Umeandikwa na Juma Duni Haji

 

 • In an enviroment where falsehood is a phenomenon speaking facts is revolutionary so today let us Speak facts. “Penye Bahari ya uwongo ukisema kweli ni sawa na kufanya Mapinduzi basi, wakati ni huu sasa tusiache kusema kweli”
 • “A lie on the throne is a lie still, and truth in a dungeon is a truth still,    and  a lie on the throne is on the way to defeat   and truth in the dungeon is on the way to victory”(Henry David Thoreau). Uongo ni uongo tu hata Kama unasemwa Na Mfalme au Rais, na ukweli ni ukweli tu hata kama unasemwa na Topasi. Ukweli lazima utashinda tu
 • Every generation must wage a new war against new forces which seek through new devices to enslave mankind. The fight for freedom like the fight for justice is unending and will always be there (American Progressive Party: 1924). Vijana wa kila karne lazima wapambane kudai uhuru wa kweli unaodhibitiwa na wenye nguvu na vituko vipya kwa lengo la kurudisha dunia katika utumwa. Kupigania uhuru wa kweli kama vile ilivyo kupigania haki ni jambo la kudumu.

 

    0.0   DIBAJI

 

0.1       Katika gazeti la Rai (Toleo Na.667 (ISSN 0856-4973) la 11/5/ 2006) muliandikwa makala ndefu sana ya Mhe. Hussein Siyovelwa yenye kichwa cha maneno yasemayo “Muungano wetu hauna mwisho mwema “.

 

0.2       Makala hayo yamefanya uchambuzi wa kina wa sifa na tabia ya ndoa inayolazimishwa kuvunjika na mwanamke asiyemtaka mumewe. Muandishi amehakikisha kwamba ametoa kila sifa na ila mbaya za mwanamke wa aina hiyo na mwishowe bila kificho akaeleza kwamba hiyo ndiyo tabia ya wazanzibari katika kulalamika kwao kwa Muungano uliopo. Imenisikitisha sana kwamba Mhe Hussein haelewi yale anayoyasema katika waraka ule kwamba hayasaidii hata kidogo kuondoa udhaifu wa Muungano ambao umeendelea kuwepo kwa miaka 45 sasa. Kumbe mawazo ya Mhe. Hussein Siyovelwa ni mawazo ya wabunge wa Tanganyika na viongozi wake wa Kitaifa kutoka Tanganyika. Maneno ya Mhe. Pinda yalikua ni kielelezo cha hoja ya Hussein Silyovelwa. Lakini kumbe Mhe. Kikwete mwenyewe ana mawazo ya ajabu zaidi hata kumshinda Siyovelwa, maana yeye amesema katika hotuba yake kwa wabunge mwezi wa Augusti 2008, kwamba wanaozungumza mashaka ya Muungano ni Machakubimbi. Wengi wetu hatungetegemea Rais wa Tanzania afike hapo pa kutumia maneno ya mitaani kuwadharau wenzake wanaoeleza ugumu wa hali ngumu ya kisiasa ya nchi. Hawa ndio vijana wa Mwalimu walopewa vihunzi vya madaraka ya nchi.

 

0.3 Ni ukweli usio shaka kwamba hoja na matatizo ya Muungano yamekua yakizungumzwa sana kila mwaka unapofika mwezi wa April na kwa bahati mbaya hakuna hatua ya vitendo iliyofanyika kuona kwamba matatizo hayo yanamaliza au angalau yanapungua. Kila mara tumebaki kuitisha makongamano  ambayo watu na wataalamu huja kuonyesha umahiri wao wa kitaalamu au wanasiasa kueleza yale yanayowakera na kisha kila mmoja huondoka na kungojea kongamano lingine. Wataalamu wa sheria na wanasayansi wa siasa hujifanyia utafiti na kujipatia digrii za kwanza za pili na hata PhD kwa eti kufanya uchambuzi  wa matatizo ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.  Matatizo gani hayo yasiyokwisha maisha?

 

0.4 Kutokana na hoja ya Muungano kuibuka tena hasa pale Mhe. Pinda alipotamka Bungeni kuwa Zanzibar si nchi, nimelazimika kuweka kumbukumbu yangu hii kama wafanyavyo wengine, akina Mwalimu Nyerere, Mzee Warioba na wengi wengineo kutoka Tanganyika na Zanzibar. Baada ya kuona na kusoma dharau isiyomipaka ya baadhi, na si ajabu ya wote wanaoandika kuhusu Muungano kutoka Tanganyika, kama ilivyothibitishwa na wabunge wote kutoka Tanganyika walipokua wakichangia Bajeti ya 2008 ya Wizara ya Muungano ya Mhe. Muhammed Seif Khatib katika Bunge Dodoma nami nimeona nieleze yale ninayoyaelewa kwa kuona au kwa kuyasikia yakisemwa.

 

Waafrika ndivyo Tulivyo

 

0.5 Ni kawaida yetu Waafrika, kupata uchungu uso kifani pale tusikiapo au kuona mzungu akimnyanyasa na kumnyima haki muafrika na jina sahihi tunalompa mzungu huyo ni kumwita mkoloni au Kaburu. Bado manyanyaso, mateso au nchi moja ya kiafrika kuitawala nyingine ya kiafrika haikupata jina sahihi kisiasa. Prof. Ali Mazrui aliuita Muungano wa Zanzibar na Tanganyika kama mfano wa ukoloni, kwani Tanganyika kuifanya Zanzibar kuwa koloni lake ni sawa na (African Self-colonisation).

 

0.6 Marehemu Mwalimu Nyerere akipenda sana kutuambia kwamba ubepari hauna rangi, ni sahihi pia kusema kwamba na ukoloni vile vile hauna rangi. Watu wa Indonesia waliitawala (self-colonized) East Timour na hawakuiachia mpaka kwa kulazimishwa na Umoja wa kimataifa tena baada ya maisha ya watu wengi kupotea. Nchi za aina hiyo zinazopenda kuwatawala wengine katika bara la Afrika zimeanza kuchipuka kwa kasi sana. Mfano wa wazi ni ule wa Ethiopia na Eritrea na hivi karibuni Ethiopia kuivamia Somalia.  Kuna mzozo wa aina hii kule Uganda kati ya Utawala wa jadi wa Baganda na Serikali ya Museveni ya Uganda. Kiwango cha mahusiano ya Tanganyika na Zanzibar kilivyofikia kimethibitishwa na Profesa Mazrui kama nilivyosema hapo juu kuwa ni Tanganyika kuvifanya visiwa vya Zanzibar kuwa koloni lake. Prof Mazrui ansema hivi juu ya Muungano huu:

 

“For cold war reasons President Nyerere in 1964 was under pressure from President Lyndon Johnson of the United States, who was in favour of ending the independence of Zanzibar in order to evert the risk of an East African Cuba under a Marxist regime on the Clove Islands. The sovereignty of Zanzibar was extinguished without consulting the people in a referendum. It was in the final analysis, a case of inter-African Colonisation, with the blessing of United Stetes and NATO. Was this a case of African Self-colonisation? —-. But Tanganyika never lost sovereignty. Its representation in the United Nation, the Common wealth and other international bodies continued under its own flag, its own National anthem and under the leadership of its own President Nyerere. There was simply a change of name, Tanganyika to Tanzania.” (Prof. Ali A.Mazrui: 2nd May 1994: Kenye Sunday Nation)

                       

Kilichotokea 1964

 

0.7 1964 Rais wa Zanzibar alikubaliana kwa hiari na Rais mwenzake wa Tanganyika kuunganisha maeneo maalum ya taasisi zao zinazoitwa Serikali na kuunda Taasisi mpya inayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Hizi ni taasisi za nchi, (organizations) siyo nchi. Nchi ya Tanganyika kabla ya Muungano ilikua na Taasisi yake inayoitwa Serikali ya Tanganyika na nchi ya Zanzibar ilikua na Taasisi yake inayoitwa Serikali ya Jamhuri ya watu wa Zanzibar. Baadhi tu ya idara za Taasisi hizo ndizo zilitegemewa kuwa zimeunganishwa kuzaa taasisi mpya ya shirika iliyoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kumbe Mwalimu hakua na lengo hilo. Lengo lake ni kuanzisha Jamhuri ya Muugano wa Tanganyika kwa kutumia ulaghai wa kikatiba na kisheria. Kwa maandishi amefanikiwa lakini badala ya kupata taasisi ya shirika kwa faida ya nchi ya Tanganyika  na nchi ya Zanzibar amekufa na kuacha mgogoro wa miaka 45 usiomalizika. Waswahili wanasema akili nyingi huondoa maarifa. Mwalimu ni mkombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika, wakati huo huo Mwalimu ni muuwaji wa nchi inayoitwa Zanzibar.

 

0.8 Dk. Harrison Mwakyembe na Rais Kikwete wanaweza kuwadharau Wazanzibari katika kiwango hicho, lakini kuendelea kuwadharau hata wale wataalam wa Kitanzania wanaoheshimika kimataifa katika taaluma zao kama Prof. Issa Shivji, Jaji Francis Nyalali na Jaji Robert Kisanga na wengi wengineo walioeleza udhaifu wa Muungano na kushauri marekebisho, ni  dalili ya wazi ya upofu wa akili iliyokomazwa  na itikadi ya chama kimoja na propaganda za vyou vya ki-itikadi ambavyo baada ya kutoa nafasi ya vijana wa kizazi kipya kuona ukweli bado wamejaa kiburi hata kuwashinda wageni waliowatawala babu zao hapo zama za ukoloni.

 

0.9 Nae Muandishi maarufu Makwaiya wa Kuhenga katika kipindi chake cha Televisheni cha “Jee tutafika?”,  aliwahi kumuuliza Maalim Seif Sharif: “Vipi  Maalim Seif baada ya miaka 40 ya ndoa leo bado munauliza kwamba baba yenu ni wa halali au si halali!?” Maneno kama hayo yamekua yakisemwa ndani ya Bunge na hata katika mikutano ya kisiasa ya CCM mbali mbali.

 

0.10 Kuna mwaka mmoja mara tu baada kuachiwa kutoka jela kwa ile kesi iliyoitwa eti ya uhaini, tulikutana na Mhe. Sinde Warioba pale Hoteli ya Mazsons Unguja. Tulimueleza kwamba hawana budi kama watawala wakuu wa nchi hii kumaliza matatizo wanayoyaita kero za Muungano.  Kwani kama wanatuona sisi akina Duni ni wakorofi kizazi kinachokuja nyuma yetu kinaweza kuonekana ni kikorofi zaidi maana hakuna anaekubali kufanywa koloni katika karne hii ya 21. Alicheka na kutukejeli kwamba hayo ni mawazo ya uchungu wa kutoka jela. Leo kesi ya Muungano ilishawahi kufikishwa mahakamani tena imepelekwa na vijana wadogo sana wala si wanasiasa maarufu. Ushahidi wa maneno yangu yale umedhihirika pale Mhe. Pinda alipotamka kwamba Zanzibar siyo nchi.

 

0.11 Tume ya Mhe. Jaji Nyalali ilipita nchi nzima kukusanya maoni ya aidha tuwe na Serikali mbili au tatu. Jaji Kisanga alitumwa kufanya hivyo na Mhe. Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa. Kuna Kamati za Serikali aina kwa aina ikiwemo ile ya Shelukindo na Mhe. Amina Salim Ali zikijaribu kutafuta ufumbuzi wa masuala haya ya Muungano.

 

0.12     Makala nyingi zimekua zikiandikwa katika magazeti na vipindi vya redio na TV kuoneshwa. Kwa jumla kila Rais mpya anapoingia huja na kasi mpya ya ahadi nyingi kwamba suala la muungano atalishughulikia kwa nguvu mpya na ari mpya.

 

0.13 Nakumbuka vyema wakati Rais Mhe. Mkapa alipoingia madarakani aliahidi mbele ya Bunge kwamba matatizo ya Muungano angeyamaliza kwa kipindi cha miezi sita tu. Leo ni miaka 10, Mhe. Mkapa ameuacha Muungano katika hali mbaya zaidi kuliko alivyoukuta yeye.

 

0.14     Hadi leo ripoti ya Mhe. Mbita haikuchukuliwa hatua. Jee huo ndio uhuru tulioutafuta kutoka kwa waingereza na waarabu ya kwamba waache wazanzibari tuwauwe kwani babu zao waliwatesa babu zetu? Kwa nini tunahukumiwa kwa madhambi ya watu wengine?

 

Wazanzibari Hatuthaminiwi

 

0.15 Kwa upande wa Tanganyika ushahidi umeonekana pale mara tu Mhe. Kikwete alipochukua madaraka, ambapo wafanyabiashara wanne waliuliwa na polisi kwa kisingizio cha ujambazi. Ushahidi huo ukamlazimisha Mhe Kikwete kuunda Tume kuchunguza vifo hivyo, na wahusika wamefikishwa mahakamani kujibu mashitaka ya mauaji. Wakati wa maandamano  askari wa Zanzibar na Tanganyika  waliwauwa wazanzibari Unguja na Pemba tarehe 27/01/2001 .Wakati  wa uandikishaji wa Daftari la kudumu  waliuliwa pia  wazanzibari. Waliofanya mauaji hayo yote wanajulikana, baadhi yao wakiwa ni  Maafisa wa Polisi na KMKM lakini hadi leo hakuna hatua iliyochukuliwa na viongozi wa kitaifa au polisi dhidi yao.

  

0.16 Hivi karibuni imetangazwa kwamba aliyemtesa Mbwa wa mzungu kule Mererani amefungwa muda usiopungua mwaka mmoja, lakini wazanzibari wameuliwa kwa makusudi tena bila kosa na wauaji kupewa vyeo, tena si mara moja wala mbili. Wenzetu wa Taganyika wanasema kulalamika kwetu kwamba tumeuliwa ni tabia ya kutaka kuachwa.

 

0.17 Ni vizuri tukumbushe kwamba wakati wa ukombozi wa Zimbabwe, Wazanzibari walishiriki kama wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Wakati wa kumuondoa nduli Idi Amin wa Uganda alipochukua sehemu ya Tanganyika kule Bukoba, Wazanzibari walishiriki kama wananchi wa Jamhuri hiyo ya nchi mbili.

 

0.18     Vita vyote vya ukombozi wa Kusini mwa Afrika ambavyo Tanzania ilipeleka askari wake, walikuwemo Wazanzibari tena wengi na wamepoteza maisha kwa niaba ya Watanzania wote wa nchi mbili.

 

0.19 Kwa nini pale panapoonekana maslahi ya fedha au rasilimali asili tu, ndipo Wazanzibari walazimishwe kukubali yasiyoelekea? Mahusiano yetu kati ya Tanganyika na Zanzibar katu hayakua ya Mkubwa kummeza mdogo, au mdogo kuolewa na mkubwa, bali kujenga umoja wenye nguvu ili wengine waone na kutuunga mkono. Ukweli ulivyo ni kwamba miaka 45 sasa hakuna hata nchi moja jirani yetu aliopendekeza kujiunga nasi.

 

0.20 Mwaka huu 2008, wakati akiwa safarini Marekani Rais Kikwete alitamka bayana kwamba Shirikisho la Afrika mashariki litakua na faida tu kama wananchi watalikubali siyo viongozi watatu pekee. Hivyo pia ndiyo inavyopaswa kusemwa kwa Zanzibar na Tanganyika

 

0.21 Kama hoja ya kuonekana mafuta  huko Pemba na Unguja ni kushtua watawala  kwa kukataa yasichimbwe na hivyo kuwakera wakubwa, mbona hakuna kiongozi wa Tanganyika aliyesimama na kutetea wazanzibari juu ya  kutumika kwa mafuta na gesi asilia ya Songosongo ambayo hivi sasa gesi ya Songosongo inatumika kuendesha mitambo ya umeme wa Tanesco? Miujiza ya Muungano huu ni kwamba, chao watanganyika ni chao, lakini chetu wazanzibari ni chao pia. Kwa watanganyika huo ndiyo Muungano aliouasisi Mwalimu Nyerere na Mzee Karume na wanapenda tuusifie na tuuenzi.

