Na Farouk Amour

UMOJA, UHURU, UADILIFU

Ifuatayo ni Qauli ya Umoja wa Wazalendo

Kukhusu Pendekezo la Katiba ya Zanzibar

na Mfumo wa Uchaguzi

Kujenga Umoja, Kuondowa Mfarakano

Katika juhudi na mbinu zetu za kujenga Umoja na kuondowa mfarakano, ni dharura kutambuwa misingi na miko ya Umoja wa kweli. Umoja wa kweli na ambao unatarajiwa kudumu na kuleta matunda ya kheri, ni “Umoja wa Kizalendo”, Umoja unaojengwa katika misingi ya “kushauriyana na kushirikiyana”. Kinyume cha hivi ni ule umoja wa kikoloni, umoja wa maneno bila ya vitendo, ni mtawala kumburura mtawaliwa kwa maslaha ya mtawala.

Kuzingatia haya, Umoja wa Wazalendo unatambuwa kwamba:

§ Njia sahihi na ya dhati ya kujenga Umoja wa Kizalendo, ni kubomowa mfarakano na kujenga mshikamano.

§ Njia sahihi na ya dhati ya kubomowa mfarakano na kujenga mshikamano ni kujenga ushirikiano katika madaraka.

§ Njia sahihi na ya dhati ya kujenga ushirikiano katika madaraka ni kujengwa Katiba katika misingi ya ushirikiano.

Ili kusaidia katika ujenzi wa Katiba ya hali hio, Umoja wa Wazalendo unapendekeza na kushauri ifuatavyo:

Ushirikiyano ni Msingi wa Maendeleo

Mfumo wa uchaguzi tunaokwenda nao nchini mwetu kwa miaka hadi hivi sasa – mfumo wa: “mmoja kuchukuwa vyote na wa pili kuondokea patupu” (the winner take all) ni mfumo fisadi. Kila siku inazidi kutudhihirikia kuwa mfumo huu ndiyo sababu kuu ya mizozo na mapambano yenye kufika kupotezwa mali na roho kadhaa wa kadhaa katika kila uchaguzi. La uovu zaidi ni hivi kuwa mfumo huu wa uchaguzi huleta “mfumo wa utawala wa kidikteta”. Utawala wa kidikteta ni utawala ambao wengi kuwatawala wachache bila ya ridhaa zao, au wachache kuwatawala wengi bila ya ridhaa zao.

Hukosekana ridhaa za wananchi (baadhi yao , wakiwa wengi au kidogo), kwa vile kuwa Wawakilishi wao wananyimwa fursa za kushiriki katika mipango ya uwendeshaji wa mambo ya nchi yao ; badala yake huwekwa ni “wapinzani”. Kutokana na hali hii, huu mfumo wa kidikteta unaendelea kuwa ni msingi wa kila uovu na adui mkuu wa maendeleo na amani. Hivi ni kwa vile kuwa mfumo huu daima unajenga na unakuza mapambano baina ya wananchi na wananchi, na baina ya wananchi na watawala. Kwa hivi kuubaini uovu huu, Wazanzibari tumeamuwa kubomowa kabisa upambano na kujenga ushirikiano. Katika kufanya hivyo, vilevile tutakuwa tumo katika kujenga na kuhifadhi misingi ya utawala bora na dimokrasia ya kweli.

Kwahivyobasi

 1. Kutakuwa na Serikali ya Zanzibar (SZ) ( Zanzibar Government (ZG)), yenye kuongozwa na kusimamiwa na Waziri Mkuu (Prime Minister), yenye kusailika na kuwajibika juu ya (answerable and accountable) Baraza la Mawaziri; itakayokuwa katika mfumo wa Sirikali ya Umma (National Government). 
  
 2. Rais atakuwa ni Mkuu wa Dola*. 
  
 3. Waziri Mkuu atakuwa ni Mkuu wa Sirikali. 
  
 4. Kutakuwa na uchaguzi mmoja (tu) - uchaguzi wa Wakilishi wa Baraza la Wawakilishi. 
  
 • Atakuwa Rais wa Kikatiba (Constitutional President). Atakuwa Mkuu wa Nchi na alama na hishima ya Nchi. Atakuwa si mwenye madaraka wala wadhifa wa kisirikali.
  1. Hakutakuwa na uchaguzi wa Rais**.
 1. Baraza la Wawakilishi mara tu likikaa kwenye kikao chake cha kwanza litachaguwa kwa kura ya siri Spika wa Baraza la Wawakilishi wa muda . 
  
 2. Baraza la Wawakilishi katika kikao chake hiki (6 juu) litatunga shuruti na utaratibu wa kuchaguliwa Rais, Waziri Mkuu, Spika na Makamu. 
  
 3. Wakushika nyadhifa zifuatazo watachaguliwa na Baraza la Wawakilishi kwa kura ya siri kulingana na ujuzi, maarifa na shuruti zilizotungwa na Baraza la Wawakilishi (7 juu):

Jaji Mkuu, Kamati ya Jaji Mkuu, Wakuu wa Mikoa, (Regional Commissioners), Mkuu wa Polisi, Mkuu wa Jeshi, Mkuu wa Usalama, Mkuu wa Magereza, Muendeshaji Mashtaka Mkuu wa Serikali (Attorney General), Mabalozi; na nyadhifa zote nyeti na zenye dhamana kubwa za mfano wa hizi tulizozitaja.

 1. Kwa kuwa Umoja wa Taifa (National Unity) ndio lengo kuu kulingana na Uhuru na maendeleo ya nchi, sirikali itakuwa katika mfumo wa “Sirikali ya Umma” (National Government).
 •    Ukiwepo upungufu wa utekelezaji katika Baraza la Mawaziri, na kwa mapendekezo ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wasiopungua thuluthi mbili, Rais kwa kushauriana na Waziri Mkuu ataweza kumuagiza Waziri Mkuu kuvunja Baraza hilo la Mawaziri na kuundwa Baraza la Mawaziri jengine. 
  
