Na Ngaridjo Onana

Mwaka wa 1963 nilikuwa nikiishi na bibi yangu mzaa mama Mola amlaze mahali pema peponi AMIN, na wazee baba na mama wakiwa wapo Pemba na ilikuwa nikipenda kwenda Pemba kwa kuwa ninakuwa nimepumzika na sendi Chuwoni, hayo ni mambo ya kitoto.

Ikiwa December skuli imefungwa tunaelezwa tukachukue ticket wizara ya Elimu ili tuweze kupata kwenda Pemba . Marehemu mzee alichokifanya nikuandika barua Wizara ya Elimu ili tupewe Ticket na ticket hiyo alikuwa hakatwi kwenye mshahara wake bali ilikuwa moja ya mema ambayo mfanyakazi hutendewa.

Taib! Nakumbuka kaka yangu akiwa anaendeshs baskeli ya Humber ambayo kairithi kwa mzee baada ya mzee kununua gari na mie naendesha Raleigh ambayo kakayangu yeye hiyo ndio ilikuwa ni yake. Tunatoka nyumbani Kikwajuni huku mjamaa kaongoza na kunisemesha maneno ya hapa na pale, lilokuwa kubwa tunakwenda kuonana na karani wa Wizara ya Elimu, Al-Marhum Mzee Mohammed Turkey, tunaulizana tutamkuta? Bwana huyu kwa kumbukumbu zangu alikuwa akipenda kazi, akiingia mwanzo kazini na akitoka mwisho kazini na akitoka kazini kabla ya wakati basi ametoka kwa haja.

Msfara unaanzia kutoka nyumbani tunakatisha Chanoni Wirless kisha tunalikuta duka la Bhalo akiuza vitu vya Muziki, pahali hapo palikuwa na mandhar nzuri, kutokea hapo tuanfika Sokomuhogo ikiwa tunaitafuta Wizara ya Elimu, tunafika Posta tunasema hebu tuangalie barua, sanduku la Posta tuliokuwa tukilitumia na tulitumialo hadi leo ni P.O. Box 1008 Zanzibar . Nakumbuka tunapata barua kutoka kwa mzee akitusisitiza tusisahau kwenda kuwaaga wazee wetu mbalimbali kabla ya kuelekea Pemba . Tunafika Wizara ya Elimu tunaegesha mikweche yetu tunamkuta Bawna Mohd Turkey akitukaribisha na kutuambia kishazungumza na baba yetu na anatupa ticket zetu na kutuambia twende na mapema Bandarini.

Hiyo ni 1963 tunamuaga bibi yetu akiwa anabakia na mke wa mzee wetu na mtoto mdogo wa mikononi, sisi ikiwa mimi, kaka angu na dada angu tunaelekea Pemba . Hapa najiuliza aaah, kweli kulikuwa yaliokuwa twapewa ticket za bure kwa kuwa baba ni Mwalimu Mkuu, basi sio hayo tunapanda meli ya Syd Khalifa (MV Jamhuri) kwenye daraja la Pili (Second Class), na kule kujuwana na watu kushikamana tunapewa mzee Al-marhum Babatee mfanya kazi wa Melini atutizame, Babatee alikuwa Seamen wa maiaka na alikuwa akiishi Liverpool mzee alipokuwa naasoma England . Tunaingia melini usiku haooo, kwa safari ya Pemba , Asubuhi saa 12 tumeegesha Mkoani, mzee mwenyewe kaja na gari yake mwenyewe wala sio ya Skuli ya Syd Abdall (Fidel Castro) miaka yasasa ingekuwa kinyume. Mama yetu naye kaandamana na mzee kuja kuptupokea kila mmoja anataka kujuwa ya nyumbani, sisi kila mmoja anaelezea lake nakutoa salamu. Mdogo wetu anasema kilahaja ya Pemba naanafurahi kuwaona ndugu zake.

Haooooooooo. Mkoani, Chake Chake, tupo Madungu, tunafika kwa Babu Wanji tunanua baadhi ya vyakula kisha tunafika Macho mane kunakouzwa nyama tunanua kitoweo, na bado miaka 45 imepita pahala hapo kunaendelea kuendesha biashara ya nyama, tunapita Airport kisha tunaingia nyumbani palipo Castro leo.

Hii miaka 45, leo naandika haya kwa kuwa wiki nzima nipo Pemba, sasa nilichokifanya napita kila ambapo tulikuwa tunapita na mzee nipate kumbukumbu (Dhikrayati).

Nafika Castro kwenyewe nyumba ya Mwalimu Mkuu, wakati huo ilikuwa ukipita barabarani unaiona nyumba, leo lazima uipekue kwa kuwa kuna kichaka sirahisi kuiona, doooh. Nipo barabarani kuelekea kwenye nyumba hiyo huku najiuliza nikenda nikasema hapo kale nikiishi hapa wenye nyumba watanipokea vipi? Hapo nikasita zikanijia kumbukumbu za Maruhum Salum Machupa, Mmanga Fereji, Idi mpishi, Mzee Sabuki, Mzee Jaffar Ali, Salim Mbwana nawakumbuka hao wakiwa walikuwa wafanya kazi wa castro nawaona kwa kuvuta hisia kwanjia ya kumbukumbu naitizama Castro kisha naleta Taswira ya December 1963 tupo nyumbani, kisha inanijia Taswira nyengine tumetoka Castro tumekuja mjini tunakutana na Inspector wa Polisi naye ni Marehemu akiitwa Mzee Aboud Saidi akimwambia mzee kuwa tukisikia aina yoyote ile ya fujo basi tusibakie Castro tuondoke halan tuje mjini.

