Makala “Ujumbe wa Rais Kikwete umewafikia CUF” iliyochapishwa na gazeti la Mtanzania katika toleo lake namba 4646 la Januari 31 mwaka huu, inahitaji kujibiwa ili kuweka rikodi sawa.

Dhana ya mawasiliano ya binaadamu inazungumzia kuwa mawasiliano huwa yametokezea pale panapokuwepo na pande zinazowasiliana (sender and sendee), njia ya mawasiliano (channel or medium), ujumbe (message) na maana moja katika mawasiliano hayo (shared meaning). Kwa hivyo, wakati kichwa cha habari kinasema ukweli wa upande mmoja, ukweli wa upande wa pili nao pia upo: kwamba ujumbe wa CUF umemfikia Kikwete, na makala hiyo ni ishara za kuwepo kwa hiyo shared meaning (Soma Human Communication cha Judy Pearson na wenzake, McGraw Hill, 2003).

Makala yenyewe iligawiwa katika nukta kuu nne ambazo ni sera ya Chama cha Wananchi (CUF) inayosemwa kuwa ni jino kwa jino, ujanja wa CUF kupindisha ukweli, maendeleo ya Pemba na mpishano baina ya kilichosemwa na Rais Jakaya Kikwete kisiwani Pemba na lawama zinazotolewa na CUF dhidi ya kauli hiyo.

Mambo matatu ni vyema niyaweke wazi mwanzoni. Kwanza, tafauti na mwandishi wa makala hiyo ambaye hataji maslahi yake kwenye mjadala huu, mimi nabainisha maslahi yangu: mimi ni mwanachama wa CUF na ni Mzanzibari, kwa hivyo mjadala huu unagusa maslahi ya chama changu na ya nchi yangu.

Pili, makala inayotajwa iliwacha kugusia kauli ya Rais Kikwete juu ya utayarifu wake wa ‘kuyalinda’ Mapinduzi ya Zanzibar dhidi ya wanaoyachezea kwa gharama zozote zile. ‘Kulinda’ na ‘kuchezea’ Mapinduzi ni kauli yenye maana na uzito wa pekee panapohusika siasa za kidemokrasia.

Tatu, wakati mwandishi wa makala hiyo anaonesha mpishano baina ya alichokisema Kikwete visiwani Zanzibar na lawama za viongozi wa CUF, mimi naonesha kuwa kuna uwiano mkubwa baina ya kauli hizo na ‘sera za Muungano’ kuelekea Zanzibar. Uwiano huo ndio unaoendelea kuleta mpasuko wa kisiasa na ilikuwa haki, kwa hivyo, kwa viongozi makini kama wa CUF kuonesha khofu zao.

Kwa makusudi nataka nidharau madai yasiyo mashiko kwamba CUF ni chama cha Wapemba, cha Waarabu, cha fujo, kilipaka vinyesi kwenye visima na skuli za Pemba au kinachotaka kuvunja Muungano. Mjengeko wa kiuongozi, msimamo, na kwa hakika hata sera ya CUF kuhusiana na maendeleo ya nchi, umoja wa kitaifa, Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano ni mambo yanayonajieleza zenyewe na hayataki kusaidiwa. Labda kwa faida ya msomaji, asome ilani za uchaguzi za mwaka 1995, 2000 na 2005, Katiba ya CUF na hata maandishi ya viongozi wakuu wa chama hicho, ambayo yanapatikana bure kwenye http://hakinaumma.wordpress.com na kwenye rekodi nyengine.

Ikiwa msingi wa madai haya ni matokeo ya kura kwa mujibu wa matangazo ya Tume za Uchaguzi (ZEC ya Zanzibar na NEC ya Tanzania), basi msomaji pia anashauriwa kuhakiki hasa zoezi zima la uchaguzi katika visiwa vya Zanzibar kabla hajarukia kwenye hitimisho la mwandishi wa makala ile. Rekodi za chaguzi hizo zinapatikana kwenye mitandao na maandishi mbali mbali nchini kama vile taarifa za waangalizi wa ndani (TEMCO). Kinachohitajika ni mtu kujipa tu muda na uhuru wa kuyasoma.