 

0.21     Huko miaka ya 1967 hadi 1977 kulikua na umoja unaoitwa (Umoja wa Afrika Mashariki)  “East African Community” na kwamba Mwalimu Nyerere kwa kiburi cha kutompenda Mhe Charles Njonjo, mwanasheria Mkuu wa Kenya alifunga mipaka kati ya Tanganyika na Kenya na hatimae akauvunja umoja huo. Sina hakika kwamba na Mwalimu alipokua akilalamika ni kwa sababu ya kukataa mume mkenya au kwa sababu ya kuona kwamba ulikua hauna maslahi na yeye Mwalimu na kwa Tanganyika. Si hilo tu ila pia Tanzania  ilijitoa katika umoja wa Biashara ya nchi za Mashariki na kati (Comesa) kwa maelezo kwamba umoja huo ulikua hauna faida kwa Tanganyika Pamoja na kubembelezwa na nchi nyenzake bado  Tanganyika imetoka katika umoja huo.  Walifanya hivyo kwa sababu kulikua hakuna manufaa na Tanganyika. Kwa nini iwe kosa kwa Zaanzibar? Maneno ya Mhe. Pinda kwamba Zanzibar siyo nchi ndiyo tafsiri sahihi na hali ya Zanzibar.

 

1.0       Matatizo ya Muungano

 

1.1 Marehemu Mwalimu Nyerere badala ya kutatua matatizo ya Muungano, alilokua  akifanya ni kuyaahirisha matatizo hayo kwa kuwatisha wanaoyaeleza, au kwa kuwafukuza katika uongozi wa chama na Serikali, au kuwafungulia kesi za kubuni za uhaini na uchochezi na kama hayo hayangefaa basi hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar kuchafuka na viongozi kushikishwa adabu.

 

1.2 Mwalimu alifanya hivyo kwa sababu yeye ndie kiini cha matatizo yenyewe na aliona aibu kujulikana kwamba dhamiri yake ya kuunda Tanganyika mpya. Hadi sasa bado vitisho vinaendelea kuwazuia wazanzibari wasieleze aibu hiyo. Aibu hiyo ndiyo kiini cha kuwepo mgogoro wa Muungano na mimi naomba nieleze kadhia ya Muungano chini ya vifungu vifuatavyo:

 

 • Kuwepo au kutokuwepo kwa Serikali ya Tanganyika
 • Tume ya fedha ya Muungano na  Mahakama ya katiba
 • Kuchezewa kwa Mkataba wa Muungano
 • Mchango wa Zanzibar katika Matumizi na Mapato ya  Muungano
 • Kuanzishwa kwa Benki Kuu na haki  za Zanzibar katika Benki hiyo

 

Kuwepo au kutokuwepo kwa Serikali ya Tanganyika

 

1.3 Imekua ni mtindo wa viongozi wa siasa wa Tanganyika kutetea kwa kusema kwamba eti hakuna Serikali ya Tanganyika na hivyo haingewezekana kufanya mazungumzo juu ya mgogoro  huu kati  ya Serikali  hiyo na ile ya Zanzibar. Kila mtu anafahamu kwamba Muungano huu ni kati ya nchi mbili Tanganyika na Zanzibar. Popote penye Muungano lazima kutakua washiriki zaidi ya mmoja. Mwalimu Nyerere alisema hayo alipohojiwa na gazeti la Observer la Uingereza tarehe 20.  4. 1968 na akasema:

 

If the mass of the people of Zanzibar should, without external manipulation, and for some reason of their own, decide that the union was prejudicial to their existence , I could not bomb them into submission……The Union would have ceased to exist when the consent of its constituent members was withdrawn.” (Nyerere:  London Observer: 1968)

 

 Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hautokuepo kama wale walioungana watatoweka au watakuwa hawapo

 

1.4 Mwalimu ni mtu wa hekima na ni vyema kukumbuka yale aliyokua akisema na kuandika. Maana kama hivi sasa hakuna Serikali ya Tanganyika na kwa maana ya Mwalimu Nyerere basi kungekua hakuna Muungano tena tangu hapo aliposema.

 

1.5 Jee kweli Serikali ya Tanganyika haipo? Na kama haipo kaifuta nani na kwa nini ikafutwa? Ukitaka kuelewa hoja hii ni vyema msomaji akarudia kwenye sheria zilizosababisha kuamrisha kufutwa kwa Serikali hiyo.

 

1.6 Makubaliano ya Muungano ya 1964 kifungu Na.(iv) kinasomeka

 

“And in addition (the Union Parliament) shall have exclusive authority in respect of all other matters in and for Tanganyika.”

 

1.7 Hiki ndicho kifungu cha makubaliano kilichotumika kuanzisha mgongano wa Muungano. Maneno “and in addition” maana yake kwamba Bunge linatekeleza shughuli za mamlaka mbili. Lakini Mwalimu akaifanya kuwa mamlaka moja ili ionekane kwamba Bunge la Tanganyika halipo na Rais wa Tanganyika hayupo.

 

1.8 Mara zote tunapotaja Tanganyika wengi ya wale walio Tanganyika hasa viongozi wa dola na wale wa CCM huwa hawapendi na hutuona sisi kama tunawarejesha nyuma katika kuimarisha Muungano. Ukweli ni kwamba jina hilo halipendwi kwa sababu kunafichwa aibu fulani iliyofanyika hapo 1964 ambayo ndiyo kiini cha mgogoro wa Muungano. Katika makubaliano ya Muungano hakuna kifungu kinachotoa ruhusa kufutwa kwa Serikali ya Tanganyika. Serikali ya Tanganyika imelindwa na Kifungu Na. (v) cha Makubaliano hayo kinachosomeka kwamba,

                       

“The existing laws of Tanganyika and Zanzibar remains in force in their re            spective territories.”

 

“Sheria ziliopo za Tanganyika na Zanzibar zitaendelea kutumika katika nchi zinazohusika hata baada ya Muungano.”

 

1.9 Katiba ndiyo sheria mama kwa hivyo katiba ya Tanganyika haijaagizwa kufutwa na Makubaliano ya Muungano, Katiba hiyo inapaswa iwepo na viongozi wake wawepo kusimamia mambo ambayo si ya Muungano.

 

Na kama hakuna katiba sheria hizo zingetumikaje katika Tanganyika isiyo          katiba?

 

1.10. Lakini inasikitisha sana kuona baada ya makubaliano hayo Bunge la Tanganyika lililokaa kupitisha sheria ya kukubali Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa makusudi lilikubali kuifuta katiba ya Tanganyika na hivyo kuifuta Serikali yenyewe. Maana ukishafuta katiba hizo sheria nyingine za Tanganyika zitasimama kwa katiba ipi? Katika sheria (Na.22 ya 1964) kifungu chake cha 7 kinasomeka hivi:

 

“On the commencement of the Interim constitution of the United Republic, the Constitution of Tanganyika shall cease to have effect for the Government of Tanganyika as a separate part of the United Republic.”

 

“Mara tu itapoanza kutumika katiba ya muda ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, katiba ya Tanganyika itasita kutumika kwa ajili ya Serikali ya Tanganyika kama ni sehemu nje ya katiba na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.”

 

1.11 Hili lilifanyika kwa maksudi ili viongozi wa Tanganyika kujipa nafasi kujikweza na kuikweza Serikali yao iliyouliwa na Bunge la Tanganyika na kujibadili na kuwa ndiyo Serikali ya Muungano. Kwa kizungu ni kwamba “The government of Tanganyika underwent metamorphosis to become a Union Government.” Serikali hiyo iiljifananisha na Amoeba na kujibadilisha umbo.Serikali ya Tanganyika ilijiumbua na kujipa umbo jipya na kua Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar

 

1.12 Huu ndiyo udanganyifu wa kutumia kalamu ulivyofanyika hapo 1964. Sheria Na 22 ya 1964 inayoitwa “Union of Tanganyika and Zanzibar Act 1964 ilipitishwa na Bunge la Tanganyika 25/4/64 kabla Muungano kuanza. Wakati huo na siku ile kulikua hakuna Bunge la Muungano maana lililazimika liundwe baada ya sheria hii kupitishwa na wawemo wabunge wasiopunga 32 kutoka Zanzibar (wajumbe wa Baraza la Mapinduzi).

 

Mwanzo wa Udanganyifu

 

1.13 Makubaliano ya Muungano kisheria hayawezi kubadilika au kubadilisha katiba ya Tanganyika. Kufuta katiba ya Tanganyika hakuna uhusiano wowote na makubaliano yale. Hata kama katiba hiyo ndiyo iliyotumiwa kuweka katiba ya muda ya Muungano baada ya kufanyiwa mabadiliko ilipatikana katiba mpya ya muda ya Muungano na kuiacha ile ya Tanganyika pekee iendelee kutumika kwa shughuli za Tanganyika zilizo nje ya Muungano.

 

1.14 Hakuna mahali katika makubaliano ya Muungano palipoagiza kufutwa katiba hiyo wala kumuondoa Rais wake wa Tanganyika. Muda wote wa utawala wake Mwalimu alistahiki kuwa Rais wa Tanganyika na Rais wa Jamhuri ya Muungano kama ambavyo Mzee Karume alivyobaki kuwa Makamo wa Rais wa Jamhuri na Rais wa Zanzibar. Maelezo haya yanaweza kufananishwa na hali ya Mhe Kikwete hivi sasa. Kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa chama chake cha CCM hakumfanyi asiwe Rais wa Jamhuri. Hizi ni dhamana mbili tafauti.

           

1.15 Kitendo hiki ndicho kilichotumika kuharibu utaratibu na mfumo mzima wa mwenendo wa utawala wa shughuli za Muungano kwa miaka 45 sasa. Siku ile ile wafanyakazi wote wa Serikali ya Tanganyika wakawa wafanyakazi wa Muungano, Mahakama ya Tanganyika ikawa ndiyo ya Muungano, na Majaji wake wakawa ndio majaji wa Muungano. Muhuri wa Tanganyika nao ukawa ndio Muhuri wa Muungano (Public Seal). Kwa nini udanganyifu huu? Kwa sababu ya ukosefu wa nia njema (No good will, wrong intention).

 

1.16 Katika sheria ile Na. 22 ya 1964, Rais wa Tanganyika amejipa madaraka ya kutunga kanuni zilizompa uwezo wa kutoa maagizo yanayohusu mambo ya Muungano kwa kutumia kanuni (Decrees) za sheria ya Tanganyika. Pamoja na kupewa madaraka hayo na makubaliano ya Muungano, lakini kanuni hizo zilikua zitungwe na Bunge la Muungano siyo Bunge la Tanganyika.

 

1.17 Siku ilipopitishwa sheria hii Na 22 pia zilipitishwa kanuni (decree) mbili zilizotokana na kifungu Na. 5, 6 (3), na kifungu cha 8 cha sheria hii.Kanuni hizo juu ya mamlaka ya umiliki wa muda (“The provional Transitional Decree 1964) na ile ya mamlaka ya katiba ya muda (“The Interim Constitutional Decrees 1964), zote hizi hazikua halali maana ni kanuni zilizopitishwa na Bunge la Tanganyika zilizotokana na sheria ya Tanganyika.

 

 Kifungu Na.3 (i) cha (kanuni ya muda ya katiba) kinasomeka hivi:

 

“Every person who holds office in the service of Republic of Tanganyika immediately before the Union Day, on Union day be deemed to have been elected, appointed or otherwise selected to the corresponding office in the service of the United Republic.”

 

“Wafanyakazi wote wale waliokua wanafanya kazi katika Serikali ya Tanganyika kabla Muungano watakua wamechaguliwa au kuteuliwa moja kwa moja na kua watumishi wa Serikali ya Muungano.”

 

1.18 Mheshimiwa Pius Msekwa analifahamu vyema suala hili. Yeye kwa kiburi na majigambo anasema hivi katika waraka wake alioutoa kwenye maazimisho ya Muungano hapo Tanga Hotel ya Mkonge tarehe 25—27 Februari 1994.

 

“The transitional decree 1964 published on 1/5/64, transferred persons who were holding office in the service of Republic of Tanganyika to the corresponding office in the public service of the United Republic. By the same decree the High Court of Tanganyika also became the High Court of United Republic of Tangayika and Zanzibar and the public Seal became public seal of the United Republic.” (Msekwa Tanga: 1994)

 

Tafsiri ya maneno haya ni sawa na maelezo ya hapo juu kuhusu wafanyakazi wa Serikali ya Tanganyika.

 

Kundi la G55 na  Sera ya Chama cha CCM

 

1.19 Mwaka 1993 kundi lilojiita G55 walijaribu kurejesha Serikali ya Tanganyika kwa Azimio la Bunge. Mhe. Njelu Kasaka alieleza kwa ufasaha kabisa hoja hii. Amri ya Mwalimu Nyerere ambae wakati ule hakua Mbunge wala Rais akazuia Azimio la Bunge kutekelezwa badala yake Bunge likaazimia kukitaka chama na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kutayarisha mazingira ya kuifanya Tanzania kua na Serikali moja.Yaani badala ya kusahihisha makosa ya miaka yote ya uhai wa Muungano wakubwa hao wakalenga kumaliza pale palipo baki pa kuuwa taifa la Zanzibar ambalo 1964 waliungana nalo kwa hiari.

 

1.20 Eti sababu ikatolewa kwamba kurejesha Serikali ya Tanganyika ni kinyume na Sera ya Chama cha CCM. Lakini katika Makubaliano ya Muungano hapana mahala ambapo chama cha ASP au TANU kilishiriki, ingawa vilikuwepo wakati Muungano ukiwekwa sahihi. Makubaliano yalikuwa kati ya Rais wa Tanganyika kwa niaba ya watanganyika na Rais wa Zanzibar kwa niaba  ya wazanzibari. Wakati huu yanapotokea haya chama kinatumiwa kujenga hoja ya kisiasa kwa kutumia msimamo wa chama kushika hatamu za dola, hoja ambayo ililazimishwa ili kufikisha lengo hili la serikali moja. Mwalimu anasema hivi katika kitabu chake cha Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania: “Ukifufua Tangayika iwe na Serikali yake utaua Tanzania.” (Mwalimu:1993;28)

 

Kuchafuliwa kwa Makubaliano

 

1.21     Kwa hivyo tangu 1964 mara tu baada ya kuwekwa saini makubaliano ya Muungano yamekuwa yakichafuliwa kwa makusudi na kutoa nafasi upande mmoja wa Muungano kujinufaisha chini ya kivuli cha kuimarisha Muungano huku upande wa pili ukidimia. Prof. Shivji katika moja ya mihadhara yake juu ya Muungano anasema hivi:

 

“One of the essential features of that scheme was and is the distribution of Power between the Union Parliament and the Zanzibar Legislature. That scheme was implicitly made immutable and a fundamental condition of the association of the two states. To tamper with those provisions is the surest way to destroy the legal foundations of the Union. Addition to and subtle alterations of the reserved list on union matters is like hammer-blows delivered to the core of those foundations. The moral and political responsibility of those of us who simply watch the blows is probably greater than those who deliver them.” (Prof. Shivji: 1994 University of Dar es Salaam)

 

Profesa anasema kwamba kuivuruga misingi ya makubaliano bila kuitetea ni sawa na kutizama mtu akipigwa ngumi na wewe unachekelea. Wajibu wa wale wanaoyaona hayo na kunyamaza kimya ni sawa na yule anayeyavuruga makubaliano hayo.

 

1.22 Kwa hivyo matatizo ya sasa ya Muungano ni matatizo ya kujitakia yaliyotokana na vitendo vya makusudi vya kijanja dhidi ya makubaliano hayo. Serikali ya Tanganyika ilipandishwa daraja na kujifanya ndiyo mmiliki wa Zanzibar (African Self-colonisation).

