Na Ally Saleh

Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi alikuwa na ziara ya siku kadhaa katika mikoa mitano ya Zanzibar akifanya kazi ya Kiserikali na pia ya chama chake.

Hiyo ni moja ya ziara nadra za Rais Kikwete ambaye ana sehemu kubwa zaidi ya Tanzania Bara kuitembelea kuliko Visiwa viwili vya Unguja na Pemba. Kwa muda aliokaa kwa hakika inaonekana kama amefanya upendeleo.

Ziara ya Kikwete imeelezwa ni ya kutimiza ahadi yake aliyoitoa wakati alipokuja kuwashukuru wananchi wa Zanzibar kwa kumchagua kushika Urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa 2005. Kwa maneno mengine bado kuna muendelezo wa kutoa shukurani kwa tukio hilo la miaka minne iliyopita.

Katika ziara yake hii Kikwete amehusishwa na kauli mbili zenye utata na zote kwa hakika zina uzito wake. Kwanza ni kwa utata wa kauli hizo lakini pili ni kwa ajili ya uzito wake na tatu ni kutokana na kutoka kwenye kinywa chake yeye.

Akiwa kisiwani Pemba, Rais Kikwete ameelezwa kusema kuwa itakuwa ni vyema kwa wanachama wa chama cha upinzani kutoa ushirikiano na chama tawala CCM kuiletea Pemba maendeleo kwa sababu serikali wanayoitaka ya chama cha CUF inaweza ikakawia kuja lakini kubwa zaidi huenda isije kabisa.

Ingawaje Kikwete amekuwa mjanja kidogo. Ili asilaumike kama ambavyo imetokea, kuwa ametoa kauli ya maamuzi kuwa hata CUF ikishinda serikali haitapewa kuongoza nchi, wengi wamekuwa na msimamo kuwa hivyo ndivyo alivyokusudia hasa.

Na hilo humu Visiwani si geni. Kwamba CUF haitatawala ni matamshi ya kawaida tu na wakati mwengine yakishindikizwa na kauli kuwa kilichotoka kwa mtutu wa bunduki hakitatolewa kwa karatasi ya kisanduku cha kura.

Ujanja alioutumia Kikwete ni kuwa CUF haiwezi kuwa na nafasi ya kushinda kwa sababu CCM imekuwa ikitimiza wajibu wake wa kuwaletea wananchi wa Zanzibar maendeleo.

Akihutubia katika Uwanja wa Kibanda Maiti, Kikwete aliorodhesha msururu wa mafanikio ya Serikali ya Zanzibar na chama chake kutimiza ilani ya Uchaguzi Mkuu wa 2005, ambapo wananchi walisikia majigambo hayo hivi juzi watu wakati wa Sherehe za Mapinduzi kutoka kwa Rais wa Zanzibar, Amani Karume.

Kikwete alisema sababu kubwa ya Wapinzani kushindwa ni kule kukataa kwao kukubali kuwa kumekuwa na kiasi kikubwa cha maendeleo. Alisema wana wajibu wa kwanza kukiri kilichofanikiwa na kisha waeleze wao watafanya kitu gani cha ziada.

Alitoa mfano wa kuwa ikiwa ipo mifereji ambayo tayari inatoa maji basi wapinzania waje na programu ya kueleza ni vipi wao wataweza kutoa maziwa katika mifereji hiyo.

Lakini kauli ambayo nataka zaidi kwa leo kumhusisha nayo Rais Kikwete ni ile ya kulileta tena suala la Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 na kama kawaida linapotajwa suala hilo malaika huwasisimka watu. Alisema haiwezekani kabisa kuchezea Mapinduzi hayo ambayo sasa yana umri wa miaka 45.

“ Kama hajipendi ajaribu…kama hajitaki ajaribu…Yote chezeeni Mapinduzi hapana…ukiyachezea Mapinduzi unawarudisha watu kwenye utumwa, unawarudisha watu kwenye utwana. Hili liliondoka Januari 12, 1964 na halitarudi tena….haiwezekani.”

Hiyo ndio kauli ya neno kwa neno ya Rais Kikwete ambayo inanifanya nijiulize masuala chungu nzima na hasa kuhusisha kauli hiyo na suala zima la demokrasia na ushiriki wa kisiasa hapa Zanzibar.

Kwanza kauli ya Kikwete ina alama ya vitisho ingawa vitisho hivi havionekani kukaziwa lakini hakuna shaka yoyote kuwa anaetaka kuchezea mapinduzi atakiona maana itakuwa hajipendi na hajitaki.

Hilo haliwatishi sana Wazanzibari kwa sababu wameshaambiwa mara kadhaa wa kadhaa kuwa kucheza na Mapinduzi ni kucheza na moto. Tokea 1964 hadi hivi leo kauli hiyo haijabadilika kabisa.

Na hapo ndipo penye hoja yangu. Hoja ya kwanza ni kuwa hivi baada ya miaka 45 bado kuna wasi wasi kuwa Mapinduzi yanaweza kuchezewa? Kama upo wasi wasi huo basi Mapinduzi yenyewe yana wasi wasi hata baada ya miaka 45 na kuambiwa kuwa yamejizatiti.

