Na Ally Saleh

Mada ya makala yangu ya leo siku zote imekuwa ngumu katika mazingira ya Zanzibar. Mara nyingi waandishi wanaojaribu kuogelea eneo hili hupata lawama, lakini hii haiwezi kutuzuia kuandika kila tunapopata fikra mpya.

Tarehe 10 Disemba, 1963 Zanzibar ilipata uhuru wake kama ilivyokuwa kwa nchi zote zilizokuwa chini ya Muingereza kwa mfumo wa kwenda Lancaster House na vyama vyote vilivyokuwa vimeundwa katika nchi husika.

Kutokana na mfumo wa utawala uliokuwapo hapa Zanzibar, visiwa hivi vilikuwa viko chini ya Ufalme ambao ulikuwa ni wa kikatiba, na kila mtu alijua kuwa utolewaji wa uhuru hautaondosha ufalme.

Mjadala mkubwa umefanywa iwapo vyama vilivyokabidhiwa uhuru Zanzibar Nationalist Party ZNP na washirika wake Zanzibar and Pemba People’s Party ZPPP vilistahiki heshima hiyo kwa maelezo kuwa Afro Shirazi ndio iliokuwa ikidhulumiwa kwa mipango ya Ufalme na Mwingereza.

Tuseme tukubali hivyo kuwa ASP ilikuwa na uungwaji mkono mkubwa zaidi na kuwa ilikuwa ikishinda chaguzi zote ambazo zilifanyika Zanzibar na ndio yenyewe ilistahiki pale Disemba 10, 1964, jee ni sahihi kuwa kulirekebisha hilo kulistahiki kufanywa Mapinduzi?

Naseme hivi kwa sababu tunapotizama kipindi baina ya tarehe ya uhuru ya Disemba 10, 1963 na tarehe ya Mapinduzi siku ile ya Januari 12, 1964 tunatizama upande wa matokeo tu na fikra zetu zinakataa kabisa kufikiri juu ya kiini na athari yake kama yasingefaulu.

Wengi wetu tunapenda kuyahalalisha Mapinduzi hayo kwa hoja kuwa yalitaka kuung’oa Ufalme na kwamba yalikusudia kurudisha hadhi na heshima ya mnyonge mtu mweusi wa Visiwa hivi vya Zanzibar, ambavyo hata hivyo sehemu kubwa kidogo ya watu wake wakati huo na hadi leo sio weusi.

Mimi huwa najaribu kujiuliza siku zote. Hivi Serikali iliyopinduliwa ilikuwa kweli ya Mfalme? Kama ingekuwa Afro Shirazi ndio iliopokea vyeti vya uhuru pale Disemba 10,1963 na wao ndio wangeunda serikali, basi jee serikali hiyo ingekuwa ya Kifalme? Maana kwa vyovyote vile Mfalme angeendelea kuwepo.

Na kwa sababu hiyo jee Mapinduzi yale hayakuwa ni kitendo cha kupindua Serikali halali? Au ni kwa sababu ya kujenga hoja tu kuwa uhuru ulitolewa kwa vyama visivyostahiki ndipo uhalali wa kitendo cha kufanya Mapinduzi kinapopatikana?

Tumefikiria nini kingetokezea iwapo Mapinduzi yangeshindwa? Matokeo yangekuwa ni uhaini na viongozi wake wangekamatwa na kuhukumiwa kwa sheria za nchi kuwa ni wahaini na sio kuwa ni wakombozi kama ambavyo tunapotizama matokeo tunavyotaka kuamini kwa sababu uhuru ulikuwa tayari umeshatolewa.

Na nikifikiria hivi leo siamini kuwa Afro Shirazi iliyoshindwa katika jaribio la Mapinduzi katika nchi ambayo ilipokea vyeti vya uhuru ingepata imani ya Afrika kuwa ilikuwa ikitaka kuendesha ukombozi na hivyo kuwekwa hadhi moja na vyama vya ukombozi kwa njia ya mtoto barani Afrika wakati huo.

Nimeandika makala hii baada ya tukio la wiki iliyopita hapa Disemba 10 pale kikundi kimoja hapa Zanzibar kilipojitokeza kuamua kusherehekea sherehe za uhuru wa Zanzibar ulipatikana mwaka 1963 hadharani kwa mara ya kwanza kwa kipindi cha miaka 45.

Lakini pili nimeamua kuandika mistari hii kutokana na matamshi ya Waziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano Muhammed Seif Khatib, ambaye sio tu alipinga hatua hiyo lakini aliwaita watu hao kuwa ni wale wanaotaka “kurudisha ubwana na utwana.”

Mimi binafsi siguswi wala siumwi na chochote iwapo sherehe ya Uhuru itafanyika kama ambavyo inavyofanyika sherehe ya Mapinduzi. Kwangu yote ni matukio ya kihistoria na ambayo sina sababu yoyote ile ya kuyapinga.

Ila nimekuwa nikishangazwa kwa miaka yote hii hapajawahi kutokea watu ambao wanaweza kusimama na kusema kuwa haki ya kusherehekea Uhuru ipo kama vile ilivyo haki ya kusherehekea Mapinduzi, na ndipo kilipotokezea kikundi hiki moyo wangu ulifurahi sana.

Nchi zilizopata uhuru kwa Muingereza ni nyingi. Ni pamoja na Nigeria na Ghana na nyengine nyingi. Nazo hizi baada ya kupokea uhuru pia zilipindua viongozi wao waliowaletea uhuru.

