Na Ibrahim Mzee Ibrahim
Disemba 2008, Zanzibar

 1. Ujenzi wa Demokrasia
  1.1 Historia ya Zanzibar katika takriban karne mbili zilizopita inathibitisha kutokea kwa mabadiliko mengi na maendeleo makubwa katika ukuwaji wa demokrasia. Lengo la mada hii ni kuchambua kwa kifupi kabisa mchakato wa ukuwaji na maendeleo ya demokrasia hususan demokrasia ya kibunge (Parliamentary Democracy) katika Zanzibar kwa kuonyesha wapi tulikotoka, wapi tulipo sasa na wapi tunakoelekea.
  1.2 Ni vyema tukakumbuka kwamba hata nchi za Ulaya ya Magharibi na Marekani zilichukua karne kadhaa na vipindi mbali mbali vya mivutano migumu ya kijamii na kitabaka na mapambano makali ya kisiasa katika kujenga misingi ya kidemokrasia katika nchi hizo. Kwa mfano, nchini Uingereza kati ya mwaka 1471 na 1535 maspika sita (6) wa Bunge (House of Commons) walinyongwa kutokana na kutofautiana na wafalme wa wakati huo . Matukio hayo yanatukumbusha kuwa ujenzi wa misingi ya demokrasia ni safari ndefu na ngumu.
  1.3 Historia pia inaonyesha kwamba harakati za kidemokrasia zilipata nguvu zaidi kwa kupitia mapinduzi ya kibepari. Kwa mfano, Mapinduzi Matakatifu (Glorious Revolution) ya Uingereza ya mwaka 1668, Mapinduzi ya Marekani ya mwaka 1776 na Mapinduzi ya Ufaransa ya mwaka 1789. Hii ndiyo sababu iliyopelekea hata mwanataaluma maarufu wa sosiolojia ya siasa Barrington Moore kwenye kitabu chake cha ‘Social Origins of Dictatorship and Democracy’ (1966) kuthubutu kusema kwamba ‘no bourgeois, no democracy’ akimaanisha kuwa bila ya mabepari hakuna demokrasia.
  1.4 Katika muktadha huo ndio maana nadharia nyingi zinazokubaliwa na wengi hivi sasa kuhusu demokrasia ni zile ambazo misingi, chanzo na falsafa zake zinatokana na ukuwaji na maendeleo ya mfumo wa kibepari duniani. Halikadhalika, kuanguka kwa falsafa ya ‘Ukuu ndani ya Demokrasia’ (Democratic Centralism) ambayo ilikuwa ndiyo aina ya “demokrasia” chini ya mifumo ya kikomunisti nako kumetoa nafasi muwafaka kwa mfumo wa kibepari kijiimarisha zaidi katika dunia yenye mazingira mapya ya karne hii ya ishirini na moja (21) kwa jina la ‘Utandawazi’.
 2. Dhana ya Demokrasia
  2.1 Demokrasia ni dhana au msamiati uliopata bahati ya kutafsiriwa na kuchambuliwa katika namna tofauti kulingana na nani anaefanya uchambuzi huo, wakati unapofanyika uchambuzi au tafsiri, na mahala husika. Hatahivyo, uchambuzi na tafsiri zote hizo zinakubaliana kuwa ‘demokrasia ni utawala wa watu’. Tofauti zinajitokeza katika kutoa tafsiri na uchambuzi wa mambo mawili makubwa: (i) Watu ni kina nani? (ii) Njia gani au mambo gani yafanywe ili kufikia na kuimarisha utawala wa watu. Kwa mfano, katika Ugiriki ya enzi za kina Plato watumwa hawakuhesabika kuwa ni watu. Huko Afrika ya Kusini chini ya mfumo wa ubaguzi wa rangi (Apartheid) kabla ya mwaka 1994 watu weusi hawakutambuliwa na sheria za nchi hiyo kama ni watu wanaostahiki kujitawala. Hata Zanzibar nako, kabla ya mwaka 1946 hakuna muafrika aliyepata fuers ya kuwa mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria (LEGCO) ingawa Baraza hilo linahesabika kuwa ni chachu ya kidemokrasia katika Zanzibar ya wakati huo. Vile vile, kuna walioamini kwamba mfumo wa siasa za vyama vingi ndiyo njia nzuri na sahihi ya kufikia demokrasia kwa maana ya utawala wa watu; wengine walidhani kuwa ukomunisti na mfumo wa chama kimoja cha siasa ndiyo unaofaa katika kujenga utawala wa watu (Demokrasia); pia kuna waliodai kwamba mfumo wa kutokuwa na vyama vya siasa ‘no party system’ unafaa zaidi katika kujenga na kuimarisha utawala wa watu.
