Na Harith Ghassany

Kwanza napenda kukushukuru kwa kuwawekeya sawa wanaukumbi wasiotujuwa kuwa sisi ni marafiki ambao huonana na kuzungumza mara kwa mara.

Pia, tunatambuwa kuwa urafiki wetu ni muhimu lakini hautuzuwii kukubaliana au kukhitalifiana kimawazo halafu tukarudi kunako udugu na urafiki wetu. Hiyo ndio faida ya kuhishimu uhuru wa kubadilishana mawazo kwa njia ya kustahmiliana na si za kulumbana.

Nashukuru pia kwa kuniwekea sawa baadhi ya fikra zako kuhusu mapinduzi ambazo sikuwa na bahati ya kuzijuwa na ndio maana nikakuomba unipe maelezo yako. Alionieleza kuhusu kipindi cha “A Week in Perspective” alikuwa ameghadhibika na fikra za kigozi zilizotolewa kunako hicho kipindi na akasahau, na mimi sikumuuliza ulisema nini na ndio maana nikaona bora niyasikie kutoka kwako mwenyewe kabla sijakuhukumu.

Napenda kukuhakikishia kuwa haya mazungumzo yetu si “academic exercise” ingawa inawezekana yakaonekana yako hivyo. Kuna mengi muhimu kwa binaadamu ambayo huanza kama ni “academic exercise” au “basic science” na ya kawa na faida katika maisha ya mwanaadamu.

Suala la Mapinduzi ya Zanzibar ni tafauti sana na yale ya Cuba, Oman, Libya, nk. Kwanza, mapinduzi ya Cuba yalifanywa na wa Cuba (pamoja na “Companero” Che Guevara mwenye asili ya Argentina) ingawa waliondokea Mexico na kwenda Sierra Maestra. Historia hiyo haikufichwa, na ingawa hakuna siasa za vyama vingi Cuba, Wa Cuba hawajaendelea kupinduliwa kila baada ya miaka mitano kwa mapinduzi yaliompinduwa Batista. Manake anopinduliwa hivi sasa Zanzibar kunako kila uchaguzi wa miaka mitano ni kizazi cha Mzanzibari yuleyule ambaye hakushirikishwa kunako mapinduzi ya tarehe 12 Januari 1964.

Kwa msingi huo mapinduzi ya Zanzibar yana umri wa miaka 45 lakini yana uendelezaji na utekelezaji mpya kuanzia uchaguzi wa 1995, 2000, 2005, na 2010, na kuendelea kwenye kila chaguzi na kila itakapoonekana Wazanzibari wanaitetea Zanzibar kwa kasi, ari, na nguvu mpya.

Bahati mbaya wako Wazanzibari wasiyofahamu hayo na wanaamini kabisa kuwa wanayalinda mapinduzi yao yaliokuja kuwakombowa kwa kuwauwa na kuwatesa ndugu zao ilhali wanautumukia mfumo ulio dhidi yao, dhidi ya ndugu zao, na dhidi ya nchi yao wanayotaka kuidai, kwa kujuwa na kufuata maslaha na matumbo, au kwa kutekwa akili na waliotuzidi maarifa bila ya wenyewe kutambuwa.

Mabadiliko yaliotokea Oman yameleta maendeleo makubwa ndani ya nchi ambayo hakuna MuOmani ambaye alifikiria kama yangeliweza kufanyika katika maisha yao au ndani ya dahari yoyote ile iliopita. Na mabadiliko yaliotokea Oman na Gulf pia yamekuwa na faida kubwa kwa Wahajirina kutoka Zanzibar ambao walipokelewa na kusomeshwa baada ya kufukuzwa kule walikozaliwa na kuishi makarne kwa makarne.

Libya, kama Masri kabla yake, na Algeria, nk, ilipinduliwa na kikundi cha wanajeshi wa Kilibya. Haikuvamiwa na wa Libya wenye mizizi mifupi Libya, au wageni waliokuwa wakiishi Libya na kudai kuwa Libya ni nchi yao kwa sababu wao ni Waafrika weusi na wenyeji wa Libya ndio ni wageni, na walioungwa mkono na nguvu za Dola la Masri au Algeria. Omar Mukhtar (1858-1931) hakuipigania Libya dhidi ya ukoloni wa Kitaliana kwa kushirikiana na Wamasri au Waalgeria waliokuwa wakiishi Libya na kutowashirikisha Walibya!

Zanzibar haikupinduliwa na Wazanzibari Ally na ndio maana hii leo JK anaweza kuitangazia dunia kuwa Wazanzibari hawatoweza kuitawala Zanzibar kwa sababu Zanzibar ina wenyewe na wenyewe ni hao walioifuta nchi ya Zanzibar, halafu wakalifuta jeshi la Zanzibar, uraia wa Zanzibar, na kiti cha Zanzibar katika Umoja wa Mataifa. Madam Wazanzibari wataendelea kuidai nchi yao au mafuta yao, basi Tanganyika itawapelekea majeshi kufa kupona.

