Na Harith Ghassany

Nakushukuru kwa kuileta hii mada muhimu kuhusu marehemu Abdulrahman Mohammed Babu khasa katika wakati huu kwa sababu ni mada ambayo inahusu ya sasa hivi ya Zanzibar na ya mustakbal wa Zanzibar na sio ya tathmini ya Babu peke yake.

Nafikiri wakati hauko mbali kumbukumbu ya Babu kuja kuwekwa sawa. Wazanzibari tuna mambo mengi sana ya kuyaweka mahala yanapostahiki kuwekwa.

Kisiasa, Wazungu hawakumpenda Babu na si kwa sababu alikuwa Mkoministi au Msoshalisti. Huo “Ukoministi” wa Babu ulitumiwa vizuri na Wazungu kulifunika kombe lao…apite.

Wazungu walimtumia Babu kama ni kisingizio tu cha kuiwachia Zanzibar imezwe na waliyemtaka aimeze. Wazungu hao hao wanakubali kuwa hakuna mwanasiasa aliyekuwa shupavu Zanzibar kama Babu na ripoti ya CIA inamalizia kwa kusema hivi:

“Able, aggressive, extremely opportunistic, and charming – Babu was by all odds the most gifted of the Zanzibar government leaders. Moreover, he had powerful contacts. His great liability was that he was Arab. He and his Umma Party followers were always vulnerable on that account. On the whole, he was considered by most observers, to be the man most likely to emerge as the real power in Zanzibar.”

Ripoti inaendelea:

“The possibility that Babu and his followers might come to dominate the Government of Zanzibar was an anathema; to Nyerere, it would have been a repudiation of the Zanzibar revolution…Nyerere could have been expected to do anything and everything in his power to prevent such an eventuality.”

Bahati mbaya Babau akikiona kila kitu kwa miwani buluu ya “class” na kila pahala akiona buluu ya “class.” Wenzake alotaka kushirikiana nao hawakujali kama yeye ni mpigania haki za wanyonge. Walimvalia miwani yenye kuona kitu kimoja tu, nacho ni Uwarabu = Uislamu.

Babu alilirukia rikwama la mapinduzi ambalo nahodha wake hakutaka kuwa karibu na Janab wa “Kiarabu.” Masikini Babu akavalishwa blanketi la kuwa yeye ndo mpinduzi mkubwa kwa kutarajia kuwa atakuja kupata nafasi ya kuja kuyafanya mapinduzi yake na kuinusuru Zanzibar lakini ilikuwa tayari haiwezekani mwisho kwa sababu haikuwezekana mwanzo.

Babu atakuja kuhukumiwa vingeni na wako watakaokuja kumsameh na wako wachache watakaokuja kuendelea kumuonea huruma.

Babu aliiependa sana Zanzibar lakini mapenzi yake yalikuwa ya aina nyingine kabisa na mapenzi ya waliomtumia kwa yao, na yeye kuwatumia kwa yake, na kumfanya Babu kuwa ndio mbaya wa wabaya kumbe wao walitaka kuihalalisha khiyana yao juu ya Zanzibar kwa kuonyesha kuwa hata “Mwarabu” yuko nao katika kuifisidi Zanzibar kwa hiyo mapinduzi hayakuwa dhidi ya Waarabu = Uislam.

Kila kiongozi mwenye kuitetea Zanzibar anaonekana ni Mwarabu tu. Akisema ni Mshirazi basi anafahamika moja kwa moja kuwa ni Mwarabu. Akisema ni Mpemba basi ndo usiseme. Akitoka bara na akatafakhari kuwa ni Muafrika Muislamu basi hilo ndo jaarabu lenyewe! Basi hii “poo simo! mimi ni Mgazija, mimi ni Mhadimu, mimi ni Musilamu Muafrika, mimi ni Mhadhrami, lakini mimi ni Mhindi bwana!” ni kujifanya karagosi ndani ya mikono ya adui khasa wa Zanzibar.

Ukishakataa kama wewe si Mwarabu wakati Uwarabu una maana nyengine ambayo ni kinyume unavofikiria wewe, basi tayari, kwa kutowa mfano, umeshageuzwa mbwa mwenye kulitafuna gongo kumbe gongo limeshikwa na mkono mrefu ulioko upande wa pili wa Zanzibar. Babu alitafunishwa gongo na yeye akafikiri anaukata mkono wa adui khasa wa Zanzibar – tabaka za kijamii. Kumbe sivyo.