Badala yake ni Chama cha Mapinduzi (CCM) ndicho kinachoweza, kwa ushahidi kabisa kuhusishwa na kuitendea maovu Zanzibar kwa misingi ya ubaguzi, uvunjaji wa haki za binaadamu, kuvunja umoja wa kitaifa na hata kuiondolea mamlaka yake ya kujiamulia kama nchi huru. Kwa mfano, ni CCM ndiyo ambayo imekuwa ikijichorea yenyewe taswira ya chama cha kibaguzi kinachoendeshwa kwa misingi ya historia potofu ya Uarabu na Uafrika na ushahidi mmoja wa wazi ni pale, kwenye kinyang’anyiro cha tiketi ya kugombea uraisi wa Muungano mwaka 2005, kilipomkataa Salim Ahmed Salim kwa sababu tu yeye ana asili ya Kiarabu na ni Mpemba (Soma waraka wa Joseph Bukuku na kitabu cha Makwawaiya wa Kuhenga, CCM na Hatima ya Tanzania).

Ni CCM ambayo mwaka 1995 ilipitisha na kusimamia sera ya kuwafukuza kazi Wazanzibari wenye asili ya Pemba, kuwavunjia nyumba zao na kuwazuilia fursa za masomo ya juu (Soma waraka wa CCM, Ofisi Ndogo Kisiwandui kama ulivyonakiliwa katika Uafrika au Uzanzibari? cha Juma Duni).

Ni CCM ambayo mwaka 2001 iliwaua, kuwatesa, kuwanajisi na kuwaibia mali zao Wazanzibari hao wakiwa kwenye kisiwa chao (tembelea mtandao wa Human Rights Watch usome taarifa “Risasi Zilinyesha Kama Mvua”, http://hrw.org). Kwa hakika, CCM inategemea sana fujo katika kuishi kwake kuliko msamiati wa ‘amani na utulivu’ inaouhubiri.

Ni CCM ambayo ina makundi ya Janjaweed, mote Unguja na Pemba, ambayo huwavamia raia wenye asili ya Pemba, wenye asili ya Kiarabu na wale wote wanaodhani kuwa ni wapinzani wao, kuwapiga, kuwabaka na kuwachomea moto nyumba zao (Soma kitabu cha mwaka 2007 cha Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu kwenye sehemu iliyoitwa Zanzibar Chapter). CCM ni baba wa fujo na vurugu. Nje ya fujo, haina uwezo wa kuvuta hewa kwa maana ya kwamba haiwezi kubakia madarakani.

Kwa hivyo, ikiwa hoja ya Upemba wa CUF ilijikita juu ya kukataliwa kwa CCM katika chaguzi hizo tatu na Wazanzibari wenye asili ya Pemba, mwandishi wa makala hiyo anashauriwa kwamba aangalie mwenendo wa siasa za vyama vingi kuanzia mwaka 1992 hadi sasa kabla hajarukia kwenye hitimisho la hoja yake. Maana viashiria (premises) vyote vya hoja anayoijenga vinaelekea kwenye hitimisho tafauti na hilo alilolitoa.

Kama nilivyosema, wacha tuyadharau kwa makusudi madai hayo kwa sababu yanadharaulika. Na kwa hali hiyo, hata nukta ya mwanzo ya kuihusisha CUF na fujo kwa sababu ya kauli yake ya ‘jino kwa jino’ haina nafasi tena ya kujadiliwa, maana inaingia katika mkumbo huo huo wa madai yasiyo mashiko, huku kinyume chake kikiwa ni kweli. Nakusudia kusema kwamba, ukweli ni kuwa CUF ndicho chama cha amani – mfano kimeendelea kuamini njia za kisiasa na kidiplomasia hata katika wakati ambapo CCM inalazimisha matumizi ya fujo kwa kuapndikiza chuki za ukabila na uzawa huku ikivunja haki za binaadamu na kuwadumaza Wazanzibari wasiendelee pale inapotuma vikosi vyake vya Janjaweed kuharibu, kuchoma moto na kuiba mali za watu (Pitia rikodi za uchaguzi wa 2005 kuanzia uandikishwaji katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura).