Hilo halitosita mpaka Wazanzibari walioko ndani na nje ya Zanzibar watakapoifungulia mashtaka Tanganyika na Tanzania Bara kwenye mahakama za kimataifa kwa dhambi ya kuivamia na kuifuta Dola ya Zanzibar na kuendelea kuukaba upepo wa mabadiliko, mpaka Zanzibar itakapojireshejea nchi na hadhi yake ya kimataifa.

Bila ya hilo hakuna lugha watakayoifahamu na sisi tuendelee kujibunia majina mapya mapya ambayo hatufurahikiwi nayo Ally kwa sababu tunaona yanaingia ndani ya “grand design” ya adui wa Zanzibar. Si ndo aliyoyasema Mwalim Nyerere ya dhambi ya ubaguzi na akajifanya yeye si mlaji mkubwa wa nyama ya Kizanzibari!

Wala suala la Zanzibar haliwezi kufananishwa na mfano wa mama na mjukuu wake aliyezaa nje ya ndoa na mwishowe ikambidi amkubali mjukuu wake. Zanzibar iliingiliwa kwa nguvu kwanza halafu ikaolewa kwa hila na kwa khadaa za kila aina. Mzee anaweza akaingiwa na imani akamkubali mjukuu wake lakini dhulma iliotendewa Zanzibar ni dhulma iliyoifuta Zanzibar kama ni nchi, na isitoshe, KUENDELEA kuidhibiti na kuyazuwia mabadiliko ya amani na kukataa suluhu kwa mantiki ileile ya miaka 45 iliopita!

Kukataliwa kwa Miafaka MITATU inatokana na khofu ya Wazanzibari kuja kuungana na kuja kumuwacha mkono Mkoloni wa Tanganyika. Na hili si la kuirudisha serikali ya ZNP na ZPPP. Hili ni suala la Wazanzibari wa ndani na wa nje, walioporwa nchi yao halafu wakaambiwa kinagaubaga kuwa Zanzibar si nchi na madam hakuna nchi na uraia wa Zanzibar pia ni alfola!

Uharamu au uhalali wa mapinduzi hauotokani na yaliotokea miaka 45 nyuma peke yake, bali kuendelezwa hivi sasa yaliotokea miaka 45 nyuma kwa kuona kuwa kuna uwezekano wa “democratic process” kuwarudishia Wazanzibari nchi yao ndani ya mfumo wa vyama vingi va siasa.

Utauzuwia vipi upepo huo wa mabadiliko Zanzibar? Utafanya vilevile, na zaidi, kama ulivoyakataa matokeo ya uchaguzi wa July 1963 na uhuru wa Zanzibar. Huko nyuma kisingizio kilikuwa Sultani. Leo Zanzibar hakuna Sultani wala hakuna Hizbu lakini Wazanzibari bado wanateswa na kupingwa kwa sababu wanaidai nchi yao.

Wala uhuru haukuwa uhuru bandia wa Wazanzibari wenye asili ya Kiarabu peke yao, lakini kwa vile Wazanzibari hawakushirikishwa katika mapinduzi basi wenye kuidai Zanzibar wote wanaonekana kwa miwani za kipropaganda kuwa ni “Waarabu” kwa kisingizio cha kuwatia khofu wananchi kuwa wanataka kurudisha utumwa.

Huenda CUF ilipima na kuamini kuwa ikiyaunga mkono mapinduzi basi labda hilo litawatowa khofu viongozi wahafidhina wa Zanzibar na wafuasi wao na kuwapa serikali baada ya kushinda uchaguzi. Ni kweli pia CUF imetaka kuyakubali mapinduzi ili iweze kuutowa wasiwasi umma mkubwa wa wapiga kura lakini hilo haliwezekani kwa sababu umma mkubwa umedanganywa, umekhadaiwa, umetekwa na umezugwa kuhusu mapinduzi ya Zanzibar, na wamefanywa kuamini kuwa Hizbu ni nguruwe najis kwa Wazanzibari “Waafrika” na CUF inataka kumtia tahara.

Tanganyika watawala wanajuwa kuwa uongozi wa CUF na wa CCM Zanzibar ukiaminiana na kushirikiana utakuja kuzikamata khatamu za utawala Zanzibar na wao watakuwa waladhaalin. Lakini bado Wazanzibari hawaaminiani na kuna wenye uzalendo wa msimu lakini dalili za kushirikiana pia zipo lakini tabia ya khiana ya kuigeukia Zanzibar dakika ya mwisho bado ipo kunako tabia za baadhi ya viongozi wa Zanzibar.

Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ambaye anapendwa na kundi kubwa la Wazanzibari amejengewa usanii wa kisiasa kuwa alikuwa jemedari mkuu wa mapinduzi hali hakuwa mpishi wa hayo mapinduzi ingawa alijuwa kuwa yatafanyika na baadae alipewa huo ujemedari.

Kwa hiyo wenye kumpenda Mzee Karume wanahitaji kuilimishwa kuwa kiongozi wao hakuwa kunako huo usukani ambao ulikuwa na lengo la kuivamia na kuimeza Zanzibar. Picha ya Mzee Karume itabidi ibadilishwe kwenye vichwa va umma mkubwa wa wapiga kura.

Umeandika “kuwaamsha watu hakutoshi kuwa msaada?” Kunatosha sana na ndio msaada mkubwa kwani Mwenye Enzi Mungu ametuambia kwenye Qur’ani Tukufu:

“Hayo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu habadilishi kabisa neema alizo waneemesha watu, mpaka wao wabadilishe yalioyomo ndani ya nafsi zao. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.” Surat Al Anfaal, Aya ya 53.

Umeuliza: “Baada ya miaka 45 lipi la kufanya?” La kufanya ni kufikiria upya suala la mapinduzi ya Zanzibar na namna linavotumiwa LEO kuyazuwia mabadiliko Zanzibar kwa mfumo wa miaka 45 wenye kujirudia. Hapo ndipo tulipokwamishwa na kukwama na hapo ndipo ilipokaa kwa kujificha, khofu ya kikundi kidogo sana chenye kuongoza siasa za mkono wa chuma Zanzibar.

Tukipaelewa hapo basi kutakuwa hakuna haja ya kuwepo kwa kundi la “Waza-nje” na “Wazandani”, “Wamaka-nje” na “Wamaka-ndani”, bali kutakuwa na Wazanzibari Wahajirina na Wazanzibari Ansari, kuna Wazanzibari waliokwenda nje na walioko ndani, na hili tulikubali kwa kuzifahamu khadaa zilizoimeza na kuifuta Zanzibar, zikiwemo hizo sheria za uraia ambazo ni sehemu kubwa ya kutufanya tusielewane ili tufarakane.

Ni muhimu sana tuungane na tuifunguliwe mashtaka Tanganyika kwa kuivamia na kuimeza Zanzibar na kuyaendeleza mazoweya ya kuwauwa tena na tena ndugu zetu wa Kizanzibari.

Mapinduzi, na kumezwa Zanzibar na Tanganyika, na kutanganziwa dunia kuwa Wazanzibari maisha yao hawatoitawala Zanzibar ni mbegu, mzizi na tawi moja. Kwa hilo hakuna wa ndani wala wa nje. Kuna Wazanzibari kulifahamu hilo na kuutumia muamko wetu kutujengea hilo daraja ambalo kwa sasa nia yako imekuwa haieleweki vizuri si kwa kuwa unafikiri upya bali unafikiri upya ndani ya boxi la mfumo utakaompendeza adui wa Zanzibar.

Tutakapoweza kuviinua vichwa vyetu na kuufahamu mfumo wa khadaa na hila ulioziteka akili za umma mkubwa wa wapiga kura wa Zanzibar basi yale maneno yako uliyoyaandika tarehe 26 Disema 2008 yatakuwa kweli tumeweza:

“kwa sasa ni ukweli wa kitakwimu kuwa cuf wameongeza wanachama katika kila jimbo, hata majimbo ambayo ccm inaendelea kuyashikilia. lakini jee inatosha? la haitoshi kabisa.

Cuf inahitajika iwapo inataka kushinda urais ishinde angalau majimbo 8 ya unguja. mtu asiniambie kuwa wanashinda lakini wanapokonywa. la sitaki maelezo hayo.
cuf inahitajika ijikite katika majimbo hayo kiasi ambacho wananchi wa majimbo hayo waweze kuja juu peke yao kuwa wao wamekipa ushindi cuf na wasingeweza kukubali vyovyote vile kura zao ziwape ushindi ccm.

ifike wakati kama huo, ndipo cuf itashinda. sasa wanaitakia mema cuf wawasaidie kufikia lengo kama hilo na si kitu ambacho hakiwezekani.”

Kuufikia wakati huo ni kuufikia muamko ambao ni kinyume cha uzito wa miaka 45 ya mapinduzi juu ya Zanzibar ya LEO na jinamizi la kihistoria ambalo bado halijawekwa sawa na bado linaendelea kuwa tishio kwa utulivu wa Zanzibar na mapatano baina ya Wazanzibari wenye mizizi mrefu (waliopinduliwa na wanaoendelea kupinduliwa) Zanzibar na Wazanzibari wenye mizizi mifupi (waliopinduwa na wanaoendelea kupinduwa).

