VIONGOZI wa imani ya Kikristo wanastahiki kusifiwa kwa kuzitumia sikukuu na mikusanyiko yao ya kidini kuzungumzia sio tu Uokovu, Uzima wa Milele na Uokovu, bali pia mambo yanayogusa khatima ya nchi na wananchi wa nchi zetu.

Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.
Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.

Huko nyuma wamewahi kuzungumzia masuala kadhaa makubwa makubwa likiwemo hili maarufu la ufisadi na, angalau kwa kufanya hivyo, wamekuwa wakionesha wapi Kanisa linasimama katika masuala ya kitaifa. Ni jambo la kusifiwa na ni viongozi wa dini nyengine wafanye hivyo bila ya khofu ya kuandamwa na Dola kwamba wanachanganya dini na siasa.

Stahiki hii ya sifa, hata hivyo, haimaanishi kwamba kila linalosemwa na viongozi hao ni sahihi lisiloweza kukosolewa. Kuna wakati viongozi wa Kanisa, ama kwa makusudi au kwa bahati mbaya, hutoa kauli ambazo zina makosa.

Hizi si vyema zikaachiwa bila kukosolewa, maana kwa nguvu walizonazo viongozi hao, kauli zao zinaweza kusababisha upotoshaji na hivyo maumivu makubwa. Hilo linaweza kuporomoa heshima ya Kanisa kama ambavyo imewahi kutokea kwa dhima ya Kanisa Katoliki kwenye historia ya mauaji ya Wayahudi Barani Ulaya; na hicho si kitu chema hata kidogo.

Nukta ya mjadala hapa ni tabia iliyoanza kujengeka hivi sasa ya ama viongozi wa Kanisa kutumia madhabahu yao kujaribu kutetea rekodi mbaya ya Rais Mstaafu Benjamin Mkapa au kumpa mwenye Mkapa fursa ya kutumia Kanisa kujisafishia kwa uovu wake.

Sisi tunaamini kuwa, ukiwacha kauli ya Askofu Mstaafu wa Kanisa Anglikana, John Ramadhani, wa Zanzibar aliyeripotiwa kumtaja Rais Mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa, kama kiongozi aliyeheshimu haki za binaadamu katika utawala wake wa miaka kumi (1995 – 2005) kwa sababu hakupitisha hata adhabu moja ya kifo kwa kipindi chote hicho.

Hii ni kauli iliyokwenda upande sana. Labda ni suala la mjadala ikiwa kutokupitisha adhabu ya kifo ni kigezo cha kuheshimu haki za binaadamu na pia ikiwa adhabu yenyewe ya kifo ni uvunjwaji wa haki hizo, lakini si kitu cha mjadala hata kidogo kwamba Mkapa alizivunja haki za binaadamu katika siku za utawala wake.

Hili ndilo linalokusudiwa kuthibitishwa na makala hii ambayo lengo lake kuu ni kuweka rikodi sawa, maana – kama ilivyosemwa hapo juu – kauli kama hii inaweza kusababisha maumivu makubwa. Na maumivu hayo yanaongezwa uzito na sababu mbili zaidi: kwanza ni mahala ambapo kauli hiyo imetolewa, yaani Zanzibar, ambako kulishuhudia kiwango cha hali ya juu cha ukandamizwaji wa haki za msingi za raia wasiokuwa na hatia.

Pili ni kwa kuwa mwezi mmoja tu tangu kutolewa kwa kauli hii, Watanzania watakuwa katika kumbukumbu za mauaji ya kutisha yaliyofanywa kuanzia Januari 26, 2001 na vyombo vya dola, wakati huo Mkapa akiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama.

Kwa Watanzania hawa na hasa kwa wahanga wa mauaji yale – vilema, wajane, mayatima, walionajisiwa na waliopoteza watoto, ndugu, jamaa na wenzi – kauli ya Baba Askofu Ramadhani ni kejeli na ni kile wanachokiita Waswahili “msumari mmoto juu ya donda bichi!” Ni maumivu!