 •    Yote haya tuliojaaliwa kuyataja humu yataorodheshwa na wataalamu wanao khusika kuwa ni sehemu ya muswada wa Katiba ya Nchi. 
  
 • ** Hapa kwetu, mara zote imethibiti ya kwamba uchaguzi wa kumchaguwa Rais ndiwo unaosababisha vurugu kufika watu kuuwana, hivi pia ndivyo ilivyo thibiti kwa majirani zetu – Kenya na Zimbambwe – hivi karibuni.

  Matengenezo ya Lazima Kabla ya Uchaguzi

  Katiba ya Nchi

  Mfumo wa kisiasa wa zaidi ya chama kimoja uliletwa Zanzibar mnamo 1992. Mara tu baada ya kuletwa huu mfumo wa zaidi ya chama kimoja kuondowa mfumo wa chama pekee, ilikuwa ni lazima kuundwa Katiba yenye kulingana na huu mfumo wa zaidi ya chama kimoja. Haikufanywa hivyo, na mpaka hii leo haijafanywa hivyo.

  Hivyo ni kwamba japo kuwa imesemwa kuwa nchini kuna mfumo wa zaidi ya chama kimoja, hakika ni kwamba nchi bado imo katika mfumo wa chama pekee, kwa sababu Katiba ya nchi ni ile ile ya chama pekee.

  Hivi kuendelea nchi katika Katiba ya chama pekee hakuna maslaha kwa nchi. Ni hali yenye kuleta madhara kwa nchi na wananchi. Zaidi ya hivyo, inadhihirisha hakika ya kwamba kuletwa nchini mfumo wa siasa ya zaidi ya chama kimoja ni nadhariya maneno bila vitendo, ni wino tu juu ya karatasi. Hali hii imekuwa ni ya khatari zaidi kuliko pale nchi ilipokuwa katika mfumo wa chama pekee. Ikijuulikana hivyo, na ikitambulika hivyo na ikiendwa na kutendwa katika hali hiyo; hapakuwepo ufahamu mpotofu kuwa ni kisingizio. Tafauti na hivyo, ni hivi ilivyo hii leo kwa kusemwa kuwa nchi imo kwenye mfumo wa kisiasa wa zaidi ya chama kimoja, na kwa hakika kimwendo na utendaji sivyo hivyo. Hali hii, yaani hali ya ubabaifu; ndio hali yenye kusababisha madhara yote haya yanayoyakumba nchi na wananchi kwa jumla tangu pale kuletwa nchini (kinadharia) mfumo wa zaidi ya chama kimoja.

  Madhali Katiba bado ni ile ile ya chama pekee, basi suala la mfumo wa kisiasa wa zaidi ya chama kimoja; litaendelea kuwa ni “nadharia” tu, yaani ni wino juu ya karatasi, si hakika ya hali.

  Kuingia Katika Uchaguzi Kwa Katiba Kongwe

  Baada ya kuletwa nchini (kinadharia) mfumo wa zaidi ya chama kimoja, wananchi walijitokeza na kuunda vyama vya kisiasa mbali mbali. Idadi kubwa ya vyama hivi viliingia kwenye uchaguzi, tangu ule wa 1995 na ya baadae kwa Katiba ile ile ya chama pekee. Sote tunakumbuka kwamba ni Mchungaji Mtikila ndie tangu awali aliehadharisha kuingia kwenye uchaguzi katika mfumo wa zaidi ya chama kimoja kwa katiba ya chama pekee. Inasikitisha kwamba kuhadharisha kwake huku Bwana Mtikila hakukupata sikio wala kuzingatiwa na waongozi wa vyama vya kisiasa nchini. Walipuuza. Lenye kusikitisha zaidi ni kwamba vyama viliingia kwenye uchaguzi wa 2000 na mpaka huu wa 2005 kwa Katiba ile ile ya 1984 – katiba ya chama pekee.

  Imeelekea kwamba na hata uchaguzi wa 2010 vyama vitaingia katika uchaguzi kwa katiba hii hii kongwe ya chama pekee.

  Madhara ya kufanya hivyo sote tunayajuwa na tunayaona, haina haja ya kuelezana kukhusu suala hilo . Wananchi wanakuwa wakijiuliza kwa masikitiko, kwa nini viongozi wanawatia katika uchaguzi kwa Katiba kongwe na kusabishiwa kila maovu, bali zaidi kukosekana natija yoyote ile. Hufika kujiuliza ya kwamba hivi ni kukosea au ni kubahatisha. Yote mawili ni maovu, haiwi kukosea mara mbili, na ikiwa ni kubahatisha basi hivyo ni uovu zaidi; haiwi kubahatisha mara mbili, hakuna kubahatisha katika suala hili. Muhimu ni kwamba, “Muumini haumwi na nyoka mara mbili pango moja”.

  Kwahivyobasi

  Katiba mpya yenye kulingana na mfumo wa vyama zaidi ya kimoja itengenezwe na itumike kwa haraka na kabla ya matayarisho ya uchaguzi wa 2010.

  Itendwe hivi ili tuepukane na maafa yote yale yaliyotokea katika uchaguzi uliopita, yaani uchaguzi wa 1995, wa 2000 na wa 2005. Tusiendelee kutenda kosa lile kwa lile.

  Miongoni mwa yenye kuhitajika kuwemo kwenye hio Katiba mpya ni matengenezo na mipango yote ya uchaguzi, na kila linalokhusiana na uchaguzi; likiwemo suala la Tume ya Uchaguzi.