 

1.23 Tabia hii imejenga jeuri kwa wale wasioelewa mwanzo wake na hufika kuthubutu kulinganisha makubaliano haya kama kwamba ni ndoa. Aa! vipi nyinyi Wazanzibari munauliza uhalali wa baba yenu baada ya miaka 45 ya ndoa ni maneno ya kawaida hata kwenye vikao vya kiserikali. Ala! Kwani hivyo Zanzibar imeolewa na Tanganyika?  Kwani hivyo Nyerere alimuoa Karume pale 1964?

 

 Uwingi na Uhaba wa Watu

 

1.24     Tabia ya ukubwa imejenga kiburi kwa Watanganyika, kufika hadi kusahau kwamba zilizoungana ni nchi mbili.Wengi utawasikia wakisema huaje watu 1,000,000 wawe na wabunge 50 katika Bunge la Muungano.  “Eti wabunge wanaotoka katika Vitongoji kule Pemba wanataka wawe ndiyo wakuu wa upinzani bungeni “anasema Mbunge wa Tanganyika tena wa chama cha upinzani. Ala!! Leo udogo na uchache wa wazanzibari unaaza kuhojiwa kwamba hauna haki sawa na mkubwa wake ambae 1964 waliungana kwa hiari kama ni mataifa sawa sawa. “The size and population of Zanzibar become the justification for its marginalization.” Wachache na wadogo wanatengwa kwa sababu ya uchache na udogo wao.

 

1.25 Watanganyika wanajipa kusahau na wanakejeli maamuzi ya Mwalimu Nyerere na Mzee Karume walokubali ukweli kwamba wameungana wakijua kabisa kwamba mmoja ni mdogo na mmoja ni mkubwa lakini yote ni mataifa yaliyokua huru.  Hawa wanaosema haya bado wanakubali kwamba China ina watu 1500 milioni lakini china inakiti kimoja katika Umoja wa mataifa (UN) . Ushelisheli una kiti kimoja katika Bunge la Afrika sawa na Sudan. Solomon Islands ina watu wasiozidi 100,000 wana kiti kimoja sawa na Ujerumani au Ufaransa.  Wanakubali kwamba Ushelisheli wana kiti kimoja katika Umoja wa Afrika na Sudan nayo inakiti kimoja kama vile ilivyo Jamhuri ya watu wa Congo ambazo ni kati ya nchi mbili kubwa sana kuliko Ushelisheli.  Kwa hawa hili ni sawa , lakini kwa Zanzibar kua na haki sawa na Tanganyika wanaona halistahiki! Wanajifanya zumbukuku kutokuelewa kwamba hadi leo kiti cha Zanzibar kipo na kina nafasi yake pale Umoja wa Mataifa (UN) bila kutumiwa na Zanzibar. Pamoja na udogo wake Zanzibar kama ilivyo Tanganyika ilipewa kiti kimoja kama ilivyopewa nchi nyingine.

 

Kuchezewa kwa Mkataba wa Muungano

 

1.26 Utamaduni huu wa kukosa nia njema umezaa upotofu wa kila hali ikiwemo maandiko ya katiba na sheria mbali mbali. Kwa mfano ukiangalia vifungu vya katiba vifuatavyo vimeandikwa kwa jeuri kabisa huku waandishi wa katiba hii wakijua na Bunge la Jamhuri likijua kwamba ni makosa.

 

1.27 Kifungu Na.133 cha katiba ya Jamhuri ya Muungano ya 1977 kinachozungumza Tume ya Pamoja ya Fedha (Joint Financial Commission) kinasomeka hivi:

 

The government of United Republic shall maintain a special Account to be known as the Joint Finance account which shall be part of the consolidated   Fund of the United Republic into which shall be paid all the moneys contributed by two Governments in such proportion as shall be determined by the Joint Finance Commission in accordance with a law enacted by Parliament for the purposes of the business of the United Republic in relation to the union matters.

 

“Serikali ya Muungano itafungua Account ya akiba ya Benki itakayoingizwa mapato yatakayochangwa na Serikali mbili, ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Zanzibar”.

 

1.28 Maandiko ya kifungu hiki yanathibitisha kwamba hata katika kuchangia mambo ya Muungano upande wa Serikali ya Muungano wao wanajitambulisha kwamba ndiyo Tanganyika huku ikieleweka vyema kwamba hapa wanaostahiki kuchangia kwa ajili ya mambo ya Muungano ni Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar na siyo Serikali ya Muungano na ya Zanzibar. Ndiyo maana wengi wetu tunaamini kwamba kuuliwa kwa Serikali ya Tanganyika hakukuwa na nia njema ya ushirikiano wa nchi mbili na hakukufanywa kwa bahati mbaya. Mwalimu Nyerere ameeleza katika kitabu chake cha “Uongozi wa Nchi yetu na Hatima ya Tanzania” kwamba kama kungekua na Serikali tatu mzigo wote wa kuendesha Serikali ya Jamhuri ya Muungano ungebebwa na Tanganyika.

 

Shirikisho la Serikali tatu lingekua ni gharama kubwa mno kwa Tanganyika anasema Mwalimu katika kitabu chake cha Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania (uk. 15—16)

 

1.29 Sura ya kujiona katika umbo hilo kumejitokeza pia katika Kifungu cha Mahakama ya Kikatiba ambacho kinasomeka hivi:

 

The special constitutional court shall consist of members of whom one half shall be appointed by the Government of United Republic and the other half shall be appointed by the Revolutionary government of Zanzibar.

 

“Kamati maalum ya katiba itakua na wajumbe ambao nusu yake watatoka kutoka Serikali ya Jamhuri ya Mungano na nusu watatoka Serikali ya Zanzibar.”

 

1.30     Huaje wajumbe wa Mahakama nusu wawe wanatoka katika Serikali ambayo ndiyo inayoshtakiwa. Waliostahiki kuwemo katika kamati hii ni wajumbe wa Tanganyika na wajumbe wa Zanzibar”

 

1.31     Maelezo ya vifungu vyote hivi viwili yanathibitisha kwamba Serikali ya Muungano ndiyo inayowakilisha matakwa na haki za Tanganyika, jambo ambalo linaonesha jeuri ya kutojali makubaliano mpaka kwenye katiba yenyewe inayoitwa ya kudumu ya Muungano.

 

1.32     Tarehe 10/12/2002 hadi 14/12/2002 nilihudhuria Kongamano pale hoteli ya Golden Tulip lilojadili masuala ya kikatiba na kusoma waraka uliotolewa na Mhe. George Liundi aliyekua Mwanasheria wa Serikali wakati wa Mwalimu Nyerere ambae anaeleza majuto yake jinsi sheria za Muungano na katiba ya Muungano zilivyokua zikivurugwa na watawala bila kujali Makubaliano ya Muungano. Mzee George anasema hivi kuhusu jina la Tanzania:

 

“Prior to the enactment of the Interim constitution of 1965, another constitutional problem appears to have been created by the change of name of the United Republic from the United Republic of Tanganyika and Zanzibar to the United Republic of Tanzania, with effect from 11th December 1964 (declaration of Name Act 1964 (section 3). This change of name calls for scrutiny, because on the face of it the measure appears to have put into question the constitutional status (in terms of national sovereignty) of both the territories formerly constituting the Republic of Tanganyika and Zanzibar respectively.”

 

Anachosema Mzee Liundi ni kwamba majina ya Tanganyika na Zanzibar yalipaswa kubaki ili kulinda uhalisia wa nchi zilizoungana. Kubadilisha jina la nchi hii ni makosa na wala hakuna maagizo hayo katika Makubaliano ya Muungano yaliyotoa ruhusa kubadili jina la asili la nchi hii.

 

1.33 Mwenye kusoma makala hii na hasa Mhe. Pinda wanapaswa kufahamu kwamba haya hayakufanywa kwa kubahatishwa ila kwa nia ya kuiua Zanzibar kwa kutumia kile alichokiita Prof. Mazrui “African Self –colonisation” na kuidhoofisha Zanzibar kwa makusudi.

 

1.34 Prof. Shivji kila mara huwa anatoa mfano wa mahusiano kati ya Tanganyika na Zanzibar kwenye Muungano huu kwa kutumia maneno mawili ya kizungu: “Creator and creature.”

 

The creator of the Union is the Peoples’ Republic of Zanzibar and The Republic of Tanganyika” Union is a creature and therefore it is the one that is to be discussed. In the present circumstances the creature has decided to sit with one of the creators and discusses the problems of the creature. This is an abnormality. “Muumba na Muumbwa wanakaa pamoja kujadili matatizo ya Muumbwa wake.”

 

Mzanzibari Kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano

 

1.35 Katika tabia ya kuonesha jeuri ya ukubwa dhidi ya Zanzibar ni kitendo cha Rais wa Tanzania, Mhe. Rais Mkapa, Rais mbabe, kuvunja utamaduni uliowekwa na Mwalimu mwenyewe. Tangu Mwalimu Nyerere alipoacha madaraka aliweka utamaduni kwamba katika uongozi wa Tanzania, na katika haja ya kulinda msingi ya kudumisha Muungano, kipindi kimoja cha uongozi wa kitaifa (Rais) atoke upande mmoja na kipindi kingine atoke upande wa pili wa Muungano.

 

1.36 Pamoja na makosa yake mengi juu ya Muungano, Mwalimu hili alilidumisha. Alilidumisha kwa kuficha hadaa ya kuonekana kama anaimeza Zanzibar, maana mzanzibari akichaguliwa kua Rais wa Tanzania bado wazanzibari wangejiona kwamba Muungano bado unawatambua. Hata kama lilikua na ubabaifu ndani yake lakini alipomaliza alimpisha Mhe Ali Hassan Mwinyi ingawa na yeye Mzee Mwinyi alijitambulisha kwamba ni mtu wa Tanganyika pale alipotangaza  uwanja wa Amani kuwa jina lake  la ukoo ni Nzasa. Jina hili ni jina la kijiji kimoja cha maeneo ya vijiji vilivyo karibu na Dar es Salaam. Alipomaliza Mzee wetu, mzee Ruhsa akachukua madaraka Rais mbabe Mstaafu Mhe. Mkapa aliefika hadi kutukomesha Wazanzibari juu ya jukwaa alipokua akihutubia pale skuli ya Lumumba mjini Unguja.

 

1.37 Lakini kwa kiburi kile kile cha kukosa nia njema Mhe Rais Mkapa akaamua bila kukubaliana na Zanzibar kwamba eti hakuna maandiko ya kikatiba au ya kisheria yanayosema hivyo.Ni ajabu yale yaliyomo kwenye katiba na maandiko ya Muungano wakubwa hawayafuati. Yale yaliyowekewa utaratibu wa kudumu yanajengewa hoja kwamba hayamo kwenye katiba.

           

Kuondolewa Wadhifa wa Makamo wa Rais

 

1.38 Dhamiri mbaya ya Mwalimu Nyerere ndiyo pia iliyozaa mpango wa kinafiki wa kufutwa kwa nafasi ya Rais wa Zanzibar kuwa  Makamo wa Rais wa Jamhuri ya  Mungano wa Tanganyika na Zanzibar. Dhamiri ya kuzaa fikra ya Mgombea Mwenza ni kumuondoa Makamo wa Rais ili Rais wa Zanzibar akose uwakilishi halali wa Zanzibar katika vyombo vyaMuungano na pia akose  uwezo wa kujitambilisha mbele ya Jumuia ya kimataifa kwamba yeye ni kiungo cha Muungano wa nchi mbili na hivyo kubaki na uwezo kuizungumza Zanzibar kimaendeleo nje ya Tanzania. Dhamiri ya mgombea Mwenza ni kuua nafasi ya Zanzibar kutafuta misada ya kiuchumi nje ya nchi. Hili nalo limetokana na kiburi hiki cha kujiona Tanganyika ndiyo Tanzania.

 

1.39 Mhe. Karume kama alivyoapishwa Dk. Salmin Amour ameapishwa kuwa waziri asiye wizara maalum. Huaje Rais wa nchi awe waziri wa Serikali nyingine. Huaje Rais wa nchi awe waziri wa Muungano bila kuwa mbunge kama alivyo Mhe.Karume? Mhe. Karume wala Mhe. Dk. Shein hawawakilishi Zanzibar katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya Muungano. Wao ni wajumbe wa Baraza hili kama Watanzania wengine, hawawezi kusimama kama wawakilishi wa Zanzibar ndani ya Baraza lile. Kama Chadema wangeshinda uchaguzi hapo 2005, basi mgombea mwenza wa Chadema angeweza kuwa Makamo wa Rais wa Tanzania ingawa si mzanzibari kama makubaliano 1964 yalivyo.

 

1.40 Matokeo yake ni kwamba Wazanzibari wamenyanganywa nafasi yao ya umakamo wa Rais na  pia wamekataliwa na kufutiwa uwezekano wa mzanzibari wa kua Rais wa Tanzania. Wazanzibari tukisema, majibu yake tunaambiwa walalamishi tunataka kuachwa. Hali hii ndiyo inayofanya Zanzibar isionekane kama ni nchi sawa na alivyotetea Mhe. Pinda.

 

1.41     Matokeo yake ni kwamba kuanzia sasa hakuna mzanzibari ambae ataweza kuchukua madaraka ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania maana  hakuna tafsiri sahihi wa nani Mtanzania na nani mzanzibari katika utaratibu wa madaraka ya urais na umakamo wa Rais ulivyowekwa hivi sasa. Hali iko hivyo hivyo katika mfumo wa Uongozi wa Chama cha Mapinduzi CCM.

 

1.42     Mwananchi ajifunze matokeo ya kesi ya Mama Ana Komu na Mgombea Mwenza wa Chadema Mhe Jumbe ambae baadae alifariki dunia kabla uchaguzi Mkuu wa 2005. Watu wawili hawa uwakilishi wao ulizua hoja kali ya jinsi uzanzibari wao ulivyotafsiriwa na Tume ya Uchaguzi ya Muungano.  Kwa tafsiri ya Tume, Mgombea Mwenza na au Rais anaweza akatoka bara hata kama haishi wala hakuzaliwa Zanzibar maana wanasema sheria  ya uchagzi juu ya mzanzibari  iko kimya. Jee ni kweli iko kimya au tangu ilipoandikwa iliandikwa kwa nia hiyo ya kubaki kimya ili baadae itumike kama ilivyotumika?

 

1.43     Baada ya miaka kumi suala hili litakua ni chanzo cha mgogoro, maana kutakua hakuna Muungano wenye pande mbili. Kiungo kikubwa kilikua nafasi ya Makamo wa Rais na au ubadilishanaji wa Urais (alternate presidency) kati ya Tanganyika na Zanzibar, ambayo yote mawili yameuliwa kwa ujanja kidogodogo. Vijana wa Mwalimu wameendeleza lengo lake taratibu kama mwenyewe alivyokua akifanya.

 

Mchango wa Zanzibar katika Shughuli za Muungano

 

2.1       Hoja hii nayo imeleta jeuri na kiburi kikubwa sana kwa upande wa Tanzania bara. Kama vile linavyoelezwa tatizo la uhaba wa wazanzibari, kutokuchangia kwa Zanzibar katika mfuko wa Muungano kunaonekana kuleta bugudha kubwa kwa wazanzibari.

 

2.2 Kama tulivyoonesha hapo juu kwamba wanaostahiki kulipia mchango huo ni Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyika ambayo imefanywa iwe haipo. Kwa bahati nzuri tena baada ya muda mrefu kupita mwaka 2004 Tume ya Pamoja ya fedha imeundwa ingawa haionekani kufanya kazi zake. Kumekua na hatua za kutayarisha ripoti ili kutoa picha halisi ya jinsi mchango wa Muungano uwe vipi. Inaonekana kamati hii nayo haiwezi kufanya kazi maana wakiwa wa kweli lazima suala la haki za Zanzibar katika Benki Kuu ya Tanzania na jinsi nchi mbili hizi zitakavyochangia Muungano litajitokeza tena na tena.

