yetu haya safari hii yatazingatiwa kwa uzito sawa na yale ya kulinda katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo sote tutaiamini na kuiheshimu. Naamini, kwa dhati ya nafsi yangu, kwamba iwapo ripoti yake ya mwisho itazingatia hoja zetu hizi za msingi, kazi ya kuzishauri serikali zetu mbili juu ya namna mwafaka ya kugawana gharama na faida ya rasilimali ya mafuta na gesi asilia itakuwa nyepesi.

Aelewe kwamba mafanikio ya ripoti ya kampuni yake si kuwa na hati iliyoandikika na kueleweka tu, lakini ambayo kila upande utakuwa tayari kutekeleza ushauri wake.

Mhe. Spika,
Baada ya kutafakari kwa kina mapendekezo ya rasimu ya mashauri Mwelekezi, haya sasa ni mapendekezo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa Baraza hili tukufu:
• Ardhi na bahari ndani ya Zanzibar (territorial waters) maeneo ambayo kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar, Sura ya Kwanza, Kifungu cha 2(1) ni miliki ya Zanzibar, katika maeneo hayo, usimamizi, udhibiti na uendeshaji wa shughuli zote zinazohusikana na utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia, uwe wa Zanzibar pekee kama katiba yetu na matakwa ya Wazanzibari yanavyoelekeza. Dhana hii inapata nguvu kwa kuingatia kuwa yanaweza kusababisha uharibifu mkubwa wa eneo la visiwa vya Zanzibar na maji yake (territorial sea) eneo dogo sana ukizingatia maeneo ambayo yametengwa kitaifa kwa shughuli hii.

Uharibifu wa eneo hilo ni uharibifu wa Zanzibar na hatima ya watu wake. Hili ni jambo zito kwa kulikabidhisha kwa taasisi yoyote nje ya Zanzibar kwa maamuzi, kama ilivyo sasa kwa mkataba wa Antrim bila kuhusisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Vyenginevyo itakuwa tumekabidhi mustakbali wa Zanzibar katika mikono ya Wizara ya Nishati na Madini inayosimamiwa na Waziri aliye nje ya mamlaka ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanziabr. Kwa sababu hio, ni budi kuangalia mifano mengine zaidi ikiwa pamoja na mifano ya nchi yenye miundo ya Muungano iliyofanana tu na yetu kama zilivyofafanuliwa kwa upana zaidi katika waraka wa Mshauri Mwelekezi (ukurasa 32-40).

• Serikali inashauri kuwa sasa wakati umefika kwa Zanzibar kuwa na chombo chake kusimamia mambo yote yanayohusiana na utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia na mengineyo yanayoandamana nayo. Chombo hiki kitakuawa sawa na ile TPDC kwa Tanzania Bara. Chombo hicho kuwa na mamlaka yake kamili hapa Zanzibar kwa kusimamia masuala ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia. Hii ni njia pekee ya kuondoa migongano ya madaraka na maslahi (vested interest) na pia ni njia pekee ya kuhakiksha haki za Zanzibar na watu wake zinalindwa kwa sasa na hasa mbeleni.

• Kwa upande wa bahari kuu (EEZ) serikali inashauri Baraza la Wawakilishi kukubali mashirikiano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa eneo hilo pekee kwa makubaliano maalum na sio kwa muundo wa sasa wa taasisi na sheria na kwamba Zanzibar itakuwa na ushiriki sawa (Equal Partner) kwa makubaliano yote yatakayofikiwa kwa eneo hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ili kugharamia shughuli za Muungano, utaratibu wa kuchangia kama unavyoendeshwa sasa uendelee na kila upande ulazimike kuchangia kwa kiwango kile kitakachokubalika kwa thamani aidha ya fedha taslim au kiwango cha mafuta chenye thamani ile.

Mhe. Spika,
Mapendekezo hayo ya serikali yamesisitiza maeneo hayo matatu, kwani mengineyo ikiwemo mikataba na aina ya mikataba, kodi za mapato, kodi za ardhi, mafuta yatakayozalishwa (production oil), mafuta yatakayofidia gharama (cost oil), mafuta yakayobaki kwa faida (profit oil), mrahaba, mazingira na kadhalika, ni mambo mazito lakini yana uwiyano duniani kote (standard with variation from country to country) na yatajadiliwa kwa miafaka kati yetu baada ya kutatuliwa haya ya msingi.

Mhe. Spika,
Kama nilivyotangulia kusema, hoja hii imelenga katika kuimarisha Muungano wetu kwa kuondoa “kero mama” ya Muungano, imejengwa kwa kufuata mifano halisi ya nchi zenye Muungano unaofanana kwa namna fulani na wetu na, kwa hivyo, mapeandekezo haya hayatakuwa mageni ndani ya ulimwengu huu wa utandawazi.

Zanzibar, kama mshiriki sawa katika Muungano, ina haki kabisa kupeleka mapendekezo yake kwa pale inapohisi ni sawa kufanya hivyo kwa maslahi yake na maslahi ya Muungano wetu, kwa nia ya kuepusha migogoro isiyokuwa ya lazima.

Naambatanisha na rasimu za Shirika la Mafuta la T.P.D.C linaloonesha maeneo yanayoendelea na shughuli za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia katika Tanzania.

Mhe. Spika,
Kwa heshima na taadhima kubwa naomba kuwasilisha.

Ahsante.

MANSOUR Y. HIMID (MBM)
WAZIRI, WIZARA YA MAJI UJENZI NISHATI NA ARDHI
ZANZIBAR

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.