  Tume ya Wasimamizi Uchaguzi

  Wasimamizi (watizamaji) uchaguzi mara nyingi walifika kuwa na maoni tafauti kuhusu uchaguzi kwa jumla. Wako waliosema kuwa uchaguzi umeendeshwa barabara na bila ya ghishi wala khiyana. Wako walioona na kusema kuwa uchaguzi haukuendeshwa barabara na umeingizwa ndani yake ghishi na khiana.

  Lakinibasi, wote hawa; hapana hata mmoja ambae maoni yake yaliyeweza kubadilisha lolote katika yale yaliotangazwa na Tume ya Uchaguzi. Kwa sababu kwa muibu wa Katiba iliopo, Tume ya Uchaguzi ndio yenye (imepewa) nguvu zote kuhusu shughuli zote za uchaguzi – tangu mwanzo mpaka msisho.

  Tunasahau kwamba, “Nguvu zinaharibu, na nguvu bila mipaka; huharibu bila mipaka”. (Power corrupts, absolute power corrupts absolutely).

  Hali hii inathibitisha kuwa katika uchaguzi hapakuwepo wasimamizi wa kimataifa waliopewa uwezo wowote ule. Waliokuwepo ni watizamaji tu (si wasimamizi). Uwezo wao ilikuwa ni kutoa maoni yao binafsi, kwa maslahi yao wenyewe binafsi, kazi zao au nchi zao walizoziwakilisha. Maoni yao haya hayakuwa na taathira yoyote juu ya vile ilivyoamuwa Tume ya Uchaguzi, Tume iliopewa uwezo wote Kikataba. Tume ambayo neno lake ndio la mwisho.

  Hata Mahakama haina uwezo wa kubatilisha neno la Tume, neno lake ni “kun-faya-kun”. Hivi ndivyo ilivyo Katiba iliopo.

  Kwahivyobasi

  Sirikali ya Mshikizo (Interim Government)

  Mengi ya yale yanayotokea katika yenye kukhusu matengenezo na matayarisho mbali mbali ya uchaguzi – kabla ya uchaguzi – na yale yanatokea baada ya uchaguzi, khasa yale yanayo khusiana na utangazaji wa matokeo ya uchaguzi; na mengineo; ni kwa sababu sirikali iliomo madarakani kupitia chama tawala, na wao vilevile ndiwo wenye kuwania kubakia madarakani kwa kupitia uchaguzi huu.

  Kutokana na hali hii, ni dharura sirikali inaokuwepo madarakani ijiuzulu siku tisiini (miezi mitatu) kabla siku ya uchaguzi, badala yake pauundwe “Sirikali ya Mshikizo”, (Interim government).

  Hii “Sirikali ya Mshikizo” (Interim government) ndiyo itakayo shika madaraka yote ya Nchi. Sirikali hii itaendelea kwa miezi mitatu baada ya uchaguzi, kuhakikisha kwamba sirikali mpya ishakabidhiwa madaraka kamili.

  Hii Sirikali ya Mshikizo itaundwa na Jaji Mkuu kwa kuteuwa nje ya Baraza la Wawakilishi, Rais, (Waziri Mkuu) Waziri Kiongozi, Naibu Waziri Kiongozi, Mawaziri na Manaibu Mawaziri. Hii “Sirikali ya Mshikizo” lazima iwe sirikali ya ushirikiano na ipate muwafaka wa thuluthi mbili ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi. Kutekeleza hili, itaepusha uwezakano wa kun’gan’gania madaraka baada ya natija ya uchaguzi, vile vile itasaidia kuepusha ushawishi na uingiliyaji wa sirikali katika uchaguzi na katika harakati zote za uchaguzi – za kabla ya uchaguzi na za baada ya uchaguzi.

  Wasimamiaji Uchaguzi wa Kimataifa

  Ili kuondowa upungufu, kero na madhara yanayotokea katika kila uchaguzi ni dharura iwepo tume ya kimataifa ya kusimamia uchaguzi – (Wasimamiaji Uchaguzi wa Kimataifa). Kwa kushirikiana na kushauriana na “Sirikali ya Mshikizo”. Tume zote hizi mbili, zitengenezewe hududi rejea, yaani “terms of reference” na kuwajibika kuzifuata na kuzitekeleza kikamilifu. Vilevile hii Tume ya Wasimamizi Uchaguzi wa kimataifa ipewe uwezo katika utangazaji wa natija ya uchaguzi, kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi (mpya) itayoteuliwa na “Sirikali ya Mshikizo”.

  Vikosi Vya Kuhifadhi Amani

  Vikosi vyote vya usalama vya sirikali, pamoja na vya jeshi, pamoja na majeshi ya kujitolea; vyote hivyo viamrishwe kubakia kambini mwao na ihakikishwe kuwa hawana silaha wala uwezo wa kupata silaha katika wakati wote wa Sirikali ya Mshikizo (Interim Government). Iwe nimarufuku kabisa kwa kikosi chochote cha usalama cha sirikali kuonekana nje ya kambi zao kwa muda wote huu wa Sirikali ya Mshikizo na mpaka pale kuingia sirikali mpya madarakani; kama inavyoelezwa humu.

  Kwahivyobasi

  Badala ya vikosi vya amani vya nchi, viletwe vikosi vya polisi kutoka Jumuiya ya Madola (UNO). Vikosi hivi vipewe dhamana yote ya amani na salama ya nchi chini ya uwongozi na amri ya mkuu wao kutoka katika vikosi vyao UNO yenyewe. Vikosi hivi vibakie nchini kwa muda usiopunguwa mwaka mmoja, ikihitaji waweko kwa muda zaidi wataongezewa muda kwa kuwafikiana pande zote. Vilevile iwepo mahkama itakayo simamiwa na UNO kuangalia na kuhukumu mashtaka na lawama zozote zile tangu za matengenzo ya uchaguzi, za uchaguzi, na baadae; katika huu muda ambao wao UNO watakuwepo kwa kuweka salama na amani nchini.