 

2.3 Mawazo kwamba ni upande wa bara tu ndio unaotoa fedha nyingi umeendelea kujenga uhasama usiokuwepo kwa upande wa Zanzibar. Ninashangaa kuona hata Marehemu Mwalimu  Nyerere hilo la upande wa bara kuchangia zaidi halipendi, ingawa alikubali na akakubali  kutoweka kwa Taifa  la Tanganyika ili alinde Tanganyika isilipe zaidi bali inufaike zaidi kuliko Zanzibar.

 

2.4 Kwa bahati nzuri umefanywa utafiti wa kina juu ya mambo gani hasa ni ya Muungano na yepi siyo ya Muungano. Kwa bahati nzuri mara baada ya kufukuzwa Mhe. Rais wa Zanzibar Aboud Jumbe, Mwalimu Nyerere aliteua Tume maalum kuchambua matatizo ya Muungano. Mmoja wa wajumbe hao kutoka Zanzibar nilikuwa mimi Juma Duni Haji pamoja na akina mzee Kazaura wakati huo akiwa katibu Mkuu fedha wa Serikali ya Muungano, Dk. Mujuni alikua katibu Mkuu mipango na pia alikuwemo Marehemu Prof. Kigoma Malima. Kwa upande wa Zanzibar alikuwemo Mhe marehemu Said Mugheiry, Marehemu Abdulla Juma Khatib, Mhe Muhamed Seif Khatib na Mhe. Muhammed Fakih.

 

2.5 Tulifanya kazi kubwa kuchambua masuala haya na kuwasilisha ripoti yetu kamati Kuu ya CCM lakini ikapigwa pute kwa sababu wanaojiita waume zetu hawakuipenda yaliyopendekezwa maana utafiti ule ulifichua kwa uwazi kabisa nini hasa mambo ya Muungano na nini ni mambo ya Tanganyika.

 

2.6 Badala ya kutatua matatizo ya michango ya pande mbili hizi za Muungano yaliyojitokeza ni kuchafuka kwa hali ya hewa, Mwalimu akaendelea kuwafukuza akina Maalim Seif Sharif na kundi lake kwa kutolewa nje ya Serikali na nje ya CCM. Mgogoro ukaendelea kupea kwa sababu tu wakubwa kuelezwa udhaifu wao.

 

Tume ya Fedha ya Muungano (Joint Financial Commission)

 

2.7. Hivi karibuni baada ya kuundwa Tume ya Fedha ya Muungano “Joint Finance Commission” kuna kampuni fulani ilipewa kazi kama ile tuliyoifanya mwaka 1984 na kufanya uchambuzi halisi wa mambo gani ya Muungano halisi na yepi ya Tanganyika na yepi ya Zanzibar. Baada ya orodha huo kupatikana watafiti wakatafuta matumizi halisi ya bajeti ya vifungu hivyo kwa muda wa kiasi ya miaka 10 iliyopita. Watafiti hao walikwenda mbali zaidi ya hapo na kukusanya mapato yote kwa kila kifungu cha mambo ya Muungano halisi. Mwishowe wakalinganisha, jee mapato yanakidhi matumizi au yanaupungufu?

 

2.8 Kwa mwaka wa fedha wa 2003/2004 matumizi halisi kwa vifungu vya Muungano ilikua shs.537,258.4 bilioni na mapato halisi kwa mwaka huo ilikuwa ni shs.1,030,826.1 bilioni. Tafauti ya vifungu hivyo vimetoa ziada ya Shilingi 593,569.5 bilioni kwa mwaka huo. Ziada hii haingizi mapato yanayotokana na misaada kutoka nje au mikopo. Mhe. Pinda na wenzake hawataki masuala haya yatambulike kwamba ziada hii hutumika kwa shughuli za Tanganyika au Tanzania bara na wala siyo Zanzibar.  

 

2.9 Ukweli umeonesha kwamba kumbe hakungekua haja yeyote ya SMZ au Serikali ya Tanganyika kulipia fedha za ziada kama wahusika watatunza na kuweka kumbukumbu sahihi za mapato na matumizi ya mambo ya Muungano hasa na siyo yale ya Tanganyika kuchanganywa na ya Muungano na kutumika kwa maslahi ya Tanganyika. Mambo yasiyokua ya Muungano ya Tanzania Bara yalipotengwa nje ya yale ya Muungano halisi gharama za mambo ya Muungano zimejidhihirisha wazi bila kujificha na kuonesha kwamba zinaweza kufidiwa na mapato ya mambo ya Muungano kikamilifu kama kulikua na nia njema.

 

2.10 Lakini hili limekua rahisi kwa kukubali ukweli kwamba kuna mafungu matatu ya matumizi katika Serikali zetu mbili. Mafungu hayo ni ya SMZ, ya Mambo ya Muungano na ya Mambo yasiyokuwa ya Muungano ya Tanzania bara (ya Tanganyika)

 

2.11 Ndiyo maana kwa miaka 15 sasa chama cha CUF kinaamini na kitaendelea kuamini kwamba ufumbuzi wa masuala ya Muungano ni rahisi kama kutakuwa na serikali tatu. Kwa nini CCM wanajificha chini ya Serikali 2 ni kwa sababu ya (African Self-colonisation) na kukosa nia njema ya kuweka mbele maslahi ya Tanganyika na Zanzibar badala ya kung’ang’ania maslahi kibinafsi ya Tanganyika.

 

2.12 Kuna viongozi wa CCM akiwemo Mwalimu Nyerere, ambao wamekuwa wakiitumia hoja ya hasara kuonekana kubwa kuendesha Serikali tatu kama ni moja ya sababu za kuepuka kuwepo kwa serikali hizo. Hoja hii ni dhaifu sana.

 

2.13 Wameshasahau kwamba wakati wa siasa za Chama kushika hatamu tulikuwa na mamlaka tatu zilizokua zikitumia fedha kwa ubadhirifu bila kuhojiwa. Kulikua Chama cha CCM kilichokua na Halmashauri Kuu ya taifa na vikao vyake vya mara kwa mara (sawa na Bunge). Chama hiki kilikuwa na Kamati Kuu (sawa na Baraza la Mawaziri) na kilikua na Scretariat iliyokuwa na mawaziri wake ambao huitwa wakuu wa Idara za Chama. Wakati ule chama kikitumia mfuko wa Serikali na wala hakuna mamlaka iliyokua na uwezo wa kukizuia au kukihoji. Mapesa mengi yaliyopotea kwa kupewa vyama vya ushirika na Shirika la Chama la Sukita ilikua ni wakati huu. Sikuwahi kusikia Mkaguzi Mkuu wa fedha za Serikali akisema wahusika wapelekwe Mahakamani kwa ubadhirifu. Badala yake waliokula na kuharibu fedha zile wakiitwa Dodoma na mambo yakaisha huko huko sawa na hali ya fedha za EPA, Richmond na Meremeta hivi sasa. Hoja ya ukubwa wa matumizi haiwezi kutetewa vilivyo.

           

Sio Serikali Mbili Nchi Moja, Bali Nchi Mbili Serikali Moja

 

2.14 Zaidi ya maelezo hayo, cha msingi ambacho hakisemwi ni kwamba hivi sasa Tanzania hakuna Serikali mbili bali ni Serikali moja yenye tawi lake visiwani Zanzibar chini ya Chama cha CCM. Serikali mbili zitakuwepo pale Serikali ya Zanzibar itakapokua ni ya chama kingine ambayo haitaweza kupokea amri zinazovunja maslahi ya nchi ya Zanzibar. Ni pale Rais wa Zanzibar atakapokua ni Makamo wa Rais wa Muungano mwenye kuwakilisha Wazanzibari katika Serikali ya Muungano na Bunge litakapokua halina mamlaka ya kufanya maamuzi juu ya kuwepo au kutokuwepo kwa Serikali hiyo ya Zanzibar.

 

2.15 Kuwepo kwa Serikali mbili hivi sasa ni kivuli cha kuwababaisha wale wasioelewa ukweli huo. Na ndiyo maana hivi karibuni jeuri za akina Shamhuna za kujigamba kwa Uzanzibari wao, Serikali ya Zanzibar imeshindwa kupitisha Azimio la Wazanzibari katika Baraza lao la Wawakilishi. Mhe. Spika Kificho na Mhe. Nahodha Waziri Kiongozi wamevunja taratibu za Baraza na kulinyima Baraza hilo kujadili hoja hiyo ya kutetea utaifa na utambulisho wetu. Watu wawili hawa kwa kushirikiana na Mwanasheria Mkuu Mhe. Idi Pandu Hassan wamewasaliti Wazanzibari kutokana na woga wa kukosa vyeo.

 

Dhamiri ya Mwalimu Nyerere ilikuwa nini? Ilikuwa ni kuunda Tanganyika mpya yenye jina jipya na mipaka mipya.

 

2.16 Sasa ukweli umedhihiri kwamba kilichokua kikifanyika kwa miaka yote ya Muungano na hata kabla hapo ni kujenga Tanganyika mpya yenye mipaka mipya na jina jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika. Hii ndiyo maana halisi ya maneno ya Mhe. Mizengo Pinda Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika “THE UNITED REPUBLIC OF TANGANYIKA!”

 

2.17 Kilichojidhihirisha ni kwamba viongozi wa Tanganyika ndio sababu ya kushindwa kupatikana ufumbuzi wa matatizo ya Muungano. Viongozi wanaoibeza Zanzibar hawajawahi kukatazwa, kufunguliwa kesi kubwa za kihaini, au kuchukuliwa hatua na CCM au Serikali ya Muungano. Dr. Salmin alipotaka kubadilisha katiba ya Zanzibar ili ajiongezee muda wa kubaki madarakani alichukuliwa hatua mara moja hata bila vikao vyovyote vya chama au Serikali kwa sababu angefanya hivyo kungeathiri maslahi ya Tanganyika.

 

2.18 Kila palipotokea dalili za kutaka maslahi ya Tanganyika kuharibiwa kwa Wazanzibari kuinua sauti kukosoa Muungano huo, papo hapo huchukuliwa hatua kwamba wanahatarisha Muungano. Kuhatarisha Muungano ni kueleza kwamba Makubaliano ya 1964 yanavunjwa, lakini wenye kuvunja hasa makubaliano, maisha wanalindwa. Kila siku zilivyopita mambo ya Muungano yanaengezwa dhidi ya Zanzibar. Ili uelewe hoja hii ni vyema nitoe mifano halisi ya kihistoria yanayothibitisha lengo la kuundwa Tanganyika mpya yenye jina jipya na mipaka mipya.

 

3.0       Kuanzishwa kwa Benki Kuu ya Tanzania

 

3.1       Benki kuu ya Tanzania iliundwa kwa sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya 1965. Kabla ya hapo nchi zote za Afrika Mashariki zilikuwa zikipata huduma za ki-Benki Kuu kutoka Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki “The East African Currency Board” ambayo ilikuwa na Makao yake makuu mjini Nairobi Kenya. Sarafu (currency) ya Afrika mashariki ndiyo iliyokuwa ikitumika kwenye nchi zote zilizokuwemo kwenye Bodi hiyo. Mbali ya Kenya, Tanganyika, Uganda na Zanzibar, Somalia na Aden (Yemen ya Kusini) nazo zilikuwa wanachama. Lakini kabla ya uhuru wa Tanganyika nchi hizo zilijitoa, zikasalia nchi nne (4) nilizotangulia kuzitaja. Kila nchi ilikuwa na mwakilishi wake kwenye Bodi hiyo kuangalia maslahi ya nchi yake.

 

3.2 Baada ya uhuru wa Tanganyika, katika mwaka 1961, ambao uliutangulia ule wa Uganda (1962), Kenya (1963) na Zanzibar (1963) kukawa na haja ya kufikiria muundo mpya wa Bodi kwani kabla ya hapo mtawala wa nchi hizo, Muingereza ndiye aliyekuwa akiendesha na kusimamia Bodi hiyo. Sera za mambo ya fedha na Uchumi (fiscal and monetary policies) za nchi hizo zililingana kwa kuwa mtawala alikuwa ni mmoja. Ndiyo maana kukawa na haja baada ya uhuru kufikiria vipi Bodi hiyo itaendeshwa kwani sera za nchi hizo changa zinaweza kutafautiana sana na hivyo kufanya mifumo ya kiuchumi nayo kutafautiana.

 

3.3 Tanganyika wao wakamuajiri Dr. Erwin Blumenthal wa Bundesbank ya Ujerumani kuwa mshauri wake juu ya mfuko mpya wa Bodi hiyo.  Wenzetu wa Uganda nao wakamuajiri bwana mmoja anaeitwa Newton kufanya kazi hiyo. Kenya na Zanzibar wao hawakuwahi kuajiri washauri wao. Dr. Erwin Bluementhal alipendekeza kuwepo kwa East African Central Bank ambayo iwe na State Banks kwenye miji mikuu yote ya nchi wanachama. Hivyo basi kungekuwa na State Bank ya Tanganyika, Kenya na Uganda na ya Zanzibar mbali na hiyo Central Bank ya Afrika Mashariki. Newton yeye alipendekeza kuwepo na Benki Kuu ya kila nchi. Wakati Watanganyika wanatafakhari mapendekezo ya Blumenthal, Uganda ikakubaliana na mapendekezo ya Newton, hivyo wakaanza utaratibu wao kuanzisha Benki Kuu yao. Kenya pia walifanya hivyo na Tanganyika nao wakaamua kuanzisha Benki Kuu ya Tanzania, BoT. Kwa mukhtasari hii ndio historia fupi ya Bodi ya sarafu ya Afrika Mashariki ilivyobadilika.

 

 • Kuchukuliwa kwa Rasilmali za Zanzibar kwa nguvu kinyume na Makubaliano ya Muungano ya 1964

 

3.4 Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki (EACB) iliendelea kutoa huduma huku wakisaidia uanzishwaji wa Benki Kuu ya kila nchi za Afrika Mashariki huku wahusika wakiendeleza utaratibu wa kuifunga Bodi hiyo. Mambo yalichanganyika pale Uhuru wa Zanzibar wa tarehe 10 Disemba 1963 ulipofuatiwa na Mapinduzi na baadae Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Zanzibar miezi mine tu iliyofuata. Hata hivyo Zanzibar iliendelea kuwa mjumbe kwenye Bodi hii na Tanganyika pia ilibaki kuwa mjumbe hata baada ya Muungano. Serikali ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar (kwa kuwa hapakuwepo na Serikali ya Tanganyika) ndiyo ikiiwakilisha Tanganyika.

 

3.5 Wakoloni waliokuwa wanaendesha Bodi hiyo pamoja na Watanganyika waliokuwemo kwenye Bodi hiyo akiwemo Mwenyekiti wa wakati huo wa Bodi hiyo ambae nae alikuwa Mtanganyika, hawakufurahi na kuendelea kuwepo kwa mjumbe wa Zanzibar. Kuitoa Zanzibar haikuwa tabu kwani hata Idara ya Sheria ya Jumuiya ya EACB walipania kusaidia mbinu za kuitimua Zanzibar itolewe kuwa mjumbe kama maelezo yafuatayo ya Katibu wa Bodi hiyo yalivyo kwenye kumbukumbu.

 

“Indeed it could be highly embarrassing as a measure likely to give further encouragement to the separatist elements on the island” (Inasema barua ya J.B. Loynes ya 1st June 1964 akiandika kumueleza muwakilishi wa Tanganyika.)

