Visiwa vya Zanzibar ni katika nchi chache za Kiafrika kusini mwa Jangwa la Sahara zilizokuwa maarufu sana katika historia na fungamano zake za kibiashara na nchi mbali mbali kwa karne nyingi….Maendeleo na kiwango kikubwa cha ustaarabu kilichofikiwa na watu wa visiwa hivi na mwambao mzima wa Afrika ya Mashariki, yamethibitishwa na masimulizi na maandishi mengi ya watu wa kaze waliowahi kuzitembelea sehemu hizi zaidi ya miaka elfu mbili nyuma. Mwanajiografia na mnajimu mashuhuri WA Alexandria Ptolemy, Kwa mfano, amethibitisha kuweko kwa miji mingi katika mwambao wa Afrika ya Mashariki…..Maandishi ya wasafiri na wanajiografia wa baadae wa Kiarabu akina al-Masud (96), Ibn Batuta (1304- 1369) yametoa maelezo mengi zaidi yenye kuhusiana na maisha ya wenyeji wa sehemu hizi.

Hamad H. Omar

Utangulizi: Historia Fupi ya Zanzibar

Zanzibar ina historia ndefu kana kisiwa kilichoendelea kibiashara na pia katika mahusiano ya kimataifa. Kama ni kisiwa kikawa kinatembelewa na wageni kutoka nchi nyingi ulimwenguni na kufaidika na ujuzi na utaalamu wa ageni hawa. Wengi wao wakafanya maskani yao hapa bada ya kuvutiwa na mandhari na tabia za wakaazi wake. Visiwa hivi vikaendelea kuwa na neema na pia wananchi wake kupendana na kuheshimiana. Utamaduni na hulka za Wazanzibari zikawa zikipigiwa mfano.

Leo, wakati bado baadhi yetu tuhai tunawarithisha watoto wetu uoza, mpaka tukafikiwa kuambiwa kuwa Zanzibar si nchi. Vijana wetu walioelimika japo kidogo wanaihama nchi kutafuta maisha; matajiri wanahamia bara kwenda kutajirika zaidi; tumesalia wazee waliokwisastaafu pamoja na waliokosa nafasi ya kuondoka. Heshima ya Zanzibar iliojengeka kwa makarne haipo tena.

Wale ambao ndio wa kushiriki katika kuijenga Zanzibar wanahama; badala yake nchi inasheheni wauza miwani, karanga pamoja na vibaka kutoka bara. Imekuwa aje!

Kuna usemi maarufu unaosema: “Zumari likipigwa Zanzibar walio nyanda hucheza”

Leo ukweli ni kwamba magoma yakipigwa Bara, Wazanzibari wanahemka!

Nyerere ananukuliwa kusema: “ningelikuwa na uwezo wa kukiburuta kisiwa cha Zanzibar na kukipeleka katikakati ya bahari ya Hindi, hapana sifanyi MZAHA, naogopa kitakuja kutupa taabu sana baadae”.

Kuepekuna na taabu hizo Nyerere aliamua kwamba Zanzibar lazima iuwawe kama Dola na kubaki wilaya inayopokea amri kutoka Tanganyika.

Nyerere na wenzanke pamoja na Watanganyika wengi wa hivi sasa wana amini kabisa kwamba Zanzibar ilikuwa sehemu ya Tanganyika. Haya ni maajabu kutoka kwa msomi kama Nyerere, kwani Zanzibar sio siri kwamba Zanzibar ikijulikana ulimwenguni hata kabla Tanganyika “kuvumbuliwa”.

Yalipopotokea mapinduzi ya Zanzibar, Nyerere akaona sasa nafasi ya kutekeleza ndoto yake imejitokeza; lakini hakufurahiwa na akapata mashaka alipotambuwa kwamba akina Abdulrahman Babu ndio waliokuwa nguvu muhimu nyuma ya mapinduzi hayo.

Kutokana na usuhuba wake na nchi za Magharibi, ule woga wake wa Zanzibar kumpa taabu ukazidi alipata kiwewe. Ikabidi atafute njia za haraka za kuliviza “tishio” la Zanzibar.

Khofu zake zililingana na zile za Mabwana zake wa wakati huo, Marekani na Mngereza, Zanzibar itakuwa Cuba ya Afrika ya Mashariki! Lazima idhibitiwe haraka. Mbinu zikabuniwa haraka haraka za kuiuwa Zanzibar haukuwa Muungano tokea siku ya mwanzo (day one), tumefutwa! Hiyo ndio ilikuwa azma ya Nyerere, lakini masikini Karume akaona anahakikishiwa utawala wake dhidi ya “Makomred”.