Nukta ya ujanja wa CUF kupindisha ukweli na inayomsifu Kikwete kwamba ni kiongozi anayejua wapi aseme nini na vipi ndiyo inayoweza kujadiliwa. Nukta inadai kuwa kutokana na uweledi huo, akiwa kisiwani Pemba, Kikwete “alihimiza umoja wa wananchi, ushirikiano wa vyama vya siasa katika kuwaletea watu maendeleo.” Bila ya shaka, hakuna ubaya katika hilo, lakini ubaya ambao makala ile hauusemi ni kuwa Kikwete alitumia ubaguzi kukemea ubaguzi. Nitafafanua.

Ukweli ni kuwa Rais Kikwete anapenda sana kuwasakama Wapemba kama Wapemba na si kama Watanzania wengine; na hili ndilo lililotufanya tangu mwanzoni kuishuku dhamira yake aliyoitangaza Bungeni Disemba 30, 2005 ya kutafuta suluhu ya kudumu kwa ‘mpasuko’ wa Zanzibar. Kwamba hata katika hotuba hiyo ya Bungeni alisema wazi kuwa anashangazwa na Wapemba ambao ambao wamezagaa katika pembe zote za Jamhuri ya Muungano, lakini wakawa wanataka kujitenga!

Kisa? Walikuwa wamekipa chama kisichokuwa CCM madaraka ya kukiongoza kisiwa hicho. Mwaka 1995, karibuni Kilimanjaro nzima ilikuwa mikononi mwa NCCR Mageuzi, lakini Wachagga hakuambiwa kuwa wanajenga hisia za kujitenga. Kwa nini Wapemba tu?

Kabla ya hapo na baada ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa 2005, Kikwete alihojiwa na gazeti moja la Kiswahili litolewalo kila siku Dar es Salaam na akayaelezea matokeo ya uchaguzi huo kama muakisiko wa Upemba na Uunguja, na hata lile jimbo la Mji Mkongwe la Unguja lililokwenda kwa CUF, alisema, ilikuwa hivyo kwa sababu wapiga kura wa hapo ni Wapemba watupu. Kikwete amewahi kuishi Unguja akifanya kazi Kiswandui, karibu kabisa na Mji Mkongwe, lakini hasemi kweli anapodai kuwa jimbo hilo linakaliwa na Wapemba tu, au hata kama wengi wa wakaazi wa hapo ni Wapemba.

Mara nyingine alikuwa katika ziara za ‘kuwashukuru’ wananchi wa Pemba na Unguja kumchagua mwanzoni mwa mwaka 2006 na tena akiwa visiwani huko akapiga tena mfano wa wakaazi wa Kisiwa Panza wanaogomewa na wenzao kusafirishwa kwenye mtumbwi kwa kuwa tu wao ni wana-CCM.

Upotofu wa mifano hii si ukweli au uongo wake, bali ni muamala wake. Kwamba Kikwete hataki kusema kuwa kile hasa kinachomfanya mwana-CUF kumgomea mwana-CCM ni ukweli kwamba huyo CCM anayegomewa ndiye huyo huyo ambaye aidha alikwenda kupeleka fitina polisi dhidi ya mwana-CUF anayegomea na matokeo ya fitina hiyo ni mwana-CUF kuvamiwa nyumbani kwake, kupigwa mbele ya watoto wake, kubakiwa mke wake, kuibiwa na kuharibiwa mali zake, kuchomewa moto nyumba yake na mwisho yeye mwenyewe kuwekwa ndani kwa kesi ya kuvuruga ‘amani na utulivu.’