 

3.6 Kwa sababu suala la sarafu, mambo ya fedha na Mabenki hayakuwa mambo ya Muungano Waziri wa Fedha wa Tanganyika J.D. Namfua alijibu kwa EACB kwamba lazima muwakilishi wa Zanzibar aendelee kuwemo kwenye Bodi hiyo.

 

“As you will appreciate the Act of Union between Tanganyika and Zanzibar does not specifically transfer matters relating to currency to the Union Government, and pending any relevant modifications as may be agreed, the membership of Zanzibar in the Currency Board remains unaffected”. (Inasomeka barua ya J.D. Namfua ya 9th June 1964) akijibu barua kutoka kwa katibu wa Bodi hiyo alietaka kujua nafasi ya Zanzibar baada ya Muungano).

 

3.7 Baada ya barua hii Bwana Loynes mzungu wa kingereza alijitokeza wazi wazi kutopenda kwake kuiona Zanzibar kuendelea kubaki mjumbe wa Bodi hiyo na aliandika barua fupi kumwambia katibu wa Bodi hivi.

 

“We clearly do not want Zanzibar at our next meeting and I should hope that ways should be found of keeping them out. All I should like to do now is to remind you on this point so that no papers are sent across the water until we are clear where we stand”. (Inasomeka barua ya J.B Loynes 8th September 1964 akimuandikia Katibu wa EACB Bwana Hirst baada ya kuagizwa na Mwenyekiti wa Bodi)

 

3.8 Kwa hivyo baada ya hapo kilichobaki ilikua ni kubadilisha katiba ya muda ya Jamhuri ya Muungano ili iingize masuala ya fedha na mabenki kuwemo katika orodha ya mambo ya Muungano wakati uamuzi wa kutengwa Zanzibar kutoka EACB ulishachukuliwa zamani tangu 1964 hata Benki kuu yenyewe haijaanzishwa.

 

Fedha za Zanzibar Zaibiwa Kijanja (Makubaliano ya Muungano yachezewa tena)

 

3.9       Kazi ya kwanza ya Tanganyika ikawa kuingiza shughuli za matumizi ya sarafu ya Tanganyika na utawala wa mabenki ya Tanganyika kuwa ni shughuli za Muungano. Kwa kutumia katiba ya muda ya Muungano (1965), sheria Na 43 ya 1965 (1965 Act. No. 43 of 1965), Mwalimu alipeleka Bungeni marekebisho ya kifungu Na. 85 cha Katiba hiyo na kuongeza kifungu kidogo Na.XII cha orodha wa Makubaliano ya Muungano kinachohusu masuala ya fedha, mabenki, sarafu, fedha za kigeni na udhibiti wa fedha za kigeni kuwa katika orodha ya mambo ya Muungano kama inavyosemeka.

 

“The following matters are hereby reserved to the Parliament and Executive of the United Republic and declared Union matters: currency, coinage and legal tender (including paper money; banks (including saving banks) and banking; foreign exchange and exchange control; and subsection (1) of the section 68 of the Interim constitution is hereby amended by adding the said matters as a new item (xii) to the definition of “Union matters” therein.” (Interim Constitution 1965)

 

3.10     Gazeti la Serikali ya Muungano la tarehe 18 Juni 1965 ndilo lililotangaza kufanyika marekebisho hayo ambayo ni kinyume kabisa na makubaliano ya Muungano ya 1964. Baada ya kufanyika marekebisho hayo Mzee Mtei aliandika barua rasmi kwa katibu wa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki EACB na kumueleza kwamba kuanzia tarehe 29.12.1965 yeye ndiye atawakilisha Tanzania katika Bodi hiyo, jambo ambalo lilikuwa likisubiriwa sana na Bodi hiyo na kujadiliwa katika vikao jinsi ya kuitoa Zanzibar.

 

3.11     Pamoja na maelezo hayo bado Mzee Mtei alikubali kwamba haki na mgawanyo wa faida za Bodi hiyo ubaki kama ulivyokua na kwamba Zanzibar iendelee kupewa haki zake na faida yake kutoka Bodi kama zamani.  Baadhi ya maneno ya barua hiyo inasomeka hivi:

 

“ One of the effects of this Act is that I will represent the whole United Republic on the board, but as it was recognised at the meeting, this will not effect the reckoning of the distribution of profit or the purchase of treasury bills or other securities in respect of Zanzibar.”

 

 (Barua Ref. TYC.46/01/582 ya Mzee Mtei kwa Katibu wa Bodi ya 29th December 1965)

 

3.12     Kumbukumbu tulizokusanya zinaonesha mawasiliano marefu kati ya Dar Es Salaam na Nairobi  kujadili njia sahihi kisheria itakayoweza kuzichukua fedha za Zanzibar na kuziingiza katika Account za Tanganyika maana katibu na Mwenyekiti wa Bodi EACB hawakutosheka na barua ya Mzee Mtei kama  inaweza kuwalinda Bodi wasidaiwe baadae. Bodi ililazimika kuwapelekea Dar Es Salaam Rasimu (draft) ya barua ambayo ikipelekwa kwenye Bodi itawalinda Bodi baadae wasije kudaiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar baada ya kuungana (au wasije kudaiwa na Serikali ya Mapinduzi iliyokuwepo Zanzibar kabla kuungana na Tanganyika.)

 

3.13     Baada ya kukamilika kufanyika marekebisho haya ya katiba ya muda ya Jamhuri ya Muungano, Waziri wa Fedha wa wakati ule Mhe. Amir H. Jamal alimuandikia barua (Kumb.Na. TYC.46/01 ya tarehe 22 Machi, 1966) Mwenyekiti wa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na kumuagiza rasmi kwamba haki zote na amana zote (assets) za Zanzibar zilizokuwemo katika Bodi hiyo zipelekwe katika Benki Kuu chini ya Serikali ya Muungano na kwamba kuanzia pale ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania pekee ndiye tu ataeiwakilisha Tanzania katika Bodi hiyo. Haya yalifanyika baada ya kulazimisha kuingizwa kifungu Na .(xii) katika orodha ya mambo ya muungano ambacho hakikuwemo kabisa katika makuabaliano ya Muungano ya 1964. Baadhi ya maelezo ya barua ya Mhe. Amir  H. Jamal yanasomeka hivi:

 

“On behalf of  the Government of  United Republic of Tanzania (hereinafter referred to as “the Government”) I have to say that in view of sub-clause xi and sub-clause xii of the definition of  “Union matters” in section 85 of the Interim Constitution of Tanzania 1965 (No. 43 of  1965) barua inaendelea  —— (a) —-,

 

(b) all distributions of capital or profits made by the Board in respect of Tanzania including any share which but for the provisions of  the Interim Constitution, referred to above, would be payable direct to the  Executive for Zanzibar, are due and payable only to the Government

 

3.14     Huu ni wizi wa kalamu. Kwanza kuongezwa masuala ya fedha kuwa ya Muungano ni kosa la kisheria na kikatiba maana halingeweza kufanyika kwa idhini ya upande mmoja pekee. Lakini sababu ya pili ni kwamba Waziri wa fedha wa Serikali ya Muungano hakuwa na  wala hajawa “Waziri wa  fedha wa Muungano” na ndiyo maana hadi leo kuna Wizara za fedha mbili .

 

3.15     Wizara ya ulinzi au ya Mambo ya nje au ya Mambo ya ndani ni ya Muungano hasa maana hatuna Waziri wa Wizara hizo Zanzibar, lakini siyo ya fedha. Kwa hivyo si waziri wa fedha wa Tanganyika wala Gavana wa Benki Kuu angeweza kuamrisha chombo kinacho mahusiano ya kifedha na Serikali ya Zanzibar kwamba atoe amana za Zanzibar na kuzipeleka katika hazina ya Benki Kuu au hazina ya Muungano.

 

3.16 Kilichofanywa kuwa cha Muungano baada ya marekebisho ya katiba ya muda ni usimamizi wa taratibu na utoaji wa sarafu, na pili udhibiti wa mwenendo wa kubadilisha thamani ya shillingi ya Tanzania (currency and exchange rate control).

 

3.17 Tafsiri hii siyo maana yake kuchukua amana za Zanzibar. Maana huko EACB kulikua na amana za nchi nne, lakini wangereza walijua hazikua zao zilikua za Makaloni yake na ndiyo maana kila mmoja ya nchi hizo alipewa fedha (amana zake) baada ya kuvunjwa Bodi au baada ya kupata uhuru.

 

3.18 Kama kazi ya AECB ilikua ni kumiliki amana hizo basi waingereza wasingekuwa na sababu kuzigawa kwa makoloni husika baada ya kupata uhuru wake.  Barua ya Serikali ya kingereza wakati ikijitoa kwenye shughuli za kuisimamia EACB ilieleza wazi kwamba inakabidhi dhamana za uwakilishi wa Bodi  kwa Makatibu wakuu wa Wizara za fedha na siyo kwa Gavana wa Benki na barua hiyo ilitumwa na ikaagizwa kutangazwa rasmi katika magazeti ya Serikali (official Gazette) . Barua hiyo Ref. LEG/199 ya 13/9/1963 imepelekwa kwa makatibu wakuu fedha wa nchi zote tano, Kenye, Uganda, Tanganyika, Aden na Zanzibar baada ya Mwenyekiti wa Bodi hiyo kutoa Notice yake juu ya uamuzi wa waziri wa Makoloni wa Uingereza.

 

3.19 Kwa nini Serikali ya Muungano wakazichukua amana za Zanzibar na pia kuingiza kifungu katika sheria ya Benki Kuu kwamba haki na amana hizo zote ziwe za Benki Kuu. Huu ni ushahidi mwengine wa kukosa nia njema, na ni ushahidi unaothibitisha kwamba tangu awali dhamiri ni kufuta utaifa wa Zanzibar kihadaa.

 

3.20 Kama kulikuwa na nia nzuri, si ingekua vyema kwa Tanzania kuwa na wawakilishi wawili kwenye Bodi moja? Kwa nini iwe sisi wenyewe kwa wenyewe tunaojiita ndugu ndio tulofanya jitihada ya kuitoa Zanzibar na kuitaka Tanganyika ibaki peke yake kuiwakilisha Zanzibar wakati rasilmali fedha (assets) si Muungano?

 

3.21     Kulikuwa na mawasiliano makubwa kati ya Serikali ya Muungano na Bodi hii hata kufikia kufanikisha nia yao ya kuing’oa Zanzibar kwenye Bodi. Kuna wakati “Prospective Governor”(Mkuu wa Benki hiyo mtarajiwa) aliwasiliana na uongozi wa Bodi akiwashauri kikao kilichopangwa kufanyika Dar es Salaam, kihamishiwe mji mwengine kwa hofu kuwa Wazanzibari huenda wakapata taarifa kwa urahisi juu ya kikao chao hicho cha siri.

 

3.22     Bila kujua nini kikifanyika nyuma ya mgongo wake, Waziri Abdul AzizTwala ambae wakati huo wa 1964 ndiye aliyekuwa waziri wa fedha wa Zanzibar aliandika Barua nyingi kupinga hatua za Waziri Jamal za kuanzisha Benki Kuu bila kwanza kukubaliana juu ya mahusiano ya benki hiyo yatakavyokua na Serikali ya Zanzibar, hasa juu ya haki na amana (assets) za Zanzibar zilizokua katika EACB. Vikao mbali mbali vilifanyika kati ya Zanzibar na Dar es Salaam kujadili masuali hayo bila mafanikio.

 

3.23 Kwa sababu tayari uamuzi wa kuzichukua amana (assets) za Zanzibar ulishafanyika tangu 1964, kwa makusudi kabisa Waziri Jamal na Balozi Nsekela pamoja na Mzee Bomani wakatayarisha sheria ya Benki Kuu iliyoacha kwa makusudi kuyalinda maslahi ya Zanzibar. Sheria hiyo iliingiza kifungu kilichoshusha hadhi ya Serikali ya Zanzibar kuwa sawa na Baraza la Manispaa na pia kuingiza kifungu kwamba haki zote za Zanzibar zilizokuwa katika EACB zihamishiwe katika BOT bila Zanzibar kulipwa chochote.

 

3.24 Katika tafsiri ya neno Public Authority ya sheria hiyo (hapo 1966) limepewa maana kwamba “Public Authority means any political subdivision of the United Republic including the Executive for Zanzibar.” Maana ya maneno haya ni kwamba kwa Mzee Mtei na Marehemu Amir Jamal Serikali ya Zanzibar ni sawa na Serikali ya mtaa  au Baraza la Manispaa mbele ya Benki Kuu hiyo na hivyo hawana tena nafasi kama nchi au Serikali yenye mamlaka ya Kidola kama ilivyokua chini ya EACB.

 

3.25 Leo munaposikia Mhe. Pinda akisema Zanzibar si nchi maana yake ni hiyo kwamba Zanzibar ni sawa na Serikali ya mtaa tu. Kwa muda wote wa Muungano. Mwalimu na vijana wake wakijua wanalofanya. Wazanzibari tumesalitiwa na tukakubali kuhadaiwa na wale wanaojiita ndugu zetu bila kujua.

 

3.26 Hakuna mahala popote katika makubaliano ya Muungano panapotoa amri kwamba fedha za kigeni zichanganywe au zitakua za shirika. Hata baada ya kuandikwa Katiba ya Muungano ya kudumu bado fedha za kigeni ziliendelea kuwa ni za nchi mbili mbali mbali. Wapi walipata madaraka ya kuichukua amana ya fedha iliyomo EACB zichukuliwe na Tanganyika?

 

3.27 Maana kubadili katiba hakukutoa madaraka ya kumiliki mali za Zanzibar. Kilichofanyika ni kwamba kuanzia pale utawala wa fedha ni suala la pamoja na kwamba Zanzibar hawatakua na sarafu yake ya ndani wala ya kigeni kama vile ilivyo Marekani au Uingereza. Haikua na maana kwamba fedha za kigeni ni zetu shirika au zichanganywe. Fedha za Zanzibar zikaibiwa kimachomacho na baada ya hapo wizi huo ukahalalishwa kwa kuingiza kifungu katika sheria ya BoT kwamba mali zote za Zanzibar ziingie huko. Tunaposema hakuna nia njema ya Muungao huu, hivi ni baadhi ya vigezo vya ushahidi unaoonesha hadaa iliyofanyika tangu kuasisiwa Muungano huu.

 

3.28 Baada ya kukamilisha wizi wa kalamu, Waziri Jamal alimuandikia Waziri Twala juu ya maamuzi yake hayo siku moja tu baada ya kwisha kuiagiza EACB kuhamisha haki za Zanzibar kwenda BOT huku sasa akidhania kwamba ana nguvu za kusema suala hilo ni la Muungano.

 

3.29 Wakati anapoandaa rasimu ya kuongeza kifungu Na (xii) kupeleka Bungeni apate mabadiliko ya katiba Waziri Jamal aliacha kuwasiliana na Waziri Twala kwa sababu alikua hawezi kuchukua fedha za Zanzibar wakati hana kinga ambayo angeitumia kama kisingizo chake. Ndiyo maana barua ya kuhamisha fedha za Zanzibar kuingiza BOT iliyopelekwa EACB iliandikwa tarehe 22 March 1966 (Ref Na. TYC.46/01) na ile ya kujibiwa Mheshimiwa Twala ikaandikwa tarehe 23  March 1966 (Ref  Na. TYC.46/08/01).

 

3.30 Prof. Shivji anasema hatua zote zilizofanyika za kuhamisha fedha hizi hazikua hatua zenye uhalali wa kikatiba wala kisheria. Prof. Shivji anasema kwamba kuongeza kifungu cha 12 katika katiba ya muda ni kinyume na makubaliano kwa hivyo haikua halali kikatiba na hivyo hata sheria ya fedha za kigeni kutumika hadi Zanzibar pia si halali.(Shivji :2008)

 

3.31     Katika kufanya marekebisho haya ya kisaliti Mwalimu pengine kwa maksudi alitafuta safari ya nje akajiondoa ili ije ionekane kwamba Mzee Karume alikubali mabadiliko hayo maana aliyeweka saini yake kwenye sheria hiyo ya mabadiliko ni Mzee Karume. Huu ulikua ni mpango mahsusi wa usaliti na hadaa iliyokua ikifanywa na Mwalimu nyuma ya mgongo wa Rais mwenzake.

