Na Prof. Ibrahim Noor

Fikra ya kuwa Zanzibar haiwezi kuishi bila ya Tanganyika najua kuwa si sawa, ni fikra iliyokwisha kuelezwa na wakoloni wa Kiingereza kama tulivyonaqiliwa na Dr. Harith qabla ili kutujaza woga tusiweze hata kuhoji ukweli na uwongo wake. Kwanza tukumbuke kuwa nchi jirani zisizokuwa na vita hazina budi zishirikiane kwa namna mbalimbali. Haiwezi Tanganyika kuifunga milango na madirisha yake wala haiwezi kuisusia Zanzibar milele. Pili, Nchi yoyote iliyokuwa i-huru inaweza kupata tumbi ya faida ambazo katika muungano kama huu wa Tanganyika na Zanzibar haiwezi kuzipata. Nitakutolea mifano michache tu:

 1. Balozi mbalimbali zitafunguliwa Zanzibar , na hivyo wananchi wengi kujipatia kazi katika mabalozi hayo, na Zanzibar ilivyokuwa nchi ndogo, kazi hizo hazitakuwa kidogo kwa mujibu wa idadi ya Wazanzibari walioko nchini.
 2. Mabalozi hayo na nchi zao zitakuwa na mambo mengi ya kibiashara na kimisaada ambayo itakuwa inafanywa baina yao na Zanzibar bila ya kupitia Tanganyika na, kama tulivyoshuhudia kwa miaka 44 faida hizo kujepwa na Bara.

 3. Kuna nchi nyingi ziko tayari kuisaidia Zanzibar kwa hali na mali tena kwa kiwango kikubwa sana , lakini sio kupitia Muungano. Hivi sasa wakifanya hivyo watashambuliwa kwa maneno yasiokuwa na maana na ya fedheha, kwa hivyo wameona bora nusu ya shari na kuangalia tu mpaka Wazanzibari wenyewe wajiamulie kuwa huru.

 4. Umoja wa Nchi za Kiislamu (OIC) wako tayari kuipa Zanzibar mamilioni ya dola iwapo ni mwanachama na bila ya uhuru Tanganyika inatumia nguvu zake kuizuilia Zanzibar isifaidike.

 5. Wataalamu mbalimbali wa Kizanzibari walioko nje wako tayari kurudi na kuisaidia Zanzibar katika nyanja mbalimbali ili kuipeleka mbele kiuchumi, kiilimu, kiziraa na kila namna na wengi wao bila ya malipo.

 6. Wataalamu hawa wameishi nchi mbalmbali; wanazijua nchi hizo na mpaka lugha zao na wanajua namna ya kuipatia Zanzibar kila namna ya misaada itakayoiinua Zanzibar hadhi yake na hali yake katika kila uwanja.

 7. Kuna na mengineyo ninayoyajua yatakayokuwa na manufaa na Zanzibar huru (mengine ya kuiletea Zanzibar utajiri mkubwa sana) ambayo siwezi kuelezea humu barazani. Kwa hivyo tumia khayali yako asaa ukaelewa.

Kwa hivyo mimi sioni faida yoyote ya muungano. Sharia za muungano ni kama ulevi, na muungano wenyewe ni wa kilevi, vyovyote utakavyorakibishwa, khasara zake ni kubwa zaidi kuliko faida zake.

Angalia hivi sasa khasara iliyopata Zanzibar kutokana na muungano:

 1. Watanganyika wanateremka Zamnzibar bila ya mpango. Hatuwezi kutoa hoja kuwa: jee na Wazanzibari nao si wanateremka Tanganyika bila ya mpango! Wazanzibari wote wakihamia Tanganyika , basi hata hawatagutuka kwa sababu Tanganyika ni nchi kubwa na yenye mamilioni nyingi sana ya watu kuliko Zanzibar , lakini kumi tu katika mia ya Watanganyika wakihamia Zanzibar basi Wazanzibari ndiyo ameshapinduliwa mapinduzi ya milele! Na hilo ndilo lengo khasa la mafisadi na huko ndiko walikolenga!
 • Angalia hali ya uchafu unavyoteremshwa Zanzibar kutoka Tanganyika , kuanzia malaya wao na madanguro yao .