  2.2 Kimsingi, ingawa kuna kutofautiana katika tafsiri na uchambuzi wa dhana ya demokrasia kama nilivyokwishaeleza hapo juu, tafsiri iliyotolewa na Abraham Lincoln kwamba demokrasia ni ‘utawala unaomilikiwa na watu, unaoendeshwa na watu, kwa ajili ya watu’ inaonekana kukubalika zaidi katika duru nyingi za kisiasa na kitaaluma. Mambo yanayojitokeza katika tafsiri hiyo ni kwamba umiliki, uendeshaji na madhumuni/maslahi ya utawala wa kidemokrasia ni watu.
  2.3 Kwa sasa, aina ya demokrasia inayoangaliwa zaidi na kufuatwa katika nchi nyingi ni ile Demokrasia ya Uwakilishi (Representative Democracy) tofauti na ile aina ya Demokrasia ya Moja kwa Moja (Direct Democracy) ambayo ilitekelezwa na jamii nyingi duniani zilipopitia kwenye mfumo wa Ujima (Primitive Communalism). Kwahivyo, katika Demokrasia ya Uwakilishi, suala la uchaguzi wa wajumbe wa kuingia kwenye mabaraza na vyombo vya maamuzi linapewa uzito mkubwa.
  2.4 Mambo yanayotajwa sana kwenye mijadala kuhusu demokrasia ni pamoja na ushirikishwaji wa wananchi, chaguzi huru na za haki, uhuru wa vyombo vya habari na mawasiliano, usawa mbele ya sheria na mamlaka ya mwisho kuwekwa mikononi mwa wananchi kwa kuwashirikisha wananchi kwa ujumla wao, kwa kupitia asasi za kiraia (civil society organizations) au mtu mmoja mmoja. Kimataifa, nchi zimejiwekea mikakati na malengo kadhaa ya kufikia demokrasia kwa kuainisha matakwa ya nchi hizo kwa pamoja na vigezo muhimu vinavyoitambulisha nchi kuwa ni ya kidemokrasia au la. Kwa mfano, miaka kumi iliyopita nchi za Jumuiya ya Madola zilikubaliana mnamo tarehe 19 Juni 1998 kwa kupitisha ‘Latimer House Guidelines For the Commonwealth’ . Miongozo hiyo inatilia mkazo misingi muhimu na maadili ya kidemokrasia katika nchi za Jumuiya ya Madola, uendelezaji wa michakato na taasisi za kidemokrasia, utawala wa sheria, uhuru wa mahkama, serikali ya haki yenye uaminifu na uwajibikaji, haki za binadamu na kupinga ubaguzi wa aina zote na kutilia mkazo usawa na haki za wanawake.
  2.5 Kuwepo au kutokuwepo kwa demokrasia katika nchi kunategemea pia aina ya misingi ya kikatiba inayoongoza nchi husika. Kanuni maarufu za demokrasia ya kikatiba katika nchi nyingi duniani ni hizi zifuatazo: (i) Utenganisho wa Madaraka (Separation of Powers) baina ya mihimili mitatu ya mamlaka kuu za nchi. (ii) Ukuu wa Bunge au Ukuu wa Katiba (Sovereignity of Parliament or Supremacy of the Constitution). (iii) Uhuru wa Mahkama (Independence of the Judiciary). (iv) Utawala wa Sheria (Rule of Law).