 

3.32 Pamoja na Mzee Karume kuweka saini, Prof. Shivji anasema saini hiyo haitowi uhalali wa jambo lenyewe maana tangu awali lilikua ni kinyume na makubaliano ya Muungano.

 

“Clearly therefore the list of the union matters could not be amended during the interim period and neither the President nor the Parliament had the power to do so. It could therefore be argued that the addition of item 12 on the list was in breach of Articles and Acts of Union and therefore invalid.

 

“None of these laws could be considered legitimate either.The Zanzibar side did not then or later accepted, by conduct or otherwise the twelth item or exchange control ordinance. The powers to extend relevant Tanganyika laws to Zanzibar were in respect of Union Matters only.” (Prof. Shivji 2008:140)

 

3.33     Kwa hivyo katika Benki Kuu ya Tanzania kuna mchango wa Serikali ya Zanzibar ambao kwa muda mrefu Serikali ya Zanzibar ilipokuwa ikidai ikipata hujuma eti inahatarisha Muungano. Si hivyo tu ila pia kumbu kumbu zinaonesha kwamba wakati wa kuanzisha Benki Kuu za kila nchi ulipofika, Bodi hii iliamua kutoa fungu kuzisaidia nchi hizo kuanzisha Benki Kuu zao. Tanganyika ilipewa Paundi za Kiingereza 668,884 sawa na Kenya na Uganda

 

3.34     Zanzibar kwa vile ilikua imeungana na Tanganyika haikupewa chochote wakati ule, kwani uongozi wa Bodi ya sarafu tayari ulishaambiwa kwamba Tanganyika ndiyo Tanzania kwa maelezo hayo hapo juu, uliona kuwa kutaanzishwa Benki Kuu moja, hivyo watoe mchango kwa Benki kuu moja ya Tanzania “by virtue of being partners in the Union”

 

3.35     Bahati njema Bodi ilipeleka Paundi za kiingereza 82,840 kama ni mchango wa Zanzibar katika uanzishwaji wa Benki Kuu ya Tanzania. Fedha hizo zilimezwa na Tanganyika na kuundwa Benki Kuu moja, The Bank of Tanzania (BOT) kwa mtaji wa Paundi za Kiingereza milioni moja wakati huo ikiwa ni sawa na Shilingi milioni ishirini (20,000,000) za Afrika Mashariki (East African Shillings) Kasoro ya kufikia pauni 1,000,000 ilijazwa na Serikali ya Muungano. Kwa urahisi zaidi tazama hesabu hizi chini:

 

 Mchango wa Serikali ya Tanganyika ni Pound za     Kingereza 668,884

 

Mchango wa Serikali ya Zanzibar ni Pauni za Kingereza 82,840

    Jumla ndogo (ST + SMZ) ni pauni 751.724 🙂

 

    82,840*100 /751,724  = 11.025%

 

    82,840 *100/668,884   = 12.388482%

 

           

3.36     Muda wote ule wa uhai wa EACB, Zanzibar ilikuwa ikipata si chini ya asilimia 12.40 (12.4 %) ya mgao wowote ule unaotolewa na Bodi kwa Tanganyika. Ukweli huu unathibitishwa kwa kuangalia mgao uliofanyika wakati zikigawiwa fedha za mwisho zilizobaki katika Account za Bodi hiyo kama zilivyooneshwa katika kumbu kumbu ya Bodi hiyo za (21st August 1972 zilizoandikwa na Mr. A.C.C.Roberts).

 

—–“Shs. 10,120,000 apportioned according to the Board’s distribution formula would be:-

 

            Accounts with Cenntral Bank of Kenya shs. 3,239,169

            Accounts with Bank of Uganda             shs. 3,239,169

            Accounts with Bank of Tanzania                       shs. 3,641,662

                                                                                    shs.10, 120,000

 

Fedha zilizopelekwa Benki Kuu ya Tanzania ziko tafauti na zile za Kenya na Uganda kwa (shs. 3,641,662 – 3,239,169 = 402,439). Fungu hili ni ziada kwa Benki            Kuu hii kwa sababu ni fedha za Zanzibar. Kima hiki ni sawa na asilimia:

 

 402,493*100 / 3,239,169 = 12.42581%

 402,493*100/3, 641662   = 11.0525 % 

 

Sawa na ile iliyotolewa kwa ajili ya kuanzisha Benki Kuu hapo juu.

 

3.37 Barua Ref. No.INV/EA/F/196 ya 21st March 1964 iliyoandikwa na H.R.Hirst kumpelekea Mr. J.H. Butter inathibitisha Formular iliyokua ikitumiwa kugawa faida na fursa za huduma za Bodi hiyo kwa nchi wanachama wote.

 

“It is stated in the 1961/62 Reports that the Board agreed a new formular for sharing of dstributable profits. The same formular is applied to fix the Government portions of the fiduciary issues and that Tanganyika,  Kenya and Uganda have been given  precisely equal shares.——My own view, therefore, is that it would probably do more harma than good to “hedge” on the percentages which  are of course 28.1/6 % each for Tanganyika, Uganda and Kenya. 12% for  Aden and 3 1/2 %  for Zanzibar.”

 

Kumbukumbu hizi ni sawa na kusema:

 

 

Kenya                          28.1667 %

Uganda                        28.1667 %

Tanganyika                   28.1667 %

Jumla                          84.5001 %         

Aden                            12. 0000

Jumla                          96.50001 %

Zanzibar                       3.50000 %

Jumla                          100.00000 %

 

Na ndio maana utaona kuwa hata kwenye mchango wa uanzishaji wa Benki Kuu ya Tanzania, Zanzibar ilipewa asilimia yake kwa mujibu wa Formular ya kugawana kati ya nchi hizo nne kuingizwa katika kuanzisha Benki hiyo. Mlinganio wa sehemu ya Zanzibar na ile ya Tanganyika ni 3.50/28.16667 ni sawa: 12.426%, sawa na mgao uliotolewa hapo juu wa sh. 10,120,000 za mwisho.

 

3.38 Amana za Zanzibar katika Benki Kuu, zipo si kwa sababu Zanzibar ni partner wa Muungano tu bali zipo amana zetu kama wana hisa wa Benki hiyo (shareholders).  Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania haikutaja kabisa kama Zanzibar ni mmoja ya wenye hisa wala haikutaja kwamba Tanganyika nayo ina hisa. Kinyume chake mwenye hisa 100% kwa sheria hiyo ni Serikali ya Muungano peke yake. Si Serikali ya Tanganyika wala Serikali ya Zanzibar ingawa sheria ile ikijua kwamba Tanzania maana yake Tanganyika kama nitavyonesha baadae.

 

3.39 Lakini kwa mujibu wa hesabu hizo hapo juu wenye hisa katika B.O.T ni watatu, Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano. Kila moja ikiwa na hisa zifuatazo:-

 

668,884 x 100 = 66.9% Hisa za Tanganyika

               1,000,000

 

82,840 x 100 = 8.3% Hisa za Zanzibar

      1,000,000

 

248,246 x 100 = 24.8% Hisa za Serikali ya Muungano (ST + SMZ)

        1,000,000

 

Kwa sababu katika hizi Paundi 248,264 asilimia 11.02 ni za Zanzibar basi, 11,02% x 248,246 = 27,356.71 ni za Zanzibar. Jumla ya fedha za Zanzibar katika uanzishwaji wa Benki Kuu ni 110,196.7 ambazo ni sawa na 110,196.7 x 100 / 1,000,000 = 11.02% kama ilivyochambuliwa hapo juu.

 

3.40 Pamoja na ukweli huo bado, Serikali ya Zanzibar haikutajwa kabisa kwenye sheria hiyo. Badala yake sheria ya Benki Kuu iliingiza kifungu ambacho kiliiteremsha hadhi Serikali ya Zanzibar kwa kuilinganisha kuwa sawa na Serikali ya Baraza la Manispaa.

 

3.41 Matokeo yake ni kama Serikali za mitaa zisivyoweza kukopeshwa na Benki Kuu, vivyo hivyo na Zanzibar nayo haikuweza kukopeshwa. Kama Serikali ya Zanzibar inahitaji kukopa, basi inabidi ifanye hivyo kupitia Serikali ya Muungano. Mtiririko wa mawasiliano na mijadala mikubwa kati ya Mhe. Waziri Twala na Amir Jamal inathibitisha wazi kwamba kulifanyika njama za makusudi kuuwa uchumi wa Zanzibar ili usiweze kujitegemea wenyewe. Huu ni usaliti dhidi ya Zanzibar

 

3.42 Hali hiyo ndiyo inayojitokeza hivi sasa na pamoja na madai mengi ya SMZ kutaka kufanyike mabadiliko ya sheria hiyo ya Benki Kuu lakini hakuna hatua yeyote iliyochukuliwa. Katika haja ya kuzibwa macho SMZ, Viongozi wa Serikali ya Muungano wamefanya ujanja wa kuiingiza kifungu ndani ya katiba kinachosema kuwe na Tume maalum ya fedha kushughulikia masuala ya Muungano. Hali imeachwa hivyo kwa makusudi kwa sababu wenzetu hawakuwa na nia njema tangu awali hapo 1965. 

 

3.43 Mtu anaweza kusimama na kauli kwamba Sheria ya Benki Kuu iliitambua Serikali ya Muungano pekeee kama mwenye hisa. Kwa nini Serikali ya Muungano ya Tanzania, baada ya kupokea “Divedends” (faida za Benki hiyo), wakiweka wao tu bila ya kugawana na Zanzibar, wakati wao ndiyo waliopokea fedha kutoka EACB, fungu la Tanganyika na la Zanzibar kuanzisha Benki hiyo?

 

3.44 Kwa miaka 31, Benki Kuu ya Tanzania ilikuwa ikitoa “Dididends” kwa Serikali ya Muungano bila ya Serikali ya Zanzibar kupewa chochote. Baada ya vita vya maneno na baadhi ya viongozi wa Zanzibar kutafsiriwa kwamba ni maadui wa Muungano na kutolewa kejeli kwa  wazanzibari kuonekana wasaliti wasokwisha kunung’nika, kwenye mwaka 1996, ndiyo IMF imependekeza eti SMZ ilipwe na Serikali ya Muungano 5% tu ya “ Dividends“ kuanzia mwaka huo.?  Sura hii inatoa picha ya wazi kwamba Benki hiyo wenyewe ni Watanganyika na kwamba Wazanzibari eti wanajipachika tu.

 

3.45 Hali ya ubishani wa aina hii umeshajitokeza tena hivi sasa juu ya suala la mafuta ambalo nalo liliingizwa kinyemela na matokeo yake kutoa tafsiri kama kwamba mafuta hayo ni ya Tanganyika.

 

3.46 Hali hii iko kwa kila taasisi ya Muungano. Na ndiyo maana nikasema kwamba hakuna nia njema, Sheria zote za Muungano zinatungwa kama kwamba ni za Tanganyika siyo za shirikisho na Zanzibar. Huu ndiyo udhaifu wa Muungano unaofichwa usisemwe. Huu ndiyo usaliti na hadaa za Mwalimu Nyerere dhidi ya Zanzibar. Mwalimu alifanya haya kwa sababu alikusudia kujenga Tanganyika mpya yenye jina jipya na mipaka mipya. Nina sababu ya kusema hivyo.

 

3.47     Hapo 1964 neno “Jamhuri” lilitafsiriwa kisheria kwa maana kwamba kila lilipo katika katiba ya Tanganyika lisomeke kwa maana ya “Jamhuri ya Muungano”. Lakini neno hili hili lilibadilishwa maana na kutakiwa litafsirike kila penye neno Jamhuri katika katiba na sheria zote zilizopitishwa baada ya Novemba 1972 lijulikane kwa maana yake mpya ambayo ni Jamhuri ya Tanganyika maana hiyo inajumlisha popote pale palipoandikwa Jamhuri ya Muungano. Katika sheria hiyo Na. 30 ya 1972 inasomeka hivi:

 

All acts and all Public documents made or issued before or after November 1972 “ The Republic means the Republic of  Tanganyika and including “United Republic” (Section 3 of the Interpretation of Laws and General Clauses Act 1972 (No. 30 1972)

 

 

 

 

Kwa mujibu wa sheria hii, Jamhuri tuliyonayo sasa si Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, bali ni Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika.

 

Jee tunakosa gani tukisema kwamba dhamiri halisi ilikua ni kuunda Tanganyika mpya yenye jina jipya na mipaka mipya. “The United Republic of Tanganyika”?

 

4.0       Daraja na Nafasi Halisi ya Serikali ya Zanzibar ilivyo hivi sasa

 

   4.1    Msomaji zingatia masuala yafuatayo na halafu uone daraja ya Zanzibar kama Serikali au nchi ikoje?

           

 • Serikali huwa na Jeshi la ulinzi na usalama. Jee Zanzibar inalo jeshi ukiacha Janjaweed ambao wanatumiwa chini ya maagizo ya watawala wetu kupiga ndugu zao?
 • Serikali huwa na bendera yake. Tumepewa bendera yenye kuonesha kwamba sisi ni himaya ya Tanganyika maana katika bendera yetu kuna bendera ya watawala wetu.
 • Na ndiyo maana Mhe. Kisumo mmoja ya wazee walioshiriki kuidhalilisha Zanzibar wakati wa Mwalimu Nyerere akathubutu kusema bendera ya Zanzibar haina tafauti na Bendera ya kilabu ya mpira. Angalia bendera kadhaa za nchi ambazo zina umoja wa shirikisho ya kweli. Mfano Ujerumani ina mataifa 16 (16 states). Kila moja kati ya hizo zina bendera yake tafauti na nyingine na tafauti na ile ya Taifa kubwa (Union).
 • Bendera ya SMZ ina tafauti gani na Bendera ya jeshi la Polisi, ambalo ni kikosi kimoja tu kati ya vikosi vingi vya Wizara ya mambo ya Ndani
 • Serikali huwa na sarafu yake. Tumenya’nganywa uwezo huo tangu 1965 na rasilmali fedha (assets) zetu kuchukuliwa           
 • Serikali huwa taifa pale wananchi wake wanapokua na uraia. Imedhihiri mwaka huu kwamba kumbe sisi ni wakaazi tu siyo raia tena wa Zanzibar. Mkaazi maana yake ni mgeni. Na ndiyo maana kipande chetu cha ukaazi kinamalizika 2010.
 • Serikali huwa na Polisi na masuala ya uhamiaji (citizenship). Zanzibar hatuna vyote.
 • Serikali huwa na uhusiano na nchi za Nje. Zanzibar hatuna na wala hatuthubutu kuwa nao. Kumbuka suala la OIC lilivyopingwa wakati lilikua ni halali na jinsi Rais wetu alivyodhalilika.
 • Serikali humiliki Benki Kuu. Zanzibar hatuna
 • Serikali huwa na madaraka ya kupitisha sheria za ushuru na kodi kwa faida ya maendeleo ya nchi yake. Zanzibar hata kodi inakusanywa na watawala na sisi kugemewa watakacho
 • Serikali humiliki eneo la anga lake na eneo lake la bahari. Vyote hivyo havipo kwa Zanzibar maana hata leseni za kutumia bahari sasa lazima ukakate Dar es Salaam.

