Na Salim Said Salim

UCHAGUZI wa Marekani umeweka historia mpya kwa taifa hilo ambapo kwa mara ya kwanza, mtu mweusi ataiongoza nchi hiyo. Uchaguzi huu ulikuwa tofauti na chaguzi zilizopita na ndio maana ulivutia watu kila pembe ya dunia. Wengi walitaka kuona kama mtu mweusi, Barrack Obama, angepewa nafasi ya kuiongoza Marekani. Tulichoshuhudia ni kuwa amepewa kura nyingi; tena kwa kishindo cha kweli: sio kwa njia ya wizi, au mizengwe yoyote. Sauti ya umma imeruhusiwa kusikika.


Wamarekani na watu wengi duniani wametaka mabadiliko kutokana na kuchoshwa na siasa za kibabe za Rais George Bush za kuilazimisha dunia iridhie Marekani kuwa polisi wa kimataifa na kuwa na haki ya kuvamia nchi yoyote na pia kutaka nchi zote zitunge na zifuate sheria za Kimarekani kama zile za kupambana na ugaidi.

Nchi nyingi za Ulaya, Asia, Arabuni, Amerika ya Kusini na Afrika zilitiwa kitanzi na kuburuzwa na Bush, baadhi yao kwa kuogopa na nyengine bila ya kutambua athari zake. Sasa uchaguzi umemalizika na kinachofanyika ni tathmini na watu katika nchi mbali mbali wanajiuliza wamejifunza nini katika uchaguzi huu wa Rais wa 44 wa Marekani.

Hapa nchini, miongoni mwa waliowataka Watanzania wajifunze baadhi ya mambo kutokana na uchaguzi huu ni Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa. Lakini namna alivyowataka Watanzania kujifunza inatia mashaka na kujiuliza kama Tendwa alielewa alichokisema au alidhani Watanzania ni mbumbumbu na hawana uwezo wa kutofautisha kati ya changa na pevu, mbichi na mbivu, shaba na dhahabu, mto na kitanda au mto na bahari.

Tendwa alimsifu mgombea wa Republican, John McCain, kwa kukubali kushindwa bila ya kinyongo na kuwataka wanasiasa na Watanzania kujenga utamaduni huu wa kukubali matokeo ya uchaguzi kwa vile hali hii inasaidia kuweka mazingira mazuri ya kujipatia maendeleoa baada ya uchaguzi.


Ni wito mzuri, wa hekima na busara ya hali ya juu. Lakini alichofanya Tendwa ni sawa na kutanguliza gari la farasi mbele na kutaka farasi aliyepo nyuma afanye safari ya kuelekea kule kwenye gari lake.


Kama kweli Tendwa alikuwa anatoa maoni yake kutoka moyoni na kwa nia njema, basi alipaswa kuzungumzia mazingira yaliyozunguka uchaguzi wa Marekani na kulinganisha yanayoonekana Tanzania wakati wa uchaguzi.

Angezungumzia hali inavyokuwa wakati wa uandikishaji, wakati wa kampeni, kwenye vituo vya kupiga kura na mazingira yanayoonekana ya wizi wa kura na matokeo kutolewa baada ya wiki nzima hata kwa majimbo madogo kama ya Zanzibar ambayo wapiga kura wake hawazidi 11,000 na baadhi ya majimbo huwa na urefu wa robo kilomita tu.


Tanzania, vyama vya upinzani huwekewa mikwara visifanye mikutano katika baadhi ya sehemu za nchi na hukataliwa kutumia viwanja vya Manispaaa au shule wakati chama tawala CCM hakipati vikwazo hivyo. Makamanda wa polisi wanaokandamiza upinzani hupandishwa vyeo kama tunzo kwa kazi nzuri waliyoifanya.


Katika uchaguzi wa Marekani, polisi hawakuonekana kutisha watu kwa kubeba silaha karibu na vituo vya kupiga kura au barabarani, lakini Tendwa hakuligusia hili.

Vile vile katika uchaguzi wa Marekani hatukusikia kuwepo vikundi vya vijana vinavyoshambulia vituo na kupiga watu nondo na mapanga kama inavyoonekana Tanzania wakati wa uchaguzi na hasa Zanzibar, na wanaofanya hivi hawakamatwi na kushitakiwa kwa uhalifu huu.


Wamarekani hawakwenda vituo vya kupiga kura na kuambiwa wasubiri karatasi za kura hazipo. Tendwa anajua kuwa ni kawaida Tanzania kwa vifaa vya kupiga kura kufika vituoni masaa sita baada ya muda wa kupiga kura kutarajiwa kuanza au kuokotwa mitaani. Jee haya ni mazingira yanayohakikisha kuwepo uchaguzi huru na haki?

Tendwa ni Msajili wa vyama vya siasa. Kati ya majukumu yake ni kuhakikisha nchi yetu inafanya uchaguzi wa haki na huru kwa kufuata sheria. Mbona hajauliza kwa nini hata mtu mmoja wa watu zaidi ya 5,000 waliorodheshwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar kwa kujiandikisha zaidi ya mara moja hawajashitakiwa na kuwajibishwa kisheria au hata majina yao kuwekwa hadharani?

Hivyo haoni kuwa hali kama hii inachafua uchaguzi na hata kupelekea anayeshindwa kutokubaki matokeo? Au kwa anavyoona Tendwa hii ni kwa vile udanganyifu umeanza kutoa sura kama sehemu ya chaguzi zetu?


Kinachoonekana ni kwa Msajili kuona umuhimu wa watu kukubali matokeo ya uchaguzi, hata pakiwepo mizengwe iliyokuwa wazi. Ni vizuri kwa Tendwa na wenzake katika ofisi yake na wale wa Tume za Uchaguzi wakaelewa kuwa wamekubali dhamana na wanao wajibu wa kuhakikisha wanazitekeleza kwa mujibu wa katiba, sheria za nchi na za uchaguzi.

Yaliyotokea Marekani ni fundisho kwa Msajili wa Vyama vya Siasa na tume zetu za uchaguzi. Ni lazima tukubali kubadilika na kuruhusu sauti za wananchi ziheshimiwe kupitia masanduku vya kura.

Tendwa, akiwa Msajili wa Vyama vya Siasa, anapaswa kuelewa kuwa amebebeshwa dhamana ambayo kama hawezi kuitekeleza kwa uadilifu basi asijaribu kuupotosha umma kwani mawazo ya hekima na busara huwa na maana pale yule anayeyatoa anapoonekane kwanza anayaamini na anayatoa kutoka moyoni na sio mdomoni.

Tendwa umenena,lakini hujatenda. Wanachotaka Watanzania, Bara na Visiwani, ni kuona unatenda yale unayoyasema katika kusimamia vyama vya siasa.

Muda upo, lakini unakimbia kwa kasi. Juzi hujaweza, jana hukuweza na je leo hutaweza kufanya la maana baada ya kuona uchaguzi wa Marekani ulivyofanyika? Ni vema kwa wewe na wenzako katika ofisi yako kwanza kujifunza misingi ya uchaguzi huru na haki ambao matokeo yake hukubalika bila manung’niko kisha ndio muwe walimu wa kutoa mafunzo ya kuwataka Watanzania wajenge utamaduni wa kukubali matokeo ya uchaguzi.

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.