Baadhi ya washiriki wa Kongamano wakifuatilia kwa makini mada kwenye kongamano hilo
Baadhi ya washiriki wa Kongamano wakifuatilia kwa makini mada kwenye kongamano hilo

Kongamano la siku mbili na la kihistoria lililojumuisha kwa mara ya mwanzo Wazanzibari wa kila mrengo na itikadi kwa madhumuni ya kuunda mbinu za kutetea maslahi ya Zanzibar na kupigania mustakbal wa Zanzibar uliodhalilishwa na muundo na mfumo usio muafaka wa Muungano, limemalizika jijini London Uingereza, jana Jumapili.

 

 

Kongamano hilo lilioanza tarehe 13 Disemba na kumalizika tarehe 14 Disemba, 2008 liliwakusanya Wazanzibari kutoka sehemu mbali mbali  Ulimwengu wakiwemo Wataalam, Wahadhiri, Viongozi mashuhuri, waandishi wa habari na wana harakati mbali mbali walichangia kimaandishi na ki kauli na kulifanya Kongamano hili kuwa la manafanikio makubwa sana.

 

Mada mbali mbali zinazoelezea historia ya Zanzibar na kukosoa mfumo wa sasa wa Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar na athari za Muungano dhidi ya Zanzibar ziliwasilishwa.  Makala hizo zilizowakilishwa zilijadiliwa kwa mapana na marefu na kutiliwa mkazo katika upungufu wa uhalali wa Muungano.

 

Mada zilizowakilishwa na kujadiliwa ni Majukumu na Malengo ya MUWAZA iliyotolewa na Dk. Yussuf S. Salim, Jukumu la Waza –Nje ya Ally Saleh, Nini Zanzibar cha Kujivunia iliyotolewa na Juma Duni Haji, Mategemeo ya ZNZ 2015 ya Salim S. Rashid, Nadharia ya Utaifa iliyowasilishwa na Mohamed Saleh, Muungano ya Enzi Talib Aboud / Salim  Rashid, Maendeleo ya Demokrasia ya Ibrahim Mzee Ibrahim, Mgogoro wa Kikatiba iliyotolewa na Abubakar Khamis Bakari, Utaifa na Ujananchi (Patriotism) ya Msaidizi Prof.  M.Adam M. Dosi/Dk. Mbarouk Shariff, Kuporomoka kwa Utamaduni Zanzibar ya Ali Mohammed Said na Zanzibar ni Nchi ya Muhammed Bakari 

 

Kongamano hili la Kihistoria la mwanzo ya aina yake liliweka wazi yafuatayo:

 

Malengo na majukumu ya MUWAZA

 • Malengo na majukumu ya MUWAZA ni kuunganisha Wazanzibari kwa kupitia kutafuta mbinu za kuondosha uhasama baina ya Wazanzibari.
 • Kukumbusha kwamba mizizi ya uhasama imetokana na mbinu za ”wagawe uwatawale” zilizotumiwa na Wakoloni wa Kiingereza na sasa kutumiwa na Serikali ya Muungano kuwagonganisha Wazanzibari.

 

Baada ya kuporwa kwa mamlaka ya Zanzibar kwa muda wa miaka zaidi ya 44, kutoridhiwa kwa Hati/Mkataba wa Muungano, kutoundwa kwa Baraza la kutunga Katiba kwa miaka 13, kuongeza kwa vipengele vya Hati ya Muungano kutoka 11 hadi 23 (38) kupitia Chama na Bunge la Tanganyika bila ya kushirikishwa kwa Baraza la Mapinduzi , Baraza la Mawaziri la Zanzibar au Baraza la Wawakilishi kunaifanya Hati/Katiba ya Muungano kuwa Battilli na isio na misingi ya kihalali na kulazimika kufutwa kwa mara moja.

 

Mambo mengi yametendwa na utawala wa Tanganyika (unaojificha chini ya mwaavuli wa Muungano) kwa madhumuni ya kuitawala Zanzibar kwa misingi ya Kikoloni.

Wafadhili wajiwajibishe

Wachochezi wa kuitawala Zanzibar walikuwa ni Marekani na Uingereza kwa kuogopa Afrika ya Mashariki kuelekea mrengo wa kushoto. Walimshajiisha Mwalimu Nyerere   ambae aliwatumia Mawakili wa Kikoloni kutunga Hati/Katiba iliokuwa na mfumo wa Kikoloni sawa na Ireland ya Kaskazini, bila ya kushirikisha Wanasheria wa Zanzibar, Baraza la Mapinduzi au Baraza la Mawaziri. Idhini, ridhaa na upitishaji wa Hati/Katiba yote yalipitishwa kupitia Chama na Bunge la Tanganyika. Marekani, Mngereza na Wafadhili wengine wanaendelea hadi leo kuulinda na kuutetea Muungano. Kila mmoja na maslahi yake, wengine kiutawala/kisiasa, wengine kidini na wengine kiuchumi na kiutamaduni. MUWAZA ina azma ya kuwashirikisha wafadhili hao katika ufumbuzi wa migogoro ya mfumo wa Katiba hiyo isiyo halali.