 

4.2 Kwa hivyo ni wazi kwamba Zanzibar imepoteza kila sifa ya nguvu ya Serikali na kubaki bamba tupu kama anavyosema Prof. Shivji katika maandiko yake kwamba:

 

‘The addition and amendments to the reserved list discussed herein are repugnant to section (5) of the Act and articles of the Union. In a serious and fundamental way, they undermine the basic scheme of the Union provided in the orignal agreement. If such additions and amendments of the Union matters were held to be lawful, Zanzibar’s autonmy and the federal principle in which the association is rooted would be an empty shell.” (Shivji: Legal Foundation of the Union: 1990).

 

Prof. Shivji anachosema hapa ni kwamba kama maongezo ya mambo yasiyokua ya Muungano yataendelea kuongezwa kwenye orodha ya mambo ya Muungano ni kuvuruga kifungu Na (iv) cha Makubaliano ya Muungano na kufanya hivyo ni kuiacha Zanzibar kubaki gamba tupu la chaza. Ni nchi isiyo uwezo wowote wa kidola.

 

4.3 Wakati akihutubia Halmashauri ya taifa 1988, mkutano ambao ndio uliowafukuza akina Maalim Seif na wenzake Mwalimu Nyerere inasemekana alisema hivi:

 

Mtwara na Mwanza zilikua nchi mbili aliziunganisha Mjerumani kwa bunduki. Tanganyika na Zanzibar zilikua nchi mbili mbali mbali. Sisi tumeziunganisha kwa “kalamu.” (Mwalimu Nyerere 1988: Dodoma)

 

4.4 Suala la kujiuliza Sisi maana yake nani? Kwa Mwalimu, sisi maana yake wao Watanganyika wanaotetea visiwa vyao ambavyo wanaamini kwamba kama si kosa la Mjerumani kuvikabidhi visiwa hivyo kwa Muingereza hapo tarehe 1 Julai 1890, basi vingeliweza kuwa ni sehemu ya Tanganyika. Hicho ndicho alichokuwa akikipigania Mwalimu katika uhai wake wote na sasa ndicho kinachoendelezwa na warithi wake. Na ndiyo maana Mwalimu anasema hivi katika kitabu chake cha Uongozi na Hatima ya Tanzania:

 

“Pwani ya Tanganyika na Zanzibar ya sasa zilikua pamoja kwa muda mrefu sana kabla ya kutengwa na Wakoloni Waingereza na Wajerumani. Kama zingebaki zimetengana kwa “Wazalendo” hao hiyo, ingekuwa ni halali maana zilitengwa kwa hila na mitutu ya bunduki za mabwana. Lakini uamuzi wa Tanganyika huru na Zanzibar huru kuungana na hivyo kuwaunganisha tena ndugu waliokuwa wametengwa na Mabeberu, tendo hilo kuna viongozi wetu wanaosema kuwa halikua halali.”(Mwalimu Nyerere: 1994:58)

 

4.5 Mwalimu akiamini hivyo kwamba ni makosa kwa Zanzibar kubaki kama nchi. Lakini Mwalimu huyu anakubali mipaka ya nchi nyingine ibaki kama ilivyoachwa na wakoloni kama alivyoshauri katika kikao kimojawapo cha OAU huko Addis- Ababa mwaka 1963. Hivyo kosa ni Zanzibar tu?  Mwalimu akijua kwamba Zanzibar ilikua Dola kubwa hata kabla Taifa la Tanganyika halijakuwepo. Kwa nini Utaifa wa Zanzibar hautakiwi, au kwa sababu ya kuwa ni visiwa jirani na Tanganyika?

 

4.6 Wewe msomaji unaweza kuzinduka kwamba Uingereza ni taifa kubwa lakini ni visiwa vilivyo karibu na fukwe za magharibi ya bara la Ulaya, lakini sijawahipo kusikia wajarumani au wafaransa kusema kwamba kwa sababu visiwa hivyo vipo karibu na fukwe la nchi zao basi visiwa hivyo ni vyao.

 

4.7 Japan ni Taifa kubwa sana, na ni visiwa viliopo karibu na pwani ya fukwe za Korea. Sijawahipo kusikia wakorea wakidai visiwa vyao. Singapore ni karibu sana na fukwe za Malaysia, lakini sijawahipo kusikia Malasia ikidai kisiwa chao. Kwa hapa Afrika, Mauritius ni kisiwa kidogo kuliko hata Unguja pekee, ni nchi kamili. Pamoja na kwamba kipo karibu na Madagaska bado Madagaska hawajakinyakua. 

 

4.8       Kosa la Zanzibar ni kuwa karibu sana na fukwe za Tanganyika na kwa tafsiri ya Mwalimu lazima visiwa hivyo viwe vya Tanganyika! Huu ndiyo udhaifu wa mgogoro wa Muungano, tangu awali malengo ya Muungano siyo yale yaliyomo kwenye maandishi ya makubaliano. Maandishi ni babaisha toto.

 

4.9       Na ndiyo maana Mhe. Aboud Jumbe anasema ni mara moja tu wakati wa kupitisha Makubaliano ya Muungano hapo Dar es Salaam kwenye Bunge la Tanganyika ndipo  Mwalimu aliwahi kumwita Mzee Karume kama Rais wa Zanzibar  

 

“This is one of the rare occasions when Nyerere spoke to Karume as an equal partner. President of Tanganyika speaking of or speaking to the President of Zanzibar, both of them enjoying the same status (as Presidents). From then on except in the incident quoted above it was the Union President meeting or talking to his Vice president be it on Union matters or non- Union matters. The President of Zanzibar never again met his counterpart to discuss non- Union matters which were finally absorbed unconstitutionaly by Union Government into Union matters. Surely Nyerere must have known what he wanted all the time in the light of what followed after wards”. (“The Partnership”: by Jumbe: 1994:14)

 

Maelezo haya yanathibisha kwamba Mwalimu alitusaliti Wazanzibari. Imani aliyopewa na Mzee Karume aliitumia kuua utaifa na kuua kuwepo kwa nchi inayoitwa Zanzibar.

           

 5.0 Wazanzibari Nawauliza, Lipi la Kujivunia?

 

5.1 Kwa miaka 50 sasa tangu tukiwemo Serikalini, tumekua tukilisema hili. Kwenye majukwaa tumekua tukieleza kwamba wenzetu wanajua wanachofanya. Wanalengo la muda mrefu taratibu wamefanya yafuatayo huku baadhi yetu tukishangilia na kutetea,

 

 • 1964 walichukua nguvu zetu za utaifa na udola (uraia,ulinzi, mambo ya nje,)
 • Wakachukua uwezo wetu wa kiuchumi (sheria za forodha na za             biashara, sheria za fedha, mahusiiano na nchi za nje, misaada na mikopo)
 • 1977 wakahakikisha kwamba hatuna chama cha watu cha kutetea         maslahi yetu (ASP). CCM ni TANU iliyobatizwa jina kama vile Tanganyika ilivyobatizwa na kuitwa Tanzania Bara.
 • Mwishowe wameingia hata katika utamaduni wetu.

 

5.2 Na ndiyo maana si makosa kutafsiri kwamba Mwalimu alilenga kuanzisha Tanganyika mpya, yenye mipaka mipya na jina jipya, Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika.

 

Prof. Shivji anasema kwamba, kwa sababu katiba ya Tanganyika ilifanyiwa marekebisho ili iweze kutumika kwa Mambo ya Muungano ambayo yalijumlisha shughuli zilizokua za Serikali ya Zanzibar, imezaa mawazo yasiyo shaka kwamba Mwalimu kama kwamba alijiandaa kabla ya Muungano azichukue shughuli hizo.

 

           

“…the fact that the constitution of Tanganyika was amended to accomodate the Union and the laws of Tanganyika on union matters were extended to Zanzibar creates the perception that the framework of Tanganyika, by another name.” (Shivji: 2008:98)

 

Maelezo haya ya Prof. Shivji yanapata nguvu pale msomaji atapoelewa kwamba kumbukumbu za kijasusi za kiingereza zilizopatikana  mwaka 1959 zinaeleza kwamba katika kikao cha siri cha kutatua mzozo wa chama cha ASP juu ya kushirikiana kwa chama hicho na ZNP ili kudai uhuru kwa pamoja, Mzee Karume alilazimika kutoa barua iliyotoka kwa Mwalimu Nyerereili kuthibitisha kwa wenzake kwamba hata kama wangeshirikiana na ZNP, chama cha ASP kilikua na kinga ya Tanganyika na chama cha TANU (Tanganyika African National Union). Ripoti hiyo ya siri za kijasusi kutoka kwa waingereza zinaeleza, pamoja na mambo mengine, kwamba barua ile ya Mwalimu ilikua na maagizo ya kuziunganisha nchi mbili hizi mara tu zitakapo pata uhuru. Moja ya kifungu hicho kinasomeka ifuatavyo:

 

“Until Abeid Karume produced to the meeting a document signed by Julius Nyerere and purpotedly to be a statement of TANU policy. It is said to confirm that the two territories would be joined together in one African Republic. The document ended by requesting the signature of Abeid Karume and Othman Sharif if the policy was accepted and both signed.” (A.Babu:1996)

 

 Maneno ya aina hii yanathibitishwa tena na Mwalimu Nyerere pale aliposema mwaka wa 1965 wakati akilihutubia Taifa kutoa  salamu zake za mwaka kwamba “hata kama ASP ingepata Serikali kwa njia ya kikatiba na siyo kwa njia ya kufanya Mapinduzi, Muungano ungelikuepo tu!” (Wanaandika Duggan na Civille, 1976).

 

5.3 Na ndiyo maana mimi naamini kwamba Tanganyika mpya yenye jina jipya na mipaka mipya iliandaliwa kuwepo hata kabla Muungano. Kulitumika kila njia kutekeleza azma hiyo, katiba ya bandia, sheria potofu, vitisho na hata kufukuza viongozi wa Zanzibar kama wanavyosema wataalam wa fani ya migogoro ya shirikisho hapa chini.

 

5.4 Kwa mujibu wa McGarry na O’Leary wataalam wa masuala ya migogoro inayotokana na Serikali za Shirikisho, wameeleza kwamba shirikisho lolote lile la nchi mbili zilizotokana na siasa za chama kimoja huishia kuvunjika kutokana na tabia zake za aina tano; 

 

 • Coercision to come together
 • Authoritarianism to stay together
 • Maltreatment of the smaller partner
 • Distribution conflicts (Economics policies)
 • Centralising processes

 

5.5       Tafsiri ya vipengele hivi ni:

 

 • Shirikisho hilo kuanza kwake limelazimishwa
 • Kuwepo kwake huendelea kulazimishwa
 • Taifa dogo huonewa na kutishwa ili waogope kudai haki zao
 • Taifa dogo hunyimwa maslahi ya kiuchumi ya shirikisho hilo
 • Kila mara taifa dogo huendelea kupunguzwa nguvu zake na kuhamishiwa kwa taifa kubwa

 

5.6       Uchambuzi wa makala haya unathibitisha nadharia ya wataalam hawa kwa kila hali.

 

 • Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kuanza kwake kumelazimishwa, kuwepo kwake kunalazimishwa
 • Zanzibar imekua ikionewa na watu wake kupigwa kwa mabomu na kufukuziwa viongozi wake ili waogope
 • Maslahi yake ya kiuchumi yanaporwa kwa nguvu na ujanja kwa kutumia nyaraka batili na hatimae
 • Kila siku zilivyopita nguvu zake za kiutawala na kidola zimekua zikipunguzwa chini ya    kivuli cha kuimarisha Muungano.

 

5.7 Huu ni utabiri wa wataalamu ambao unaweza ukatokea kwa Tanzania kama vile ulivyoweza kutokea kwa Muungano wa Misri na Libya, Gambia na Senegal na hata Taifa kubwa la Urusi lilisambaratika kutokana na mfumo huo.

           

Jamhuri ya Muungano wa Afrika PAN-AFRICANISM (Uafrika)

 

5.8 Moja kati ya misingi ya kujenga umoja wa Africa (Pan-Fricanism) ni kuepuka mataifa ya Afrika yasilazimishwe katika kujiunga huko. Inasemekana kwamba sababu iliyomfanya Mwalimu Nyerere aitambue Biafra ilipotaka kujitenga kutoka Nigeria, ni kulitetea jimbo hilo lisilazimishwe kubaki ndani ya shirikisho la Nigeria kwa kutumia nguvu za kijeshi. Msingi huu Mwalimu alikua hautaki kwa Zanzibar na hata pale njia ya Dimokrasia na Kikatiba ilipotokea kila mara alitumia nguvu za Chama kushika khatamu kuzuia hilo lisitokee kwa  kutufukuzia viongozi wa Zanzibar pale alipotangaza propaganda ya kuchafuka kwa hali ya hewa na akamfkuza Rais wa Zanzibar aliyechaguliwa na wananchi wa Zanzibar. G55 walidai Serikali yao ya Tanganyika, lakini hawakufukuzwa chamani na wala hawakupewa adabu kwa kutaka hilo, ingawa  uamuzi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ulivunjwa  kwa amri yake.

 

5.9 Mimi siioni tafauti ya yale yaliyotokea Nigeria kutumia Jeshi na lile la kumlazimisha Mzee Jumbe kujiuzulu. Mote muwili zimetumika nguvu. Katika siasa za Tanganyika na Zanzibar Mwalimu alikosa kusimama na kutembea katika maneno yake. Akitumia hadaa na nguvu zaidi kuliko uadilifu aliokuwa akisifiwa kuwa nao.

 

5.10.    Nilishaeleza kwa urefu huko nyuma kwamba Wazanzibari, tumepoteza nguvu za nchi yetu katika maeneo yote yanayofanya tuitwe nchi iliyo huru. Naomba nirudie tena:

           

 • Kwanza tulisalimisha kwa Tanganyika uraia wetu, nguvu za kijeshi na utambulisho wa kwamba sisi ni Taifa (Sovereignty)
 • Tukazisamilisha nguvu zetu za kiuchumi, kwa kupoteza uwezo wa kutunga sheria za kodi huku tukielewa kwamba uchumi wa visiwa ni uchumi wa kibiashara wa kuuza na kununua (Import and export trade). Kuletwa kwa Mamlaka ya Tanzania Revenue Authority ilikua ni kuweka msumari wa mwisho katika sanduku la maiti
 • Tukalazimishwa kutoa uwezo wetu wa kuwa na sarafu yetu na  umiliki wa Benki Kuu
 • Hapo 1977 tukakabidhi sauti ya umma, nguvu zetu za kisiasa kwa kukubali kukiua chama chetu cha Afro-shirazi Party (ASP)
 • Na hatimae kuvurugika kwa utamaduni wa Zanzibar na hadhi yake.

 

Ndiyo maana naendelea kuuliza baada ya miaka 47 ya Muungano, Wazanzibari tuna kipi cha kujivunia?

 

6.0 Nini Kifanyike?

 

6.1 La msingi kuliko yote ni kukubali kwanza kwamba sisi vizazi vya Zanzibar viliopo leo hatuwezi kuhukumiwa kwa makosa yaliyofanywa na watawala wa Zanzibar wa miaka 1850 mpaka 1963. Kututia adabu Wazanzibari wa leo ni kufanya makosa yale yale yaliyofanywa na warabu waliotawala wakati huo, kama kweli walifanya hivyo inavyoelezwa,

 

6.2 Na kama babu zetu hayo waliyaona ni mateso na wakapambana nayo, walifanya hivyo ili sisi kizazi cha leo tuishi maisha ya uhuru ya heshima na ya umoja.  Hilo limekosekana Zanzibar kwa miaka 47 sasa baada ya kuingia kidudu mtu mwenye dhamiri potofu ya waafrika kuwatesa waafrika kwa kutumia kivuli cha Muungano.

 

6.3       Kwa hivyo kilicho muhimu ni Nia Njema na hivyo:

           

Lazima viongozi tubadili utamaduni na kuona kwamba Muungano huu si wa mtawala na matawaliwa au wa mkubwa na mdodogo. Sisi ni nchi mbili huru zilizokubali kupunguza baadhi ya madaraka ya Serikali zake kwa faida ya umoja huo.