  HADHARI!!

  Kuingia katika uchaguzi bila ya kutengenezwa haya si busara hata kidogo, bali ni khatari sana . Ni busara kutoingia katika uchaguzi mpaka haya yatengenezwe.

  Tumeyaona yale yaliyotokea kwenye uchaguzi, tangu ule wa 1995, wa 2000 na wa 2005. Kuingia katika uchaguzi kabla ya mambo haya kutengenezwa ni kuitia nchi katika gharama na kuwatia wananchi katika khatari. Walioko katika uwongozi ndio watakao kuwa dhamana na wenye kuhisabika kwa lolote lile litakalo wafika wananchi kwa huko kuingia katika uchaguzi bila ya kutengenezwa hali muwafaka kwa kutengenezwa hayo tuliyoyataja hapo juu. Ni hakika kuwa viongozi ni dhamana na ndiwo wenye kuhisabika, lakinibasi, watakao kuwa dhamana wa mwanzo na wa kuhisabika mwanzo ni wananchi wenyewe kwa kuona wanatiwa katika khatari na wao wakakubali na kuridhia kutiwa katika khatari hio. Wao wananchi, ndio watakao kuwa mas-uli mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu Subhaanahu wa Ta’aala kwa lolote lile litakalotokea natija ya huko kuingia katika uchaguzi kabla ya kutengenezwa haya tuliojaaliwa kuyataja humu; kwani itakuwa wanajitia katika hilaki kwa mikono yao wenyewe; jambo ambalo Mola wetu Mlezi Subhaanahu wa Taáala ametukataza. Kutokana na haya yote tuliojaaliwa kuyataja humu tunawaomba ndugu zetu walioko katika uwongozi kwanza wajitahidi haya tuliyoelezana kuwa ni yenye kuhitajia kutengenezwa, yatengenezwe kikamilifu; hapo tena tumuombe Mwenyezi Mungu Mtukufu Subhaanahu wa Taáala na yaanze matayarisho mengine ya uchaguzi, na Inshaallah utakuwa uchaguzi wa kheri na baraka – Aamyn.

  Kufikilia Sirikali ya Umma

  Katika juhudi na mipango yetu ya kuundwa mfumo wa Sirikali ya Umma kama tulivyoeleza humu, tunashauri kutumia huu mfumo wa uchaguzi wa njia hii ufuatayo:

  “Uwakilishi Kulingana na Kura ”

  “Proportional Representation” (PR)

  Yafuatayo ni maelezo ya nyaraka mbili zilizoandikwa na wataalamu wa Kimarekani wa ufatiliaji mambo ya kisiasa kukhusu uchaguzi katika mfumo wa “Proportional Representation” (PR), au kama tunavyoweza kuuwita kwa lugha yetu ya Kiswahili, “Uwakilishi Kulingana na Kura ” (UKK).

  Nini Uwakilishi Kulingana na Kura (UKK)

  “Proportional Representation” (PR).

  Huu ni mpango ambao unatoa fursa ya kuchaguwa Wawakilishi wa Umma katika vyombo vya sirikali kwa njia ambayo nyingi zaidi za kura zitapata Wawakilishi katika vyombo hivi kwa kulingana na wingi wa kura. Hivi ni maana kwamba sehemu kubwa ya kura zitapata uwakilishi. Mpango huu ni tafauti na ule mpango ambao unampa uwakilishi pekee mtetezi ambae amepata sehemu ya kura zaidi kuliko mashindani wake, hata ikiwa ziyada hio ni kura moja tu, au asilimia ndogo kabisa. Mpango ambao unajulikana “winner-take-all”, yaani “mshindi achukuwe vyote”; hali hii haina tafauti hata kidogo na uchezaji kamari. Kwa Waumini kamari ni haraam, kwahivyobasi, tunaingia katika uchaguzi katika njia ya haraam ni haraam, hivi ndio maana maisha yote kila uchaguzi unaleta balaa na maafa, kwa sababu umo katika mfumo wenye haramu ndani yake. Natija ni kuwa yule anayepata kura kasoro kidogo kuliko mwenziwe (mshindani wake) huwa ndio kashindwa, na hapo huondoka na ghadhabu, chuki na machozi; hapo tena huingia katika kufikiria mipango ya chini kwa chini ili kuleta vurugu la kisiasa na kuharibu utulivu wa mipango na hata wa nchi kwa jumla. Yote hayo ni kwa sababu mpango wa uchaguzi uliotumika sio mzuri, yaani mpango wa “mshindi achukuwe vyote na wa pili aondoke patupu”.

  Mpango huu wa Uwakilishi Kulingana na Kura (UKK), sio mpango mpya wa uchaguzi; huu ni mpango unaotumika tangu zamani sana katika nchi za kidimokrasia za kimagharibi. Wataalamu wa ufuatiliaji wa kisiasa waliofanya uchunguzi juu ya mwenendo huu wamegundua kuwa takriba nchi nyingi zenye kufuata mfumo huu wa uchaguzi zinafaidika kwa vile kuwa wananchi wao wengi wanashiriki katika chaguzi zao. Vilevile ushindani wa vyama vya kisiasa unakua vizuri na hayy zaidi. Zaidi ya hivyo, ni sababu ya kupatikana uwakilishaji mzuri na wa usawa; hata vijikundi vidogo vidogo vyenye fikra mbali mbali za kisiasa vinapata kuwakilishwa. La muhimu zaidi, mfumo huu wa uchaguzi huondosha mtindo wa walioko utawalani “kugawa mjimbo ya uchaguzi vile wanavyo penda wao” – ili ushindi uwe ni wao siku zote. Isitoshe, hakuna hata moja kati ya nchi zinazofuata mpango huu yenye kufikiria kurejea katika ule mpango wa zamani wa mfumo wa “mshindi achukuwe vyote”, hii ni ithbati kwamba mfumo huu umethibisha kufuzu.