Haya yalijidhihirisha kwa vitendo na mapema; Wazalendo wa Kizanzibari waliyatambuwa zamani, ila wakawa hawana hila na woga umewazidi baada ya ukandamizaji wa miongo kadha.

Khofu ya Nyererere haikuwa Ucuba tu, bali Uislam. Nuru ya Uislam Zanzibar ilizagaa duniani kote. Ilibarikiwa na Maulamaa waliobobea. Zanzibar ikawa kivutio kwa Wacha Mungu- leo Zanzibar ni kivutio cha wala unga na mafisadi wa kila aina.

Nyerere alikuwa Mkatholiki mzuri, na hili halikuwa siri. Wakati anawabana Wazanzibari na kuonesha kama huu ndio mfano mzuri wa Umoja wa Kiafrika, hakusita kuiunga mkono Biafra ya Kikristo kujitenga na Nigeria!

Hapa Zanzibar ikapata adui mwingine: Kanisa. Zanzibar ilipopata uhuru wake Dec 10, 1963, ilikuwa na makanisa manne: la Kimoto, Minara Miwili, Mbweni na Machui. Leo Zanzibar ina Makanisa karibu mia tatu Haya yanadhihirisha nini? Ni jambo lisilo na ubishi kwamba Wailsam Zanzibar wakipindukia 97%? Au tumepata wahamiaji kwa maelfu na maelefu ambao watayatumia makanisa haya, au ni uchokozi wa makusudi wa kutujengea makanisa yasiyosaliwa ?! Yote haya mawili yanadhihirisha moja katika nia ya muungano kuuminya Uislam.

Kwa kupitia Muungano kanisa limeizuia Zanzibar kujiunga na Jumuia ya Nchi za Kiislam.

Watawala wetu wamekuwa wakitumia mbinu nyingi, za makusudi na zilizojitokeza, kuifisidi Zanzibar kiuchumi, kimaadili na kisiasa. Wamefanikiwa kiasi cha kuwashangaza hata wenyewe!

Mheshimiwa Pinda akawaamsha waliolala, Wazanzibari tunamshukuru, kwa kuelezwa waziwazi kwamba hii si nchi; na akakariri tena kwa kujiamini kwamba Zanzibar sio nchi wala sio kwamba ulimi umeteleza. Hizo ndio jeuri za watawala wetu. Kifikra yeye hakuwa na shaka kwamba Zanzibar haipo tena, na ikadhihirika kwamba hayo ndio mawazo ya viongozi wengi wa Tanganyika ambao walionesha hasira kubwa kwa wale Wazanzibari “waliothubutu” kupinga kauli ya Pinda. Kwao Zanzibar haina tafauti na kisiwa cha Mafia!

Utalii
Zanzibar imebahatika kuwa na kivutio kikubwa kwa watalii kutokana na historia yake ndefu pamoja na majengo ya asili, pamoja na mivutio ya fukwe za kupendeza. Hatuhitaji vinyago wala michoro ya tinga tinga.

Ni dhahir kwamba utalii umetumiwa kama moja katika nyenzo za kuifisidi Zanzibar sio kuiletea maendeleo. Athari za utalii Zanzibar si kwamba ni mambo yaliyojitokeza tu, lakini ni njama.

Laiti Utalii huu ungedhibitiwa na Wazanzibari wenyewe, wenye kujali utamaduni, hulka na maendeleo ya Zanzibar, utalii huu ungelichukuwa mwenendo nwingine. Seychelles ni kisiwa kidogo hata kuliko Zanzibar, lakini kimepiga hatuwa kubwa kiuchumi kutokana na utalii. Huko hawaingii wala unga wanaokwenda huko ni watalii ‘wastaarabu” na wenye mapesa wanayoyatumia. Kinyume na utalii wetu wa kuwakaribisha mimafia ya Kitaliana, wasioingiza pesa isipokuwa ufisadi. Baada ya kuifisidi Malindi, Kenya wamehamia Zanzibar. Watalii hawa hawaingizi chochote mbali na kodi za uwanja wa ndege. Malipo yote yanalipwa huko huko Rome na Milan. Hapa tunahesabu vichwa tunaingiza watalii laki na wanaendelea kuongezeka, jee wanaingiza dola ngapi? Kimya!