 

Chambuzi na maandishi kadhaa na tofauti yameandikwa kukosoa mfumo uliopo. Wanzanzibari wa kila aina, wakiwemo wanasiasa wa hadhi za juu kabisa na Wazanzibari walala hoi, wamekuwa mara kwa mara wakisimama kutaka sauti zao zisikike katika kutetea maslahi ya Zanzibar. Miaka nenda miaka rudi, kila kukicha Zanzibar inamegwa na kumegwa tena.

 

Zanzibar katika Bara la Afrika ilikuwa ni kati ya nchi iliyoendelea kwa hali ya juu kabisa na kuongoza katika daraja ya maendeleo. Leo ikiwa imetawaliwa na Mkoloni masikini ambae mwenyewe anaishi kwa misaada ya wafadhili, itatarajiwa iweje Zanzibar zaidi ya kuwa fukara ya kutupwa.

 

Wazanzibari Tuungane na Tushikamane

 

Hakuna medani au fani yoyote ya Zanzibar isioporwa, kutaka au kupangiliwa kuporwa. Zanzibar haiwezi kuibuka mradi jinamizi hili limeikalia kichwani. Pale tu Wazanzibari watakapoamua kuungana, kushikamana na kusimama pamoja  ndipo tutapata matumaini ya kutetea mustakbal wa Zanzibar. Hili la Wazanzibari kuungana limeonekana kuwezekana bila ya shaka yoyote. Mifano miwili hai ya ”Mafuta” ya ”Zanzibar si Nchi” yamewaamsha Wazanzibari na kutambua njama halisi za Serikali ya Muungano na kuwaaunganisha pamoja. Sasa Wazanzibari tumetanabahi zaidi ya siku zote kwamba sisi sote ni wamoja, ndugu, tuko macho na tumeungana. Na yoyote yule anaetaka kuiuwa nchi yetu basi ana azma na njama yakutaka kutua sisi sote kwa pamoja na wale watu watatu wakiwemo katika kundi hilo hilo.

 

Kongamano la London linasisitiza kuwa Wazanzibari tushikamane  kudai haki zetu tukiwa ndani na nje ya nchi.

 

Waza-nje

 

MUWAZA na Wazanzibari wengine walio sehemu mbali mbali nje ya Zanzibar wanahimizwa kutoka Zanzibar washikamane katika kila meddani katika kutafuta mbinu za kuinua maisha duni ya Mzanzibari aliye nyumbani. Tuige mifano ya harakati zinazokwenda sambamba na maendeleo kama ya wenzetu wanavyoshirikiana kwa sababu  ya walivyosakamwa na maafa yaliofanana na yetu sisi. Kongamano limekumbushwa jinsi Wazanzibari kwa vipindi tofauti wamehamia sehemu tofauti na kwa sababu tofauti. Ingawa kuna mengi yanayotofautisha WAZA-Nje lakini kuna mengi zaidi yanayotuunganisha hasa pale tutaponuia kusaidia kwetu. 

 

Waza-Nje ikiwemo MUWAZA tunakumbushwa wajibu mpya uliotukabili na kwa wakati huo huo tukitanabahishwa na kukumbushwa kwamba tuwache ile mitindo ya zamani ya sisi tulio nje kutaka kuwaamulia wa ndani na kuwa na mbinu za kutaka kupandikiza siasa zetu tukiwa nje.

 

MUWAZA inaihakikishia Zanzibar kuwa haina njama hizo wala haiko tayari kushirikiana na yeyote mwenye lengo kama hilo. Mtu au watu kama hao hawakaribishwi kwenye MUWAZA.