Upotofu ni kutokusema kuwa, mwana-CUF huyu mnyonge, baada ya kufanyiwa unyama wote huo na mwana-CCM huyo akishirikiana na dola ya CCM, analazimika kutoa fedha nyingi ili atolewe ndani na anarudi kijijini kwake akiwa uso chini. Ameshapoteza kila kitu: mali, nguvu na, kikubwa kuliko yote, utu na heshima yake.

Upotofu ni kutokusema kwamba, kwa unyonge wake mwana-CUF huyu halipizi kisasi cha kumpiga yule mwana-CCM aliyesababisha haya kama alivyopigwa, kumbakia mke wake kama alivyobakiwa, kumharibia mali kama zake kama zilivyoharibiwa wala kumchomea nyumba yake moto. Lakini anachofanya pekee ni kukata mawasiliano na mahusiano tu na yule mbaya wake. Anamgomea mwana-CCM hata kama ni ndugu yake wa damu, maana ndugu huyo hakuthamini udugu wao ndio maana alithubutu kumfanyia aliyomfanyia.

Kuna unyonge kuliko huo? Kuna namna dhaifu zaidi ya kueleza hisia za mdhulumiwa kama huko? Sasa Kikwete anapozungumzia upande mmoja tu wa ‘mgomo’ huo unaotokezea Pemba, anafanya nini kama si huo ujanja wa kupindisha hoja? Kwa hakika ni Kikwete na CCM ndio wanaopindisha hoja panapohusika suala zima la Pemba na la Zanzibar kwa ujumla wake.

Nukta nyingine inahusu mpishano wa kile alichokisema Kikwete na lawama ambazo anatupiwa kutoka uongozi wa CUF. Kwa kuanzia ni kwamba makala ile inadanganya inaposema kuwa Rais Kikwete hakusema kuwa wapinzani hawawezi kupewa nchi. Kikwete alisema hivyo. Lakini, kwa manufaa ya mjadala, tujadili kile kile tu kinachosemwa na makala hiyo kuwa kilisemwa na Kikwete, yaani ni serikali iliyoko madarakani tu ndiyo yenye jukumu la kuleta maendeleo na kwamba wawakilishi na wabunge ni wapiga kelele tu.

Huu ni upotoshaji wa makusudi. Licha ya kuudharau mfumo wa demokrsia ua uwakilishi, upotofu mkubwa hapa ni kuueleza sivyo mfumo wa uendeshaji nchi unaofuatwa na Tanzania na Zanzibar, ambao ni ule wa mgawanyo wa madaraka baina ya mikono mitatu ya serikali: Baraza la Mawaziri (the Executive), Bunge au Baraza la Wawakilishi (Legislature) na Mahkama (Judiciary). Kikwete na Amani Karume, kimsingi wanasimamia tawi moja tu kati ya hayo, yaani Baraza la Mawaziri. Ni kweli kuwa ni tawi hilo ndilo lenye dhamana ya kuleta maendeleo, lakini ni kwa maagizo na idhini ya Bunge na au Baraza la Wawakilishi, mabaraza ambayo Rais Kikwete anataka kutuaminisha kuwa kazi yake ni kupiga kelele.

Ndio maana, kwa kuwa kazi ya mabaraza hayo si kupiga kelele bali kuisimamia serikali, kila mwaka matawi yanayoongozwa na Kikwete na Karume hupeleka bajeti zao Bungeni na Barazani na kuomba ziidhinishwe na wabunge na wawakilishi. Si Kikwete wala Karume anayeweza kukurupuka, chini ya utawala wa sheria, kwa mfano, akachota mapesa kutoka Hazina ya nchi akajenga barabara Pemba bila ya fedha hizo kuidhinishwa na kukubaliwa na Bunge, hata kama kujenga barabara kunaweza kuwa jambo la kimaendeleo kwa Pemba. Akifanya hivyo, kama ilivyotokezea kwa Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), utakuwa ni ufisadi wa kutumia madaraka vibaya.