Wao sababu zao hazikuwa kama za Afro Shirazi kwamba uhuru walipewa wachache na kuwa wachache hao walikuwa bega kwa bega na Ufalme. Ila wao walisema hao viongozi wao wa uhuru waligeuka kuwa Wafalme na nchi zao zikakwama kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Sote tunajua baada ya hapo mapinduzi mangapi yamefanywa katika nchi hizo. Lakini mpaka leo nchi hizo zinaendelea kusherehekea uhuru wa nchi zao na hatujawasikia wakikana tukio hilo hata iwapo Muingereza aliwapa watu ambao walishindwa kutimiza matumaini ya umma.

Wanaojaribu kukataa kutofanyika sherehe za uhuru wana mawazo kuwa Mapinduzi kilikuwa ndio kitu muhimu na cha mwisho (vital and ultimate) kwa maana hapana kitu cha kufananishwa na hicho katika kufikira matarajio ya umma.

Lakini ni ukweli leo miaka 45 baadae Mapinduzi hayo yana mengi ya kuhojiwa kwa maana ya kutimiza malengo yake hasa katika hili la kujenga umoja wa watu wake ndani ya uwanja mpaka wa kifikra na kuamini mtu apendalo.

Inatisha kumsikia kiongozi wa kisiasa leo akisema kuwa wanaotaka kujihusisha na kitendo cha sherehe za uhuru ambacho kwa kweli si lolote si chochote zaidi ya kuwa ni alama ya kumbukumbu (symbolic only) wanapakwa rangi za watu waliokaribu na mabwanyenye na wanaotaka kuendeleza ubwana na utwana.

Iwapo mwanasiasa kama Waziri Muhammed Seif Khatib wana fikra kama hizo mpaka leo, basi ni ukweli tosha kuwa Mapinduzi yameshindwa kufanya wajibu wake mkubwa wa kuunganisha Wazanzibari na kuondosha matabaka kwa umri wa miaka 45 ya Mapinduzi hayo.

Inatisha kuwa Waziri Muhammed Seif anaamini kuwa nchi hii bado ina mabwanyenye na yeye akiwa ni mwanasiasa wa kazi (career politician) akipitia tokea Umoja wa Vijana wa ASP, CCM na kushika nafasi za juu za uongozi, na ni kuonyesha kumbe nchi hii iko kama ilivyokuwa miaka 45 iliyopita.

Kwa maneno mengine kama si hivyo, ni kwa nini basi yeye Waziri Khatib na watu kama yeye wanaogopa watu kusherehekea uhuru ilhali Mapinduzi yameshaimarika na hayatarudi nyuma (irreversible) vyovyote vile itavyokuwa?

Hii haiwezi kuwa hoja kuwa Mapinduzi pia yameshindwa kutibu vidonda kwa kukataa muda wote ukweli kuwa yalipaswa kuwa shirikishi kwa wote (all inclusive) na sio kama ambavyo yameendeshwa kiasi ambacho hadi leo nchi hii ina wananchi wanaoitwa Afro Shirazi na wale waliopigwa chapa ya Uhizbu?

Waziri Khatib anakataa nini watu kusherehekea uhuru wa Disemba 10, 1963 wakati yeye ni mmoja ya watu wanaoendeleza siasa za chuki za vyama vya siasa vya wakati wa uhuru au kabla Mapinduzi? Si yeye anaebembeleza lugha hiyo na dhana hiyo?

Nani asiejua kuwa kwa siasa za Zanzibar ni vigumu mno kwa Wapinzani kuwashutumu Watawala kuendeleza siasa za kizamani, lakini ni rahisi sana kwa Watawala kutoa shutuma nzito nzito na hata kufananisha wazi wazi kwa mfano CUF na Hizbu na huku wakijua kuwa huko ni kuchochea chuki.

Kwa fikra zangu sherehe za uhuru wa Disemba 10, 1963 si kitu cha kumuumisha mtu kichwa na kukosa usingizi. Vyovyote vile wanaotaka kusherehekea hawajai hata kiganja kimoja. Nionavyo kuwashambulia ni kuwapa umaarufu wa bure.

Kama kusherehekea kwao kutawafanya watoe joto lao na kama kusherehekea kutawarudisha kundini ili wasaidie kutibu majeraha yao na kujenga umoja, sioni sababu gani wapigwe vita.

Kwa hakika kwa Serikali yenye sifa ya kuwa zingatifu na kujali umoja wa raia wake, ni fikra zangu sherehe hiyo hata yaweza kuwa ya Serikali, si lazima kwa hadhi moja na ile ya Mapinduzi kwa ajili ya kujenga maridhiano, maana si Waswahili wamesema kuwa mavi ya kale hayanuki?

One thought on “Sherehe za uhuru zitatibu vidonda, kuimarisha umoja”

  1. hi ni kweli na pia hatuambiwi kabisa ni nani alohusika kupindua kwani bi fatma karume anasema alikuwa na mumewe ndani wakati mapinduzi yakifanyika na bi fatma alimuuliza mumewe nini kinaendelea na karume akajibu kuwa ni wanaume hao wanafanya mapinduzi(kama iilivyotolewa na tvz) sasa kama ni hivyo kiongozi alikuwa amelala au kamagazeti la tanganyika standard lilvyoripoti ni kuwa kiongozi wa mapinduzi alikuwa okello sasa ni nani kiongozi wa mapinduzi?karume alolala na mkewe au okello alokesha kuuwa watu usiku ?

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.