Mzee anakwenda Barazani kuzungumza na sisi tunakwenda Madungu kwa rafiki yake. Baraza ya Mzee ilikuwa ya watu wa Thakafa kina Mzee Abdoo baraza hiyo ipo pembezoni mwa Bank ya Watu wa Zanzibar , sasa ni Tawi la CUF haiba ya hapo pahali imekimbia na kutokomea.
Tunarudi na kufanya safari ya Castro tunakwenda kwa Bohora anayeuza Sambusa ikiwa palipo hoteli ya Chake Hotel ikiwa sasa jumba limegeuzwa kuwa ni Bank ya Barclays, tunachukua Sambusa ambazo zikiuzwa na kuliwa kwa Chatine. Haooo tunarudi Castro, mzee akipenda kusikiliza BBC na wakati huo kulikuwa na kipindi cha “Huku na Huku na Titus Mbutu”, mdogo wangu yeye akisema “Uko na Uko na Mbutu,” nikipenda kumsanif. Ingawa alikuwa ni mdogo sana huyu ndugu yangu akiwa na umri wa miaka 4 lakini akipenda kusikia Muziki wa Salum Abdalla (Sal Davis) kati ya nyimbo hizo akizipenda ni: Makini akili, Moyo usende mbali na Poor little girl, akiziimba kimbele kinyume.

Nikipenda kuja mjini kwa gari la Castro lilokuwa likiendesha na Marehemu Bw. Salim Machupa, akija mjini kuchukua chakula, mikate mie nipmo kwenye gari, nakumbuka Bw. Machupa siku moja akiniambia kuwa Maalim kamwambia kuwa mambo sio Shwari, sijajua akisema nini nakutoakana na umri wangu miaka 45 hiyo iliyopita nikiona ananipigia kelele, mie nikiakaa mbele ya gari ya Matwana kisha akiendesha mbio akikata korosi mie hupiga makofi kwa raha, hata siku moja yalipelekwa mashtaka kwa mzee kuwa anaendehs gari mbio, nayeye akajibu “Hamza ndio anayesababisha”, Dooh! Nusra anikoseshe ureda kwani nikawa sitakiwi kwenda mjini na gari la Mzee salum Machupa.

Mzee akirudi kazini ilikuwa tunasali naye jamaa ya watu 3, kisha anapumzika kisha tunasali Alsiri, kisha tukisha Sali Magharibi hufunguliwa BBC na halafu husoma Quraan kwa sote kabla yakupata chakula cha usiku, hapo sisi sote huwa na mzee ndio Baraa kwani hana wakuzungumza nao. Mzee anaangusha Sera, “Mzee Aboud Saidi kasema kukitokea zogo, twende mjini, nini anamanisha?’ Mama yetu anasema yanini kwenda mjini sio turudi Unguja ikiwa kuna hali hiyo?

Asubuhi ya tarehe 13 January 1964 Radio Zanzibar haijajiunga na BBC khofu imetuingia na mzee Aboud Saidi anasema wameitwa na Kamanda wao na Mzee Ahmeid Islam akiwa anakaa Chachani anatuambia kuwa Unguja kuna machafuko tuondoke Castro tuje mjini na ameshawasiliana na Mzee Aboud Saidi, Dooh, tunaondoka kwa siku kisha tunarudi, lakini hatuna mawasiliano na familia huko Unguja na huku sasa tunamsikia Field Marshal John Okello akimwaga cheche, tukajuwa Serikali imepinduliwa na mzee ahmeid Islam kutokana akiweza kuzungumza na mitambo ya simu moja kwa moja akitujulisha yanayoendelea.

Miaka 45 Ramadhan imefika Mapinduzi mie nipo Pamba na wazee na ndugu zangu leo kuelekea Sherehe ya Mapinduzi nipo Pemba, hisia na afkar mbalimbali zanjia, Fidel Marshal kuja Pemba, Comrade Ali Sultan, Rashid Abdalla, Mzee Diria na wengineo nakisha naitizama Pemba ya hukooo na ninaingalia ya sasa napata hisia na taswira za kila namna ambazo kuiznadika sisiwezi.

Hii Pemba najiuliza ndio Pemba? Hii Pemba imesogea? Hii Pemba inapelekwa wapi? Yahapo na Yasasa yepi ndio yepi?

Hizo nikumbukumbu nimeona nisikae nikazikumbuka pekee bora nizizungumze.
Narudi Unguja sio kwa Meli narudi kwa ndege na Skuli zilipofunguliwa 1964 ikawa Meli hakuna nilirudi na ndege na Bi. Khadija ambaye alikuwa ni mtu mzima yeye alitakiwa anitoe khofu mie, lakini mie ndio nikimtoa khofu yeye, ndani ya ndege kafunga macho, na kumbuka Marhumat Bi. Asya Jabir akiniambia mzee wetu mtizameni, kweli ilikuwa tunamtizama kafunga macho safari nzima Pemba mpaka Unguja.

Miaka 45 iliyopita nina mengi lakini utulivu sinao kwahiyo siwezi kwenda zaidi.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.