Kwa hivyo, alichokisema Rais Kikwete ni nusu uongo na nusu ukweli na ndio maana viongozi wa CUF – kama walivyo watu wowote makini – wameguswa na sehemu hiyo ya uongo na wakamlaumu Kikwete.

Lakini tuende mbele zaidi katika kauli zake, maana kwa hakika hilo si pekee alilosema na kutukera wengi wetu. Alipokuwa Pemba alisema kwamba huenda wapinzani wasiingie kamwe madarakani na alipokuwa Unguja alisema kwamba yuko tayari kuendelea kuyalinda Mapinduzi. Kauli hizi zina maana kubwa kwa siasa za Zanzibar, maana zinaakisi hasa matashi na ‘Sera ya Muungano’ kuelekea Zanzibar. Ni kauli kongwe na ambazo kila zinapotolewa huwa na maana ile ile moja. Mkapa aliwahi kuzisema na matokeo yake ndiyo ya 2000, 2001 na 2005.

Kwa hakika hasa, tafsiri ya utayarifu wa kuyalinda Mapinduzi ni kuzuwia mchakato wowote wa kidemokrasia visiwani Zanzibar. Kuhakikisha kwamba CCM ndiyo inayotawala milele kwa gharama yoyote ile – kama kwa kutumia mauaji kama yale ya Januari 2001 au vikosi vya majeshi vyenye silaha nzito kutoka Bara na Janjaweed wa 2005. Kunamaanisha kuiweka Zanzibar ‘mahala’ pake kwa kiwango ambacho uhusiano baina ya Zanzibar na Tanzania Bara unahusika kupitia kivuli cha Muungano. Mahala hapo ni pale ambapo kiongozi wa Zanzibar lazima awe ni yule aliyeridhiwa na Tanzania Bara “kulinda maslahi ya Muungano”, kwa kutumia maneno ya Rais Mkapa.

Hili haliitii khofu CUF kama CUF tu, bali ni khofu ya Wazanzibari tulio wengi na ni khofu ya kila muumini wa uhuru wa mwanaadamu na maendeleo ya demokrasia. Tunajiuliza hivi nini maana ya uhuru wetu kama watu wa nchi hii? Tunajiuliza nini dhamira ya Wazanzibari kufanya Mapinduzi na kujitawala ikiwa mpaka leo tumedhibitiwa na kuhakikishiwa kwamba hatuwezi kufanya maamuzi kama sisi na maamuzi hayo yakasimama? Ni suala la uhuru wa kujiamulia wa Wazanzibari ndio uliopo hatarini hapa na si suala la CUF tu kutokuingia madarakani. Ni bahati mbaya sana kwamba CUF tu ndio ambao wamekuwa wakiongoza hisia za Zanzibar iliyo bora na huru zaidi kuliko ilivyo sasa, pamoja na kuwa ina sera nzuri sana ya Muungano.

Kuna hoja ya Profesa Issa Shivji katika kitabu chake Pan Africanism or Pragmatism, kinachoangalia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kwamba matatizo ya kisiasa ya Zanzibar na kero za Muungano ni pande mbili za sarafu moja. Ni kauli kama hizi na utekelezaji wake, ndio unaofanya wengine tukaamini kuwa kiini cha matatizo ya Zanzibar hakipo Zanzibar, bali kipo Dodoma kwenye vichwa vya viongozi aina ya Kikwete ambao wanaamini kabisa kwamba kuidhibiti Zanzibar ndiko kudumisha Muungano.