 3. Historia ya Muamko wa Demokrasia na Uchaguzi katika Zanzibar
  3.1 Kabla ya kuja kwa watawala wa kigeni katika Visiwa vya Unguja na Pemba kulikuwa na watawala wa jadi waliowaongoza watu wao kwa mujibu wa taratibu za mila za wenyeji walioishi kwenye Visiwa hivi. Wenyeji hao walijiwekea taratibu zao ambazo zilifuatwa kwenye jamii husika . Kwa kiasi kikubwa taratibu hizo zilitokana na wananchi wenyewe.
  3.2 Karne ya 19 ni kipindi muhimu sana katika historia ya Zanzibar kwasababu katika karne hiyo Zanzibar ilishuhudia kuimarishwa kwa ukoloni wa waarabu kutoka Oman, kuibuka kwa Zanzibar kama nchi tofauti na Oman na pia kuanzishwa kwa ukoloni wa kiingereza hapa Zanzibar. Mnamo mwaka 1832 Seyyid Said aliifanya Zanzibar kuwa makao makuu ya utawala wake . Mnamo tarehe 2 April mwaka 1861 Governor-General wa India (Lord Canning) ambayo ilikuwa ni koloni la Uingereza alitoa uamuzi wa usuluhishi alioufanya kuwapatanisha watoto wa marehemu Seyyid Said (alikufa 1856) kwa kuigawa Zanzibar na Oman kuwa nchi mbili tofauti ambapo mtoto mkubwa Seyyid Thuwain bin Said alirithishwa Oman na mtoto wa pili Seyyid Majid bin Said alirithishwa Zanzibar . Mnamo mwaka 1890 Sultan wa Zanzibar alitiliana saini na Uingereza mkataba wa kukubali Uingereza ishughulikie masuala yote ya Zanzibar kuhusu mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa ili kupata hifadhi na ulinzi wa Muingereza .
  3.3 Mfumo na muundo wa utawala Zanzibar wakati wa ukoloni ulikuwa umejengwa kwa kuzingatia maslahi na matakwa ya Sultani na ukoloni wa kiingereza. Kabla ya mwaka 1890 Sultani alikuwa ndiyo kila kitu: mtungaji wa sheria, mtawala, na hakimu. Mnamo mwaka 1891 Muingereza alifanikiwa kumshawishi Sultani kuanzisha utawala wa kikatiba na ndipo General Sir Lloyd Mathews aliteuliwa kuwa Waziri wa Kwanza wa Sultani (His Highness’s First Minister). Kwahivyo, huyu alikuwa akimsaidia Sultani katika uendeshaji wa serikali kuhusu kazi za kila siku za mambo ya ndani ya nchi. Hatahivyo, mamlaka ya kutunga sheria yalibakia mikononi mwa Sultani mwenyewe. Kwa upande wake Uingereza nayo ilikuwa na Balozi wake Zanzibar anaemuwakilisha Mfalme wa Uingereza ( His Majesty’s Agent and Consul-General). Huyu alishughulikia mawasiliano yote ya mambo ya nje ya Zanzibar . Mahkama za aina mbili zilianzishwa: kwanza, kulikuwa na Mahkama za Sultani ambazo zilihusika na raia wote wa Sultani na waafrika wengine, pili, kulikuwa na Mahkama za Kiingereza ambazo zilihusika na raia wote wa Uingereza, raia wa mataifa rafiki ambayo mahkama zao za kibalozi zilifungwa, na raia wa mataifa mengineyo ya kikristo ambayo hayakuwa na mabalozi Zanzibar .