  Nchi zenye kufuata mpango huu, aghlabu ya vyombo vyao vya sirikali, tangu uraisi, uwaziri na vyenginevyo huwa vinaundika katika mpango wa kushirikiana ndani yake vyama mbali mbali, kulingana na uwakilishi vinavyopata kutokana na uchaguzi, yaani “Sirikali ya Umma” (National government). Nyingi ya sirikali hizi za ushirikiano (Umma) zimedumu kwa miaka bila ya kuvunjika ushirikiano wao. Kwa mfano katika Scandinavia sirikali hizi za ushirikiano zinaendelea kwa miaka na miaka. Na kwa vile kuwa ni sirikali za ushirikiano wa vyama kadhaa wa kadhaa, kunakuwepo ushauriano baina ya vyama hivyo. Kwahivyobasi, wananchi wengi zaidi wanapata kushirikishwa katika mipango ya vyombo vya sirikali na sauti zao kupata kusikilika kwa kupitia Wawakilishi wao. Kutokana na hali hii ya kushirikiana na kushauriana, sirikali hizo zimeweza kupasisha kanuni zenye manufaa zaidi kwa wananchi na ambazo ni madhubuti zaidi, kulinganisha na zile za sirikali za nchi ambazo zinatumia mfumo wa uchaguzi wa “mshindi achukuwe vyote” na kuweko serikali/upinzani – kama vile ilivyo huko Marekani na Uingereza, (na hapa kwetu Zanzibar; kwa hivi sisi kuendelea kufuata mfumo huu, ambao ni Muingereza ndie alietuleteya tangu siku za utawala wake juu ya nchi yetu).

  Vipi Unafanyakazi Huu Mpango Wa

  Uwakilishi Kulingana Na Kura (UKK)

  Watafiti hawa wa Kimarekani wanatueleza kuwa huko kwao kunaendelea mfumo wa uchaguzi chini ya mpango wa muwakilishi mmoja kwa jimbo moja na kuwa yule anaepata voti zaidi (hata zaidi hio ikiwa ni voti moja) ndiyo anakuwa mwakilishi pekee kwa jimbo hilo . Wanaendelea kwa kusema kuwa huu mpango wa “Uwakilishi Kulingana na Kura ” (UKK), huenda hivi mwanzo ukaonekana ni kitu kigeni. Sisi tunaelewa vyema kuwa hilo sio ajabu, kwani mazowea yanataabu na ni maumbile ya binaadamu mara nyingi kuogopa (bali hata kupinga) mabadiliko. Lakinibasi, ni wajibu wetu kuzingatia na kudurusu fikra zozote zile na kuchukuwa yale yanayotufaa kulingana na hali zetu na haja zetu; na kuwacha yasiotufaa, kutofanya hivyo ni kujiharimishia maendeleo. Wanaendelea waandishi hawa kwa kutueleza ya kwamba mpango huu wa (UKK) unafanyika kwa kutumia njia mbali mbali, lakinibasi; ilivyo khasa ni kuwa hauna pingamizi wala ugumu hata kidogo. Bali njia zake zote za utekelezaji ni nyepesi kufahamika na kutumika, la zaidi ni kwamba mfumo huu wa uchaguzi (UKK) umethibitisha kufuzu katika nchi zote unako tumika.

  Ya Misingi Katika Mpango Huu

  ¨ Idadi kubwa sana ya wenye kupigakura wanapata wawakilishi wanao wachaguwa wenyewe.

  ¨ Vyama vyote vya kisiasa vyenye kushiriki kwenye uchaguzi vinapata uwakilishi kulingana na kura wanazopigiwa.

  Yaani, kila mpigakura anakuwa na fursa ya kupata muwakilishi anaempigiyakura. Kwahivyobasi, sehemu kubwa zaidi ya wa pigiwakura (watetezi) wanapata kuwaakilisha wapigakura wao. Ili kufikiya haya, ziko njia mbali mbali zinazotumika katika huu mpango wa (UKK). Kila moja ya njia hizo zipo nidhamu maalumu zenye kutumika katika ufanyikaji wa uchaguzi kwa huu mfumo wa (UKK), kati ya hizo ni:

  Kwanza, mfumo wa mpango wa zaidi ya kiti kimoja kwa Mkoa mmoja. Huweza ikawa viti vitano, sita, au hata zaidi ya hivyo. Huenda hata ikawa viti kumi na zaidi, inategemeya wingi wa wapigakura katika Mkoa. Idadi ya viti katika Mkoa huwa kwa kulingana na idadi ya wapigakura katika huo Mkoa, huwa hivyo hivyo kama itavyo bainishwa katika Katiba ya nchi.

  Pili, badala ya kupigakura jimbo moja moja, hupigwakura Mkoa mzima, ukiwa ni (kama) jimbo moja. Mkoa ambao katika hali ya hivi sasa huweza ukawa unayo majimbo kadhaa wa kadhaa.

  Tatu, uwakilishi hugawika baina ya vyama/watetezi kulingana na wingi wa kura wanazopigiwakura watetezi/chama. Kwa mfano Mkoa wenye viti kumi, chama kitachopata 40% ya kura kitapata viti vinne au 40% ya viti vyote katika Mkoa huo. Ikiwa chama chengine kitapata, tusema; 20% ya kura basi kitapata viti viwili au 20% ya viti vyote katika Mkoa huo, na hali kadhaalika. Inadhihiri wazi kuwa hapatakuwepo chama/mtetezi kitakacho/atakae ondekea chuki na machozi tu, bali (aghlabu yake) kila mtetezi/chama atapata/kitapata uwakilishi kulingana na kura atakazo/kitakazo pigiwakura. Muhimu zaidi ni kuwa hapana kati yao atakaekuwa “mpinzani”, bali wote watakuwa Wawakilishi wa Umma na sehemu ya hio sirikali yao – Sirikali ya Umma (National government).