 • Pamoja na umalaya uliozidi, kuna na magojwa ya khatari yasiyokuwa na dawa na yenye kuambukiza.

 • Mabalaa ya ulevi usiokuwa na vizuwizi.

 • Wizi uliozidi.

 • Mauwaji ambayo hapo qabla ya mavamizi ya Watanganyika ya 1964 tukiyaona katika sinema na kuyastaajabia!

 • Khasara ya nyoyo za watu kubadilika kuelekea kubaya na upungufu wa dini na imani uliosababishwa na muungano ni khasara isiyoweza kuhisabiwa kwa mapauni, madola wala kwa vinoo vya dhahabu! Usiangalie kijuujuu tu na ukadhania hayo yote niliyokutajia hayakupangwa na mafisadi tokea qabla ya mavamizi ya 1964. Ukifikiria hivyo hadi utakuwa umetekwa kimawazo na propaganda zao zilizojaa uzushi na owongo.

 • Nakuachilia mwenyewe ujaze pengo nyinginezo nilizoziacha za khasara inayopata Zanzibar kwa ajili ya muungano. Iwapo Wazanzibari hawataamka na kupigania uhuru leo kabla ya kesho, basi na tuiangalie nchi inavyotumbukia katika shimo la moto lisilokuwa na ombe!

  Wala usidanganywe na mtu, Zanzibar kujipatia uhuru wake ni jambo rakhisi zaidi kuliko kuurakibisha muungano. Wazanzibari wakiug’ang’ania muungano basi wataendelea kuchezwa shre na kupinwa miereka na kusononeka, na hali zao kudhofika mpaka wamalizwe kabisakabisa.

  Unauliza: vipi, Wazanzibari, kujipatia uhuru ni rakhisi zaidi kuliko kurakibisha sharia za muungano?

  Jawabu: Si tumeshaona miaka nenda miaka rudi Wazanzibari wakidai hilo na badala ya kurakibishwa mkataba kwa manufaa ya Zanzibar na Tanganyika , ndiyo inda ya wakoloni wa Tanganyika ilipozidi kwa kuzidisha mambo yanayozidi kuikwamisha Zanzibar na kuipeleka pabaya zaidi!

  Kwa hivi sasa, mmojawapo — ama Mhishimiwa Amani au Maaalim Seif — wakiita mkutano wa ummati wa Wazanzibari na wakaitagazia Ulimwengu kuwa hawataki tena muungano na wanataka uhuru kamili, nakuambia changu hichi, wakoloni maqatili, mafaqiri walioko Tanganyika watakwenda mbiyo kwa kizaazaa wasijue la kufanya. Kwanza, ummati wa Wazanzibari watakaounga mkona sauti hiyo waingojeayo kwa hamu kuu yatakuwa ya “asiyekuwa na mwana aelekee jiwe” na wakoloni watakuwa marungu wala mirututu ya bubduki hawawezi kuitumia; watajikuta wamepwerewa; na hao makaburu wanaowategemea kuwaunga mkono hawatakuwa nao tena, kwani Wazanzibari watakuwa wanadai uhuru wao kwa njia za kidemokrasia ambazo, kama utakumbuka, hata Mwingereza mwenyewe, mkuu wa wakoloni na nguvu zake zote, hakuweza kuzifanyia mazingaombe na kuuzuia uhuru wa nchi alizozitawala hapo wananchi walipodai uhuru wao.

  Mwanasiasa yoyote yule atakaesimama Zanzibar katika juukwaa na kuidaia uhuru Zanzibar kwa kinywa kipana ndiye atakayekuwa anaadhimishwa kama mkombozi mkuu wa Zanzibar. Na siyefanya hivyo, au kuunga mkono wito huo, atakuwa ndiye khaini mkubwa katika nyoyo za Wazanzibari.

  Mara nyingine njia nyepesi za kujitatua na matatizo huwa zipo lakini wenye akili nyingi huzidi kujitata katika matatizo yanayotokana na nafsi zao wenyewee, ama kwa upungufu wa akili au kwa khofu zilivyowajaa!

  2 thoughts on “Zanzibar bila Muungano inawezekana”

  Leave a Reply

  This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.