 

Dharau ya Wazanzibari

 

Ikiwa Wazanzibari hatutaki tena kuitwa Machakubimbi na kudharauliwa kwa kila aina ni lazima tuzindukane na kuendelea kuwa macho mpaka tupate haki zetu. Mamlaka ya Zanzibar yameshakwangurwa na hali halisi ilivyo, inaonyesha dhahiri kwamba mfumo wa serikali uliopo hivi sasa kwa mujibu wa tafsiri ya Tanganyika, ni kuwa kuna Serikali moja tu, na Bara inauwezo wa kutumia nguvu zake na kubatilisha lolote lile litakaloamuliwa na Baraza la Wawakilishi. Wanavyo  vyombo vyao vitatu koleo, spana na nyundo. Hata kama Baraza zima la Wawakilishi litaamua kwa maslahi ya Zanzibar vyombo hivyo vitatu vinaweza kuyabirua maamuzi ya wengi.

 

Pongezi kwa Wawakilishi na Wabunge wa Kizanzibari

 

Kwa vyovyote ilivyo Wawakilishi na Wabunge wa Kizanzibari wanastahiki sifa kwa kukataa kunyooshea shingo zao lile bisu la kuwakeketa kama kuku. MUWAZA inawapongeza wote hao na kuwaomba waibebe Zanzibar katika viganja vyao, juu na juu tena.

 

Serikali Tatu au…

 

Kongamano linaona haja ya kuwa na upeo wa mipango ambayo itairejeshea Zanzibar daraja ya maendeleo yake kama ilivyokuwa karne za nyuma, mradi Wazanzibari wataondosha tofauti zao za kijuu juu na kujizatiti na kupania ama kurekibisha Katiba ya Muungano na kukubali kuweko kwa serikali tatu au kila mmoja  aheshimu uhuru wa mwenzake na hatimae kushirikiana kama majirani wema.

 

Hili linawezekana kama tutasaidiwa kwa kuingilia kati kwa mataifa yalio marafiki zetu na yenye nia njema nasi na kusimamia majadiliano hayo.

 

Mazungumzo yawe ya uwazi yatayoshirikisha wataalam sawa wa pande zote mbili kwa maslahi ya nchi zote mbili na sio kama yale baina ya watu wawili, Mzee Abeid Amani Karume na Mwalimu Julius Nyerere tu, mmoja akiwa hana washauri wa aina yeyote na mwengine akiwa na wataalamu wa utungaji katiba waliojificha na kuandika kisirisiri. Yasiwe yale ya kushirikisha Bunge moja na sio Bunge jengine. Yasiwe yale ya mtu mmoja kuchanganya mchanga wa nchi mbili? Wakati Rais mwengine anakodolea macho tu bila ya kupewa ruhusa hata kumimina mchanga wan chi yake, (kama mchanga huo kweli ulikuwa unatoka Zanzibar?)

 

Kuwaiga Uswissi

 

Njia mojawapo muhimu ya kuepuka na kujizonga wenyewe kwa wenyewe imependekezwa katika Kongamano ni kuondoa mtindo wakujitia katika maboksi ya kifikra  na kuendelea kuzunguka mumo kwa mumo kila mmoja akiwa na fikra zake katika kijiboksi chake. Zanzibar ikiwa ijikwamue kutoka katika hivyo vijiboksi ni kutambua kwamba maslahi yetu ya pamoja yajengeke katika misingi kama ile ya serikali ya Kiswissi, ya kila mmoja kuchukua juhudi za makusudi za kuheshimu tofauti za mwenzake.

 

Utaifa, Uzalendo na Hisia za Kijananchi

 

Kutambua na kuthamini kwa utu, haki na maisha ya kila Mzanzibari kunatokana na kuwa na heshima na thamani ya Utaifa. Kuheshimu na kutukuza maisha ya kila Mzanzibari ni lengo muhimu linalomuongoza mtu kuthamini utaifa wa mwanataifa mwenziwe, jambo ambalo linaukuza utaifa na kila kilichomo ndani yake. Tutukuze maisha ya kila Mzanzibari kama nchi nyengine ulimenguni zinavyotukuza maisha ya wananchi wake kiasi kwamba kama mwananchi mmoja anafikwa na maafa Fulani basi taifa zima linasimama kmtetea na kumlinda mwananchi wake. Ujananchi, uzalendo na upenda nchi/taifa (nationalism & patriotism) ni misingi inayosimamisha taifa na udugu baina ya wananchi.

 

Utamaduni, Mila na Heshima Yetu

 

Chini ya muungano utamaduni wetu umekuwa ukikanyagwa kanyagwa na kudharauliwa. Mila zetu zimekuwa kama matambara mabovu kwa watawala wetu. Mzanzibari amekuwa hathaminiwi, ikiwa yeye ni Raisi wa Zanzibar au ni mwananchi wa kawaida. Njama maaluum zinapangwa kupiga vita dini yetu, misikiti yetu na utu wetu.