 

Kuzingatia kwa moyo safi malalamiko ya muda mrefu ya pande zote mbili na kuyatafutia ufumbuzi

 

6.4 Njia sahihi na ya kidemokrasia ni kuupitia tena Mkataba wa Muungano kwa nia ya kuuimarisha na siyo kuudhofisha upande mmoja kwa faida ya mshiriki mwenzake.

 

Ijulikane wazi kwamba mjadala wa matatizo ya Muungano si wa wengi dhidi ya wachache. Ni mjadala wa wawakilishi wa Zanzibar na wa Tanganyika. Muungano ndiyo unaojadiliwa na hivyo viongozi wa Tanganyika ambao kwa sasa ndio wanatawala Serikali ya Muungano  wasijikweze na kuona wao  wapo juu  ya wale wa Zanzibar. It is the creators that are disccusing the problems of the creature. United Republic of Tanganyika and Zanzibar is a creature!

.

6.5 Zanzibar na Tanganyika ziheshimiane. Karne ya 21 hakuna aliye tayari kutawaliwa kwa nguvu. Vinginevyo Muungao huu hivi ulivyo mimi sioni la kujivunia, wewe jee? Karne ya 21 ni karne ya Mabadiliko, Wazanzibari tutoke hapa na kauli mbiu ya kuleta mabadiliko.

           

Hoja kuu ni kwamba tujitambue kwamba tunaweza kubadili hali iliyopo. Hoja ya pili ni kwamba tuwe majasiri kwa maneno na vitendo kubadili haja hio ya mabadiliko. Hoja ya tatu ni kwamba tuazimie kwamba 2010 zanzibar hakuna uchaguzi wa CCM na CUF bali ni uchaguzi wa kujikomboa ili tupate heshima na kuheshimiwa. Yote haya yatawezekana ikiwa kauli yetu ni moja nayo ni “Sisi ni Wazanzibari.”

 

7.0 HITIMISHO

 

 • Clean Politics Better Governance (Siasa Safi ni Uongozi Bora)

 

7.1 Dhamiri ya waraka huu mfupi ni kuwaelezea watakaousoma kwamba kama kuna nia njema ya kisiasa mgogoro wa Muungano ni mwepesi mno na wala hautaki miujiza yatoke kutoka mbinguni au kwa wazungu.

 

7.2 Zaidi nilikusudia kuwaeleza wale wenye kutukejeli kama Mhe Husein Siyovelwa na sasa Mhe Pinda kwamba sisi tunadai utambulisho wetu uheshimiwe. Sisi ni Wazanzibari twenye nchi yetu kama watanganyika wanavyo nchi yao inayoitwa Tanganyika. Kama walivyodai haki watanganyika kutoka kwa waingereza, na sisi tunadai haki za Wazanzibari kutoka kwa wale wanaojigamba kwamba ni ndugu zetu. Kuungana kwetu hakufanyi tupoteze utaifa wetu na kamwe hatuko tayari kuupoteza, maana huo ndio utambulisho wetu tuliopewa na Muungu

 

7.3 Kila mara ninapopata nafasi hua natoa mfano hai wa Afrika ya Kusini, kwamba kilichofanya Afrika ya kusini itoke katika mapambano ya wenyewe kwa wenyewe ni viongozi waliokuwa na khatamu za Dola (yaani De’Clerk) kuheshimu na kutekeleza makubaliano yake na African National Congress (ANC). Angeweza kabisa De’Clerk kudharau makubaliano kama alivyofanya Mwalimu kwa sababu De’Clerk nae alikua na kila uwezo wa kudharau.

 

 7.4 Nani haelewi kwamba Afrika ya Kusini ina uwezo mkubwa sana kijeshi lakini mbona De’Clerk hakuzitumia nguvu hizo. Hakufanya hivyo kwa sababu alikuwa ana Nia Njema. Alijua kwamba lenye faida kwa wazungu ndilo lenye faida kwa waafrika walio wengi. Huyu ndiye aliyejua maana ya maslahi ya taifa, siyo Mwalimu aliyetusaliti wazanzibari na kutuhadaa chini ya kivuli cha Muungano.

 

7.5 Mfano mwengine wa kuigwa ni ule wa nchi ya Bakinafaso nchi ambayo mara tu baada ya uhuru ilikumbwa na Mapinduzi ya kijeshi mara 5. Baada ya miaka 10 ya mfumo wa vyama vingi kiongozi wa nchi hiyo aligundua kwamba chama chake kilikuwa kina wabunge wengi mno kuliko vyama vya upinzani na hivyo kuwanyima wananchi wake nafasi ya kutetea maslahi yao katika chombo chao. Kati ya viti 111 vya Bunge chama tawala kilikuwa na wabunge 104 na kuacha viti 7 tu vya wapinzani.

 

7.6 Katika kumchagua Rais chama hicho kikipata si chini ya 76% ya kura zote za urais. Rais Kampaore hakujisifu kushinda kwa kishindo cha Sunami.

 

7.7 Rais Blaisse Compaore, baada ya kuruhusu mjadala wa kitaifa juu ya udhaifu huu alifanya mabadiliko makubwa ya mfumo wa Tume ya uchaguzi kwa kuwashirikisha wadau wote, na kubadilisha utaratibu mzima wa kupiga kura. Kuanzia uchaguzi wa 1998, chama tawala kilibaki na 51% ya kura za Rais na viti 57 vya Bunge na kuwaachia  asilimia 49 za kura na viti 54 katika Bunge  wapinzani. Haya yaliwezekana kwa sababu Rais alikua na nia njema.

 

7.8 Matatizo ya viongozi wa nchi nyingi za Kiafrika ni ukosefu wa Nia Njema. Kwa sababu ya ukosefu huo hata sheria ambazo wamezitunga wenyewe na hazina matatizo yeyote kiutekelezaji, basi wahusika wanashindwa kuzitekeleza. Kutekeleza sheria au ahadi hakuhitaji msaada kutoka nje au mshauri kutoka Benki ya Dunia. Tume za Uchaguzi wanaziteuwa wao, sheria za uchaguzi wanazitunga wao, lakini Tume hizo hazitekelezi mchakato wa uchaguzi kwa kufuata sheria hizo. Matokeo yake vurugu, muda na rasilmali nyingi zinatumika kwa viongozi hao kwenda huku na kule kutafuta suluhu ya matatizo yaliyotayarishwa na wao wenyewe.

 

 • Ukombozi wa Afrika Umekwenda Kombo!

 

7.9 Ukombozi wa bara la Afrika baada ya kuwasaidia Waafrika imekua balaa kwao. Maana mbali na kushamiri kwa nchi moja kuitawala nyingine na kuzaa ukoloni mpya, lakini hata kuuwawa kwa wafrika tumeacha kukuonea aibu na hivyo tunashindwa kulani wanaofanya hivyo. Hali ya mauaji na mateso yaliyofanyika Msumbiji kwa miaka 18, hakukuwashtuwa waliopigania uhuru wa nchi hiyo wala Jumuia ya Umoja wa Afrika. Mateso na madhila ya njaa yanayowapata watu wa Zimbabwe ni makubwa sana, lakini bado Mzee Mugabe alikaribishwa na kuachwa kutamba katika vikao vya Umoja huo eti kwa sababu anawapinga waingereza na wamarekani. Eti tunamuona shujaa kwa sababu kathubutu kuwapinga wazungu.  Hivyo shujaa ni yule anaelinda uhuru wa nchi yake kwa kuwanyanga’nya mashamba wazungu kwa gharama ya kuuwa raia wa nchi yake?

           

7.10 Kwa Waafrika eti hiyo ndiyo tafsiri ya ukombozi.  Uchaguzi unafanyika Rais aliyeko madarakani wananchi wanamkataa kwa sababu ya kuchoka na mateso na shida za njaa. Mauaji yale na shida za wananchi wale, viongozi wa kiafrika hawakuyaonea aibu na hakuna kiongozi hata mmoja aliesimama kuwapa pole waliopata maafa hayo si Rais Robert Mugabe mwenyewe wala Morgan Tsvangirai, wala Mwenyekiti wa Umoja wa Jumuia ya Nchi za Afrika, Rais Kikwete. 

 

7.11 Eti suluhisho la mauaji yale ni serikali ya kulazimisha, aliyeshindwa kubaki madarakani na aliyeshinda kugaiwa Uwaziri Mkuu. Kila mmoja na baraza lake la mawaziri.  Eti hiyo ndiyo Falsafa ya viongozi wa Afrika Kutatua tatizo la Kiafrika kwa njia ya Kiafrika. Eti hii ndiyo “African Solution to African Problems”. Udhaifu huu mimi nauita “African hopelessness to African helplessness.” Upumbavu wa waafrika ulioshindwa kuwasaidia.

 

7.12. Jee katika hali hiyo ya Afrika wazanzibari tuna mategemeo gani ya kupata msaada wa mgogoro wetu na Tanganyika kutoka viongozi wa Kiafrika na wale wa Ulimwengu? Jee kweli Wazanzibari tuna la kujivunia katika Muungano huu?

 

Nawashukuru huku nikiendelea kutamka kwamba Sisi ni Wanzanzibari. Uzanzibari ndio utambulisho wetu. Sisi hatuna kabila wala hatuna lugha nyingine zaidi ya Kiswahili.  Khatima ya nchi yetu imo mikononi mwetu. Tutambue na tujitambue hivyo. Tuwe majasiri kwa kusema na kwa kutenda na kwamba 2010 ni uchaguzi wa mabadiliko utakaowaunganisha Wazanzibari katika Taifa lao lenye heshima na kuheshimiwa na wale waliotayari kutuheshimu kama taifa kamili, kwa sababu Zanzibar ni nchi na itabaki kuwa nchi.

 

 

MAREJEO:

 

Seminar on NEC Proposals for  amendments to the Union and Zanzibar Constitutions, A paper    commenting on part iv –  “The Consolidation of the Union” to be discussed on the 28th July, 1983: By Wolf Dourado.

 

A professional Inaugural lecture on “The constitution of the United Republic of Tanzania 1977 – Some Riddles “; University of Dar es salaam, Faculty of Law: By B. P. Srivastava.

 

Tathmini ya mafanikio, matatizo na changamoto zinazokabili mfumo wa Demokrasia ya vyama vingi, Tanzania; Mazingira ya Kisheria: By Jaji Augustino S. L. Ramadhani.

 

Ujumbe umeeleweka kwamba Tanzania ni yetu sote: By Juma Duni Haji

 

Report of a study on Inter-governmental fiscal relations between the Government  of the United Republic of Tanzania and the Revolutionary Government of Zanzibar, White Sands Hotel Dar es    salaam 25th April, 2006: By W. H. Shellukindo.

 

100th anniversary of the Heligoland-Zanzibar Treaty: By Annette Bleckmann.

 

Joint Accord/ MNF National Dialogue on Constitutional Development in Tanzania; Contemporary Constitutional Issues in Tanzania at the Golden Tulip Hotel, Dar es salaam, 10th  to 14th  December, 2002: By George B. Liundi. Panel Discussion on the Union of Tanganyika and Zanzibar: Need for fresh start?;

 

Review and Monitoring Committee of Redet at University of Dar es salaam,

20th May,2004: By Juma Duni Haji.

 

 Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.Bill of an Act to provide for the      Establishment, Constitution and Functions of the Bank of  Tanzania  …. Received together with a letter from the Treasury of the United Republic, dated 10th November, 1965.

 

Letter from Minister of Finance (Zanzibar) Abdulaziz Twala to Minister of Finance (Dar es salaam) P. Bomani of 12th August, 1965 .

 

Letter from Principal Secretary to the Treasury Edwin Mtei to S. H. Mauly of Ministry of Finance, Zanzibar, reference no TYC 46/08/04 dated 10th November, 1965.

 

 Letter from Minister of Finance (Zanzibar) Abdulaziz Twala to Minister of Finance (Dar Es salaam) A. Jamal of 25th November, 1965 on Establishment of Central Bank and Zanzibar Bank.

 

Letter from Principal Secretary to the Treasure Amon Msekela to Minister of  Finance of Zanzibar         Abdulaziz Twala on Establishment of Central Bank for Tanzania dated 30th November, 1965 with   reference TYC 46/0804.

 

Barua kutoka kwa Meneja Mkuu wa Benki ya Watu wa Zanzibar, A. J. Khatib kwenda kwa Katibu     wa Kamati Maalumu, Chama cha Mapinduzi, Ofisi ndogo ya Makao Makuu, Dar ES salaam ya      tarehe 30th April, 1984 yenye kumbukumbu PBZ/102/1 vol. 1.

 

Letter from Minister of Finance, Zanzibar Abdulaziz Twala on Establishment of Central Bank in Dar es salaam and a Bank in Zanzibar  dated 21th  De cember, 1965.

 

Letter to Minister of Finance from Financial Expert Ebert of 2nd December, 1965.

 

Regulations defining the Constitution, duties and powers of the East African Currency Board as revised and approved under the East African Board Regulation, 1955 and 1961.

 

Letter to Currency Officer with reference SU/FU/179 and dated 20th February, 1962.

           

General Notice of East African Currency Board from Chairman A. L. Adu, Nairobi dated 13th                September, 1963.

 

Letter from Secretary of East African Currency Board  dated 13th September, 1963 with reference          LEG/199 to Permanent Secretaries to the Treasury of Dar Es salaam, Tanganyika (Ref. your No.        TYC. 46/08 of the 22nd June, 1963);

 

The Secretary to the Treasury, Entebbe, Uganda (Ref. your  No. FS. 127111 of the 14th June, 1963);

           

The Permanent   Secretary to the Treasury, Nairobi, Kenya, (Ref. your no. DFN 446/010 of the 24th July, 1963);

 

The Secretary of Finance, Aden (Ref. your 11260 –B/174 of the 1st August, 1963);

 

The Permanent Secretary (Finance) Zanzibar (Ref. your no. F/P16/C9/9 of the 27th June, 1963; J. B.   Loynes, Esq., C.M.G. (For information) .

 

            Letter from H. R. Hirst to Embassy dated 21st March,1964 with reference INV/EA/F/196.

 Letter from H. R. Hirst to Embassy dated 1st June,1964 with reference BM/A/19  to J.D. Namfua.

 

Letter from J. B. Loynes to Hirst dated 8th June 1964.

 

Letter from Minister of  Finance A. Jamal to the Chairman of East African Currency Board with reference TYC.46/01 dated 22nd March,1966.

 

Letter from Hirst  to J. B. Loynes with reference TA/ORG/C/230  dated 28th March, 1966.

 

Minutes of agenda, 10th May 1966 with reference of TA/ORG/C of East African Currency Board     concern Board’s Position in Relation to Zanzibar and The Board’s Current Financial Position and      The Action to be Taken with the Board’s Remaining Assets by Secretary H. Hirst.

 

 Letter from Minister of Finance, Tanzania P. Bomani to Minister of Finance, Zanzibar, Abdulaziz         Twala with reference TYC46/08/07.

 

            The Partner-ship: Tanganyika Zanzibar Union 30 Turbulent years by Aboud Jumbe. (1994)Letter from    J. D. Namfua  to Hirst dated 9th June 1964 with reference no  TYC/46/01/502.

 

 Letter from H. R. Hirst to Embassy dated 1st June,1964 with reference    BM/A/35   to The Secretary to the Treasury,   Entebbe, Uganda; The Permanent Secretary to the Treasury, Nairobi, Kenya and Financial Secretary, The treasury, Aden. 

 

Letter from J. B. Loynes to Hirst dated 8th September, 1964.

 

Letter from H. Hirst to Edwin Mtei with reference BM/A/(VOL. III)55 dated 14th September, 1964.

Letter from Permanent Secretary W. H. Tweed to the Secretary of the East African Currency Board, Nairobi with reference TYC.96/01/540 dated 1st October,1964.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.