Date::2/24/2009

Na Ally Saleh

HIVI sasa Serikali ya Dk Amani Karume iko katika mwaka wake wa nne tokea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, ambao kama ilivyokuwa chaguzi nyengine mbili za 1995 na 2005 ulikuwa na utata.

Si madhumuni ya makala hii kuzungumzia tata hizo kwa sababu mwandishi anaamini hayo yamepita na tunachotaka kutazama sasa ni utendaji wa Serikali iliyopo madarakani.

Hiki ni kipindi cha pili cha utawala wa Dk Karume, ndio kusema kiongozi huyo kwa sasa amebakisha muda wa miezi 20 kukamilisha ngwe yake ya mwisho kwa mujibu wa katiba.

Hatujamsikia, na inshallah Mwenyenzi Mungu aepushe mbali, Dk Karume akifanya harakati za kutaka kuzidishiwa muda wa kubaki madarakani kama ambavyo Rais aliyemtangulia Dk Salmin Amour alivyotaka kufanya ushawishi wa kubadilisha Katiba ili atawale vipindi zaidi ya viwili.

Hapana shaka Dk Karume amekuwa akisimamia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ambayo ndio iliyomuingiza madarakani.

Ilani hiyo ilikuwa au bora tuseme imekuwa na viwango na vigezo vyake ambavyo vimekuwa na vitakuwa ni visaidizi vya kupima iwapo utekelezaji wa Ilani hiyo umetimizwa.

Kwa hakika Ilani hutarajiwa kutoa mwelekeo wa Chama na muhimu zaidi ni Serikali inayoundwa ambayo kwa mnasaba wa CCM inatakiwa iwe ni serikali inayojali maslahi ya watu kwa sababu hivyo ndivyo mizizi ya chama hicho ilivyo.

Ila tunaweza kabisa kujiuliza iwapo CCM bado ina ukuruba na watu kama inavyojinasibisha maana katika utaratibu wa kutekeleza majukumu yake kuna shaka nyingi tunazoweza kuzitoboa hapa na pale.

Binafsi ninaanza kuona kuwa CCM sio kuwa inajikwaa katika vipaumbele vyake bali kuna dalili za kutosha kuwa vinawekwa nyuma ya kisogo.

Sina hakika iwapo hili linafanywa kwa maana au mantiki gani. Maana madhumuni ya CCM kutaka kuendelea kushika madaraka hayajabadilika na ndio msingi wa chama chochote kile cha siasa. Lakini kwa matendo hayo najiuliza madhumuni ya kushika au kuendelea kushika dola bado ni ya dhati?

Mambo mengi yanafanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambayo yanaonyesha kutilia shaka hayo madhumuni ya kuendeleza vipaumbele vyake lakini tukio la hivi karibuni kabisa la kununua magari ya fahari kwa gharama kubwa, hili limepita kipimo.

Haiwezi kuingia akilini na haikubaliki kabisa kuwa Serikali itumie fedha zilizosemwa kuwa ni za msamaha wa kodi, basi kukosekane la kufanya katika mambo yalio ya kipaumbele na zikanunuliwe magari ya kifahari.

Rais Karume, Mawaziri na hata Makatibu Wakuu wote kama sisi wanaishi nchi hii na kila mmoja wetu anajua fika kuwa pamoja na ukosefu wa mfumo mzuri wa usafiri ndani ya Serikali, lakini pia suluhu si kununua magari hayo ya kifahari.

Si suluhu pia idadi ya magari iliyonunuliwa maana siamini kuwa kila gari ilikwisha pangiwa wapi itakwenda.

Imeshawahi kutokezea hata pale gari inapopangiwa idara fulani, au wakati mwengine hata iwe ni ya mradi basi mwenye ubavu wake inaichukua na hakuna litalokuwa maana kila mtu anaufyata akiogopea kibarua kisiote majani.

Sipendi kuhoji au kuulizia iwapo manunuzi ya magari hayo, hata kama yasingekuwa ya kifahari, kama yalifuata taratibu rasmi za ki-tenda zilizowekwa na Serikali.

Serikali inapaswa kutambua kuwa hilo ni doa kubwa mno katika suala la utawala bora ambalo SMZ imekuwa ikijipigia debe kuwa inalisimamia kwa nguvu zote.

Nimetanguliza kujiuliza iwapo SMZ imesahau vipaumbele vyake kwa sababu fedha ambayo imetumiwa kununulia magari hayo sio kama haikuwa na umuhimu wa kutumika katika sekta nyenginezo kama afya, elimu na hata kilimo.