  3.4 Mabadiliko makubwa katika muundo na mfumo wa utawala yalitokea katika karne ya 20 mnamo mwaka 1914 kilipofutwa cheo cha Waziri wa Kwanza na cheo cha Balozi wa Uingereza katika Zanzibar na badala yake kuunganishwa na kuanzishwa cheo kimoja tu kipya yaani Mwakilishi Mkaazi Muingereza (British Resident) ambae alitakiwa kufanyakazi chini ya usimamizi wa Kamishna Mkuu (High Commissioner) ambae alikuwa ni Gavana wa kiingereza wa koloni la Kenya . Mabadiliko haya yalitokana na ukweli kwamba kuanzia tarehe 1 Januari 1914 Uingereza iliyahamisha mambo yote ya Zanzibar kutoka Afisi ya Mambo ya Nje (Foreign Office) na kuyapeleka Afisi ya Makoloni (Colonial Office) . Katika mwaka huo huo wa 1914 Sultani alianzisha Baraza la Mahmia (Protectorate Council) chini ya uongozi wa Sultani akisaidiwa na Mwakilishi Mkaazi Muingereza. Wajumbe wengine wa Baraza hilo walikuwa ni Katibu wa Serikali, Mwanasheria Mkuu na Mweka Hazina. Kulikuwa na wajumbe wengine wane wasio wa serikali ambao waliteuliwa na Mwakilishi Mkaazi Muingereza na kuridhiwa na Kamishna Mkuu. Walioteuliwa walikuwa mmoja mzungu, mmoja muarabu na wawili wahindi. Kazi kubwa ya Baraza hilo ilikuwa ni kumshauri Sultani na kuthibitisha hukumu ya kifo iliyotolewa na mahkama dhidi ya raia wa Sultani .
  3.5 Mnamo mwaka 1924 cheo cha Kamishna Mkuu kilifutwa na kikabakisshwa kile cheo cha Mwakilishi mkaazi Muingereza . Aidha, mnamo mwaka 1926 sheria ilipitishwa iliyounda mabaraza mawili: Baraza la Utendaji (Executive Council au Majlis Tanfidh) na Baraza la Kutunga Sheria (Legislative Council au Majlis Tashrii). Mabaraza haya hayakuwa na uwakilishi wa wananchi kwani wajumbe wake wengi walikuwa ni maafisa wa serikali, isipokuwa miongoni mwa wajumbe wa Legislative Council (LEGCO) kulikuwa na wajumbe sita walioteuliwa na Sultani baada ya kupata ushauri wa Mwakilishi Mkaazi Muingereza. Wajumbe hao sita waliteuliwa kwa misingi ya kibaguzi yaani ukabila na rangi. Muafrika wa mwanzo kuingia kwenye LEGCO aliteuliwa mnamo mwaka 1946.
  3.6 Mtaalamu wa mambo ya uchaguzi aliteuliwa na serikali ili atoe ushauri wa njia na namna bora ya kupata wajumbe wasio wa serikali katika LEGCO. Mtaalamu huyo Bwana Coutts alitoa ripoti yake. Mabadiliko mengine yalitokea mnamo mwaka 1956 kwa kupitishwa sheria mpya ya Mabaraza Nambari 1 ya 1956. Sheria hii ilichukua nafasi ya ile sheria ya mwaka 1926. Sheria hii mpya ilianzisha mabaraza matatu. Kwanza, Baraza la Ushauri (Privy Council) ambalo lilipewa kazi ya kumshauri Sultani katika kutekeleza kazi na majukumu yake mbali mbali ya kikatiba. Pili, Baraza la Utendaji (Executive Council) lililoongozwa na Mwakilishi Mkaazi Muingereza ambalo lilipewa kazi ya kusimamia utendaji wa kila siku wa shughuli za serikali. Tatu, Baraza la Kutunga Sheria (Legislative Council) ambalo lilikuwa na wajumbe13 ambao ni maafisa wa serikali na wajumbe 12 wasiokuwa maafisa wa serikali. Wajumbe 12 wasiokuwa maafisa wa serikali walipatikana kwa uteuzi (wajumbe 6) na uchaguzi (wajumbe 6). Ndio maana uchaguzi wa kwanza hapa Zanzibar ulifanyika mwaka 1957 ili kupata wajumbe 6 wa kuingia kwenye LEGCO.
  3.7 Chaguzi nyengine tatu zilifanyika (Januari 1961, Juni 1961, na Juni 1963). Serikali ya ndani ilipatikana tarehe 24 Juni 1963; Bunge la Katiba lilipitisha Katiba ya Zanzibar ya 1963 mnamo tarehe 27 Novemba 1963; na uhuru kutoka kwa Muingereza ulitolewa tarehe 10 Disemba 1963 na kuanza kutumika kwa Katiba mpya ya 1963.