  Mpango huu – “Uwakilishi Kulingana na Kura” (UKK) – unachangia sana katika kuleta na kuhifadhi “dimokrasia ya vyama vingi”. Kwahivyobasi, kuwepo fursa kwa vyama vidogo vidogo ya kupata uwakilishi na kuendelea kuishi na kufanyakazi bega kwa bega na ukamilifu pamoja na vyama vikubwa katika kutekeleza siasa na mipango ya nchi, bila ya ubaguzi na mibinyo; ya dhahiri au ya chini kwa chini.

  Kiwango cha Kujuzu Kupata Uwakilishi

  Ili kuepusha vurugu la vyama vidigi vidigi kuingia katika uchaguzi katika mfumo huu, na vile vile kuepusha wingi wa vyama nchini; Katiba ya nchi itaweka kiwango maalumu cha chini cha kura (threshold) ambacho mtetezi/chama lazima apate/kipate ili astahiki/kistahiki kupata (kiti) uwakilishi. Kiwango hiki huwa kama vile 10% ya kura za Mkoa wote, au zaidi au kidogo ya hivyo.

  Aina Za Huu Mpango Wa

  Uwakilishi Kulingana Na Kura (UKK)

  1. Kwa Orodha Ya Watetezi

  Hii ni aina ambayo ni nyepesi zaidi kutekelezeka na ndiyo inayotumika katika nchi nyingi za kimagharibi, inatumika Austria, Belgium, Bulgaria, Denmark, Greece, Israel, Netherlands, Norway, Spain, Sweden na Switzerland. Katika mpango huu, kila chama huweka orodha ya watetezi wake kulingana na viti vinavyo pigiwakura katika kila Mkoa. Wapigakura hupigiyakura orodha ya chama wanachokitaka, na chama hupata viti kulingana na wingi wa kura kitachopigiwa.

  Aina hii huwa katika hali mbili:

  v Ya Kwanza , ni ile ambayo chama hufanya orodha yake kwa mujibu wa nani wa kuchaguliwa mwanzo na wakufuatia wake. Mpigakura hupigakura moja tu, kwa kukipigiyakura chama kwa orodho yote ile, hapigiikura mtetezi mmoja mmoja. Watetezi wa chama hupata uwakilishi kwa mujibu ya walivyo orodheshwa katika ile orodha ya chama chao. Kwa mfano katika Mkoa “X”, chama “**” kimepata kura za kustahiki kupata viti vitatu, basi viti hivi huwa kwa watetezi watatu wa mwanzo katika ile orodha ya hicho chama.

  v Ya Pili, ni ile ambayo wapigakura wanao uwezo na khiyari zaidi kwa kuchaguwa kutokana na ile orodha ya chama mtetezi wanayemtaka awawakilshi. Kwa mpango huu mpigakura humpigia kura yule mtetezi anayemtaka, badala ya kukipigiakura chama. Mpango huu japokuwa mpigakura vile vile anakichaguwa chama maalumu, kwa vile kuwa anachaguwa mtetezi kutokana na orodha ya chama. Hivyohivyo; husababisha ubadilikaji wa mahala pa mtetezi alipoorodhishwa katika ile orodha ya chama, kulingana na kura atazopigiwa; hivyobasi, huenda mtetezi akapanda juu au akishuka chini.

  Mbali na aina hizi mbili, ziko aina nyengine kadhaa zinazotumika nchi mbali mbali katika mfumo huu wa uchaguzi. Zote hizo zimethibiti kuwa ni bora kuliko ule mpango wa “mshindi achukuwe vyote”. Humu tumetaja aina hizo hapo juu kwa vile kuwa ndizo zenye kutumika katika nchi nyingi zaidi na ambazo ni nyepesi zaidi kutekelezeka.

  Upungufu Katika Mtindo wa Uchaguzi wa

  “Mshindi Achukuwe Vyote”

  Mpango wa uchaguzi wa “mtu mmoja jimbo moja – mshindi achukuwe vyote” umeanza kutoweka pole pole takriban duniani kote kwa sababu ya ila ulizonazo. Miongoni mwa ila hizo ni vile kuwa:

  § Unasababisha wapigiwakura wengi kutopata uwakilishi. Wapigiwakura hawa huwa ni kutokana na chama kikubwa au/na vyama vidogo vidogo, ambavyo kwa jumla ya vyote pamoja hufika kuwa wamepigiwa kura na wananchi wengi kuliko kile chama ambacho kimepata wingi wa viti, si wingi wa kura, na kuendelea/kuingia madarakani. Ni huu mfumo wa “wingi wa viti wala si wingi wa kura” – kuwa ndivyo kujuzisha kuingia madarakani. Ni mfumo huu ndio wenye kusababisha hivyo vyama vyengine, japokuwa kwa jumla huwa vinayo “wingi wa kura””, lakini “havina wingi viti”, kubakia ni “upinzani”; na kunyimwa kushiriki katika shughuli za matengenezo na uwendeshaji wa sirikali yao .

  Kwa jumla mfumo huu wa uchaguzi “mshindi achukuwe vyote” husababisha:

  ¨ Uwezekano wa kupasishwa kanuni (sharia) ambazo zina upungufu. Kanuni hizi huwa na upungufu kwa vile kutomathilisha wengi wa wananchi, kwa kutojuzisha wale waliowapigiakura kupata uwakilishi.

  ¨ Ubaguzi na mibinyo juu ya vyama vidogo vidogo.