Mwisho tuongelee nukta ya dhana ya maendeleo. Alichoambiwa na ambacho hata mimi naweza kumwambia Rais Kikwete ni kwamba hajui maana ya maendeleo. Labda ndio sababu wakati alipoulizwa na jarida moja la nje kwa nini Watanzania ni masikini, akasema hata yeye hajui kwa nini. Hajui kwa kuwa hajui tafauti baina ya kuendelea na kutokuendelea, baina ya umasikini na utajiri. Kama hujui tafauti hizo, bila ya shaka huwezi kujuwa sababu zake.

Hajui kwa kuwa maendeleo hayapimwi kwa kutokuendelea, maana mfano aliopiga kuwa kila baada ya kilomita tano pana kituo cha afya Zanzibar kinyume na Bara ambako ni kila baada ya makumi ya maili unaweza tu kutolewa na kiongozi asiyejua maana ya maendeleo. Ni kama kumwambia mgonjwa aliyezimia “Bora wewe afadhali maana huyu mwenzako keshakufa kabisa!”

Zanzibar kwa historia, jiografia na utajiri wake haiwezi kuambiwa imeendelea miaka 45 baada ya Mapinduzi kwa eti kuwa na vituo vya afya (ambavyo havina dawa) kila baada ya kilomita tano (ingawa huu ni utiaji chumvi tu) au kwa kuwa watoto wake wanakwenda skuli wanakojazana 150 kwenye darasa moja, wakiwa wamekaa chini na wanafundishwa na mwalimu asiye uwezo wala vitendea kazi!

Labda nimpe mfano mmoja unaonikumbushia machungu lakini unaopingana kabisa na kauli ya Kikwete kuwa sasa mtoto wa Kizanzibari hafi tena kutokana na malaria. Mwaka mmoja tu uliopita mimi na mke wangu tulipoteza mtoto wetu wa miezi sita katika hospitali ya Mnazi Mmoja, kwa sababu hiyo hiyo ya malaria na ukosefu wa huduma za uhakika katika hospitali hiyo kubwa ya serikali. Na ukweli ni kuwa sisi si wazazi pekee wa Kizanzibari ambao kichanga chetu kilitutoka mbele na kwenye mikono ya madktari wa Mnazi Mmoja ambao hawana vifaa wala uwezo. Ni bora Rais Kikwete asitukumbushe kilio matangani, maana hapatakuwa na wa kutunyamaza tukianza kulia!

Hata hizo barabara za ‘mgongo wa ngisi’ anazozisema Kikwete kwamba ni ishara ya maendeleo ni kituko zinapolinganishwa na zile zilizopo Bara. Barabara ya Mkoani-Chake, kwa mfano, ambayo haifiki hata kilomita 50, ni nyembamba mno kuweza kuiita barabara kuu kama ya Bagamoyo inayoelekea nyumbani kwa Kikwete. Kwa hakika barabara zote za Zanzibar, Unguja na Pemba, hata ziunganishwe hazifiki robo ya urefu wala ubora wa Barabara ya Morogoro. Nchi nzima ya Zanzibar ina taa za kuongezea gari sehemu mbili tu – Mkunazini na Malindi, na hivyo vipande vyake vya barabara havina mitaro kama zilizvyo hata barabara za mitaa ya Ilala.

Ukweli ni kwamba Zanzibar inarudi nyuma kimaendeleo na hayo ni matokeo ya uongozi usio na misheni wala visheni ya kuiongoza Zanzibar. Saikolojia na falsafa nzima ya uongozi wa CCM kwa Zanzibar haina tafauti hata kidogo na ya Israel kwa Palestina au ya Marekani kwa Iraq. Kwa hakika, hivyo ndivyo hasa alivyosema Mkapa mwaka 2005 alipoulizwa sababu ya serikali yake kushusha vikosi vya kijeshi vyenye silaha nzito nzito visiwani Zanzibar: “Kwani vikosi vya Marekani vinafanya nini kule Iraq?” Ndivyo alivyojibu; na huo ndio ukweli wenyewe.

One thought on “Utetezi wa Kikwete ni chapwa”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.