  3.8 Matokeo ya uchaguzi wa kwanza 1957 ni kwamba viti vitano vilikwenda kwa ASP na kiti kimoja kilichobaki cha Mji Mkongwe kilichukuliwa na Muslim Association. Matokeo hayo yaliwashangaza waingereza na waarabu kwakuwa ZNP haikupata kiti hata kimoja. Mchezo wa kisiasa ukaandaliwa na ndipo katika uchaguzi wa Januari 1961 baada ya kuzingatiwa kwa mapendekezo ya Tume ya Blood idadi ya majimbo ya uchaguzi ikaongezwa na kufikia 22 ambapo eneo la Mji Mkongwe likawa na majimbo mawili ya uchaguzi ingawa idadi ya wapiga kura kwenye majimbo hayo ilikuwa ndogo sana ikilinganishwa na majimbo mengine. Matokeo ya uchaguzi huo wa Januari 1961 yalikuwa: ASP viti 10, ZNP viti 9, na ZPPP viti 3. Viti viwili vya ZPPP vilikwenda kwa ZNP na kiti kimoja cha ZPPP kilikwenda kwa ASP na kufanya matokeo ya jumla kuwa saare ya 11 kwa 11 kati ya ASP na ZNP. Uchaguzi ulirejewa mnamo mwezi wa Juni 1963 kwa kuongezwa jimbo moja la Mtambile Pemba na kufanya idadi ya majimbo yote kufikia 23. Uchaguzi huo ulikuwa na ghasia kubwa na watu 68 walikufa na wengine 381 walijeruhiwa. Matokeo yalikuwa ni kwa ASP viti 10, ZNP viti 10 na ZPPP viti vitatu. Kama kawaida, viti viwili vya ZPPP vikenda kwa ZNP na kiti kimoja cha ZPPP kikenda kwa ASP. Matokeo ya jumla yakawa ZNP 12 na ASP 11. Mbinu chafu iliyotumika ilikuwa ni kutokuwepo kwa usawa na uadilifu katika ukataji wa majimbo (Gerrymandering). Katika uchaguzi wa 1963 idadi ya majimbo yote ilikuwa ni 31 ambapo ASP ilipata viti 13, ZNP ilipata viti 12 na ZPPP ilipata viti 6. Idadi ya kura zote ambazo ASP ilipata ilikuwa ni 87,404 lakini ilishinda majimbo 13 tu; ZNP ilipata kura 47,943 na kushinda majimbo 12; ZPPP ilipata kura 25,610 na kushinda majimbo 6; kura 3,739 ziliharibika. Kwahivyo, kura zote za ZNP na ZPPP zilikuwa ni 73,553 lakini walishinda viti 18 kwa pamoja wakati ASP yenye kura 87,402 ilipata viti 13 tu .
  3.9 Katiba ya 1963 iliendeleza usultani wa kikatiba (constitutional monarchy) ambapo Sultani anakuwa ni Mkuu wa Nchi (Head of State) na Waziri Mkuu anakuwa ni Kiongozi wa Serikali (Head of Government). Katiba hiyo iliingiza haki za binaadamu, ilianzisha Bunge la kuchaguliwa na iliziunganisha aina mbili za mahkama (Mahkama za Sultani na Mahkama za Kiingereza) chini ya mwamvuli mmoja wa Mahkama Kuu ya Zanzibar kwa mujibu wa sheria ya Mahkama ya mwaka 1963. Uhuru huo na Katiba mpya ya 1963 vilidumu kwa mwezi mmoja tu hadi yalipofanyika Mapinduzi ya tarehe 12 Januari 1964. Muundo mpya wa utawala ukaanzishwa chini ya uongozi wa Baraza la Mapinduzi.