Pili, ni nani hao kila siku wanaoambiwa wanachezea Mapinduzi? Jee ni wale ambao wana mawazo tofauti na Mapinduzi hayo ya 1964 au wale ambao wamo ndani ya Mapinduzi lakini wamekuwa wakiyatumia vibaya na kuyadunisha kwa kushindwa kuyapa haki yake kwa kuendeleza dhulma, ufujaji wa mali na kukaba roho demokrasia?

Tatu, nin hasa maana ya kuchezea Mapinduzi? Kuyahoji ay kuyakosoa, kueleza kuwa kungeweza kuwa na njia mbadala za kuyapeleka mbele Mapinduzi hayo au kudai kuwa mpaka leo Mapinduzi yanakwamba katika kukumbatia umma wote, wote nzima na yanajibana katika kundi moja tu?

Nne, ni kuwa katika chama ambacho hakina sera za kuendeleza Mapinduzi hayo kwa sababu wanazoona wao zinawafaa? Na kwa sababu hiyo kuambiwa kuwa asiyetaka kuendeleza Mapinduzi basi asahau kupewa utawala wa visiwa hivi?

Au kuchezea Mapinduzi ni kutaka kuiondoa Serikali ya Chama cha Mapinduzi ili uwepo utawala mbadala ambao utakuwa na fikra tofauti na zilivyo hivi sasa juu ya Mapinduzi hayo na hilo likionekana haliwezi kustahamilika?

Nina wasi wasi mkubwa na kauli hii ya Kikwete kuendeleza wazo moja (cliché) kuwa Mapinduzi hayachezewi, yasichezewe na hayachezeleki wakati anajua Visiwa hivi kama ilivyo Tanzania vimo katika siasa za ushindani wa vyama.

Inawezekana kabisa, ingawa yeye anasema kuna nafasi ndogo kwa chama cha CUF kuweza kushinda uchaguzi kama si wa 2010 basi mwengine wowote unaofuata, na kwa kauli ya Kikwete kuendeleza dhana hiyo kongwe ya “Mapinduzi hayachezewi” ina maana kuwa CUF haitapewa Serikali.

Kuna hatari kubwa Rais Kikwete kuendeleza mawazo kama hayo wakati yeye akiwa ni mas-ul katika masuala ya demokrasia ndani ya nchi na akijua wazi kuwa kwa chaguzi tatu mfululizo kauli kama hizo zimekuwa zikitumika na wengi wakiamini ndizo msingi mkuu wa uchaguzi wenye msuguano hapa Zanzibar.

Kikwete, kama Rais Benjamin Mkapa na kama Rais Ali Hassan Mwinyi anajua kuwa suala la Mapinduzi Zanzibar, kwamba lazima yaendelee kulindwa kwa hali yoyote, kwa sababu tu ya kuwa chama chengine chochote kitayachezea, ndiko pia kunapelekea kukosekana maridhiano ya kisiasa hapa Zanzibar.

Nionavyo wakati umefika hivi sasa kuwa na tafsiri mpya ya kuendeleza Mapinduzi. Si vyema kukaa katika fikra kongwe kuwa anayeweza kuendeleza Mapinduzi ni yule yule aliyeyaleta wala kwamba Mapinduzi yenyewe yanaweza kufa kwa sababu tu ya kuondoka madarakani chama kilichoyaleta.

Badala ya viongozi kuendelea kuimba kuwa Mapinduzi lazima yaendelezwe ni vyema uhalali wake na maisha ya kudumu (eternity) vikawa ni vitu vinavyojengewa hoja kutokana na mapenzi na sio kwa kuyasimamisha kwa kutumia hoja ambazo wakati unazisuta sana.

Kikwete anatupigia tutu katika ngoma ambayo yeye hataicheza kabisa na kwa hili napenda kumwambia kuwa kauli kama hizo hazitaisadia Zanzibar. Badala yake kinachofaa ni kuutayarisha umma, vyovyote itavyokuwa tafsiri ya matayarisho hayo.

One thought on “Kikwete, kupi ndiko kuchezea Mapinduzi ya Zanzibar?”

  1. blaza salehe sante sana kwa mawazo yako,ni ya uhakika,ingawa mie ni wa upande mwinginewe,lakini nakubariana na fikila zako,na kwa uhakika mimi sasa nimeona heli nijitowe kabisa kayika upande huu nilionao,na nijiunge na chama cha kaf.CUF.
    Kwani utata umekuwa mgumu sana hapa kisiwani sasa,hari ni ngumu mno sina,hamna demoklasia wala usawa,ni ukali na vitisho ndio tunayoishi hapa,uspitali dawa kavu,maisha zaidi ni magumu sna,kila siku.
    mapinduzi gani sasa haya,mie nimechoka,
    asante saleh kwa kuzidi kutuamsha.
    wako ndugu.rajabu.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.