Zaidi ya asili mia thamanini ya wafanya kazi katika mahoteli haya ya kitalii ni wageni, kutoka Bara (sheria za Kamishna ya Utalii inaeleza wazi kwamba biashara za utalii itaajiri Wazanzibari tu! Eti hata tour guides wanatoka Tanganyika!), Kenya pamoja na Ulaya. Kwa hivyo hata madai ya kwamba utalii unawapatia Wazanzibari ajira ni uongo.

Mitaa ya Mji Mkongwe imefisidika kwa kila namna! Barabara ya Gizenga kuanzia posta, kupitia kwa Jani mpaka Jamati ya Maismailia, imetekwa na Wameru na kimeru ndio lugha kubwa inayozungumzwa. Hapa unazongwa na vinyago, mashanga na michoro ya tinga tinga, hapa utambulisho wa Mzanzibari makasha ya njumu, mikeka au vitu vya asili vya shaba na kama hivyo havipo. Ngome Kongwe pia imevamiwa na hao hao wenye vinyago uwanja wa ndani umejaa Wameru. “Wamasai” ndio walinzi wa majengo!

Shangani ilikuwa tulivu na yenye kupendeza leo imefura wala unga, makahba na waharibifu wa kila aina.

Kwa hivyo utalii umetumika kutuharibia maadili yenu, kutujazia wageni na kuharibu mazingira ya Zanzibar, hasa katika fukwe kama za Nungwi eneo ambalo ndio linavuma zaidi kwa uchafu wa vitendo.

Ufisadi huu haukuishia mjini bali mpaka huko mashamba, vijiji vingi vimeathirika kutokana na machafu ya watalii hawa, hata kusababisha magomvi ya kifamilia. Makahba hutoka bara, na bila ya shaka, taratibu na kwa pole pole, wasichana wa Kizanzibari wamekuwa wakiingia katika biashara hiyo. Kuna majumba yanayoonesha video za ufuska kwa kiingilio, ambamo mpaka watoto wanaingia. Moja katika hizo inaambiwa ipo mfereji wa wima, si mbali na Polisi stesheni ya N’gambo

Mabaa
Siku ya Uhuru wa Zanzibar, bar zilikuwepo mji mkongwe zikihisabika kwa vidole. Leo hazina idadi, wala udhibiti, sheria ya biashara ya ulevi imetupwa huko. Leo hata mtoto mdogo akitaka ulevi ananunuwa (katika madisco na baadhi ya “supermarkets”). Mabaa yameenea mpaka mashamba.

Katikati ya Mji Mkongwe, eneo la Soko Mhogo, kuna bar iliyofunguliwa miaka mingi iliyopita, ni bar iliyozungukwa na makuti, wala sio ndogo. Karibu hapo hapo pana na mkahawa, eneo la uchafu wa kutisha. Bar hii inaendeshwa na Mzanzibari mtu mzima kwa umri, anayeonekana mahshum. Na ndiye yeye mwenye jengo ambalo ndani wamejazana watu kutoka Bara. Hali inayoonesha kiwango tulichofikia Wazanzibari kwa kujali zaidi pesa, huku tukiwa tunasahau hata ule utu wetu, wacha uzalendo.

Moja katika athari kubwa za huu utalii wetu na sera zake ni kuja kwa wageni wengi wa Kizungu ambao wamekuwa wakinunuwa viwanja na maeneo makubwa sehemu za fukweni. Mzanzibari wa leo, huu ndio ukweli, ameweka mbele pesa na wako tayari kuuza chochote na kwa yeyote, au kusaidia kuuza (kama madalali). Inasemekana maeneo makubwa ya pwani-pwani yameshauzwa.

Kutoweka ka Uzalendo

Uonevu na ukandamizajia wa miaka arubaini ushay, vimeidhoofisha jamii ya Zanzibar kwa kila namna: kimaadili, kimawazo, kiutamaduni na umasikini uliokithiri.

Mzanzibari amepoteza utambulisho wake, na wala hana khabari, yumo mbiyoni kupambana na maisha kwa wale wenye hali duni, au kuzidi kujitayarisha kwa wale waliofanikiiwa kibiashara kama ni kwa kihalali au kiharamu!

Matajiri
Matajiri ndio waliojisahau kama wao ni Wazanzibari katika kusaka utajiri. Baadhi yao wamekuwa masahiba wakubwa wa watawala hali inayowaruhusu kufanya wanavyotaka katika kuendesha biashara zao bila ya kudhibitiwa.Wazanzibari tumeshalishwa mchele mbovu, unga mbovu na mafuta mabovu. Hapakuwa na hata mmoja aliyefikishwa mahakamani juu ya kwamba wanaeleweka vizuri.