  ¨ Wapigakura wengi kuvunjika hima na moyo. Wanavunjika moyo kwa kuona kuwa uwakilishi daima unakuwa ni kwa chama kimoja tu, hivyobasi; wao huwa ni kupoteza kura zao (na wakati wao ), bila ya kufikiwa dhamiri na makusudiyo yao ya kupigakura.

  ¨ Vyama vidogo vidogo kukosa uwezo wa kuendelea kuweko.

  ¨ Upungufu katika misingi ya dimokrasia ya kweli.

  Idadi Kubwa Kukoseshwa Wawakilishi

  Haya ni dhaahir kabisa, kwa sababu; hata yule mtetezi anayepata 49% za kura huondokea patupu kwa kashindwa na yule aliepata 51% ya kura. Kwahivyobasi, hawa 49% ya wapigakura huwa hawana wawakilishi waliowachaguwa wenyewe, hali ya kuwa wamewapigiakura wawakilishi wao. Kutokana na hali hii, matokeo ni kwamba idadi kubwa ya wananchi humalizikia kuwa hawakupata wawakilishi walio wachaguwa wenyewe kwa ridhaa zao. Natija ya hali hiyo, huwa kutoridhika na kutoshiriki kwa moyo mkunjufu katika mipango ya sirikali. Kwa jumla inathibitisha ya kwamba uchaguzi katika mfumo wa “mshindi achukuwe vyote”; japokuwa mwananchi anapewa haki ya kupigakura, wakati huohuo ananyimwa haki ya kuwakilishwa.

  Hivyo kupotezwa hakika na makusudiyo khasa ya uchaguzi.

  Kwahivyobasi, dimokrasia huwa inachezewa na kupotolewa, bali ni kuuliwa dimokrasia ya kweli na kujengwa udikteta. Isitoshe, wanachama wa vyama vidogo vidogo hulazimika kupoteza kura zao., ama kwa vile imekuwa wamempigia kura mtetezi ambae ananyimwa uwakilishi ( kama tulivyoona hapo juu); au kwa kutopigakura kabisa, kwa kuona hapana faida ya kupigakura.

  Yote haya yanaashiria upungufu katika dimokrasia ya kweli.

  Zaidi ya hivyo, mpango huu wa uchaguzi ni mpango wa kujihami vyama vikubwa na kuvibinya na kuvinyima haki vyama vidogo vidogo ili visiendelee na khatimaye kutoweka kabisa, hivyo kubakia nchini daima utawala wa chama kimoja.

  Hali hii imesababisha katika Marekani mnamo karne mbili zilizopita kutoweka vyama vidogo vidogo zaidi ya elfu.

  Hapana shaka, haya yatatokea zaidi katika nchi zetu ambazo ndio hivi sasa tumo katika juhudi za kujivuwa na mfumo muwovu wa utawala wa chama pekee. Lakinibasi, ikiwa tutaendelea na mtindo wa uchaguzi huu tulionao, yaani “mmoja achukuwe vyote na mwengine aondokee patupu”; itakuwa kutoka katika utawala wa chama pekee na kujiingiza katika utawala wa chama kimoja

  Hali ambayo ni ya khatari zaidi, na yenye kusababisha mivutano na mapambano makali baina ya wanufaika na wapenzi wa vyama.

  Kuuwacha Mfumo Mpotofu na Kuufuata Mfumo Mwongofu

  Kutokana na hizi ila tulizojaaliwa kuzitaja hapo juu, ila ambazo ni kuu na ovu sana, ndio sababu ya kimsingi kwa walimwengu wa leo; khasa wale tunaowaita/wanaojiita “nchi zilizoendelea”, (developed coutries); kuamuwa kuuwachilia mbali mfumo huu viza, mfumo wenye uwovu na khatari, mfumo wa “mmoja kuchukuwa vyote na mwengine kuondokea patupu”. Badala yake walimwengu hawa, wakaamuwa kufuata mfumo mpya, mfumo wa “Uwakilishi Kulingana na Kura (UKK)”, )Proportional Representation( (PR) ambao ni wenye kulinda na kuhifadhi dimokrasia zaidi. Hivyo ni kwa huu mpango wake wa kugawa uwakilishi baina ya vyama/watetezi kulingana na kura wanazopewa na wananchi; kwahivyobasi, kuwezesha uundwaji wa sirikali za ushirikiano wa vyama, badala ya sirikali ya chama kimoja. Vilevile, kwa kufuata mfumo wa uchaguzi katika mpango huu wa (UKK), matunda yake yamekuwa ni nyenzo kuu katika kuhuwisha mashindano mema na ya faida kwa nchi baina ya vyama (vyote) vya kisiasa nchini. Haya, kwa sababu vyama vidogo vidogo navyo vinapata haki ya uwakilishi na kushiriki katika vyombo mbali mbali vya sirikali yao , vile vile; wapigakura wanakuwa na chaguwo zaidi juu ya nani wa kumpigiakura. Zaidi ya hivyo, kwa hivi wananchi kupata fursa hii inawatia moyo na hamu ya kupigakura, kwahivyobasi; idadi ya wapigakura inakua (kwa khiyari, si kwa kulazimishwa). Hili linaleta kuundwa kwa vyombo vya sirikali (na sirikali yenyewe) ambavyo vina/inawakilishwa na wananchi wengi zaidi, pia linaondowa mpango wa sirikali/upinzani – hali ambayo ni pingamizi kubwa ya amani na maendeleo nchini – kwa vile kuundwa serikali za ushirikiano (coalition govenments).