  3.10 Zanzibar ilibadilika kutoka kwenye usultani wa kikatiba (constitutional monarchy) na kuwa Jamhuri (Republic). Mamlaka ya juu katika nchi yakawekwa mikononi mwa Baraza la Mapinduzi kwa kushirikiana na Baraza la Mawaziri . Katiba ya 1963 ilisitishwa . Mamlaka ya kutunga sheria yakawekwa mikononi mwa Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa mashauriano na kukubali kwa Baraza la Mapinduzi . Rais akawa ni Mkuu wa nchi na Amiri Jeshi Mkuu na akapewa uwezo wa kuunda Baraza la Mawaziri lenye mawaziri na mawaziri wadogo . Cheo kipya cha Makamo wa Rais kikaanzishwa . Vile vile, wajumbe wote wa Baraza la Mawaziri wakawa pia ni wajumbe wa Baraza la Mapinduzi. Katibu wa Baraza la Mawaziri nae akawa pia Katibu wa Baraza la Mapinduzi .
  3.11 Kwahivyo, mamlaka ya kutunga sheria yalitekelezwa na Rais kwa kushauriana na kukubali kwa Baraza la Mapinduzi. Vile vile mamlaka ya kiutendaji yaliwekwa mikononi mwa Rais. Mamlaka ya utoaji haki yaliwekwa kwenye mahkama mbali mbali kwa niaba ya Baraza la Mapinduzi; mahkama zilitakiwa ziwe huru katika maamuzi na zifuate sheria na sera za umma . Hatahivyo, mfumo wa mahkama ulibadilishwa mnamo mwaka 1969 kwa kuanzishwa kwa Mahkama za Wananchi ambazo ziliendeshwa na watu wasio na utaalamu wala ujuzi wa sheria.
  3.12 Tarehe 26 April 1964 Zanzibar iliungana na Tanganyika na kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mnamo mwaka 1979 Baraza laMapinduzi lilipitisha Katiba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya 1979 ambayo ilianza kutumika tarehe12 Januari 1980. Maendeleo na mafanikio makubwa yaliyopatikana kwenye Katiba ya 1979 ni kuanzishwa kwa Baraza la Wawakilishi kuwa ni chombo cha kutunga sheria. Wajumbe wengi wa Baraza la Wawakilishi waliingia Barazani kwa kupitia Kamati za Mapinduzi za wilaya na mikoa, Chama cha Mapinduzi na jumuiya zake, wajumbe wa Baraza la Mapinduzi, wabunge na wateuliwa wa Rais. Kati ya wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi ambao walikuwa ni zaidi ya 100 kulikuwa na wajumbe 10 tu (Wabunge) ambao walichaguliwa moja kwa moja na wananchi. Hivyo basi, Baraza la Wawakilishi likawa ni chombo cha kutunga sheria na Baraza la Mapinduzi likabaki kuwa ni mamlaka ya utendaji tu. Katiba hiyo ya mwaka 1979 iliweka pia utaratibu wa uchaguzi wa Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambao kwa mara ya kwanza ulifanyika mnamo mwezi wa Oktoba 1980.
  3.13 Mnamo mwaka 1984 ndipo katiba inayotumika sasa ilipopitishwa na ilianza kutumika rasmi tarehe 12 Januari 1985. Sehemu kubwa ya muundo wa utawala Zanzibar imefafanuliwa kwenye katiba hiyo ya 1984 pamoja na kwenye sheria nyengine mbali mbali.
 4. Muundo na kazi za Baraza la Wawakilishi
  4.1 Katiba ya Zanzibar ya 1984 imeweka bayana kwenye kifungu cha 9 (3) kwamba “Muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na utendaji wa kazi zake utafanywa katika utaratibu utakaohakikisha kuendelezwa kwa umoja nchini na lengo la kufikia demokrasia” (mkazo umeongezwa). Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya 1984 Baraza la Wawakilishi lina wajumbe 81 kama ifuatavyo:

– Wajumbe 50 wa kuchaguliwa kutoka kwenye majimbo ya uchaguzi.
– Wajumbe 15 Wanawake kutoka kwenye Vyama vya Siasa vyenye Uwakilishi kwenye Baraza la Wawakilishi, Nafasi hizi hugaiwa kwa uwiano wa Viti vya Majimbo.
– Wajumbe 10 wa kuteuliwa na Rais na angalau 2 watoke upande wa Upinzani.
– Wajumbe 6 huingia kwa mujibu wa nyadhifa zao. Wao ni Wakuu wa Mikoa (5) na Mwanasheria Mkuu (1).