Mkapa sio tu kwamba hakushughulika kuzilinda haki za binaadamu, bali pia alikuwa mshiriki mkuu wa kuzivunja na alikuwa na kipaji cha pekee cha kutumia ulimi wake kuhalalisha uvunjaji huo.

Tuthibitishe hilo kwa kuanzia na hotuba yake ya mwishoni mwa mwaka 2005 kwenye hoteli ya Golden Tulip, jijini Dar es Salaam, ambapo aliapa kwamba alikuwa tayari kutumia nguvu zake binafsi na za Dola kuhakikisha kuwa Chama chake cha Mapinduzi (CCM) kingelibakia madarakani.

Kisiasa, wakati huo Mkapa alikuwa akitaka afahamike kuwa anajibu tu kauli ya Chama cha Wananchi (CUF) ambacho kilikuwa kimeahidi kwamba, kama mwaka huo nao matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar yangelipotoshwa kama ambavyo ilikuwa imewahi kutokea mara mbili huko nyuma (1995 na 2000), basi kingelitumia “Nguvu ya Umma” kurejesha haki iliyoporwa!

Lakini ukweli ni kuwa Mkapa alikuwa akizungumza kijeshi kama Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama na, makhsusi kabisa, alikuwa anawatisha Wazanzibari. Historia ni shahidi kuwa uzoefu wa kutumika nguvu hizi ni mbaya kwa Zanzibar hasa inapokumbukwa maafa ya 2001 na, kwa wakati huo, vituko vilivyokuwa vimeanza kufanywa na vijana wa CCM, maarufu kama Janjaweed, kuelekea uchaguzi wenyewe wa 2005.

Ikiwa ni muhimu kurejea tena ni nini na nini kilifanywa na vijana hao, basi kwa ufupi ni kuwa walipiga watu kwa nondo, wakachinja kwa mapanga, wakachoma moto majumba na mali za watu, wakaiba, wakabaka na wakaua. Na hayo yalifanyika mbele ya macho na masikio ya Mkapa, kwa maana kwamba alikuwa akiyasikia na akiyaona kupitia vyombo vyake kama mkuu wa nchi; na wala hakuyazuia yasitokee. Hiyo ndiyo rekodi ya Mkapa ya haki za binaadamu!

Ni mtu wa mwisho tu kufikiri ndiye atakayeamini kuwa Mkapa alikuwa muumini wa demokrasia ya kweli na mchungaji wa haki za binaadamu. Anayetaka kuwa mkweli wa nafsi yake atafahamu kuwa mipaka ya demokrasia na haki za binaadamu kwa Mkapa ilianzia na kuishia pale nafasi ya chama chake kushika hatamu ilipohusika. Na kwa uhakika hasa, Mkapa alitumia ‘kila njia’ kuona kuwa demokrasia inafeli Zanzibar kila alipoona kuwa kupasi kwake kulimaamisha kung’olewa kwa CCM madarakani.

Mkapa hakuwa chochote zaidi ya dikteta mwengine tu wa Kiafrika, ambaye alifahamu neno moja tu: “power, power, by any means.” Ni njia hizo chafu na mbaya ndizo zilizotumiwa na Mkapa kuwanyima haki zao Wazanzibari, kuwanyanyasa na kuwakandamiza kadiri ambavyo andasa zake zilimtuma. Ni kama kwamba Mkapa alitumia uraisi wake kuwapokonya Wazanzibari kila kile kizuri walichokuwa nacho kwa mabavu ya vyombo vyake vya dola.

Kwa mfano, ni haki ya Wazanzibari kuona kuwa madaraka ya kuiongoza nchi yao yanachimbukia mikononi mwao. Kwa kumnukuu mwenyewe Mkapa katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi Mei 2003: “Hapana mahala bora pa kuhifadhi madaraka ya nchi zaidi ya kwa wananchi wenyewe”.