Hatuna haja ya kwenda mbali, bali katika shule zetu pamoja na kupitiliza viwango vya millennia na kuwa na vyuo vikuu ambavyo wakati wa Ukoloni au kabla ya Mapinduzi havikuwapo, lakini tunajua sote kuwa watoto wetu bado wanakaa chini katika madarasa, vyumba vya kusomea viko hali mbaya sana na hata vifaa vya maabara ni haba na vilivyoko vimechakaa.

Pamoja na hatua zinazotajwa kupigwa katika sekta ya afya, lakini fedha hizo ni wazi kuwa zinahitajika mno maana vituo havina vifaa vya kutosha na bado kuna mahitaji ya kuweko kwa vituo vya afya katika sehemu nyingi sana za vijiji vya Unguja na Pemba.

Kama Mzanzibari na mdadisi wa siasa za Zanzibar ninaweza kubahatisha ni kwa nini gari hizo zikanunuliwa wakati huu na Waziri Hamza Juma kutetea uamuzi huo hata iwapo ndani ya moyo wake anajua kabisa kuwa hauna uzito hivyo.

Mwisho wa muhula wa Serikali unakaribia na mara nyingi siasa za Zanzibar katika wakati huu huhusisha matukio ya baadhi ya watu walio madarakani kukazana kutengeneza hatma yao na inawezekana manunuzi hayo yana lengo hilo.

Lakini inawezekana pia ikawa ni njia ya kujenga mshikamano kwa watakaopewa magari hayo, na isiwe zwadi, lakini kile kitendo cha kuwa yapo chini ya mamlaka yao na kuwajengea haiba, kitawafanya wabaki karibu na katikati ya Chama au Serikali.

Ila yote na yawe hivyo basi bado mtu anaweza kujiuliza iwapo Serikali ya Zanzibar ilipima umuhimu au ulazima wa kununua magari hayo? Mtu angetamani kupata muhutasari wa kikao kilichotoa maamuzi hayo ili aone aina za hoja ambazo zinaweza kutolewa hata uamuzi kama huo kufanyika.

Maana yaliyotokea Tanzania Bara kwa fedha za kusamehewa madeni yanaeleweka na hapangekuwa na haja ya kurudia makosa hapa Zanzibar.

Hivyo ndivyo akili ya kawaida ingefikiria na kwamba hata kama tumesamehewa waliotusamehe wanatutizama na iko siku watakuja kusema.

Inaelekea CCM na SMZ haiko tena karibu na umma au watu kiasi ambacho hata vilio vyao hawavisikii. Maana kama kweli wanakumbuka vipaumbele walivyovipanga na iwapo kweli vilio vya umma vinasikika, ununuzi wa magari haya ya kifahari usingefanywa.

Tunajua kuwa hata tukisema magari yarudishwe, yauzwe kwa watu binafsi au yazuiliwe kutumika, hakuna litakalofanyika, ila tunalotaka kulifanya sisi ni kuweka rekodi kuwa watu walisema au walitanabahisha kuwa yaliyofanywa ni matumizi mabaya, yasiyozingatia matakwa ya utawala bora, yalikengeuka vipaumbele na yanatia uchungu wananchi wanaolia kwa njaa, mishahara duni na mazingira dhaifu.

Wakati kilio cha umma kitakapopuuzwa basi wananchi hawatakuwa na kufanya isipokuwa moja. Pale magari hayo yatapokuwa yakipita mitaani na viyoyozi vikiwaka na waliomo ndani hawaonekani kwa vioo vyeusi watasema kitu kimoja: ‘Tutaonana mwambani!’

TANBIHI:

Katika toleo lilopita kwenye safu hii kulikuwa na makala yenye kichwa cha habari ‘Waziri Haroun jiuzulu ulinde heshima yako’ ambapo iliandikwa kuwa Waziri huyo amesema haoni sababu ya kujiuzulu kwa kuwa Mawaziri wa Elimu waliopita pamoja na Katibu Mkuu wa CUF Seif Shariff Hamad hawakujiuzulu katika mazingira kama hayo.

Waziri Haroun anasema yeye hakutaja jina la mtu yoyote kwa kuwa anajua wajibu wake na ana heshimu mawaziri walipita. Lakini anakiri kuwa alitoa takwimu na miaka ya mtiririko wa mawaziri mbali mbali kikiwemo kipindi cha uwaziri wa elimu cha Maalim Seif kuanzia.

Ally Saleh

+255 777 4300 22

http://www.eternaltourszanzibar.net

jumbamaro.blogspot.com

Chanzo: http://mwananchi.co.tz/newsrids.asp?id=10246

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.