 

Kutokana na umasikini tuliopandikiziwa nao tumewekwa pahala ambapo heshima, uungwana na ustaarabu wetu unapotezwa. Vijana wameingizwa katika majanga ya kula unga na kufanya uchafu uliokithiri. Mengi kutoka na utaalii usionufanisha nchi yetu si kiajira wala kiuchumi kwa jumla. Ajira wanapewa wageni na faida kutokana na utalii kubaki Rome na Milan.

 

Ukuaji na Maendeleo ya Demokrasia

 

Zanzibar imepita njia ndefu kutafuta haki na demokrasia. Mngereza aliotesha  mbegu ya sumu ya wagawe uwatawale na kuwapa aliowataka haki ya kuwasilishwa katia baraza la kutunga sheria na kuwanyima asiowataka. Kulikuwa na wanaostahiki na wasiostahiki. Hii ikiwa mbegu ovu ambayo hatimae ilileta mgawanyiko na kumwagika kwa damu bure. Demokrasia imepanda na kushuka milima Zanzibar na kuleta upungufu wa demokrasia kukubalika kama ndio mitindo ya tawala bila ya kujali utu na udugu. Taaluma ya Demokrasia katika Kongamano hili  ilionekana ni elimu ya lazima kwa jamii ili kuondosha uhasama, chuki na  visasi. Ni wajibu wa Wazanzibari kuhakikisha kwamba elimu ya haki za jamii (civil rights) ndio njia moja wapo ya kuleta demokrasia, maelewano na maendeleo ya kisiasa na kijamii. Anapendekeza mtaalam aliyebobea, Sh. Ibrahim Mzee Ibrahim, Katibu Mkuu wa Baraza la Wawakilishi, katika Kongamano Ili kufikia suluhu, mshikamano na upendo baina ya Wazanzibari

 

Mgogoro wa Kikatiba

 

Kwa vile Zanzibar imeporwa mamlaka yake kikatiba, imeelezwa kwamba njia pekee kwa Zanzibar kujikwamua ni kupitia njia ya Mgogoro wa Kikatiba. Mbinu za kufikia lengo hilo zilipendekezwa na kuwasilishwa.

 

Zanzibar kama nchi ina mamlaka yake ambayo hayajawahi kufutwa hata siku moja, si ndani ya utawala wa Zanzibar au katika Umoja wa Mataifa, anasisitiza katika Makala yake kwenye Kongamano, mtaalamu maarufu ambaye ndiye aliyetunga Katiba ya Zanzibar ya 1984, Mhe. Abuubakar Khamis.

 

Njia bora itakayonufaisha nchi zote mbili ni kuundwa kwa Katiba mpya ya Zanzibar, Katiba mpya ya Tanganyika na Katiba ya Muungano. Hiyo ndio suluhu inayopendekezwa. si hivyo Mgogoro wa Kikatiba hautaepukika.

 

Zanzibar ni Nchi

 

Katika mjadala wa “Zanzibar ni Nchi” Dr. Muhammed A. Bakari, Mhadhiri Muandalizi, Idara ya Taaluma ya Siasa na Utawala, Chuo Kikuu cha Dar es salaam, anahitimisha katika makala yake kwenye Kongamano, kama hivi ifuatavyo:

 

Vyovyote iwavyo, jambo moja lililo wazi ni kwamba hadhi ya Zanzibar katika Muungano ina utata mkubwa ikiwa ni pamoja na utata wa kisheria na ndiyo maana leo hii baada ya miaka 44 ya Muungano bado kuna mjadala mzito juu ya hadhi ya Zanzibar katika Muungano. Sambamba na hilo ni kwamba mjadala unaoendelea unatokana na ukweli kwamba ama kisheria au kimatendo au yote mawili upande mmoja Muungano, yaani, Zanzibar hauridhiki na mfumo uliopo wa Muungano. Changamoto kubwa iliyoko mbele ya Wazanzibari na Watanzania ni kuhakikisha kwamba tatizo hili linapatiwa ufumbuzi wa kudumu badala ya kuendelea na matatizo na mijadala isiyokwisha.