  Maendeleo Bila ya Ushirikiano ni Kutaraji la Muhali

  Sote tunafahamu vyema ya kwamba maendeleo huwa taabu kupatikana nchini ikiwa sehemu kubwa ya wananchi hawashirikishwi katika vyombo vya sirikali yao . Vile vile tunafahamu vyema ya kwamba kutokana na huu mpango wa uchaguzi katika mfumo wa “mmoja achukuwe vyote na wa pili aondokee patupu”, sirikali/chama kinacho tawala hulazimika kuingia katika ubaguzi na mapendeleo baina ya wananchi kwa kuwafanyia vyema zaidi wanachama wao wabembelezeke ili waendelee kuwapigiakura watawala. Kwa upande wa pili, hao watawala wakati huo huo hutenda mno katika kuwabinya na kuwadhili wapinzani kwa kuwanyima haki zao za kiwananchi za kimsingi, hufanya hivi kwa makusudio ya kutaka upinzani udhoofike, hivyo upunguwe. Natija ya hali hii ni mvutano baina ya sirikali/upinzani (uwongozi), upande mmoja, na baina ya sirikali/wapinzani (wananchi) upande wa pili. Taathira ya mvutano huu ni kutokuwepo kuaminiana baina ya sirikali na upinzani na kutokuwepo ushirikiano na ushauriano katika nchi kwa jumla. Huu ni mfarakano, ambao ndio nyenzo kuu ya mtawala. Isitoshe, uwovu zaidi katika haya ni kuzidi mbinu za walioko upande wa upinzani kutaka wapate/kuchukuwa sirikali, na walioko upande wa sirikali kuzidi mbinu za kuhifadhi/kudumu katika utawala. Hapa ndio huzalika kinyang’anyiro cha madaraka. Pande zote mbili hizi hutenda hivyo kwa hali na mali na kwa thamani yoyote ile, na bila ya kujali hata kidogo maslaha ya nchi wala wananchi. Hali inapokuwa hivi, maslaha ya wakubwa wa pande zote mbili, yaani sirikali na wapinzani; na hao waliomo katika uwongozi, na wapambe wao, ikiwa upande wa sirikali, au upande wa upinzani; ndiyo huwekwa mbele, na kwa hisabu yoyote ile. Na kama kawaida, wananchi ndiwo daima wenye kuathirika kutokana na uovu wa vitendo hivi vinavyotokana na viongozi wao – wa sirikali na wa upinzai – waliomo katika upotofu. Kuendelea hali hii, kwa sababu ya viongozi kukataa kuleta mabadiliko; na badala yake kudumu katika mfumo fisadi; mfumo wa uchaguzi wa, “mmoja achukuwe vyote na wa pili aondokee patupu”. Wananchi huanza kujiuliza na kuulizana juu ya ukweli na ikhlasi ya viongozi wao, wakati huohuo; polepole itibari na imani juu ya viongozi wao hupotea. Kwajumla, hali hii hukidhoofisha chama na hukipangia mporomoko; khatimaye ni kubomoka kabisa.

  Haya yote yamefika ikiwa ni natija ya vingozi waroho wa madaraka, wafupi wa kufahamu na kutambuwa hakika; wakaona kuendelea katika mfumo uliopitwa na wakati, mfumo wa “mmoja achukuwe vyote na wa pili aondokee patupu”; utawasaidia kudumu kwenye madaraka. Walisahau kwamba baa’til haiwezi kudumu hata kama itahifadhiwa na kulindwa kwa nguvu gani.

  “Haqi lazima ije juu na baa’til lazime itoweke”.

  Baa’til ni un’gan’ganiaji madaraka, haqi ni ushirikiyano madaraka.

  Mashauri

  Kutokana na haya tuliojaaliwa kufahamishana humu, imetubainikia kwamba ni dharura kuufuata huu mpango wa uchaguzi katika mfumo wa “Uwakilishi Kulingana na Kura ” (UKK), “Proportional Representation” (PR). Tunapendelea viongozi wetu watende hivyo kwa haraka, bila ya kukawia; kwa nia na azma ya kuleta mabadiliko ya kheri kwa manufaa ya uwongozi na maslaha ya nchi. Kwa kuendelea walimwengu, kimaarifa na kiilimu; ni wajibu wetu na sisi twende na walimwengu, tutende hivyo ili tuepushe kuzidi sisi kuwachwa nyuma kwa kung’ang’ania kwetu ya kale yasio maaendeleo, ambayo yameshapitwa na wakati; na kuyakataa ya kileo, ambayo kila siku inazidi kuthibiti kufuzu katika nchi mbali mbali. Natija ya sisi kubakia na ya kale ni hivi kukhasirika kwa kuzama katika chuki na mivutano isiokuwa na msingi wala faida yoyote, tokeahapo hakuna mvutano wenye faida. Bali muhimu zaidi, inatupasa tujiendeleze kwa maslaha yetu ili pia tuweze kujitowa katika kundi la wenye kufadhiliwa. Badala yake tuwe wenye kujibeba wenyewe, na Inshaaallah tuweze kufika katika uwezo wa wenye kuchangia katika maendeleo ya ulimwengu – kama alivoahidi Waziri Mkuu wetu, Sheikh Muhamed Shamte siku alipoinganisha Zanzibar katika Umoja wa Mataifa (UNO), mwaka wa 1963. Hivyo ili tuwe mkono wa juu, tusite hivi kuwa mkono wa chini; mkono wa juu (wenye kutowa) ni wenye kupendeza na ni wenye fadhila zaidi kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu Subhaanahu wa Taáala kuliko mkono wa chini (wenye kupewa).

  Kufadhiliwa ni aibu na ni nyenzo kuu ya kumilikiwa. Muislamu anatakiwa awe mwingi wa kutowa, mchache wa kuchukuwa.

  Tunamuwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu Subhaanahu wa Taáala atujaalie kila la kheri na atuepushe na kila shari – Aamyn.

  Wa Billahi Tawfiiq

  Umoja wa Wazalendo

  Zanzibar

  October, 2008

  March 29, 2009
  Chanzo: zanzinet.net

  Leave a Reply

  This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.