Tangazo la JK kwa mwaka 2010 limeshasikika Zanzibar pamoja na Afrika Mashariki. Tukiweza kusaidia kuinusuru roho moja ya Kizanzibari basi tutakuwa kama tumeuamsha umma mzima na kuinusuru roho ya kila Mzanzibari. Pana haja ya kuuamsha umma wa Kizanzibari na wa Kitangayika kwa kuufahamisha kuwa matatizo ya Zanzibar yamesababishwa na Dola ya Tanganyika na serikali hii hi ya Tanzania Bara.

Hakuna hila au uhodari wa kuyazuwia mabadiliko Zanzibar. Ya imma Tanganyika iendelee kuwa mti uliyejigeuza kuwa rungu la kuwapiga Wazanzibari na kupoteza uhalali wake na kuivuruga demokrasia Zanzibar, au iendeleze ubaguzi wa kuwabaguwa wenyeji wa Zanzibar kuwa si “Waafrika” wa kutosha kwa hiyo hawana haki ya kuitawala Zanzibar. Zote hizo mbili si solution kwa Tanganyika.

Kwa maoni yangu njia ya kuifuata ni:

a). Kuuamsha na kuupanga upya umma wa Zanzibar na wa Tanganyika uyafahamu vilivo mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 yalioivamia, kuimeza na kuifuta Dola ya Zanzibar, na kuyaunganisha mapunduzi hayo na huu mfumo unaoendelezwa hivi sasa kunako chaguzi za kila baada ya miaka mitano Zanzibar.

b). Kukifungulia mashtaka kunako mahakama ya kimataifa kikundi kidogo cha viongozi wa Tanganyika na sasa Tanzania Bara, kilichoazimia kuendeleza maslaha yao binafsi na mamlaka yao ya kisiasa, kwa lengo la kuyazuwia mauwaji na uvurugaji wa demokrasia na haki za binaadamu Zanzibar katika uchaguzi wa 2010 na chaguzi za baadae.

c). Kuunda kamati ya suluhisho na kusameheana baina ya kizazi cha Wazanzibari wenye mizizi mrefu Zanzibar na kizazi chenye mizizi mirefu Tanganyika, Msumbiji, na sehemu nyengine kutoka bara la Afrika kwa lengo la kuwaunganisha kuitetea na kuijenga nchi ya Zanzibar.

Baada ya makala hii sitakuwa na la kusema tena mpaka watakapojitokeza wale ambao wameamua kuongozwa na ukweli na mtizamo mpya wa kuitetea Zanzibar.

5 thoughts on “Ukweli mwingi umepotoshwa kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar”

  1. Kuna msemo unaoleza (kwa Kiingereza) “The truth will make you free”. Na kinyume chake ni kweli pia. Yaani “Lies will enslave you”.

    Uongo ndio zana muhimu sana ya kuendelea kuwashikilia watu katika shemere za kutawaliwa. Kwa hivyo, daima watawala hawataacha kudanganya na kupindisha ukweli. Na mara tu ukweli utakapojitokeza na kusambaa katika umma, utumwa wa kutawalia utakuwa umemaliza muda wake

  2. Kwa nini khassa viongozi wa bara ndio wanaotetea hayo yaitwayo mapinduzi? Hii inaonesha wazi kua mapinduzi(mavamizi ) yameandaliwa na kutekelezwa na watuwanje wengi wao kutoka tangnyika.Waznz tuwe macho.Wao ndio wanaoleta jeshi kuwauwa na kuwanjisi watu wetu wakisingizia mpasuko wa kisiasa na ilhali ni askari kutoka bara ndio wanaokuja kuwauwa waznz.Hatukuona waznz kuuana sasa miaka 40 imepita ni Asakari wa kikosi cha FFU ndicho kifanyacho unyama hapa znz.

  3. Tatizo likionekana ni rahisi ufumbuzi wake, kubwa nikuamsha walio lala na tatizo ni media kuwafikia wengi wakajua ukweli, naomba njia yetu ya mawasiliano idumu ili tujue mengi. Sasa nimeelewa chanzo cha mizozo ya Zanzibar na ufumbuzi wake lakini ninani atakae thubutu kumfunga paka kengele? Sisi kama Wazanzibari tuko tayari kuungana ila ninani atakae tuunganisha kwenye sokomoko hili na kila mmoja ahofia kukolimbwa?

  4. Na mimi naomba niwe mmoja wa wapemba wanaopata taarifa za nyumbani ndani ya wakati unaofaa. Hili ni jukumu la kila mmoja wetu tukiwa wazanzibari tulishikana mikono sasa na kusahau tofauti na kujiona sasa tuko pamoja. Nimejitokez ndani ya wakati unaofaa, wakati wa uchaguzi wa uamuzi nani atakuwa mtekelezaji wa yale walikuobaliana viongozi wetu. Naomba nami niwe mshiriki sasa.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.