 

 

Mapendekezo ya Kongamano la London

 

Ili kuwaunganisha Wazanzibari Kongamano imependekeza kwamba kuundwe:

 1. Kamati ya suluhisho na kusameheana – kama ya Afrika ya Kusini
 2. Kamati ya kuondosha uhasama – conflict resolution 
 3. Kamati ya kuunganisha Wazanzibari kutetea Mustakbal wa Zanzibar
 4. Kamati ya mawasiliano ya MUWAZA nje na ndani ya Zanzibar

 

 

Waliohudhuria kutoka Zanzibar:

 

 1. Abuubakar Khamis Bakari, Mkuu wa Upinzani Baraza la Wawakilishi
 2. Ibrahim Mzee Ibrahim, Katibu Mkuu wa Baraza la Wawakilishi
 3. Juma Duni Haji, Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar) The Civic United Front (CUF – Chama cha Wananchi)
 4. Juma Khatib, Katibu Mkuu wa zamani wa Wizara ya Mawasialiano Zanzibar

 

Mada Zilizowasilishwa:

 

1. Mgogoro wa Kikatiba Abuubakar Khamis

2. Maendeleo ya Demokrasia Zanzibar… Ibrahim Mzee

3. Jukumu la Wazenj – Nje Ally Saleh – Kakosa Visa

4. Mategemeo ya Zanzibar (Vision 2015) Salim Said Rashid

5. Muungano Enzi Talib Aboud – Kachelewa ndege

6. Nationalism and Petriotism Dr. Mohamed Adam M. Dosi Ass. Prof. na Dr. Mbarouk Shariff

7. Kuporomoka kwa Utamaduni wa Zanzibar – Ali Mohammed Said

8. Nini cha kujivunia Wazanzibari kwenye Muungano Juma Duni Haji

9. Zanzibar ni Nchi Dr. Muhammed Babari

10. Nadharia na Utaifa Mohamed Saleh

11. Malengo na Majukumu ya MUWAZA Dr. Yussuf S. Salim

 

Wawakilishi wa MUWAZA walitoka kutoka Zanzibar, Ufalme wa Nchi za Kiarabu (UAE), Marekani, Ujerumani, Skandinavia, Uingereza na Ufaransa.

    

Maazimio ya Kongamano

 

Baada ya kufanikisha kongamano hili ambalo limehudhuriwa na wazanzibari wengi kutoka duniani kote, bila kujali hisia na itikadi zao za kisiasa, imeazimia yafuatayo:-

 

Sisi Wazanzibari tuliokutana mjini London tarehe 13 – 14 Disemba kujadili “Hatma ya Nchi yetu ya Zanzibar, tumekubaliana na kuazimia kama ifuatavyo:-

 

a) Matatizo yanayoingamiza Zanzibar kubaki kama nchi yenye kuheshimika na kuheshimiwa,ni ukosefu wa umoja wa wazanzibari.  Tumeazimia kwamba kuanzia sasa.

 

b) Wazanzibari wameelewa kwamba tatizo la mgogoro wa Zanzibar ni kwa kuendeleza uhasama wa kila mmoja kujiona bora na ana haki ya juu kwa Zanzibar kupita mwenziwe.

 

c). Wazanzibari wameelewa kwamba nyuma ya vitendo hivyo ni Serikali ya Jamuhuri ya Muungano.

 

Kutokana na kuelewa huko, Kongamano hili linaazimia ifuatavyo:-

 

 1. Kuendeleza harakati za kuupitia upya mkataba wa Muungano ili kulinda maslahi ya Zanzibar na heshima yake.
 2. Kuandika Katiba mpya ya Jamuhuri wa Muungano na ya Zanzibar ili kukidhi maslahi ya pande mbili za Muungano. 
 3. Katika haja ya kuleta umoja wa kitaifa MUWAZA inapendekeza kuanzishwa kwa baraza la usuluhishi, litakalojenga umoja na kusameheana.
 4. Wazanzibari watajitahidi kujenga umoja bila ya kujali asili, utaifa au mahala mzanzibari alipotoka.
 5. Kila tutakapokuwepo iwe ni ndani au nje ya Zanzibar ni kusimama na kauli ya umoja wetu na kusimama na uzalendo wetu.
 6. Kwa dhamiri ya kuendeleza hoja yetu ya kujenga umoja wa Zanzibar, huu Kongamano hili limeazimia kwamba Kongamano jengine litakalowashirikisha wazanzibari wote ufanyike sehemu, katika siku na tarehe itakayopangwa.

 

     

Kwa Niaba ya MUWAZA,

Dk. Yussuf S. Salim,

Mwenyekiti wa Muda

 

2 thoughts on “Wazanzibari wamaliza Kongamano kwa maazimio mazito”

 1. Hello,

  Could you please help me? I am trying to locate Dr. Mbarouk Shariff. Thank you.

  1. I just found your message by luck on this blog. I have been trying to look for you for some years now but in vain. My contacts are:
   e-mail – mshar25@aol.com, cell phone # 914 434 1647. I cant wait communicating with you.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.