4.2 Tume ya Uchaguzi ndiyo huigawa Unguja na Pemba katika majimbo ya Uchaguzi yasiyopungua 40 na yasiyozidi 55 kwa ajili ya uchaguzi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi. Kwa hivi sasa Unguja imegaiwa kwenye majimbo 32 ya uchaguzi na Pemba imegaiwa kwenye majimbo 18 ya uchaguzi .
4.3 Kazi ya Kwanza ya Baraza la Wawakilishi ni Kutunga Sheria. Kazi hii hufanywa ama kwa kutunga sheria mpya au kurekebisha sheria iliyopo au kufuta sheria iliyopo. Sheria zinazotungwa na Baraza la Wawakilishi ni kuhusu mambo yote ya Zanzibar yasiyo ya Muungano. Miswada ya Sheria huwasilishwa kwenye Baraza kwa kujadiliwa na ikipitishwa hupelekwa kwa Rais atie saini yake ili iwe sheria kamili. Kanuni za Baraza la Wawakilishi zinaruhusu miswada kuletwa kwenye Baraza kutoka Serikalini au kutoka kwa Wajumbe wenyewe. Hata hivyo, hadi hivi sasa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi hawajatumia fursa hiyo ya kuleta miswada binafsi.
4.5 Kazi ya Pili ya Baraza la Wawakilishi ni kuidhinisha Bajeti ya Serikali kila mwaka. Hakuna kodi yoyote itayokusanywa na Serikali wala matumizi yoyote yatayofanywa na Serikali bila ya idhini ya Baraza la Wawakilishi.
4.6 Kazi ya Tatu ya Baraza la Wawakilishi ni kuihoji Serikali kuhusu masuala mbali mbali yanayohusu Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Lengo la jukumu hili ni kupata taarifa na kuhimiza utekelezaji wa mambo mbali mbali. Kazi hii ya kuihoji Serikali hufanywa kwa njia ya maswali na majibu au kwa kupitia hoja za wajumbe.
4.7 Kazi ya Nne ya Baraza la Wawakilishi ni kuidhinisha na kusimamia mipango ya maendeleo ya Serikali katika njia ile ile ambayo bajeti ya mwaka inaidhinishwa. Kwa kawaida kazi hii hufanywa kwa kupitia Kamati mbali mbali za Baraza la Wawakilishi.
4.8 Baraza la Mapinduzi (Executive) kwa pamoja linawajibika kwa Baraza la Wawakilishi na kwa wajumbe kwa mambo yote yaliyofanywa na Rais, Waziri Kiongozi au Waziri mwengine yoyote katika utendaji wa kazi za Serikali.
4.9 Baraza la Wawakilishi linaweza kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Kiongozi. Halikadhalika linaweza kumshtaki Rais wa Zanzibar endapo atavunja Katiba au ataudhalilisha Muungano wa Tanzania.

 1. Demokrasia kwenye Baraza la Wawakilishi
  5.1 Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamepewa haki ya kikatiba kuwa huru katika kutoa maoni yao kwenye Baraza juu ya mambo mbali mbali yanayowasilishwa kwenye Baraza kwa ajili ya kujadiliwa na kufanyiwa maamuzi. Uhuru huo wa wajumbe unalindwa chini ya kifungu cha 86 cha Katiba ya Zanzibar ya 1984 na wamepewa kinga dhidi ya mashtaka ya jinai au hukukia kwa lolote wanalolisema au kulifanya wakati wa utekelezaji wa kazi zao za Baraza na Kamati zake. Uhuru na kinga hizo zimefafanuliwa kwa urefu sana kwenye Sheria ya Haki, Kinga na Fursa za Baraza la Wawakilishi, Nambari 4 ya 2007 .