Baada ya kuwekwa mazingira magumu kwa wawekezaji hapa Zanzibar pamoja na kuiuwa bandari ya Zanzibar kunakoendelezwa na Tanganyika na kwa utiifu wa SMZ, wafanya biashara hao wameamuwa kuhamishia biashara zao bara.

Ushuru na viwanda
Ni dhahir kwamba hii ni sehemu ya mkakati wa kuinyonga Zanzibar kiuchumi, kuweka ushuru mkubwa; kutowa ushuru upya bidhaa zilizopitia Zanzibar kwenda Dar; pia kuvitoza ushuru vitu vilivyotengenezwa Zanzibar kwenda Bara. Viwanda vingi vimefungwa Zanzibar kwa kunyimwa soko la Bara vikiwemo kiwanda cha Windows 2000 (kilichokuwa kikitengeneza madisirisha ya alluminium kwa technology ya kisasa), kiwanda cha kusindikia mafuta cha Alghurair, kutoka Emirates, mbali na viwanda vidogo vidogo vingi, vikiwemo vya masufuria, nyaya za umeme, nguo n.k.).

Bidhaa
Halafu Zanzibar hairuhusiwi kuagiza bidhaa zake kutoka nje ya Tanzania kwa bei nafuu, na tunalazimishwa kunuwa bidhaa za bara kama saruji, mabati na vinginevyo kwa bei ya juu kuvisaidia viwanda vya Bara! Mzanzibari anahusika vipi na kuvisaidia viwanda vya bara? Hali ya Mzanzibari inazidi kuwa ngumu kwa namna mbili, viwanda vinauliwa na kuwakosesha ajira; huku wanalazimishwa kununuwa bidhaa kwa bei ya juu, juu ya umasikini wao.

Ajira
Ajira Zanzibar ni kitu adimu. Ajira sana sana hupatikana katika mahoteli, na huku Wazanzibari sio wanaopewa kipaumbele. Waajiri wanapoajiri wanateuwa wanaowataka na kuwakwepa wasiyowataka, kisiasa zaidi kuliko kwa sifa za ajira. Hali hii inazidisha kuporomoka kwa maadili, watoto na vijana kutokana na ukosefu wa ajira hawajali tena wazee wao na wanajifanyia wanavyotaka. Vijana hawa, ni wazee na viongozi wa kesho, wanaishia kuwa wahuni, wala unga na makuwadi!
Wale ambao wametulia na kufanikiwa kibiashara, hawana habari na mustakbal wa nchi yao. Wanasalilika nchini mazezeta, rahisi kunuliwa na kutawaliwa; hii ndio hali.

Soko na bandari huru
Leo Zanzibar hakuna hata eneo moja la kutia moyo. Kilimo kimeporomoka, kila tunachokila kinatoka bara, mchele, maharagwe, mboga mboga za aina zote, hata matunda kama machungwa, mafenesi, embe n.k.. Katika kuuwa viwanda Zanzibar, Tanganyika imejihakikishia soko la Zanzibar kwa kila aina ya bidhaa.

Mpango wa bandari huru na eneo na maeneo huru ya uzalishaji yamesitishwa na wazo hilo sasa linatekelezwa Bara.

Hali ya kijamii
Hali ya afya nayo ni ya kusikitisha, wagonjwa hata wa malaria kali, au kavunjika mguu inabidi mgonjwa akimbilie DAR, au afe kama hana uwezo!
Zanzibar ilikuwa na sifa kwa wasomi, leo katika Nyanja ya masomo inaonekana Zanzibar imeshika mkia wa Afrika ya mashariki kwenye matokeo ya mitihani.

Siasa za Zanzibar
Uongozi wa kisiasa Zanzibar umeshindwa kuwaongoza nchi na wananchi. Siasa za Zanzibar zaidi za ushabik kuliko uwelewo wa kisiasa. Harakati za siasa zinashuhudiwa wakati wa kampeni za chaguzi, chaguzi ambazo zimekuwa zikiwaletea Wazanzibari maafa makubwa ya kupigwa na hata kuuwawa. Baada ya chaguzi hizo, zinaanza siasa za kuleta maridhiano baina ya vyama, ambayo nayo hayajaleta matunda yoyote. Wananchi hawaelezwi kitu kuhusu mazungumzo haya na mwisho ndio wakaambiwa mapema kwamba mazungumzo ni siri za wajumbe katika mazungumzo hayo. Mazungumzo kuhusu mustkbal wao wanaambiwa ni siri! Na hiyo siri sasa, imefichuka hamna lolote!

