Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetakiwa kuangalia upya suala zima la kurejesha utumiaji wa pasi za kusafiria baina ya Visiwa hivyo na Tanzania Bara ikiwa ni njia ya kuilinda Zanzibar na uhalifu ongezeko la watu.

Mjadala mkali umezuka katika Baraza la Wawakilishi kuhusu Sera ya Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi ambapo baadhi ya Wawakilishi wamependekeza kurejeshwa kwa hati za kusafiria (passport) kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Wakichangia Sera ya vitambulisho vya mzanzibari mkaazi, Wajumbe hao wamesema kuwa wakati sasa umefika kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kurejesha hati hiyo kwa maslahi ya Zanzibar kutokana na kukithiri wageni visiwani hapa wasiokuwa watanzania.

Waziri Kivuli wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ, Juma Abdallah Juma alisema kuwa vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi ni suala hilo linafanywa zaidi kisiasa.

Msemaji huyo wa Upinzani alisema haiwezekani Wazanzibari kuitwa wakaazi katika nchi yao na kuongeza kwamba vitambulisho hivyo havifai kutumika na kuvifelisha.

”Vitambulisho hivi kwa kweli havifai sera hii haifai isipitishwe kwa sababu inaonekana wazi kuwadhalilisha wazanzibari katika nchi yao,” alisema mwakilishi huyo.

Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni, Salmin Awadh Salmin (CCM), alisisitiza haja ya kurudishwa kwa hati za usafiri na kusema kuondoshwa kwake kwa kiasi kikubwa kumesababisha kuwepo kwa kasi ya vitendo vya kihalifu vikiwemo ujambazi na matukio mengine ya kutisha yalioibuka hasa katika siku za hivi karibuni visiwani hapa.

“Tunataka kurudishwa kwa hati za usafiri kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, tunataka kuwepo kwa udhibiti katika eneo la bandari pamoja na uwanja wa ndege,” alisema Awadh.

Mwakilishi huyo alisema sera ya vitambulisho vya Uzanzibari ukaazi lengo lake ni ulinzi kwa wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba na kuweza kuwatambuwa hasa Wazanzibari na wageni, lakini badala ya kulindwa na kupata usalama imekuwa kinyume chake.

Kwa upande wake, mwakilishi wa viti maalum (CUF) Zakia Omar, alitaka kurudishwa kwa utaratibu wa pasi za kusafiria kwa kuwa utaratibu huo ulisaidia sana kudhibiti vitendo vya uhalifu lakini sasa kutokana na kuondoshwa Zanzibar imekuwa kama kichaka cha waovu wenye kutaka hifadhi.

Alisema kuondoshwa kwa hati za kusafiria kati ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa kiasi kikubwa kumerudisha wimbi la vitendo vya uhalifu ambapo katika kipindi cha mwezi mmoja matukio zaidi ya saba yameripotiwa na jeshi la polisi kutokea visiwani hapa mwezi uliopita.

Hati ya kusafiri kati ya Tazania Bara na Zanzibar pasipoti iliondolewa katika miaka ya 1995, baada ya kubainika kuwepo kwa vikwazo vya usafiri katika nchi moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuonekana kwenda kinyume na Katiba ya jamhuri ya Muungano, ambayo hata hivyo inaangaliwa na Wazanzibari walio wengi kwamba nayo imekwenda kinyume na msingi muhimu wa Muungano huu, yaani Mkataba wa Muungano. Kisheria Mkataba wa Muungano ni mkataba wa kimataifa na ndio ulio juu ya sheria nyengine yoyote inayohusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

3 thoughts on “Paspoti irejeshwe”

  1. Kwa hilo mko sawa, kwamba watu wanaosafiri kati ya visiwani na bara watumie vitambulisho, ikiwezekana hata passport. Ila huo utaratibu uwe kwa pande zote za muungano, na si ule uhuni wa miaka ile wa upande mmoja. Si hivyo tu wabara wanaoishi visiwani waishi kwa permit maalum, vivyo hivyo wale wapemba kule dar es salaam, tanga na kwingineko wawe na work permit na vibali vya kuwaruhusu kuishi huko. Si hivyo tu wazanzibari waliojaa ma-wizarani huku bara nao waondoke waende wakafanye kazi huko smz, wanafunzi wote wa kizanzibari walioko bara need to have student’s visa. Otherwise kila mtu na kwake. kwani you are enjoying countless opportunities kwenye muungano, then mnapiga kelele. Watanganyika amkeni , hawa watu warudi kwao wakachimbe mafuta yao.kwa nini tubembeleze hivi vijisiwa ambavyo GDP yao ni sawa na mapato ya soko la kariakoo.

  2. Bwana Daudi naona kama umekasirika au? Ukumbuke hayo mambo ya vitambulisho ni kujaribu kusaidia kisiwa kidogo kisimezwe kama unavyojua watu wakia wengi sana serikali haitaweza kumiliki watu hao.Hao milioni moja waliokuwe[po wahoi, taabani!
    Na wazanzibari wakiwa wangepewa rukhsa wangekubali kukaa wenyewe na kusuluhisha matatizo yao ya kisiasa na uchumi wao.Hawajapewa huo uhuru wa kuamua maana kisiwa kinadidimia na watu wanataka kujua haki zao laini narudia tena wabebanwa.

  3. kuiba wataiba tuu mi ni mzaliwa klm kama machizi wakombA mpaka marekani unazania hivyo vitambilishio vitazua watu wenye uchu na ela …….na maendeleo kutoka maenea ya tz yote kukomba hio ni tapa ya mfa maji tunasubiria muda tuuu kutakuwa na mkuu wa mkoa nuda si mrefu usiwe na wasi ……………daudi

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.