Maana ya kauli hiyo ni kuwa madaraka ya nchi yanachimbukia mikononi mwa wananchi na ni jukumu la wanaoyatafuta, wayapatie kutoka huko. Kwa taratibu za kistaarabu, ndio ikaamulika kuwa madaraka hayo yapatikane kupitia kura za wananchi. Na ili ridhaa hiyo ya kura ihalalike, basi ni lazima iwe inatokana na mfumo wa uchaguzi huru, wa haki, ulio wazi na wenye kukidhi vigezo vya kidemokrasia.

Lakini Mkapa aliitwaa haki hiyo kwa miaka yote ya utawala wake na yeye ndiye aliyekuwa akiamua nani awatawale Wazanzibari. Alifanya hivyo 2000, akarudia 2005.

Wazanzibari walikuwa na haki ya kuishi maisha salama na huru, yaliyoepukana na hofu na wasiwasi. Katika miaka kumi ya utawala wake, Mkapa aliifanya Zanzibar kuwa pahala pa khofu zaidi kupaishi. Mwaka 2001 aliwafanya Wazanzibari waikimbie nchi yao kufuatia mauaji na utesaji wa waandamanaji wasio na silaha.

Kama ilivyotamkwa hapo juu, kuanzia mwaka 2004 aliruhusu kuwepo na kufanya kazi kwa Janjaweed ambao walivamia majumba na biashara, wakachoma moto mali na kuwakata Wazanzibari kwa mapanga. Janjaweed walikuwa pia wakiwateka nyara Wazanzibari (rejea mkasa wa Mzanzibari Zahor Shaaban (45) 12/10/2005 Jang’ombe). Kwa hivyo, sio tu kwamba Mkapa alishindwa kulinda usalama wa Wazanzibari, bali pia alishiriki kuuvunja na kupandikiza khofu na machafuko ndani ya jamii.

Ilikuwa haki ya Wazanzibari pia kuishi nje ya mipaka ya ubaguzi na unyanyasaji. Walikuwa na haki ya umoja, ushirikiano na heshima, licha ya tafauti za kiuzawa, kidini na au za kisiasa. Na hiyo ndiyo fahari ya Zanzibar.

Mkapa aliipora haki na fahari hiyo. Badala yake, kwa kutumia mawakala wake waliotapakaa kila mahala katika vyombo vya dola, vya habari na taasisi za kiserikali na za kiraia, aliutumia wakati wake kuendeleza mgawanyiko wa Wazanzibari, kwa mfano baina ya Waafrika na wasio kuwa Waafrika (rejea hotuba yake aliyoitoa Micheweni Pemba Oktoba, 2000).

Wazanzibari hawa walipotaka kutumia kura yao kuiunganisha tena Zanzibar yao, kuirudisha heshima yao na kushirikiana, Mkapa akashusha Zanzibar vikosi vya kijeshi vyenye silaha nzito nzito kuzuia hayo yasitokee.

Huyu, kwa hivyo, si aina ya kiongozi ambaye anastahiki sifa ya kuitwa mtetezi na mlinzi wa haki za binaadamu ati kwa kuwa hakupitisha hukumu hata moja ya kifo katika utawala wake.

Maana ni kijembe kuwa hakusaini watu kunyongwa, lakini aliruhusu vyombo vyake vya dola kuwamiminia risasi na kuwaua raia wake, akawaachia raia hao wanajisiwe, wapigwe, wafukuzwe katika nchi yao na waharibiwe mali zao. Mlinzi na mtetezi gani huyu wa haki za binaadamu?

Kijembe kilioje ni kuwa kuhalalisha matendo yake dhidi ya Zanzibar, mwaka 2005 alisema kwamba alipeleka vikosi vya kijeshi Zanzibar kama Marekani ilivyopeleka vyake nchini Iraq.

Na kwa hili basi, kama kuna chochote ambacho Mkapa anakistahiki kutoka kwetu, kitu hicho ni kurushiwa viatu kama alivyorushiwa Rais George Bush wa Marekani na Wairaq.

One thought on “Anachostahiki Mkapa ni kurushiwa viatu!”

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.