  5.2 Madhumuni ya haki, kinga na fursa hizo ni kuwawezesha wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waweze kuwa huru katika kutekeleza majukumu yao ya kikatiba bila ya hofu wala woga. Marehemu Shaaban Robert alipata kusema kwenye kitabu chake cha Kusadikika kwamba “nidhamu bila ya uhuru ni utumwa lakini pia uhuru bila ya nidhamu ni wendawazimu”. Kwahivyo, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamepewa haki, kinga na fursa ili watekeleze majukumu yao lakini hawaruhusiki kuzitumia vibaya au visivyo (abuse or misuse) haki, kinga na fursa hizo. Kanuni za Baraza la Wawakilishi zimetengenezwa kwa kufuata maelekezo ya Katiba ili kuweka utaratibu unaofaa katika utekelezaji wa shughuli za Baraza na kulipa uwezo Baraza lenyewe kumchukulia hatua mjumbe yoyote atakaekiuka taratibu zilizowekwa kwenye Kanuni .
  5.3 Suala la msingi la kujiuliza ni kwamba jee kutokana na haki, kinga na fursa walizopewa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kikatiba na kisheria kweli wako huru katika utekelezaji wa kazi zao? Kwa kiasi gani kinga hizo zinawasaidia dhidi ya shinikizo zinazotoka kwenye vyama vyao vya siasa na wanadhimu wa vyama vyao (Party Whips)? Wa aidha, haki na kinga za wajumbe kweli zinawasaidia kuhimili mikiki ya asasi za kiraia zinazofanya kampeni za kuunga mkono au kupinga jambo fulani linalojadiliwa au kufanyiwa maamuzi kwenye Baraza. Kwa maneno mengine ni kwamba jee kuna mpaka gani baina ya mbiu shawishi na utetezi kwa upande mmoja (advocacy and lobbying) na kwa upande mwengine uchochezi wa kumlainisha mjumbe wa Baraza akubaliane au akatae jambo.

 2. Changamoto za Uwakilishi
  6.1 Changamoto kubwa za kidemokrasia zinazowakabili wabunge au wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ni juu ya kigezo sahihi cha kutumika katika utekelezaji wa majukumu yao ya uwakilishi. Katika mjadala huu watu mbali mbali wameainisha vigezo vine vikubwa lakini wameshindwa kukubaliana ni kigezo kipi kipewe kipaumbele zaidi kwa madhumuni ya kutekeleza majukumu ya kikatiba na kuendeleza demokrasia. Vigezo hivyo ni kama ifuatavyo: (i) Mtazamo binafsi wa Mjumbe. (ii) Maoni ya jimbo analoliwakilisha. (iii) Mtizamo na msimamo wa chama cha siasa cha mjumbe. (iv) maslahi ya taifa. Kumbukumbu zinatuonyesha kwamba mwanasiasa wa kihafidhina Edmund Burke alisisitiza kwamba yeye akiwa mbunge wa jimbo la Bristol atatumia kigezo cha (i) na cha (iv) katika kutekeleza majukumu yake ya ubunge. Mwalimu Nyerere wa Tanzaniaalisisitiza kitumike kigezo cha (iii) dhidi ya Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waliodai kuundwa kwa serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano wa Tanzania. Kwa ufupi ni kwamba umahiri wa wanasiasa na ukuwaji wa demokrasia ndani ya nchi unategemea ni kwa kiasi gani wanasiasa waliopo (Wawakilishi) wameweza kuvitumia vigezo hivyo vyote kwa uwiano mzuri kulingana na haja na hoja iliyopo.
  6.2 Mafanikio ya ukuwaji na maendeleo ya demokrasia katika Zanzibar kwa kiasi kikubwa yamepatikana kutokana na mashirikiano na mshikamano wa wananchi wa Zanzibar ambao ndio wadau wakuu katika mchakato huu. Vyama vya siasa navyo vina nafasi kubwa vya ama kukuza au kudumaza demokrasia katika ushindani wa kisiasa. Katika nchi za Jumuiya ya Madola, demokrasia ya kibunge imejengeka kwenye msingi wa wengi wape na wachache wasikilizwe ‘majority have their way and minority have their say’. Zanzibar nayo ni sehemu ya Jumuiya ya Madola na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar ni mwanachama wa Commonwealth Parliamentary Association (CPA) kwahivyo linakubaliana na misingi ya demokrasia ya kibunge inayotetewa na Jumuiya ya Madola.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.