Chama cha CUF kinadai kuungwa mkono na Wazanzibari wengi, na kudaiwa kwamba kimeshinda chaguzi zote. Inadaiwa kwamba hayo madai hayajotokana na kazi iliyofanywa na chama hicho kuhamasisha na kuelimisha umma. Chama sijui kama kina taratibu za kufunza makada wa kukijenga Chama, kuuelimisha umma historia ya Zanzibar, matatizo yaliyowakabili, kiuchumi, kijamii na kisiasa na yale yanayohitajika kufanyika kuikombowa nchi yao kwa amani.

CUF-ZNZ
Chama kinaonekana kutokuwa na Jumuiya madhubuti za Vijana, Jumuiya za Wanawake, Wanafunzi, na Wazee na kila Jumuiya ikiwa na Jukumu la kuhamasisha wanachama wake, badala yake uongozi finyu wa wachache umen´gan´gánia khatamu baina yao na kuwanyima vijana na akina mama nafasi hata chembe ya kuwa na la kusema. Badala ya kukimbilia nchi za Magharibi, ambao ni washiriki katika kuikandamiza Zanzibar, wangelianzisha uhusiano mzuri na vyama katika nchi za dunia ya tatu kama Uchina, Iran, Cuba, na nchi nyingine kama hizo. Kutoka nchi hizi, CUF ingeweza kujifunza mengi juu ya kujenga Chama na jinsi Chama kinavyofanya kazi na wanachama wake kwa ajili ya maendeleo ya nchi zao.

CUF inaweza kujifunza mikakati inayotumiwa na wanaharakati madhubuti, kama katika kuinuwa hali za wanachama wao na wananchi kwa jumla, hata kabla ya kushika madaraka, wangekuwa wakijenga maskuli, mahospitali pamoja na kuwa na miradi ya kuwapatia ajira wanachama wake. Hapa ndio utiifu wa Chama unapojengeka, sio ushabik tu. Wananchi wanajua kuwa Chama kinajali maslahi yao. Kwanini CUF ishindwe kuanzisha kitengo cha uchumi na kuanzisha miradi kama ya kilimo na hata ya biashara.

CCM-ZNZ
Zanzibar inafisidika, na haina mtetezi, ASP ilipindua kwa makusudi ya kutetea maslahi ya masikini na mnyonge, kwa maslahi ya Zanzibar na Raisi wake, Bunge lake , Bendera yake. Leo ASP imeuzwa na kutiwa katika CCM ambamo haina lake hata moja. Vita vikuu vya CCM-ZNZ ni kujilinda na kung’olewa madarkani na sio kupiga vita umasikini !! Waliotajirika wanazidi kujitajirisha. Ufisadi unaofanyika Zanzibar, ukichukuliwa kwa ukubwa wake (proportionally) ni mkubwa kuliko huo wa kina Mramba, ASP iko wapi kumlinda mfukara? Na si siri. Nchi inauzwa, sasa labda nusu ya visiwa vya Zanzibar vimeshauzwa, tunaangalia tu! Wananchi wanasononeshwa na upandaji wa bei za vitu, hasa vyakula, hamna anayesema hata twi!

Wawakilishi wa CCM-ZNZ wamekubali kufungwa midomo na watu watatu tu walipokuwa pale walipokuwa wakiitetea nchi na mafuta yao.

Umeme
Zanzibar ilikosa umeme kwa mwezi mzima. Hakuna nchi yoyote duniani iliyowahi kupatwa na janga kama hilo. Wananchi wengi walikosa ajira na wengine wakaharibikiwa na bishara zao, kimya kilekile kimetanda. Si wanasiasa, wasomi au wanaharakati wa aina yoyote walioonesha hasira. Hata hao watawala wetu hawakuonesha huruma hata ya kumleta hata waziri mdogo kuwapoza wazanzibari. Hili si jambo la Muungano, juu ya kwamba siku zote wanatukumbusha kwamba sisi ni ndugu zao!

Ububu wa Wazanzibari umetufukisha pabaya. Msiba mkubwa umetufika.

Wanachokihitaji Wazanzibari kwa sasa ni siasa na diplomasia za kuikomboa Zanzibar, iwe huru tena. Demokrasia ya Kitanzania inazidi kututia kitanzi.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.