Mapinduzi yamekwisha, imekuja Jamhuri, umekuja Muungano, kimekuja chama kimoja, vimekuja vyama vingi na umri unakwenda. Lakini kitu kimoja hakijabadilika hata kama hao Waarabu hawako tena kwenye utawala. Tumeshakiona lakini bado hatujakikubali basi na mchezo unaochezewa Zanzibar unaendelea na utaendelea.

Komred Babu hakuufahamu mchezo na alipocheza nao ndipo ulipomcheza. Waliokuwa hawana chuki ya Uaarabu kama Eritreia na kwengineko walimuhishimu na kumuenzi.

Labda kuna siku na Zanzibar itamuenzi baada ya kutambua kuwa kumbe hakuwa alivotaka afahamike na kumbe mambo yalikuwa na wenyewe ambao hata yeye Babu na uwanamapinduzi wake wote wa kujifanya dhidi ya ubeberu na umwinyi wa Kiarabu kumbe na yeye alionekana na kufahamika kuwa ndo yuleyule, ndo huyohuyo Mwarabu.

Mwarabu mbaya tu akiwa mbaya akiwa mzuri maana yake Muislamu mbaya tu na hakuna Muislamu mzuri na mbaya. Tathmini ya Babu itakuja kuwajumlisha viongozi wazalendo WOTE wa Kizanzibari.

Mzee Jumbe alikuja kufahamika vipi mwisho wa utawala wake? Kwani Maalim Seif anaonekana na kufahamika vipi na Tanganyika? Dk. Salmin Amour alikuja kufahamika vipi mwisho wa utawala wake? Wenye kuitetea kweli Zanzibar ni Nchi wanafahamika kuwa ni Waarabu wenye kutaka kuirejesha Dola ya Kiislamu. Kwani Waislamu wa Zanzibar wakiwa watawala HURU wa Zanzibar si watakuwa tafauti gani na Waarabu Waislamu?

Na kila wakiukataa Uwarabu ili wakubalike basi sumu ya Uwarabu ndipo unapozidi kuchemshwa chunguni ikawachiwa ivunde. Jamani vita va propaganda havijaanza kwetu Wazanzibari na ndio maana hii safari imekuwa ndefu kutokea 1956 pale Nyerere alipozinuganisha African na Shirazi Associations.

Jee, Babu alikuwa adui wa Zanzibar na wa Afrika? Babu alikuwa adui wa nafsi yake. Babu aliipenda sana Zanzibar lakini mapenzi yake yalivaa miwani ya rangi ambayo siyo alioifanyia hisabu na kufanyiwa yeye na washiriki wake. Na tatizo mpaka kafa hakuusema undani wake ukafahamika na badala yake kawaachia wapenzi wake kazi ngumu ya kuwa hawawezi kusema ambalo Janab hakulisema kwenye uhai wake.

Babu hakuwa adui wa Zanzibar ingawa na yeye pia hakumfahamu, au hakutaka kumfahamu, adui wa Zanzibar ni nani kwa hiyo akatumiliwa na adui wa Zanzibar kumfanya yeye ndo adui nambari moja ili adui apitishe ufisadi wake.

Nina wasiwasi viongozi wazalendo wa Zanzibar wa hivi sasa wanakabiliwa na mtihani huohuo na ingawa haufanani sana na wa Babu, hatari ilioko juu yao kwa kutokumfahamu au kutokubali kumfahamu adui khasa wa Zanzibar kutakuja kukifanya kizazi cha baadae kuliuliza hili suala unaloliuliza wewe ndugu yangu BiSalma.

The greats from Zanzibar wanauliwa na kusahaulika mmojammoja kwa sababu the greats from Tanganyika hatujawafahamu ni kipi khasa wako tayari kukipigania kwa hali yoyote ile pamoja na kuuwa tena na tena ili Zanzibar isiwatoke?

Pazia la Zanzibar bado halijashuka!

Chanzo: Imechukuliwa kutoka ukumbi wa zanzinet.net, jukwaa la Wazanzibari, tarehe 18 Oktoba, 2008

Leave a Reply

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.